HISTORIA YA MUZIKI WA HIP HOP NA BONGO FLEVA NA JINSI UNAVYOONEKANA KUATHIRIWA ZAIDI NA WASHAIRI WA KIMAPOKEO KULIKO WANAUSASA
HISTORIA YA
MUZIKI WA HIP HOP NA BONGO FLEVA NA JINSI UNAVYOONEKANA KUATHIRIWA ZAIDI NA
WASHAIRI WA KIMAPOKEO KULIKO WANAUSASA
Katika makala haya tunakusudia kujadili
namna muziki wa kizazi kipya (Bongo Fleva na Bongo Fleva) kuonekana kuathiriwa
na wanajadi kuliko wanausasa. Hivyo basi ili kukamilisha hilo, kazi hii
tumeigawa katika sehemu tatu. Sehemu ya kwanza ni utangulizi ambapo tutaangalia
maana ya istilahi muhimu zinazojitokeza katika mada yetu, tutaangalia historia
ya muziki wa kizazi kipya lakini pia tutaangalia kwa ufupi wanajadi na
wanausasa ni vitu au mambo gani wanayoyasimia. Sehemu ya pili ni kiini cha swali
letu, katika sehemu hii tutaangalia vipengele vinavyoonesha kuwa wasanii wa
kizazi kipya kuathiriwa na wanajadi kuliko wanausasa na sehemu ya mwisho
itakuwa ni hitimisho.
Maana ya Hip Hop na Bongo Fleva.
Wapo wanaouona muziki wa kizazi kipya
yaani Hip Hop na Bongo Fleva kuwa ni kitu kimoja lakini wapo wanaopinga na
kutofautisha kuwa Hip Hop na bongo fleva ni aina tofauti ya muziki (Omari
2009:5, Samwel 2012:12). Ama kuhusu neno Bongo Fleva mpaka sasa bado kuna utata
kuhusu nani hasa mwasisi wa neno hili, inaelezwa kuwa, mwanamuziki wa regge,
Jah Kimbute ndiye aliyeasisi neno hili pale alipoamua kuchanganya muziki wa
asili na regge na kuziita Bongo Fleva. Mtayarishaji wa muziki P.Funk anaeleza
kuwa mwasisi wa neno Bongo Fleva ni DJ Bonnie Love ambaye aliliasisi neno hilo
mwaka 1998, Omari (keshatajwa, 10-11).
Madai haya kuhusu waasisi wa neno Bongo
Fleva linaonekana kupingwa vikali na Mtangazaji wa siku nyingi, Michael Mhagama
ambaye anadai kuwa yeye ndiye mwasisi wa neno hilo na aliliasisi katika kipindi
chake cha DJ Show kilichokuwa kinarushwa na Redio One miaka ya 1990 hususani
mwaka 1996. katika makala yake, Mhagama anasema, “Ilipofika dakika 30 za muziki
wa R & B,siku hiyo nilikuwa kwenye usukani na kwa mbwembwe nilicheza nyimbo
ya kundi la R&B lililoitwa 4Krewz Flava na baadaye kuiunganisha na nyimbo
nyingine ya Unique Sistaz.Kwa vile midundo,mpangilio,lugha na utaalamu wa
muziki wenyewe kamwe huwezi kuufananisha na ule wa Soul 4 Real au SWV kutoka
Marekani,tulipenda tutofautishe kidogo kati ya aina hizi mbili na ndipo session
hii niliibatiza jina ambalo lingetofautisha R&B ya Marekani na ile ya kwe
tu….niliipa session hii jina la BONGO FLAVA.” Wengine wanaotajwa kuwa ni
waasisi wa neno Bongo Fleva ni DJ. KBC, DJ. Phat Black, DJ. Venture na Steve B.
(Reaster-Jahn na Hacke, 2014:24).
Ingawa lengo la kazi hii si kujikita katika
mgogoro huo ila tumeona kwa umuhimu wake tuugusie japo kwa ufupi. Kama
tulivyosema hapo awali kuwa wapo watu wanaouona muziki wa Hip Hop na Bongo
Fleva kuwa ni muziki tofauti, Ramadhan Mponjika akinukuliwa na Samwel na
wenzake (2013:55) anasema, muziki wa Bongo Fleva ni kapu ambamo ndani yake kuna
miziki ya aina mbalimbali ikiwemo zouk, rhumba,regge, RnB, n.k. Kinachoelezwa
hapa ni kuwa, muziki wa Bongo Fleva ni aina yoyote ya muziki wenye asili ya nje
lakini unaimbwa kwa mahadhi ya Tanzania (Bongo) lakini si Hip Hop. Dai hili
linaungwa mkono na Michael Muhagama (keshatajwa) kupitia andiko lake, anasema,
“Hii ilikuwa mwaka 1996 na ndio ulikuwa mwanzo
wa neno BONGO FLAVA likiwa na maana muziki wenye mahadhi ya nje lakini wenye
vionjo na ladha ya Tanzania na si vinginevyo lengo kuu ni kuitofautisha na
muziki ule wa Marekani. Hip Hop ya Tanzania ilibaki na
itabaki vile vile kama ilivyo, ila muziki wowote ule wa nje, mbali ya Hip Hop
na DANSI ya Tanzania niliuita na kuufahamishakwa umma wa watanzania kama BONGO
FLAVA ndani ya kipindi cha DJ SHOW cha Radio One.” Hapa maana yake ni
kuwa, jina la Bongo Fleva lilitumika tu, kutambulisha muziki wenye asili ya nje
lakini wenye mahadhi ya Tanzania (Bongo) tofauti na muziki wa Hip Hop na dansi
ambayo yenyewe ilitambulishwa kwa jina la Hip Hop ya Tanzania/Bongo au Bongo
Hip Hop.
Ama kuhusu Hip Hop,
Mahenge (2011:8) anasema, Hip Hop ni aina ya ushairi, usimuliaji au usemaji
unaopangwa kivina kwa kufuata mdundo wa ala za muziki ambao ulisharekodiwa.
Pamoja na kwamba fasili hii ya Mahenge inatupa mwanga kuhusiana na maana ya Hip
Hop ambayo kwa kiasi kikubwa tunakubaliana nayo lakini dai la kusema usimuliaji
au usemaji unapangwa kivina kwa kufuata mdundo wa ala za muziki ambao
ulisharekediwa si sahihi kwani sasa hivi wasanii wengi wa Hip Hop wanaimba juu
ya midundo ya muziki ambayo haijarekodiwa vyombo vya muziki vinapigwa sambamba
na wao wakiimba na wakati mwingine hurap kwa mtindo unaojulikana kama mitindo
huru yaani kutoa mashairi ya papo kwa papo kwa kufuata midundo ya muziki
inayopigwa au bila kuwepo kwa midundo ya miziki yaani akapela.
Kwa maoni yetu, tunaona
kuwa Hip Hop na Bongo Fleva ni muziki tofauti, muziki wa Hip Hop ni utamaduni
unaombatana na elementi za, michoro, rap, Dj, mabreka, ni muziki ambao mashairi
yake yanaganwa kwa kutumia mashairi yenye vina na midundo mizito wakati bongo fleva
ni mkusanyiko wa muziki wenye asili kutoka nje ya Tanzania lakini yenye mahadhi
na vionjo vya Tanzania ambayo hujumuisha Zouk, Kwaito, RnB, Kwaito, n.k. Kwa
ujumla muziki huu Hip Hop na Bongo Fleva huitwa kwa jina la muziki wa kizazi
kipya ikiwa na maana ya muziki unaopendwa na vijana kizazi cha sasa (Omari
2009:5, Samwel 2012:12).
>>>>>INAENDELEA>>>>>>>>>>>