HISTORIA YA MUZIKI WA HIP HOP NA BONGO FLEVA NA JINSI UNAVYOONEKANA KUATHIRIWA ZAIDI NA WASHAIRI WA KIMAPOKEO KULIKO WANAUSASA
Aidha kabla
hatujaingia katika kiini cha mjadala wetu, tuwaangalie kwanza wanajadi na
wanausasa ni mambo gani wanayoyasimamia na kuyasisitiza katika utungaji wa
mashairi. Ushairi wa kijadi ni ushairi unaozingatia urari wa vina na mizani
kuwa ndiyo roho na uti wa mgongo wa mashairi ya Kiswahili kwao hawataki
kukiri kuwa mashairi yalaiyotungwa katika mtiririko (masivina) ni mashairi
(Mulokozi na Kahigi, 1979:1) kwa maana hiyo kwa pamoja na vipengele vingine
katika ushairi wa jadi ni kuzingatia vina kama anavyotuambia Abeid
(1952:viii), “Neno moja tukumbuke katika utungaji, nalo ni hili ya kuwa
mawazo ya mtungaji yazue vina, siyo vina kuzua mawazo.”
Madai haya yanaonekana
kuungwa mkono na wanajadi wengine kama vile, Chirahdin, Mayoka, Kandoro,
Al-amin Mazrui na Ibrahim Shariff kuwa vina na urari wa mizani ndiyo
vitambulisho vya ushairi wa Kiswahili (Mulokozi na Kahigi, 1979:11). Jambo la
msingi hapa ni kuwa wanajadi wanakumbatia sana suala la vina na mizani katika
tungo za mashairi. Ili kuwa na shairi zuri, mwanajadi Sheikh Amri Abeid anataja
mambo manne muhimu yanayopaswa kuzingatiwa katika ushairi ambayo ni, mizani,
vina, kituo na kujitosheleza. Wanajadi wengine wanaotaja mambo muhimu yanayotakiwa
kuzingatiwa katika ushairi ni pamoja na, Massamba (1983) anataja vina, mizani,
kituo, muwala, Kibao (1983) naye anataja, mizani, vina, urari, muwala,
utoshelevu na kuwa na maana wakati Komba (1977) anataja, mizani, vina, kituo na
utoshelevu. Ama kwa hakika tukiwachunguza wataalamu hao tutagundua kuwa,
wanachosisitiza shairi lenye sifa za ujadi linatakiwa kuzingatia vipengele
vifuatavyo, Mizani, vina, kituo na kujitosheleza.
Kwa upande wao,
wanausasa wanaona shairi si lazima lifuate urari wa vina na mizani, Mathalani,
Mulokozi na Kahigi (1982;25) wanasema ushairi ni sanaaa inayopambanuliwa kwa
mpangilio maalum wa maneno fasaha na yenye muwala kwa lugha ya mkato, picha,
sitiari au ishara katika usemi maandishi au mahadhi ya nyimbo, ili kuleta wazo au
mawazo, kufunza au kueleza tukio au hisi fulani kuhusu maisha au mazingira ya
binadamu kwa njia inayogusa moyo. Kwa maoni yao wanausasa wanaona kuwa shairi
ni sanaa yenye mpangilio mzuri wa maneno, lugha ya mkato na matumizi mengine ya
lugha ili kutoa mawazo wao hawasisitizi juu ya kuzingatia urari wa vina na
mizani kama wafanyavyo wanajadi.