MADA YA KWANZA: MAWASILIANO
Lugha
ni kwa ajili ya mawasiliano
Kwa kutumia lugha binadamu anaweza
kufanya vitu ambavyo viumbe wengine hawawezi kuvifanya. Vile vile lugha
hutuwezesha sisi kuzungumzia hisia zetu, matamanio yetu, kucheza, kufanya kazi
n.k. Yote haya yanawezekana kwakuwa tunayo lugha ambayo ndiyo nyenzo kuu ya
mawasiliano.
Mfumo wa Lugha
Hoja kuwa lugha ni mfumo inamaanisha
kuwa lugha ina muundo unaohusisha viambajengo mbalimbali. Viambajengo au
vipashio hivi ni sauti, neno na sentensi. Kwa pamoja, vipashio hivi
hushirikiana kuunda tungo zenye maana na kama tungo hizo hazina maana au kama
haziwasilishi ujumbe wowote basi tunasema haziwi lugha.
Dhima za Lugha katika Mawasiliano
Fafanua dhima za lugha katika
mawasiliano
Baadhi ya dhima za lugha ni pamoja
na hizi zifuatazo:
- Ujumi: ujumi
ni hali ya kutumia maneno ya lugha fulani kwa ufundi na ustadi wa hali ya
juu kwa lengo la kuburudisha na kuwavutia watu wengine. Baadhi ya watu
hutumia lugha kwa dhima hiyo, ili maksudi wasomaji au wasikilizaji wao
wavutike na kuburudishwa na Lugha hiyo. Maeneo yatumikamo lugha yenye ujumi
wa kiwango cha juu ni kwenye matangazo na kwenye fani ya utunzi wa
mashairi.
- Utambuzi: Ni
hali ya kufikiria kwa makini, kukokotoa na kutoa majibu ya maswali tofauti
ndani ya ubongo. Chombo kikuu kitumikacho kutoa majibu hayo ni lugha.
Kutokana na muktadha huo tunaweza kusema kwamba lugha hutumika kama chombo
cha utambuzi.
- Hisia: ni
fikra za ndani alizokuwa nazo kiumbe mwanaadamu. Tunapotaka kuonyesha hisia
zetu na vilevile kuwavuta wengine kwa maneno mazito yanayoweza
kumtoa msikilizaji machozi ya huzuni au ya furaha tunachagua maneno makali
yenye hisia.
- Kujielezea: Hali
ya mtu kudhihirisha mambo mbalimbali aliyokuwa nayo ndani ya moyo wake.
Kwa mfano mtu anaposema nina furaha sana. Hapa mtu anatowa msisitizo wa
kuonyesha kiwango cha furaha alichonacho, hili linafanyika kwa kutumia
lugha. kwa ufupi tunachoweza kusema hapa ni kwamba lugha hutumika kwa
ajili ya kujielezea.
- Kuamuru: Ni
kutoa maelekezo kwa njia ya kuamrisha. Kwa mfano hakimu anamuhukumu
mshitakiwa kwa kumuamuru ‘Ninakufunga miaka mitatu jela’. Hapa
lugha inatenda kazi ya kuamuru.
- Kushirikiana: ni
hali ya kutenda kitu kwa pamoja au hali ya kuwa na ubiya kwenye jambo. Lugha
huwezesha watu kujenga mahusiano ya siri baina ya watu wawili au zaidi na
kuweza kujitengenezea njia zao za kuwasiliana pasipo wengine kuelewa.
- Kuonesha: kumuelekeza
mtu kitu kwa njia ya kuashiria. Unapotaka kuonesha jambo ni
lazima utumiye lugha kwa njia moja au nyengine.
Matumizi
na Umuhimu wa Lugha
Lugha hutumika kama chombo, zana,
kifaa au njia ya kufikia lengo fulani. Baadhi ya matumizi ya lugha ni pamoja na
haya yafuatayo:
- Kuwasiliana:- Lugha
hutumika kupashana habari
- Kuunganisha- Lugha
hupatanisha na kuleta uelewano miongoni mwa wanajamii. pia lugha huweza
kutofautisha jamii moja na nyengine.
- Kujenga jamii- lugha
huleta/huhimiza shughuli za maendeleo ya jamii, huleta amani na mshikamano
katika jamii.
- Kufundishia- Lugha
hutumika katika kufundishia elimu.
- Kutambulisha- Lugha
hutumika kutambulisha jamii ya watu fulani.
- Kuhifadhi- Lugha
ndicho chombo cha kuhifadhi na kueneza utamaduni
Matamshi na Lafudhi ya Kiswahili
Matamshi ni namna ambavyo mtu anatamka neno au jinsi mtu
anavyozungumza lugha. Unaposema fulani ana matamshi mazuri ya Kiswahili utakuwa
unamaanisha anazungumza Kiswahili fasaha.
Neno moja linaweza
kuzungumzwa/kutamkwa kwa namna tofauti na watu mbalimbali kutokana na sababu
mbali mbali, sababu hizo ni pamoja na eneo la kijiografia anakotoka huyo mtu,
kabila lake, kundi lake la kijamii mfano msanii au mwanasiasa, na elimu
aliyonayo. Hizi zote zinaweza zikawa ni sababu za kufanya watu watofautiane
katika matamshi.
Dhana ya matamshi huhusisha:
- Sauti za lugha husika
- Mkazo
- Kiimbo.