HISTORIA YA MUZIKI WA HIP HOP NA BONGO FLEVA NA JINSI UNAVYOONEKANA KUATHIRIWA ZAIDI NA WASHAIRI WA KIMAPOKEO KULIKO WANAUSASA
HardBlasterz, Gang Stars With Matatizo
(GWM), Wagumu Weusi Asilia, Young Da Mob, Afro Reign, Jungle Crewz Pose, Bantu
Pound, Hardcore unit kwa kutaja machache. Wasanii na makundi ya kuimba (Bongo
Fleva) ni kama vile, Mawingu Band, Lady Jay Dee, Stara Thomas, Unique Sisters,
Nurueli, 4Kruz kwa kutaja wachache Mhagama (keshatajwa), Mbilinyi (keshatajwa),
Mwanjoka (keshatajwa).
Aidha kabla hatujaingia katika kiini cha
mjadala wetu, tuwaangalie kwanza wanajadi na wanausasa ni mambo gani
wanayoyasimamia na kuyasisitiza katika utungaji wa mashairi. Ushairi wa kijadi
ni ushairi unaozingatia urari wa vina na mizani kuwa ndiyo roho na uti wa
mgongo wa mashairi ya Kiswahili kwao hawataki kukiri kuwa mashairi
yalaiyotungwa katika mtiririko (masivina) ni mashairi (Mulokozi na Kahigi,
1979:1) kwa maana hiyo kwa pamoja na vipengele vingine katika ushairi wa jadi
ni kuzingatia vina kama anavyotuambia Abeid (1952:viii), “Neno moja tukumbuke
katika utungaji, nalo ni hili ya kuwa mawazo ya mtungaji yazue vina, siyo vina
kuzua mawazo.”
Madai haya yanaonekana kuungwa mkono na
wanajadi wengine kama vile, Chirahdin, Mayoka, Kandoro, Al-amin Mazrui na
Ibrahim Shariff kuwa vina na urari wa mizani ndiyo vitambulisho vya ushairi wa
Kiswahili (Mulokozi na Kahigi, 1979:11). Jambo la msingi hapa ni kuwa wanajadi
wanakumbatia sana suala la vina na mizani katika tungo za mashairi. Ili kuwa na
shairi zuri, mwanajadi Sheikh Amri Abeid anataja mambo manne muhimu yanayopaswa
kuzingatiwa katika ushairi ambayo ni, mizani, vina, kituo na kujitosheleza.
Wanajadi wengine wanaotaja mambo muhimu yanayotakiwa kuzingatiwa katika ushairi
ni pamoja na, Massamba (1983) anataja vina, mizani, kituo, muwala, Kibao (1983)
naye anataja, mizani, vina, urari, muwala, utoshelevu na kuwa na maana wakati
Komba (1977) anataja, mizani, vina, kituo na utoshelevu. Ama kwa hakika
tukiwachunguza wataalamu hao tutagundua kuwa, wanachosisitiza shairi lenye sifa
za ujadi linatakiwa kuzingatia vipengele vifuatavyo, Mizani, vina, kituo na
kujitosheleza.
Kwa upande wao, wanausasa wanaona shairi
si lazima lifuate urari wa vina na mizani, Mathalani, Mulokozi na Kahigi
(1982;25) wanasema ushairi ni sanaaa inayopambanuliwa kwa mpangilio maalum wa
maneno fasaha na yenye muwala kwa lugha ya mkato, picha, sitiari au ishara
katika usemi maandishi au mahadhi ya nyimbo, ili kuleta wazo au mawazo, kufunza
au kueleza tukio au hisi fulani kuhusu maisha au mazingira ya binadamu kwa njia
inayogusa moyo. Kwa maoni yao wanausasa wanaona kuwa shairi ni sanaa yenye
mpangilio mzuri wa maneno, lugha ya mkato na matumizi mengine ya lugha ili
kutoa mawazo wao hawasisitizi juu ya kuzingatia urari wa vina na mizani kama
wafanyavyo wanajadi.
Mahenge inatupa mwanga kuhusiana na maana ya Hip
Hop ambayo kwa kiasi kikubwa tunakubaliana nayo lakini dai la kusema usimuliaji
au usemaji unapangwa kivina kwa kufuata mdundo wa ala za muziki ambao
ulisharekediwa si sahihi kwani sasa hivi wasanii wengi wa Hip Hop wanaimba juu
ya midundo ya muziki ambayo haijarekodiwa vyombo vya muziki vinapigwa sambamba
na wao wakiimba na wakati mwingine hurap kwa mtindo unaojulikana kama mitindo
huru yaani kutoa mashairi ya papo kwa papo kwa kufuata midundo ya muziki
inayopigwa au bila kuwepo kwa midundo ya miziki yaani akapela.