FONETIKI AU UTAMKWAJI WA SAUTI-FONIMU ZA KISWAHILI SANIFU


Utamkwaji wa Kiglota [h]: Wakati wa matamshi ya kiglota [h], alasogezi ya ulimi hubakia chini kiasi cha kuacha nafasi kubwa kati yake na alapahala ya burutio. Mkondo wa hewa kutoka mapafuni unapopita katika chemba ya koromeo, nyuzi sauti zilizomo katika chemba hiyo ama hurindima na ikapatikana sauti [ h ], au hazirindimi na kupatikana sauti [h]. Aidha , mkondo huu wa hewa kutoka mapafuni hupitishwa moja kwa moja katika chemba ya kinywa bila kizuizi mpaka n’nje ya kinywa. Kwa mantiki hii, nyuzi sauti zinaweza kueleweka kama alasogezi ya matamshi ya sauti [h] ya fonimu /h/.

Midomo hubakia tandazi itamkwapo sauti [h]. Na alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o[h]

(ii)    Utamkaji wa Sauti za Fonimu za Kiswahili  Ki-Sampuli
Utamkwaji wa sauti ki-sampuli unabainisha kati ya sauti-endelezi na sauti-sendelezi.Utamkaji wa sauti ki-sampuli ni ule unaosababishwa na alasogezi ya ulimi na mdomo-chini inaponyanyuka kuelekea kwenye alapahala husika. Ulimi au mdomo-chini unaponyanyuka kuelekea kwenye alapahala husika, husababisha matamshi ya sampuli za sauti zifuatazo:
           
Sauti-sendelezi-konsoni ambayo wakati wa utamkwaji wake, alasogezi husika hujikweza na kujibandika kwenye alapahala husika; ambayo kwa [p b ] ni mdomo-juu, kwa [t d] ni ufizi-juu, kwa [ɟ ] ni burutio-gumu-mbele na kwa [k g N] ni burutio-gumu- nyuma kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti. Kuzuiliwa kwa mkondo huu wa hewa ni kwa muda mfupi sana. Kwa mantiki hii utamkaji wa sauti-konsonanti-katizi hauendelezeki. Mifano ya sauti-konsonanti-katizi katika Kiswahili ni [p b  t d  ɟ k g ].

Sauti-endelezi-konsoni-madende ambayo wakati wa utamkaji wake, alasogezi ya ulimi-ncha hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya ufizi-juu, kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti. Kuzuiliwa kwa mkondo huu wa hewa ni kwa muda mfupi sana. Kwa mantiki hii, alasogezi ya ulimi-ncha huonekana ikiyumbishwa kana kwamba inajigongagonga kwenye matuta ya alapahala ya ufizi-juu. Aidha, utamkaji wa sauti hii huwa katizi unaoendelezeka kwa vigongo, yaani, kimadende.

Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o. Mfano wa sauti-konsonanti-madende-endelezi ni [r].

Sauti-Endelezi-Konsoni-Kwama Kwamizi ambayo wakati wa utamkwaji wake, alasogezi husika hujikweza na kuunda mpenyo mwembamba sana kwenye alapahala husika, kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao kwenye           chemba ya koromeo hupita, lakini kwa hukwamizwa kwamizwa, unapoelekea n’nje ya Bomba la Sauti. Matokeo yake ni matamshi ya sauti-konsonanti-endelezi kwama kwamizi, kama vile: [f  θ ð s ʃ [Ɣ] h] 

Sauti-endelezi-konsonanti-tambazi ambayo wakati wa utamkaji wake, alasogezi ya ulimi-ncha hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya ufizi-juu, kiasi kwamba sehemu ya mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo haupati nafasi hapo kwenye alapahala ya ufizi-juu ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti, na sehemu iliyobakia ya mkondo huo wa hewa huchepukia pembezoni mwa ulimi na hatimaye kuelekea n’nje ya bomba la sauti.       

Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua.

Kwa mantiki hiyo, hisia za n’nje zinazosikika ni za aina ya sauti-endelezi sing’ong’o ambapo hewa yake inatambaa.  Mfano wa hii sauti-konsonanti-tambazi ni [l].
           
3.2.6   Utamkwaji wa Sauti za Fonimu za Kiswahili Ki-Ughuna

3.2.6.1  Utangulizi
Utamkwaji wa sauti ki-ughuna unabainisha kati ya sauti-ghuna ambayo husababisha nyuzi za sauti/glota zilizomo kwenye chemba ya koromeo zitetemeke, yaani hisia ya kwenye chemba ya koromeo [KO] huwa ya mawimbi-mawimbi, yaani:

 [KO:  ], na  sauti-sighuna ambayo haisababishi nyuzi za sauti/glota zilizomo kwenye chemba ya koromeo zitetemeke, na kwa hivyo, hisia inayojitokeza si ya mawimbi-mawimbi,  yaani: [KO:___________]. Aidha, hisia za sauti-sighuna  hazijitokezi kwenye Chemba ya Pua [PU:____________], wala kwenye chemba ya kinywa [KI:__________] wala kwenye Hisi N’nje [NJE:________]. Tazama kwa mintarafu ya Kielelezo 3.19. 

Kielelezo 3.19:  Utamkwaji Wa Sauti-Ghuna Na Sauti-Sighuna, Kwa Mfano,  Katika  Neno “Sasa” Kwenye Mingogramu (Mingo)
Ufasili wa Mingo hii ya Neno “Sasa”:

(a)    Sauti [s]:
(i)     ni sauti sighuna kwa kuwa nyuzi sauti/glota hazioneshi ishara ya kutetemeka/mawimbi-mawimbi kwenye msitari wa chemba ya koromeo, yaani: [KO:  ___________]

(ii)    ni sauti sing’ong’o kwa kuwa nyuzi sauti/glota hazioneshi ishara ya kutetemeka/mawimbi-mawimbi kwenye msitari wa chemba ya pua, yaani: [PU:_______].

(b)    Sauti [a]:
ni sauti ghuna kwa kuwa nyuzi sauti/glota zinaonesha ishara ya kutetemeka/mawimbi- mawimbi kwenye msitari wa chemba ya koromeo, yaani: [KO: ]

Utamkwaji wa sauti-ghuna-sing’ong’o-endelezi za Kiswahili sanifu: Katika Kiswahili sanifu, sauti-ghuna-sing’ong’o-endelezi zinazojitokeza ni [a], [e],   [i], [o], [u], [v], [ð], [z], [r], [l], [j], [Ɣ]. Sauti-ghuna hizi ndizo zinazosababisha nyuzi za sauti/glota zilizomo kwenye chemba ya koromeo zitetemeke, yaani hisia ya kwenye Chemba ya Koromeo [KO] huwa ya mawimbi-mawimbi, yaani:  [KO: ].

Kumbuka kwamba wakati wa utamkwaji wa sauti-ghuna,  alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka, kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua wakati wa utamkwaji wa sauti-ghuna-sing’ong’o-endelezi.

 (iv)     Utamkwaji wa Sauti za Fonimu za Kiswahili Ki-Ung’ong’o
Hewa hiyo inayotoka mapafuni, ikipitia chemba ya pua tu au chemba ya pua na chemba ya midomo, basi hisia za sauti itakayotamkwa zitakuwa za sauti-ng’ong’o. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejishusha kutoka kwenye ukuta wa marakaraka (paroi pharangale) ili hewa hiyo ipate kupita na kutoka n’nje ya bomba la sauti.

Utamkwaji wa Sauti-Konsoni-Ghuna-Ng’ong’o-Endelezi  [m]: Wakati wa matamshi ya sauti ya midomoni [m], alasogezi ya mdomo-chini hujikweza na kujibandika ndii... kwenye alapahala ya mdomo-juu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao mapafuni haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo. Lakini wakati huo, alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka  na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua; sauti-ghuna-ng’ong’o-endelezi [m] hudhihirishwa na ikadhihirika.


Utamkwaji wa Sauti-Konsoni-Ghuna-Ng’ong’o-Endelezi  [n]: Alasogezi ya ulimi-ncha  na alapahala ya ufizi-juu ndizo ala zinazotumika wakati wa matamshi ya kiulimincha-ufizijuu [n] ambayo ni sauti-konsoni-ghuna-ng’ong’o-endelezi.

Wakati wa matamshi ya sauti ya kiulimincha-ufizijuu [n], alasogezi ya ulimi-ncha hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya ufizi-juu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao mapafuni haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo. Lakini wakati huo huo, alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka  na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua; sauti-ghuna-ng’ong’o-endelezi [n] hudhihirishwa na ikadhihirika.

Utamkwaji wa Sauti-Konsoni-Ghuna-Ng’ong’o-Endelezi  [ɲ]: Alasogezi ya ulimi-kati  na alapahala ya burutio-gumu(kaakaa-gumu) ndizo ala zinazotumika wakati wa matamshi ya kiulimi-kati [ɲ] ambayo ni sauti-konsoni-ghuna-ng’ong’o-endelezi.

Wakati wa matamshi ya sauti ya kiulimi-kati [ɲ], alasogezi ya ulimi-kati hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya  burutio-gumu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao mapafuni haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo. Lakini wakati huo huo, alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka  na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua; sauti-ghuna-ng’ong’o-endelezi [ɲ], hudhihirishwa na ikadhihirika.


Utamkwaji wa Sauti-Konsoni-Ghuna-Ng’ong’o-Endelezi [ŋ]: Alasogezi ya ulimi-kati  na alapahala ya burutio-laini(kaakaa-laini) ndizo ala zinazotumika wakati wa matamshi ya kiulimi-kati [ŋ] ambayo ni sauti-konsoni-ghuna-ng’ong’o-endelezi.

Wakati wa matamshi ya sauti ya kiulimi-kati [ŋ], alasogezi ya ulimi-kati hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya  burutio-gumu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao mapafuni haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo. Lakini wakati huo huo, alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka  na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua; sauti-ghuna-ng’ong’o-endelezi [ŋ], hudhihirishwa na ikadhihirika.

Katika mfumo wa sauti-irabu za Kiswahili Sanifu [a e i o u ], tunagundua kwamba apana sauti-irabu-ng’ong’o hata moja baina yao, zote ni sauti-irabu-sing’ong’o. Lakini katika mazungumzo ya kimtindo, aghalabu hizi sauti-irabu-sing’ong’o huweza kung’ong’oishwa na msikilizaji akapata hisia ya sauti-irabu-ng’ong’o, kama hivi: [a e i o u ], yaani wakati wa utamkwaji wa kila irabu kivyake, hewa itokayo mapafuni lazima itoke n’nje sambamba kwa kupitia chemba ya midomo na tundu za pua, kama Kielelezo 3.25 kinavyoushereheshea.

Hewa hiyo inayotoka mapafuni, ikipitia chemba ya pua tu au chemba ya pua na chemba ya midomo bila kusitishwa, basi hisia za sauti itakayotamkwa zitakuwa za sauti-ng’ong’o-endelezi [a], [e], [o], [m], [ŋ], nk., yaani, sauti za ming’ung’uto. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejishusha kutoka kwenye ukuta wa marakaraka (paroi pharangale) ili hewa hiyo ipate kupita na kutoka nje ya bomba la sauti, bila kusitishwa!

                       

(v)    Utamkwaji wa Sauti za Fonimu za Kiswahili Ki-Mang’ong’o


Utamkwaji wa Mang’ong’o ya Kiswahili Sanifu  [mb] au [], [nd] au [], [nj] au [], [ng]  au [] 

Utamkwaji wa sauti za fonimu za Kiswahili ki-mang’ong’o, ni utamkwaji wa sauti-fonimu-mang’ong’o  [mb] au [], [nd] au [], [nj] au [], [ng]  au [].  Huu ni utamkwaji wa sauti-ng’ong’o-sendelezi, yaani utamkwaji wa MANG’ONG’O kama kielelezo3.26 kinavyotushereheshea:

Kila sauti-fonimu-mang’ong’o ni sauti-ghuna, ughuna ambao hujidhihirisha kwenye msitari wa chemba ya koromeo [KO:  ] na hususani kwenye msitari wa chemba ya pua [PU:  ] kama ilivyo katika utamkaji wa sauti-fonimu-ng’ong’o za kawaida [m n ɲ ŋ],

Kivyake, kila sauti-fonimu-mang’ong’o hutamkwa kama ifuatavyo:

(a)       Utamkwaji wa Sauti-Ng’ong’o-Sendelezi [mb] au [] 

Utamkaji wa sauti-ng’ong’o-sendelezi [mb] au []   hudhihirishwa katika hatua zifuatazo:
             
·        alasogezi ya mdomo-chini inapojikweza na kujibandika kwenye alapahala ya  mdomo-juu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo haupati nafasi ya kutoka n’nje ya Bomba la Sauti. Wakati kitendo cha hapo juu kinatendeka, kitendo kifuatacho hufanyika:

·        alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka  na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua.

·        mrindimo-ng’ong’o unapoanza kujidhihirisha kwenye nyufa za chemba ya pua, alasogezi ya mdomo-chini hujibandua kutoka kwenye alapahala ya mdomo-juu na alasogezi ya kidaka-tonge hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka; vitendo vyote hivi vitatu hutendeka wakati mmoja.  

(b)       Utamkwaji wa Sauti-Ng’ong’o-Sendelezi [nd] au []
Utamkaji wa sauti-ng’ong’o-sendelezi [nd]  hudhihirishwa katika hatua zifuatazo:
·        alasogezi ya ulimi-ncha inapojikweza na kujibandika ndii kwnye alapahala ya  ufizi-juu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo haupati nafasi ya kutoka n’nje ya Bomba la Sauti. Wakati kitendo cha hapo juu kinatendeka, kitendo kifuatacho hufanyika:

·        alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka  na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua.
·        mrindimo-ng’ong’o unapoanza kujidhihirisha kwenye nyufa za chemba ya pua, alasogezi ya ulimi-ncha hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ufizi-juu na alasogezi ya kidaka-tonge hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka; vitendo vyote hivi vitatu hutendeka wakati mmoja. 
           
 (c)      Utamkwaji wa Sauti-Ng’ong’o-Sendelezi  [nj] au []
Utamkaji wa sauti-ng’ong’o-sendelezi [nj] hudhihirishwa katika hatua zifuatazo:

·        alasogezi ya ulimi-kati inapojikweza na kujibandika kwenye alapahala ya burutiogumu-mbele kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo haupati nafasi ya kutoka n’nje ya bomba la sauti. Wakati kitendo cha hapo juu kinatendeka, kitendo kifuatacho hufanyika:

·        alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka  na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua.

·        mrindimo-ng’ong’o unapoanza kujidhihirisha kwenye nyufa za chemba ya pua, alasogezi ya ulimi-kati hujibandua kutoka kwenye alapahala ya burutiogumu-mbele na alasogezi ya kidaka-tonge hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka; vitendo vyote hivi vitatu hutendeka wakati mmoja.        
           
(d)       Utamkwaji wa Sauti-Ng’ong’o-Sendelezi , [ng]  au []
Utamkaji wa sauti-ng’ong’o-sendelezi []  hudhihirishwa katika hatua zifuatazo:

·        alasogezi ya ulimi-nyuma inapojikweza na kujibandika kwenye alapahala ya burutiogumu-nyuma kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo haupati nafasi ya kutoka n’nje ya bomba la sauti, (angalia Kielelezo 3.27). Wakati kitendo cha hapo juu kinatendeka, kitendo kifuatacho hufanyika:

·        alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka  na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua.

·        mrindimo-ng’ong’o unapoanza kujidhihirisha kwenye nyufa za chemba ya pua, alasogezi ya ulimi-nyuma hujibandua kutoka kwenye alapahala ya burutiogumu-nyuma na alasogezi ya kidaka-tonge hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka; vitendo vyote hivi vitatu hutendeka wakati mmoja.        


Jedwali 3.7 (a): Mfumo wa Matamshi ya Konsoni za Kiswahili Sanifu

Alasogezi
Alapahala
Alasogezi-Pahala
Kitamkwa/Sauti
Mdomo-chini
mdomo-juu
Midomo
[p], [], [b], [m], [w]
Mdomo-chini
meno-juu
mdomochini-menojuu
[f], [v]
Ulimi-ncha
meno-juu
ulimincha-menojuu
[θ], [ð]
Ulimi-ncha
Fizi-juu
ulimincha- fizijuu
[t], [], [d], [n], [s], [z], [r], [l]
Ulimi-kati
Burutio-gumu(kaakaa-gumu)
ulimikati-burutiogumu
[c], [], ɟ], [ɲ], [ʃ], [j].
Ulimi-nyuma
Burutio-laini(kaakaa-laini)
uliminyuma- burutiolaini
[k], [], [g], [ŋ], [Ɣ], [w]
nyuzi-sauti (nyuzi-glota)
Glota
Glota
[h].



3.2.7   Uhusiano Baina ya Fonetiki na Fonolojia
Sauti-fonimu-irabu na konsoni zilivyojipanga katika mfumo wa kifonetiki/matamshi ambao unasababisha kuwako tofauti ya maana katika jozi milinganuo finyu za lugha ya Kiswahili ndio unaotuonesha uhusiano baina ya fonetiki na fonolojia.

Upo uhusiano wa karibu sana kati ya taaluma ya fonetiki na taaluma ya fonolojia. Sifa-bainifu za kifonolojia asili yake iko kwenye sifa-bainifu za kifonetiki. Kwa mfano, (a) sauti [p] inatofautiana na sauti [b] kwa sifa ya kifonetiki ya u-ghuna; kwamba [p] ni [ - ghuna]wakati sauti [b] ni [+ ghuna]; (b) sauti [b] inatofautiana na sauti [k] kwa sifa mbili za kifonetiki: (i) sifa ya ki-ghuna, kwamba sauti [k] ni [ - ghuna] wakati sauti [b] ni [+ ghuna]; (ii)  sifa ya ki-alasogezipahala, kwamba sauti [b] ni ki-midomo wakati sauti [k] ni ki-uliminyuma-burutiolaini.


Sifa hizi za kifonetiki/matamshi ndizo zinasababisha maana ya neno ibadilike, kwani badala ya neno kutamkwa [paka] linatamkwa [baka]; au [bata] linatamkwa [kata]; nk.

Kwa mantiki hii, sifa-bainifu za kifonetiki ndizo zinazosababisha kuwako kwa sifa-bainifu za kifonolojia. Na tunazibaini fonimu (ambacho ndicho kipashio cha fonolojia) kwazo. Kwa mfano:  
(a)       pata ~ peta ~ pita ~ pota ~ puta;
Kwa mbinu ya nitoe-nikutoe (commutation), tunadiriki kudai kwamba sauti [a], [e], [i], [o], na [u] ni fonimu /a/, /e/, /i/, /o/, /u/ katika Kiswahili.

(b)       yeye ~ wewe;  yote ~ wote
Kwa mbinu ya nitowe-nikutowe, tunadiriki kudai kwamba sauti nusu-irabu [j] na [w] ni fonimu /j/ na /w/ katika             Kiswahili.
           
(c)       pawa ~ bawa ~ tawa ~ dawa ~ chawa ~ jawa ~ kawa ~ gawa.
Kwa mbinu ya nitoe-nikutoe, tunadiriki kudai kwamba sauti sauti  [p], [b], [t], [d], [c], [ɟ], [k], [g] ni fonimu /p/, /b/, /t/, /d/, /c/, /ɟ/, /k/, /g/ katika Kiswahili.

Hii ndiyo mbinu kongwe ya kiisimu ambayo inatumiwa na wanaisimu katika utafiti wa fonimu za lugha yo yote ya binadamu. Na ndiyo mbinu iliyotumiwa kuzigundua fonimu za lugha, kama vile fonimu za Kiingereza, Kifaransa, Kiswahili, nk. ambazo tunajifunza katika vyuo vyetu. 



MAREJELEO



Maganga (1997), OSW 102: Historia ya Kiswahili. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Masebo, J. A. Nyengwine, N. (2002), Nadharia ya Lugha ya Kiswahili, Kidato cha 5 na 6. Aroplus Industries Ltd: Dar es Salaam.
Nkwera, Fr. F. V. (2003), Sarufi, Fasihi na Uandishi wa Vitabu, Sekondari na Vyuo. Creative Prints Ltd: Dar es Salaam.
Powered by Blogger.