SURA YA TATU - Mikondo ya Riwaya ya Kiswahili
Charles Larson katika The Emergence of African Fiction (1972:280-1) anasema kuwa uainishaji wa kazi za sanaa aghalabu ni mchezo ulio na hatari zake. Uzoefu mbalimbali katika suala hili umedhihirisha kwamba kila mwandishi ana upekee wake na uzoefu wake. Pale ambapo uzoefu huo umeelekezwa kwenye hadithi ya kubuni matokeo yake yamekuwa ni mengi mno, yenye kufanana kwa upande mmoja na kuachana kwa upande mwingine.
Uainishaji na maelezo ya jumla katika sura hii ni matokeo ya hali halisi ya maendeleo ya uandishi wa riwaya ya Kiswahili; zoezi kama hili haliwezi kutokuwa na matatizo yake, tatizo kubwa zaidi likiwa ni lile la welekeobinafsi kwa upande wa mhakiki.
Juu ya maendeleo ya riwaya ya Kiafrika (hali hii inaihusu riwaya ya Kiswahili pia) Larson anadai kuwa kumekuwa na hali ya riwaya hii kujitoa kutoka kwenye umbo la kifasihi-simulizi na kuelekea kwenye riwaya ya majaribio inayochukua sura ya ile ya kimagharibi. Ndiyo maana, anasema Larson, ni vigumu hata kutabiri ni umbo gani ambalo hadithi ya kubuni ya Kiafrika itakuwa nalo baadaye. Wazo la Larson juu ya maendeleo ya riwaya ya Kiafrika (ya Kiswahili ikiwemo) kutoka kwenye sura ya kifasihi-simulizi na kuelekea kwenye ile ya kimagharibi linaweza kukubalika, isipokuwa hapana budi kuongezewa hoja kuwa mwelekeo wa riwaya ya Kiafrika kuchukua sura ya 'Kimagharibi' si mwelekeo wa riwaya tu, bali wa mazingira mazima ambamo riwaya hiyo inajikuta. Riwaya hiyo inajikuta inalazimishwa na hali halisi kuchukua sura hiyo. Aidha badala ya kusema inachukua sura ya Kimagharibi, ingefaa zaidi kuiita ni sura ya riwaya ya kisasa ya nchi zilizoendelea, ziwe za magharibi au mashariki, kwani zote mbili zimekuwa na athari juu ya kuibuka na kuendelea kwa riwaya ya nchi zinazoendelea. Tena si mwelekeo unaochukuliwa kwa mara ya kwanza na riwaya ya Kiafrika; riwaya za nchi zilizoendelea ziliipitia historia hiyo, ijapokuwa kwa namna ambayo mazingira yake yalielekeza. Ni mwelekeo huu ndio umesababisha kupanuka kwa riwaya na kuyaruhusu majaribio ya uainishaji.
Kasper na Wuckel (1982:157), wahakiki wa Kijerumani, wakilijadili suala la uanishaji, wanaandika kuwa usawiri wa maisha kwa kutumia sanaa ya fasihi umekuwa katika namna nyingi mno ambazo zinajibainisha katika kazi mbalimbali za kisanaa. Wanasisitiza vilevile kuwa kila kazi ya sanaa ina upekee wa kifani na kimaudhui - kwa kiasi fulani, ambao unaitofautisha kazi moja na nyingine. Lakini vilevile kila kazi ina kaida fulani za kipekee ambazo, kwa kiasi kidogo au kikubwa, zinafanya kazi moja ifanane na kazi nyingine za sanaa.
Kutofanana kwa kazi za sanaa (yaani upekee), na kufanana kwao (yaani kuwa na kaida za pamoja), kunawafanya wataalam wa fasihi waweze kuziainisha kazi za kifasihi katika makundi na aina mbalimbali. Katika nadharia ya fasihi kuna njia kadhaa za kuzigawa kazi za fasihi katika aina mbalimbali, k.m. kwa kufuata fani, mtindo, muundo, maudhui, nyakati za kihistoria, makundi ya wasomaji, n.k.
Kwa kuzichunguza kazi za kifasihi za watu wa zamani ambao kiwango chao cha maendeleo ya kijamii kilikuwa bado chini, inajibainisha wazi kuwa ijapokuwa kulikuwa na vikwazo kadhaa vilivyozitenganishajamii mbalimbali, kama vile umbali pamoja na tofauti zao za kitamaduni na kijamii, bado kulikuwa na mengi yanayofanana katika kuyasawiri matukio katika maisha yao kwa kutumia lugha. Mambo hayo mengi yanaweza kugawika katika mwainisho wa pili wa msmgi wa fasihi* ambao una makundi makubwa matatu ya kifasihi: 1) kundi la usawiri wa maisha kwa kutumia wizani, yaani mpangilio maalum wa maneno unaofuata mapigo, mara nyingine ukisindikizwa na ala maalum. Kundi hili ndilo linalobeba nyimbo, mashairi (na muziki), ijapokuwa hata riwaya na tamthiliya vinaweza kuwa na wizani pia. Hata hivyo si kawaida. 2) Kundi la pili ni lile linalosawiri maisha kwa kutumia mbinu kadhaa za mwigo. Kundi hili ndilo linalobeba sanaa za maonyesho. 3) Kundi la tatu ni lile linaloyasawiri maisha kwa kutumia masimulizi ya mjazo, yakiaridhia matukio ya kweli na ya kubuni, nalo ndilo linalobeba masimulizi ya nathari, yaani hadithi fupi na ndefu za kizamani na za kisasa. Mwainisho huu wa kifasihi unajibainisha katika fasihi za jamii mbalimbali za dunia ijapokuwa katika viwango mbalimbali vya ubora wa kisanaa; mwainisho huu, hali kadhalika unaonyesha njia tatu za msingi hadi sasa za kuyasawiri maisha kwa njia ya sanaa ya maneno yaani fasihi: mashairi (nyimbo zikiwemo), tamthilia (au drama), na nathari (au epiki**).
* Mwainisho wa kwanza wa msingi wa fasihi ni ule unaoigawa fasihi katika Fasihi-Simulizi na Fasihi-andishi.** epiki katika maandishi haya ina maana ya maandishi marefu ya kubuni, hususan tenzi na riwaya ndefu.
Goethe, baada ya kuiainisha fasihi katika tanzu kumi na nane alimalizia kwa kusema “...kuna aina asilia za kweli tatu tu za sanaa ya maandishi: ya masimulizi, ya kusisimua na ile ya kutenda ... Aina hizi zinaweza kuathiri kwa pamoja au kila moja peke yake ...” (Kasper & Wuckel, uk. 159). Kwa mawazo ya Goethe, uainishaji wa kifasihi ambao unaweza kuzaa makundi mengi mno ya kifasihi, ni shughuli ya kidhahania ambayo imefumbatwa na aina hizi kuu tatu. Aidha tunaweza kuona kuwa tanzu/aina za fasihi hazijitokezi kama tanzu bali zinajitokeza kama kazi maalum za fasihi (shairi, riwaya, tamthilia) ambazo, kama ilivyogusiwa hapo awali, zinaathiriana kwa namna moja au nyingine na kuathiri kwa kulingana au kwa kuachana.
Je, kwa nini tuainishe kazi za fasihi? Jibu rahisi ni kuwa tunafanya hivyo ili kuzielewa kazi hizo vizuri zaidi na kujua dhima zao katika jamii zenye kazi hizo. Tunasaidiwa kujibu maswali kama vile: Kwa nini jamii zilibuni mashairi, masimulizi na drama? Kwa nini katika nyakati maalum za kihistoria hujitokeza aina maalum ya fasihi? n.k.
Kabla hatujaingilia kuigawa riwaya ya Kiswahili katika mikondo, inafaa tuitazame riwaya hii katika hali halisi inamojikuta katika miaka ya sabini. Mulokozi (1976) anaielezea vizuri na kwa kifupi hali ya maendeleo ya fasihi kwajumla, ikiwemo riwaya, katika miaka ya sabini. Anaonyeshajinsi mitindo ya kifasihi-simulizi ilivyojikuta ikiendelea kutumiwa katika uandishi wa hadithi ndefu (riwaya), mathalani matumizi ya misemo, majini, mazimwi, n.k. Pamoja na kwamba fasihi ya Kiswahili ya miaka ya sabini ilijitokeza kwa nguvu na mwelekeo wa kisoshalisti kutokana na kuibuka kwa Azimio la Arusha (1967), Mulokozi anadhani kuwa riwaya, ikilinganishwa na tanzu nyingine haikuonyesha maendeleo makubwa ya kupevuka. Hata hivyo anagusia kuwa waandishi wa Ubeberu Utashindwa (1971), Kichwamaji, (1974), Dunia Uwanja wa Fujo, (1974) ni waandishi wa riwaya waliojitokeza zaidi wakijitofautisha na waandishi wengine ambao kazi zao zilikuwa zimejikita katikajadi za akina Hadley Chase na Ian Flemming. Anamwelezea Kezilahabi kama ni mwandishi aliyejitokeza na mtindo (kama tutakavyoona hapo baadaye) wenye athari za akina Thomas Mann na Albert Camus wanaoangukia katika kundi la kidhanaishi, yaani kundi la waandishi ambalo linatumia nafsi kama kigezo cha kuyapima malimwengu badala ya kuyatumia malimwengu kama kigezo cha kuipima nafsi. Ijapokuwa Mulokozi anaonyesha kuwa riwaya ya Kiswahili imejitanua kidogo tu lakini anagusia jambo muhimu kwamba riwaya hiyo inaonyesha athari za ubepari katika mahusiano ya kijamii katika dunia ya Kiswahili.
Ohly katika Aggressive Prose (1981) akiandikajuu ya maendeleo ya maandishi ya nathari katika Kiswahili na msisitizo wake ukiwa ni juu ya riwaya, anakiri kwamba riwaya ya Kiswahili ya miaka ya sabini imefikia mahali ambapo haiwezi tena ikatengwa na riwaya zingine za ulimwenguni. Hata hivyo katika mjadala wake ambao unaongozwa na hadithi au riwaya alizochagua kuzishughulikia, anajaribu kuonyesha jinsi ambavyo riwaya ya Kiswahili haijapevuka bado. Hadithi anazozipitia ambazo ni 42 anaziweka katika mikondo mitatu: mkondo wa tabaka la kati la chini, mkondo wa tabaka la kati (au wa kisomi) na mkondo wa kishamba (au kikulima). Kisha anaziainisha katika mafungu yafuatayo: 1. riwaya ya upelelezi (ya uhalifu, ya kusisimua/vituko), 2. riwaya ya mazingira, 3. riwaya ya tabia na mazingira, 4. riwaya ya vita vya msituni. Pamoja na kuwa hii inaweza kuwa ni namna mojawapo ya kuitazama riwaya ya Kiswahili ya kipindi hicho kilichotajwa, lakini uteuzi wa vitabu vilivyojadiliwa, upana wa mikondo hiyo mitatu vilimowekwa na hata ufinyu wa mawazo juu ya vitabu kadhaa vinavyopitiwa unampa msomaji mwanya wa kuhisi kwamba sura ya riwaya ya Kiswahili ya kipindi hicho katika Tanzania (au hata nje) ingeweza kutazamwa kwa makini na uzito zaidi. Idadi ya waandishi wa riwaya dhati iliyoshughulikiwa na Ohly ni ndogo mno; ni idadi ambayo inakisadifu kipindi cha mwanzoni mwa miaka ya sabini ambapo riwaya-dhati ilikuwa inaibuka.
Madumulla (1984; 1986; 1988) anakubaliana kwa kiasi kikubwa na wataalam hao wawili kwamba uandishi wa riwaya ya Kiswahili katika Tanzania umefikia kiwango kipya katika miaka ya sabini kutokana na kuongezeka kwa riwaya-dhati ambayo imejidhihirisha katika mikondo mbalimbali. Kwa jinsi hiyo, katika miaka ya sabini, riwaya ya Kiswahili inajikuta katika hatua mpya ya kujitambulisha kama kazi ya fasihi ya kitaifa, na hali kadhalika kama kazi ya fasihi ya kimataifa ambayo haistahili kutokupewa jicho la bezo tu, bali inayostahili kuangaliwa na kupimwa kwa vigezo vya kihakiki vya fasihi nyingine za dunia.
Ili kupata picha nzuri ya kujitokeza kwa mikondo ya riwaya ya Kiswahili itafaa tuiangalie kihistoria, tangu maandishi ya nathari ya Kiswahili yalipoanza kujijenga katika Tanzania.
Maandishi ya nathari ya Kiswahili ambayo yanasemekana kuwa ndiyo matangulizi na ambayo baadhi yake yaliandikwa kufuatana na kanuni za epiki ya Ulaya ya karne ya kumi na tisa (Ohly, 1982:5) yalijitokeza katika namna ya tawasifu, tena yalijitokeza kama masimulizi ya safari. Maandishi haya tumeyaainisha kama ni ya 'mkondo wa kitawasifu'. Mfano mzuri ni ule wa masimulizi ya Maisha ya Hamed bin Muhammed el Murjebi yaani Tippu Tip (1975) kitabu ambacho kimekusanya masimulizi ya visa vya Hamed bin Muhammed kwa kinywa chake mwenyewe juu ya shughuli zake za biashara ya pembe za ndovu, shanga, watumwa, n.k., kati ya maeneo ya Unguja na mrima (hasa Unyamwezini na Umanyemani) katika karne ya kumi na tisa. Mifano mingine ya masimulizi yanayoangukia katika mkondo huu ambayo yamekuja baadaye kidogo ni Tulivyoona na Tulivyofanya Uingereza (1934), kitabu kilichoandikwa na Kayamba na Uhuru wa Watumwa (1934), kitabu cha Mbotela.
Riwaya ya mkondo wa kitawasifu inapewa ainisho hilo kwa sababu masimulizi yake yanahusu kwa namna moja au nyingine, maisha ya waandishi wake. Kimaudhui masimulizi hayo yanamsawiri mwandishi ambaye ndiye mhusika mkuu akijihusisha na nyanja mbalimbali za maisha katika mazingira yake na wakati wake wa kihistoria. Kwa njia hiyo, msomaji anaweza kuyapitia matukio fulani muhimu ya kijamii kisiasa, kiuchumi, n.k. ambayo yalipata kutokea katika kipindi kinachosimuliwa. Mathalani, katika Tippu Tip tukio muhimu la kihistoria, kijamii na kiuchumi la kipindi chake ni biashara ya watumwa na pembe za ndovu vikibadilishwa kwa ushanga na vipande vya nguo. Kimsingi, hii inaonyesha mahusiano ya kijamii yaliyopogoka, yanayobainisha kufujwa na kudunishwa kwa thamani ya Mwafrika pamoja na maliasili yake. Pamoja na kuwa mhusika mkuu anatoa mchango mkubwa katika kuleta mahusiano ya karibu kati ya pwani na bara, na katika kuwasaidia wavumbuzi kama vile akina David Livingstone, Bwana Cameroon na Sir Henry Stanley katika njia zao, lakini vilevile anachangia vikubwa katika ufujaji na udunishaji huo, akidai kuwa anawaua 'washenzi'.
Kifani, riwaya ya mkondo wa kitawasifu inaonyesha mbinu zinazobadilika kadiri wakati unavyosonga mbele. Masimulizi ya Tippu Tipmathalani, yamekaa kiepiki tofauti na yale ya Uhuru wa Watumwa au Maisha Yangu. Tippu Tip ameyapanga masimulizi yake katika vifungu vidogo vidogo ambavyo vinaweza kulinganishwa na beti za kishairi ijapokuwa viko katika lugha ya mjazo, tena lugha isiyosanifiwa, iliyoathiriwa sana na Kiarabu. Kumbe katika Uhuru wa Watumwa ni tawasifu ambayo imebeba ubunifu wa kisanaa wa kiasi kikubwa mwandishi akitumia mchanganyiko wa ujumi wa jadi wa Kiafrika na wa kigeni unaojitokeza katika dini. Kisha dini kama kigezb cha ujumi katika kuumba maadili yatakiwayo na mbinu ya kuijenga jamii mpya inajitokeza zaidi katika Maisha Yangu.
Masimulizi ya mkondo wa kitawasifu yanaweza pia kuwekwa chini ya riwaya ya safari kwa sab.abu msukumo mkubwa wa matukio unajitokeza katika safari ya (au za) mhusika mkuu. Ijapokuwa mkondo huu wa kitawasifu (na wasifu pia) unaweza kuendelea kujitokeza katika riwaya ya Kiswahili (kwa mfano Maisha ya Salum Abdulla, 1975), lakini kilele chake kilikuwa ni wakati wa Shaaban Robert, yaani miaka ya sitini, kutokana na sababu itakayotdlewa baada ya kuupitia mkondo wa masimulizi unaofuata.
Mkondo wa masimulizi unaojitokeza baada ya ule wa kitawasifu/wasifu ni wa kitarafa. Huu unayafumbata yale masimulizi ambayo yanajibana katika mazingira madogo tu ambayo hususan huhusu jamii moja tu. Kwa kuwa masimulizi ya namna hii, aghalabu, yametokea kueleza amali za kijadi zajamii inayosimuliwa kwa marefu na mapana yamepata kujitokeza kama nyaraka kuukuu zajamii hiyo, na hivyo yakaitwa pia kama riwaya ya kinyaraka (Madumulla, (1980). Mifano mizuri ya mkondo huu ni Bwana Myombekere na Bibi Bugonoka (1980) kilichoandikwa na Kitereza katika lugha ya Kikerewe na kisha kikatafsiriwa katika Kiswahili na yeye mwenyewe mwaka 1945; Kurwa na Doto (1960), na Mzishi wa Baba ana Radhi (1971). Masimulizi haya ya mkondo wa kitarafa, kama ilivyogusiwa, ni masimulizi yanayohusu mazingira ya karibu ya wahusika wakuu, yakisimulia kwa undani mila, desturi na amali kadha za kitamaduni za sehemu zao.
Bwana Myombekere na Bibi Bugonoka ni masimulizi yahayohusu ada za kabila la Wakerewe katika vipengele mbalimbali vya maisha kabla ya majilio ya wageni, hususan Waarabu na wazungu. Watu wa nje waliohusiana nao ni makabila yale yaliyopakana nao. Hali kadhalika, Mzishi wa Baba ana radhi ni masimulizi ya ada ya Wapangwa (kabila mojawapo linaloishi katika milima ya Kipengere kandokando ya ziwa Nyasa, wilayani Ludewa) kabla ya wageni na Kurwa na Doto inasimulia juu ya ada na desturi za watu wa Unguja katika wakati ambao utamaduni wa Kiislam umeota mizizi tayari na kuwa ni sehemu ya maisha. ya watu wa pwani za Afrikaya Mashariki.
Fani iliyotumika katika maandishi ya mkondo huu inategemea (pia) wakati. Ukichukua Myombekere, ni masimulizi ambayo yamefurikwa na utajiri wa vipengele vya kifasihi-simulizi (methali, misemo, vihadithi, nyimbo katika sanaa za maonyesho n.k.). Aidha mtindo wake wa masimulizi unatii sana ujumi wa Wakerewe. Katika Mzishi ijapokuwa kuna baadhi ya vipengele hivyo, lakini kiasi fulani cha ujumi wa Kipangwa kinaathiriwa na matumizi ya Kiswahili sanifu. Matumizi ya Kiswahili sanifu katika Myombekere hayafanikiwi sana kutokana na mazingira ambayo yamemkuza mwandishi wake, yaani Kitereza. Mtindo wa kifasihi-simulizi, hususan mwanzoni na mwishbni mwa uandikaji wa Kurwa na Doto umejitokeza pia, ambapo mwandisbi ameifungua hadithi yake kwa 'hapo zamani za kale' na kuifunga au kuimalizia kwa 'wakaishi kwa raha mustarehe'.
Hata hivyo tunajikuta katika mtafaruku tunapozitazama kazi hizi za kisanaa kama ni kazi za fasihi ya Kiswahili au la; kwani ni vema na rahisi zaidi kuziona kama ni kazi za fasihizajamii na mazingira yao. Inakuwa hivyo zaidi tunapobaini kuwa ni fasihi ambazo zinaziakisi jamii zao kabla ya majilio ya wakoloni, yaani katika kipindi ambapo mawazo ya ujenzi wa fasihi ya kitaifa, sembuse ujenzi wa taifa lenyewe, viko katika ruia tu. Ni Kurwa na Doto tu ndicho kitabu ambacho kingepokelewa kama ni fasihi ya Kiswahili na akali tu ya watu ikatofcea kukanganywa kuhusu vipi suala la utamaduni wa Kiislamu lipokelewe.
Kisha mikondo hii miwili, yaani wa kitawasifu na kitarafa ina aina ya masimulizi ambayo upeo wao wa mtazamo ni finyu kwa namna fulani. Mkondo wa kitawasifu unamlazimisha msomaji ayaone matukio mengi kwa jicho na hisia za mhusika mkuu, na hivyo kuifanya kazi ikawa na sifa za shairi ambalo ni hisia za mshairi juu ya tukio. Hali kadhalika, mkondo wa kitarafa, ufinyu wake uko katika kuweka makini yake yote kwenye jamii fulani tu.
Katika miaka ya sabini mkondo huu wa kitarafa umeendelea, lakini kwa kuchukua sura nyingine kidogo. Mifano ni Mbojo: Simba - mtu(1971), Titi la Mkwe (1972) na vile vile Mirathi ya Hatari (19.77). Sura hiyo nyingine inasababishwa na mambo mawili. Kwanza, kimaudhui, masimulizi yanazidi kujibana katika mada moja na kuifuatilia hiyo kwa karibu zaidi; yameacha mtindo wa kusimulia maisha ya jamii maalum katika upana wake kama vile tunavyoona katika vitabu viwili vya kwanza. Katika vitabu hivi vitatu, mathalan, mada iliyozingatiwa zaidi ni ya ushirikina, lakini ni ushirikina unaotokea katikajamii maalum. Jambo la pili ni kwamba masimulizi haya yanaonekana yameathiriwa sana na utaifa kwa sababu, tofauti na yale masimulizi mengine mawili, haya yameandikwa baada ya uhuru, hususan katika miaka ya sabini ambapo Kiswahili kilikwishapata hadhi mpya kama lugha ya mawasiliano na kama chombo cha mawasiliano cha kitaifa. Na kwa jinsi hiyo dalili za ujumi wa kitaifa kwa njia ya ujamaa na siasa ya kujitegemea zinajitokeza, ujumi huo ukiupinga ule wa kijadi. Kutokana na athari za utaifa tunaona pia kuwa ijapokuwa waandishi wa kazi hizo za sanaa wanashughulikia mada hiyo moja katika mazingira yao, lakini kuna mawasiliano ya wazi na maeneo mengine, ya karibu na ya mbali. Katika Mbojo: Simba-mtu tunaona kuwa polisi, ambayo ni mojawapo ya nguvu za dola za kisasa zinazotumika kulinda haki na amani ya taifa inatumika kusaidia kutokomeza imani za kijadi, ijapokuwa imani hizo za kijadi zinaonyesha kuwa na nguvu nyingi. Katika Titi la Mkwe tunaona jinsi elimu ya kisasa ambayo inamwezesha Zenga kwenda hadi Ulaya kusoma zaidi, inavyokabiliana na imani za kishirikina na hivyo kufanya mandhari ya matukio yawe mapana zaidi, ijapokuwa yale ya Ulaya yametajwatajwa tu bila kuelezwa. Na katika Mirathi ya Hatari ijapokuwa chimbuko na mandhari kuu ya mada inayoshughulikiwa ni katika jamii maalum, lakini matukio yako hadi Dar es Salaam na Tanga. Suala la elimu linajitokeza na kuwa ni nguvu muhimu ya kulikomesha tatizo la ushirikina ambalo ndilo chanzo cha mikinzano katika masimulizi haya.
Kisha unajitokeza. mkondo wa kimaadili. Mkondo huu unafumbata masimulizi ambayo yanaoana sana kimuundo na kimaudhui na hadithi za kifasihi-simulizi. Kaida za riwaya ya kimaadili zimejadiliwa kwa kirefu katika sura inayofuata inayohusu uainishaji wa wahusika katika riwaya ya Kiswahili. Hata hivyo tunaweza kuongeza kuwa mkondo huu ulikuwa umeenea sana katika taasisi mbalimbali za mafunzo katika Tanzania kwa lengo la kufunza na kuadibu. Ni mkondo ambao uliondokea kuendeleza nafasi na dhima ya utanzu wa hadithi. Kwa jin'si hii mkondo huu haukutoa changamoto ya kutosha katika kufikirisha na kutafakurisha bali ulitoa mawaidha na maadili ya kufuatwa katika kuijenga jamii inayofaa; ulikanya dhidi ya mambo yasiyofaa katika maisha. Mifano mizuri ya mkondo huu ni vitabu vya Shaaban Robert, kama vile Kusadikika (1951), na Adili na Nduguze (1952) au MrinaAsali na Wenzake Wawili (1961) kilichoandikwa na Mnyampala.
Katika Kusadikika mwandishi analijadili suala la haki ya watu dhidi ya uongozi mkandamizi na wa kiimla. Utawala usio na kiasi wala mpaka ni utawala ambao hatimaye hukwamisha maendeleo ya nchi na watu wake kwa sababu huwanyima watu uhuru wa kufikiri na kuchangia katika maendeleo ya nchi yao. Kwa kutumia mbinu ya kejeli na tashtiti, misemo na nahau, mwandishi amejitahidi kulifikia lengo lake la kuonyesha hasara za kuyakwamisha maendeleo ya nchi.
Katika Adili na Nduguze, mwandishi akitumia zaidi visasili vya jadi ya Kiarabu, kama vile matunuzi ya majini, anaonya dhidi ya uchoyo na kuhimiza moyo wa wema, usamehevu na kutosheka. Hali kadhalika katika Mrina Asali, Mnyampala anataka kufunza wasomaji juu ya ujasiri na moyo wa kusaidiana, n.k. Kwa jinsi hii, kwa kutazama mifano hii mitatu ya mkondo huu tunaweza kuonajinsi ilivyo rahisi kuyaweka maudhui yake katika maneno machache.
Aidha, kama masimulizi ya mkondo fauuyangechunguzwa kwa makini yangejitokeza kuwa na
(a) mada sahili: muundo na mada sahili vikiwa na uhusiano mkubwa na hadithi ya kifasihi-simulizi (Mathalani msukumo na wahusika katika Adili na Nduguze na pia katika Mrina Asali, au msukumo na mhusika mkuu katika Mtu ni Utu)(b) Upatanifu wa kifalsafa: upatanifu wa nanma ya falsafa ya mtazamo wao wa maisha ambapo, kama itakavyojibainisha katika sura juu ya wahusika, kuna mvutano wa waziwazi kati ya uzuri na ubaya, na uzuri daima hushinda. Uzuri umesawiriwa kwa namna ambayo hauchangamani na ubaya, na hali kadhalika kmyume chake.(c) matumizi ya wahusika bapa: matumizi ya wahusika bapa, tena wenye nguvu na uwezo usio wa kawaida (kama vile mhusika Karama katika Kusadikika au Adili katika Adili na Nduguze). Uzuriauwema wa wahusika hao unakuwa ni ufunguo wa uwezo wao na hekima na busara yao. Mambo haya yameandamana na namna ya mubaalagha (au tashdidi) ambao unazitenganisha, kwa namna fulani, kazi hizi na ukweli halisi.
Mifano hii mitatu inaweza kusemwa kuwa inaelemea zaidi katika upande wa hadithi ya kifasihi-simulizi kutokana na ujumla na mtindo wa usimuliwaji wa mada zao ambao unazifanya kazi hizi zijitokeze kama ni kazi za wakati wote (rejea sura ijayo). Lakini mwishoni mwa miaka ya sitini kulikuwa na jaribio la maandishi yaliyohusiana sana na mkondo wa kimaadili, hususan katika msuko wao wa matukio na ujenzi wa wahusika, ijapokuwa kwa hakika ulikuwa ni mkondo mwingine uliokuwa unajitokeza.
Mfano bora wa maandishi haya ni Mtu ni utu (1971), Fadhili Msiri wa Naugua (1971) na pia kwa kiasi fulani, Simbayavene (1974) na Utotole (1978). Masimulizi haya, kimaudhui yanajitahidi kujisogeza katika matukio ya kihistoria ya baada ya Azimio la Arusha la 1967, ijapokuwa kifani bado yamefungwa katika silisila za ujumi wa kifasihi-simulizi kwa kutumia wahusika bapa (wakwezwa) na mambo ya ajabuajabu ambayo yanahusiana na ujasiri (wema) ukivutana, na hatimaye kuushinda, ubaya. Matumizi ya ushirikina na uchawi yanaongeza kuleta umbali kati ya kazi hizi na uhalisia. Masimulizi ya kundi hili, ambayo yanaondokea kuupata msukumo wake mkubwa katika itikadi ya kijamaa kwa njia ya Azimio la Arusha, yanaibua aina ya riwaya iliyojaa matumaini ya mabadiliko makubwa na ya haraka ya kijamii katika ujenzi wajamii mpya. Kwa namna fulani masimulizi haya yanakuwa ni kipaza sauti cha yale yanayozungumzwa katika majukwaa ya kisiasa kutangaza na kuzagaza siasa ya Ujamaa na hivyo masimulizi hayo yakawa na sifa ya ukasuku. Kazi hizo, zikishabihiana sana na mashairi ya Azimio la Arusha, zinaondokea kuusifu ujamaa na 'mapinduzi' yake uliyoyaleta kwajamii. Aidha mapinduzi yenyewe yanaongelewa juu juu tu bila kuigusia misingi ambayo ni muhimu katika kuleta mapinduzi. Mathalani katika Mtu ni Utu, mhusika mkuu, Sozi, baada ya kuupitia wakati mgumu wa utoto katika mikono ya baba yake mdogo na hatimaye kujiokoa kwa kutorokea kijiji kingine ambako anatunzwa na kusomeshwa hadi darasa la nne na ajuza mmoja, anainukia kuwa kiongozi maarufu wa nchi nzima na kuwa kitovu cha mapinduzi ya kijamii. lakini pamoja na ustawi unaojitokeza, kuna maswali mengi yanayoulizwa, hususan juu ya mantiki yanayoyazunguka mapinduzi hayo ya haraka ya kijamii, kasi yake na wepesi wake. Katika hadithi za fasihi-simulizi kasi na wepesi wa matukio vinawezekana kwa njia ya mbinu ya kiujumi ya uchawi na ushirikina.
Katika Mtu ni utu au masimulizi yanayoangukia katika kundi hilo ambayo lengo lao ni kuelezea mapinduzi ya kijamaa ya wakati wao na pia kuhamasisha wasomaji (jamii) na kuwashawishi waige mapinduzi hayo, mbinu ya kiujumi na kisanaa ya kuelezea kasi na wepesi wa ujenzi wa jamii mpya haiwezi kuwa uchawi na ushirikina, kwa sababu uchawi na ushirikina ni nyenzo muhimu za mhusika - mkwezwa, ambaye aghalabu ni mtu binafsi anayeweza kuwakabili na kuwashinda walio wengi. Kuitumia mbinu hiyo ya kiujumi wakati wa sasa ingekuwa ni kuibeza maana ya mapinduzi ya kijamaa. Kumbe mbmu inayofaa ingekuwa ni ile inayotetea uwingi dhidi ya upweke au usogora wa kibinafsi. Ndiyo maana kwa nanma fulani, kasi na wepesi wa matukio katika Mtu ni Utu ni masuala yaliyoachwa wazi.
Hali kadhalika jitihada za Mtu ni Utu au aina yake kuyajaribu maudhui mapya zinayapa masimulizi hayo sifa ya kuingia kwenye mkondo mwingine, ule wa kinjozi, ijapokuwa kutokana na fani yake, ni masimulizi yanayousadifu mkondo uliotangulia yaani ule wa kimaadili. Ni masimulizi, yanayodhihirisha mpito wa kifasihi, kifani na kimaudhui, na kutupatia picha nzuri ya hali ya mchangamano wa ukale na usasa ambao tunaweza kuuona katika historia nzima ya maendeleo ya kimpito ya riwaya, iwe ya Kiswahili au yoyote ile.
Mifano mingine ya riwaya zinazoangukia katika mkondo wa kinjozi ni Ufunguo wenye Hazina (1969), Njozi za Usiku (1973) na Ndoto ya Ndaria (1976). Riwaya zote tatu zinabainisha shauku ya ujenzi wa jamii mpya kwa njia ya Ujamaa. Kwa ufupi inaweza kusemwa kuwa ni riwaya za mikondo ya kimaadili na kinjozi zinazoonyesha bado upungufu wa namna ya kuyakabili kisanaa masuala ya mazingira yao, ijapokuwa, kwa kiasi fulani, zimeyagusia au kuyazungumzia matatizo yanayoikabili jamii yao, na hata kuifunza jamii juu ya maadili yafaayo. Na mikondo yote miwili ya kimaadili na kinjozi inaangukia katika tapo la urasimi kutokana na kufanana na hata kuingiliana kwa vipengele vyao vya kiujumi. Mapinduzi yaliyolengwa na Azimio la Arusha yalikuwa ni pamoja na kusisitiza na kuinua hadhi ya kilimo vijijini. Ndiyo maana, kimsingi mandhari makuu ya riwaya ya mkondo wa kinjozi yalikuwa vijijini. Kwajinsi hiyo katika mkondo huu wa kinjozi kuna masimulizi (ambayo baadhi yake ni ya kikasuku) ambayo yanalenga kuhubiri mafanikio ya mapinduzi ya kijamaa ambayo mandhari yake ni mashambani, hususan kwenye vijiji vya ujamaa (Ufunguo wenye Hazina, Mtu ni Utu, Njozi za Usiku, Ndoto ya Ndaria). Lakini vilevile kuna masimulizi ambayo yanaelekea kubainisha kwamba kuwako kwa miji na maadili yake yenye 'mkengeuko' kunarejesha nyuma maendeleo ya vijiji kwa sababu watu wengi kutoka vijijini, hususan vijana, wanafurika kwenda mijini ili kutafuta kazi, na hatimaye wanashindwa kuyamudu maisha ya mijini na kurejea vijijini kama wana wapotevu. Kwa jinsi hiyo masimulizi hayo yanajenga mvutano wa aina fulani na uhasama wa kimaadili kati ya kijiji na mji. Mifano mizuri ya masimulizi hayo niShida (1975), na Mjini Taabu (1977). Ijapokuwa masimulizi haya yanaonekana kupea zaidi katika msuko wa matukio yake na ujenzi wa wahusika wake kiasi kwamba kiwango cha uhalisia kinakuwa karibu zaidi na maisha ya kila siku kuliko ilivyo katika riwaya za nyuma, na vilevile kujaribu kuonyesha mgongano wa kitabaka unaowafanya wakimbizi wa vijijini wasiweze kuyamudu maisha ya mijini, lakini kuna upungufu wa wazi. Katika maendeleo ya kimapinduzi mji hauwezi kutengwa na kijiji: ni sehemu zinazokwenda pamoja kwa kusaidiana. Mapinduzi yaliyodhamiriwa na waasisi wa mapinduzi si kwa ajili ya sehemu moja tu ya nchi, bali nchi nzima. Upungufu huu katika riwaya unasababishwa na matumizi ya ujunu wa kimaadili yaliyoyatenganisha maisha katika sifa mbili zisizoingiliana, za uzuri na ubaya.
Hali kadhalika, miaka ya sabini ilishuhudia kuibuka kwa riwaya ya tapo la uhalisia wa kihakiki iliyojibainisha katika mikondo kadhaa. Kinadharia, kama itakavyojibainisha katika sura ya wahusika, riwaya ya kisaikolojia haitaz.amiwi kujitokeza katika mkondo wa kimaadili kwa sababu ujumi wake ulitoa nafasi kwenye utenzi tu wa matendo makubwa yaliyoandamana na lugha maalum (teule au ya heshima) na kuyafanya kuwa ni kielelezo cha kimaadili cha wakati wote. Ijapokuwa tayari mwishoni mwa miaka ya hamsini Abdulla alifaulu kuitoa riwaya kutoka katika fuko la lugha maalum na ya heshima na kuiweka nje katika maisha ya kila siku ya wahusika halisi, lakini alikuwa bado kuing'oa kutoka katika mkondo wa kimaadili. Rosa Mistika (1971) ni riwaya iliyoyajali masuala ya saikolojia na hisia ambazo ni mojawapo ya sifa za msingi katika kuipa kazi ya kisanaa uhalisi wake, pia ilibeba dalili za kiuhakiki zilizoonyesha kasoro za jamii na kudokeza suluhu. Majaribio ya namna ya riwaya ya Rosa Mistika yalikuwa ni mpito kuelekea riwaya ya mkondo wa kisaikolojia na mikondo mingineyo.
Riwaya ya mkondo wa Kisaikolojia ilijitokeza katika kazi za Mohammed S. Mohammed za Kiu (1972) na Nyota ya Rehema (1978), ikionyesha namna yake ya ubunifu wa kisanaa na usawiri wa mazingira. Kifani msanii ameujenga msukumo mkuu wa kazi yake kwa kutumia mhusika mkuu wa kike anayekumbwa na dhiki za kukengeukwa na jamii yake akakosa hata njia ya kujinasua kutokana na dhiki hizo, akamsabilia Muumba roho yake kwa kuhesabu kuwa yanayompata ni majaliwa yake. Kwa kuwa dhiki hizi zinatia huruma, ndizo zimekuwa kigezo cha kuiweka riwaya hii katika mkondo wa kisaikolojia. Riwaya hizi mbili ambazo msukumo wake unaelekea kushabihiana sana na ule wa 'kisonoko' katika hadithi za fasihi-simulizi ni riwaya pekee ambazo zimejitokeza zaidi katika mkondo huu mpaka katika miaka ya themanini.
Matumaini ya mapinduzi ya haraka ya kijamii yaliyotegemewa na mkondo wa kinjozi baada ya Azimio la Arusha yalianza kufifia hususan katikati ya miaka ya sabini. Kukaibuka riwaya ambayo iliuliza maswali kadhaa kuhusu kufifia huko. Lawama nyingi juu ya kulegalega kwa maendeleo ya kijamaa zilielekezwa kwa baadhi ya viongozi waliolewa madaraka na kuanza kuikiuka misingi ya Ujamaa kwa kujishirikisha na ubinafsi, uchochezi dhidi ya Ujamaa, ulapguzi na rushwa (Nyota ya Huzuni, (1981); Njozi Iliyopotea (1980); Kivuli, (1981). Masimulizi haya yanayoondokea kuzisaili dosari zinazofanywa na uongozi na zikakwamisha matumaini yaliyotarajiwa yameibua mkondo mpya kimaudhui, mkondo wa kiteti au msuto. Ni riwaya inayoteta au kusuta. Kwa kiasi kikubwa riwaya hii ni ya kisiasa kama ile ya mkondo wa kinjozi, ndiyo maana hata fani yake imejaa mazungumzo ya kisiasa yenye hotuba hapa na pale. Wakati mkondo wa kinjozi unashangilia na kushabikia majilio ya Ujamaa, mkondo wa kiteti unaanza kuwa na wasiwasi juu ya kufanikiwa kwa ujamaa ikiwa utatekelezwa kwa namna unavyotekelezwa.
Katika kipindi hicho hicho, yaani kuanzia katikati ya miaka ya sabini, tapo la uhalisia wa kihakiki lilizidi kupevuka, hususan mkondo wa kidhanaishi ulizidi kupata mashiko kutoka kwa muasisi wake, Kezilahabi, katika riwaya ya Kiswahili. Tunasema 'ulizidi kupata mashiko' kwa sababu tangu mwanzoni mwa muwongo huo wa sabini mkondo huo ulijitokeza kidogo katika riwaya ya Rosa Mistika. Mkondo huu unajitokeza kwa nguvu na wazi zaidi katika Dunia Uwanja wa Fujo (1975) ambamo msanii anajaribu kulitazama suala la maisha kifalsafa kwa karibu zaidi. Katika Rosa Mistika mhusika mkuu anaishi maisha ambayo hatimaye yanamkatisha tamaa na anajiua. Anapokuwa mbele ya Mungu, Mjua yote, ili kujibu shitaka la kujiua, anaonyesha kuwa jibu sahihi liko duniani kwa watu. Fumbo bilo huenda linafumbuliwa kwa namna fulani katika Dunia Uwanja wa Fujo kwa kuona jinsi maisha yalivyo katika mvurugano usio na upatanifu, na kwamba ndivyo maisha yanavyopaswa kueleweka, kuwa ni mchafukoge. Na katika Nagona (1988) mchafukoge huu wa maisha unafafanuliwa kuwa unaendelea katika namna ya mviringo myiringo ambao wataalam wengine wemeuita 'mviringo wa kihemetiki'*.
* Hii ni mbinu ya kisanaa ya kuifahamu na kuifafanua kazi ya kifasihi ambayo historia yake inaturudisha hadi enzi za akina Martin Luther na jmsi walivyojishughulisha kufafanua Biblia. Kwa kifupi, mbinu hii inadai kuwa maana ya kitu imo ndani ya kitu chenyewe. Kuitafuta maana ya kitu nje ya kitu ni kupotosha maana halisi ya kitu. Wafuasi wakubwa wa mbinu hii ni pamoja na akina A.G. Baumgarten, H. Schileiermacher, W. Dilthey, M. Heidegger, H.G. Gadamer, n.k.
Kwa kuutumia mviririgo huu wa kifalsafa kufafanua maisha, inasemakana kwamba maisha hujirudia kwa kujongea katika namna ya mviringo; na maana halisi ya maisha imo ndani ya fahamu za mtu. Lakini wahakiki wanaotumia uyakinifuwa kihistoria licha ya kukataa kuwa historia hujirudia, wanaona kwamba fahamu katika mtu hazitoki ndani ya mtu, bali nje ya mtu, yaani hutoka katika mazingira yanayomlea na kumkuza mtu huyo. Kwa hiyo maana halisi ya maisha, kimsingi, iko nje ya mtu, isipokuwa tu hatimaye mtu hujifunza maana hiyp, ikawa sehemu yake na yeye sehemu ya hiyo maana, kwa kutegemeana na hali halisi za wakati na mahali. Hali kadhalika, maisha si mchafukoge, bali ni matokeo ya sheria za kijamii na kiasili zinazoyamiliki, kuyadhibiti, kuyamudu, kuyakimu na kuyaelekeza. Kwa hiyo kuigeuza dunia kuwa 'uwaiya' wa fujo' ni kuukataa urazini ulio ndani ya mtu kwa kudhibitiwa na maziHgira ambayo humpa mtu uwezo wa kuyapanga maisha yakawa pepo ya watu wote.
Mwanzoni mwa miaka ya themanini fasihi ya Kiswahili iliyashuhudia majilio ya masimulizi ya aina yake ya tapo la uhalisia wa kihakiki yenye mwelekeo mkubwa wa kisoshalisti ambayo kimaudhui yaliyazidi masimulizi yaliyopita ya kifasihi, hususan riwaya ya kisiasa katika ukomavu wake. Mfano mzuri wa masimulizi haya ni Dunia Mti Mkavu (1980). Hata hivyo, juhudi za mwanzo za kuibuka kwa mkondo huu zilijionyesha tayari katika Ubeberu Utashindwa na baadaye kidogo Mzalendo (1977), Kabwela (1978) na Kuli (1979). Jambo linalojibainisha katika aina hii ya riwaya ni mkabala wake wa kisayansi na kiutu katika masuala ya kijamii pamoja na ufahamu wake mpana wa sheria zinazodhibiti maisha na maendeleo ya jamii. Wakati riwaya za aina nyingine zilizotajwa hadi sasa zimegusia tu au zimeshindwa kabisa kuonyesha kuwepo kwa matabaka na migongano baina yao, aina hii ya riwaya imeonyesha wazi matatizo hayo. Kisha aina za riwaya zilizotajwa nyuma zimewachora wahusika wao kwa kutumia misingi ya zamani, yaani ya kuwapatia majukumu muhimu ya kijamii wale wahusika walio na nafasi bora tu katika jamii. Lakini aina hii imeleta mapinduzi katika uchoraji wa wahusika kama tutakavyoona katika sura juu ya wahusika. Ndiyo maana aina hii ya riwaya imeitwa ya mkondo wa kimapinduzi, nayo imeguswa sana na mawazo ya Ki-Marx ambayo yameingia kwa nguvu sana katika maisha ya Mwafrika katika miaka ya sabini. Suala la ukombozi wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni dhidi ya ukoloni mkongwe na ukoloni mamboleo lilipata sura mpya na kuingia katika hatua mpya.
Pamoja na ukomavu wa riwaya ya mkondo wa kimapinduzi, kimaudhui, tatizo la wazi ambalo linaweza kuonekana hapa katika upande wa fani ni lile la matumizi ya hotuba na michuuko ya kisiasa, mambo ambayo hatimaye yanachosha na kuonyesha ushindani hafifu wa kisanaa. Hata hivyo kuna waandishi kama vile Mohammed katika Dunia Mti Mkavu na A. Saffari katika Kabwela ambao mmoja anatumia sana mifano ya kufikirisha ya kifasihi katika masimulizi yake ambayo inavipamba vihotuba vya wazungumzaji na kuufuta ule ukavu wa hotuba za kisiasa (Dunia) na undani wa wahusika wake katika maisha yao ya kila siku na kubainisha dhiki zao na jinsi wanavyonyanyaswa na kunyonywa na wakubwa wao wa kazi (Kabwela). Hivyo hotuba za kisiasa hazipewi nafasi kubwa.
Hatimaye katika miaka ya themanmi riwaya ya taharuki ambayo tunapenda kuiita riwaya-pendwa imeelekea kusitawi zaidi. Ni ile aina ya liwaya ambayo ililetwa kwa nguvu kwa mara ya kwanza katika fasihi ya Kiswahili na Abdulla mwishoni mwa miaka ya hamsini (rej. Mzimu wa Watu wa Kale: 1958), akaungwa mkono na Katalambulla (rej. Simu ya Kifo,: (1965) katika miaka ya sitini na baadaye, hususan mwishoni mwa miaka ya sabini na katika miaka ya themanini waandishi wakaongezeka sana. Kwa nini? Ili kulipata jibu inafaa turejee kwenye makala ya Madumulla (1988) na kuyadondoa kwa kirefu:
Pamoja na vilele kadhaa vya matukio ya kijamii na kisiasa ambavyo vimejitokeza katika miaka ya sabini, kilele kilichoathiri zaidi ni kile kilicholetwa na mabadiliko ya haraka ya kiuchumi kuelekea mwishoni mwa muwongo huo, na hasa baada ya bei ya mafuta na vyombo vya mashine kuongezeka... Kwa sababu hizi na nyinginezo, muwongo wa themanini ulijikuta ukitoswa huko na huko katika bahari ya kiuchumi iliyochafuka. Viwanda vilisibiwa na uhaba wa malighafi (pembejeo) pamoja na matatizo mengine kama vile uzembe, uvivu na hujuma. Mambo haya yalileta uzorotaji katika uzalishaji mali viwandani. Bidhaa zinazozalishwa ikiwa haziendani na kiasi cha matakwa, huzuka tatizo la kuzigawa. Hapo ndipo watu wachache wenye uwezo wa kuzidhibiti mali hizo chache zinazozalishwa huitumia silaha na kinga ya 'uhaba' kuchuma na kujinufaisha wenywe. Uhaba unapozagaa kila mahali, hapo ndipo rushwa, biashara za magendo, ulanguzi, upikaji wa pombe haramu, wizi wa nguvu na wizi wa kalamu, umalaya, ulevi wa aina mbalimbali, kushuka kwa thamani ya fedha, kubomoka kwa udugu na kusitawi kwa ubepari na matatizo mengine huzuka... Picha hii imejionyesha katika Tanzania tangu mwishoni mwa miaka ya sabini na kuendelea katika miaka ya themanini. Fasihi ya Kiswahili, ikiwemo riwaya, imejionyesha wazi jinsi ilivyoathiriwa na matukio haya ya kiuchumi. Kwa upande wa riwaya, waandishi wengi waliojitokeza ni wale waliofanya hivyo ili kujikwamua kiuchumi. Waandishi hawa waliuvamia uga wa fasihi-pendwa, wakashughulika na mada za mapenzi na uhalifu katika dunia ya kisasa, dunia iliyokumbwa na masaibu ambayo, kwa kawaida, yako kwa wingi katika nchi zilizoendelea, na hasa zile zenye migongano mikali ya kitabaka. Ndiyo maana baadhi ya wahakiki wamesema kwa usahihi kuwa mengi ya maandishi haya ni mwigo au mwendelezo wa maandishi ya kimagharibi. Kazi hizi zimejitokeza kwa wingi katika kipindi hiki wala si kwa lengo la awali la kuziba pengo la upungufu wa maandishi ya fasihi ya Kiswahili, bali tunadhani kwa lengo la awali la mwandishi kupigana na hali ngumu ya kiuchumi ya kipindi hild...
Riwaya-pendwa imeondokea kuitwa pia riwaya ya taharuki au vilevile riwaya ya vijana. Ni riwaya ya taharuki kwa sababu ya kimsingi ya fani yake kujigeza katika mbinu ya kisanaa/kiujumi ya taharuki. Taharuki imepewa nafasi kubwa katika aina hii ya riwaya kwa njia ya vituko vya kusisimua vinavyojibainisha kwa njia ya mikinzano iliyosukwa kwa namna za kuachana, na ufundi wa kuachana. Taharuki imejengwa kwa kutumia msukumo pofu ambao unamzungushazungusha nasomaji mbali na msukumo mkuu. Taharuki inafikia kilele wakati ambapo msomaji anafumbuliwa msukumo mkuu kwa kujibiwa vijiswali kadhaa vilivyojitokeza katika misukumopofu. Katika Mzimu wa Watu wa Kale, mathalani, swali linalojitokeza ni: nani amemwua Bwana Ali Bomani? Mbinu za awali za msanii za kumfanya msomaji awadhanie watu wasiokuwa kuwa ndiwo wauaji (Seti Sumatra na Mfanyakazi wake au Mashetani ya Mzimuni) ndizo zinazojenga misukumo pofu, yaani misukumo inayomfumba macho msomaji ili asiione kweli.
Riwaya-pendwa imeondokea kuwa na sifa ya kuwatumia wahusika walewale, hivyo ikawa na uwezo wa kujiendeleza katika vijitabu kadhaa. Karibu kila mwandishi maarufu wa aina hii ya riwaya ameandika zaidi ya kijitabu kimoja. Sifa hiyo ya kuwatumia wahusika walewale imefanya kijitabu kimoja katika mfuatano wa vitabu kadhaa vya mwandishi mmoja kionekane kama tukio linalojitegemea katika mfululizo wa matukio. Ili kuusitawisha na kuusisitiza mfuatano huo, baadhi ya waandishi wameweza hata kudondoa kazi zao za nyuma katika kazi zao za baadaye (Abdulla katika Kosa la Bwana Musa: 1984 na Musiba katika Hofu: 1988, n.k.)
Fasihi-pendwa imejibainisha katika mawanda matatu makuu ambayo ni mapenzi, uhalifu na upelelezi. Mawanda haya yanaingiliana sana katika kusanifiwa kwayo. Na vilevile fasihi-pendwa ya kipindi hiki inazo aina tatu. Ya kwanza ni aina ya Abdulla (akiwa na wafuasi wake wakuu Katambulla na Musiba). Maandishi yao ni ya mwigo wa akina Doyle (Abdulla) na Chase (Musiba). Ijapokuwa kuna mwigo huo kifani, lakini wasanii hawa wamejitahidi kuyaweka masimulizi yao katika mazingira yao na mada nyeti za wakati wao. Abdulla amejibidiisha sana na usawiri wa matatizo ya kudhulumiana mali na jinsi hatimaye haki inavyotendeka. Naye Musiba amelishughulikia sana suala la ukombozi wa kisiasa na kiuchumi wa nchi zinazoendelea dhidi ya nchi za kibepari. Kutokana na umuhimu wa masuala wanayoyajadili, vitabu vya waandishi hawa vimekubalika hata kutumika mashuleni. Aina ya pili ni ile ya Mbunda Msokile na Zainabu Mwanga. Masimulizi ya aina hii yamejitahidi sana kuonyesha matukio mbalimbali katika sura ya mapambano ya kitabaka. Kwa maneno mengine, mada zao ni pevu, ijapokuwa mkono wa kisanii unahitaji uzoevu zaidi na utulivu. Mathalani, Mbunda Msokile amekuwa akipotezea makini makubwa kwenye hisia na huruma za msomaji, akasahau kwa kiasi fulani umuhimu wa uhalisi wa matukio anayoyaumba (Nitakuja kwa Siri, 1986).