HISTORIA YA MUZIKI WA HIP HOP NA BONGO FLEVA NA JINSI UNAVYOONEKANA KUATHIRIWA ZAIDI NA WASHAIRI WA KIMAPOKEO KULIKO WANAUSASA
Kwa
maoni yetu, tunaona kuwa Hip Hop na Bongo Fleva ni muziki tofauti, muziki wa
Hip Hop ni utamaduni unaombatana na elementi za, michoro, rap, Dj, mabreka, ni
muziki ambao mashairi yake yanaganwa kwa kutumia mashairi yenye vina na midundo
mizito wakati bongo fleva ni mkusanyiko wa muziki wenye asili kutoka nje ya
Tanzania lakini yenye mahadhi na vionjo vya Tanzania ambayo hujumuisha Zouk,
Kwaito, RnB, Kwaito, n.k. Kwa ujumla muziki huu Hip Hop na Bongo Fleva huitwa
kwa jina la muziki wa kizazi kipya ikiwa na maana ya muziki unaopendwa na
vijana kizazi cha sasa (Omari 2009:5, Samwel 2012:12).
Historia
ya muziki wa kizazi kipya (Hip Hop na Bongo Fleva)
Muziki wa Hip Hop
tunaarifiwa kuwa uliasisiwa na Wamarekani wenye asili ya Kiafrika katika mji wa
Bronx huko New York katika miaka ya 1970 (Omari, keshatajwa:1). Nchini Tanzania
unakadiliwa kuwa uliingia miaka ya 1980 Omari (keshatajwa), Mwanjoka (2011), Mbilinyi
(keshatajwa), Reuster-Jahn (2014). Katika kipindi hiki vijana wengi hususani
wale waliotoka katika familia zenye uwezo walianza kuimba mashairi (muziki) ya
rap kwa kuiga nyimbo zilizokuwa zikiimbwa na wanamuziki wa Marekani wakati huo.
Chachage aliwahi kuandika kuwa, katika mazingira hayo ndipo baadhi ya vijana
waliokuwa wakijitambulisha kwa kusikiliza muziki wa Reggae wa Bob
Marley na kucheza ‘Break Dance’ katika miaka ya 1980, ili
kujinusuru na kuyasahau matatizo yao, walipoanza kujipambanua na muziki
wa Hip Hop (Bongo Fleva). Mwanzoni ulikuwa ni muziki ulioambatana na
kuiga kisisisi muziki huo. Kuiga kisisisi maana yake kuiga kitu kama kilivyo.
Madai haya ya kuiga
muzuki wa Marekani yanaungwa mkono na Mwanjoka (keshatajwa, 8) anaposema,“Mbali
na kuiga nyimbo, vijana hao wa Tanzania waliingiwa na mapenzi ya ndani
zaidi na muziki huo hata kujikuta wakiiga mavazi, mitindo ya nywele, mienendo
hadi kuongea toka kwa wanamuziki hao wa Marekani na Ulaya.”
Hivyo tunaona kuwa
wasanii wa Hip Hop na Bongo Fleva mwanzoni walianza kuimba kwa kunakiri na
kukariri mashairi ya wasanii hao wa nje na hata midundo waliyokuwa wanaitumia
ilikuwa ni midundo hiyo hiyo ya wasanii wa nje. Mbilinyi (keshatajwa, 32)
anaongezea kwa kusema kuwa, “Kama kulitokea na aliyerap kwa kutumia
lugha ya Kiswahili basi alitumia flow (kutiririka) ya nyimbo
za mamtoni zilizokuwa maarufu kama ambavyo alikuwa anafanya mkongwe Saleh Jabir
katika nyimbo kama Ice Ice Baby ya Vanilla Ice na OPP ya Naught by Nature
ilikuwa ndiyo staili ya kipindi hicho.” Ufafanuzi katika mabano ni
wetu.
Lakini baadaye wasanii
wakaachana na uigaji wa muziki wa kimagharibi na kuanza kutunga nyimbo zao
binafsi kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza jambo linaloendelea mpaka sasa
ingawa tungo za Kiswahili ndiyo hupewa nafasi kubwa. Na msanii wa kwanza kabisa
kuanza kuandika na kuimba kwa Kiswahili alikuwa ni Salehe Jabir ambaye kwanza
tunaelezwa kuwa alianza kubadilisha nyimbo za Kiingereza kwa kutumia Kiswahili
zilizotamba kipindi hicho na baadaye akaanza kutunga nyimbo zake mwenyewe. Hapo
ndipo ikachochea wasanii wengi kuona kumbe inawezekana kurap kwa Kiswahili
ndiyo nao wakaanza kujitokeza kutunga na kuimba kwa lugha ya Kiswahili,
Mbilinyi (keshatajwa) na Mwanjoka (Keshatajwa).
Baadhi ya wasanii na
makundi ya Hip Hop wanaotajwa kuwa ni waasisi wa muziki huu walikuwa ni, Fresh
XE, BBG, Adili Kumbuka, Salehe Jabir, KBC, Samia X, The BIG, Rymson, 2 proud
(Sugu), makundi ni kama vile, Kwanza Unit, Deplowmatz, HardBlasterz, Gang Stars
With Matatizo (GWM), Wagumu Weusi Asilia, Young Da Mob, Afro Reign, Jungle
Crewz Pose, Bantu Pound, Hardcore unit kwa kutaja machache. Wasanii na makundi
ya kuimba (Bongo Fleva) ni kama vile, Mawingu Band, Lady Jay Dee, Stara Thomas,
Unique Sisters, Nurueli, 4Kruz kwa kutaja wachache Mhagama (keshatajwa),
Mbilinyi (keshatajwa), Mwanjoka (keshatajwa).
>>>>>INAENDELEA>>>>>>