Vyombo vya ukuzaji na uenezaji wa Kiswahili

Ili kuimarisha matumizi ya lugha ya Kiswahili serikali iliamua kuanzisha vyombo mbalimbali vya ukuzaji wa Kiswahili. Katika mada hii utaweza kujua vyombo mbalimbali vya kitaifa na kimataifa vinavyojishughulisha na ukuaji na uenezaji wa Kiswahili. Pia utaweza kujua majukumu ya kila chombo kataka ukuaji na uenezaji wa Kiswahili.

Tangu Tanzania ipate uhuru hadi sasa kuna vyombo kadha wa kadha vilivyoanzishwa kwa ajili ya kukuza na kueneza Kiswahili baadhi ya vyombo hivyo ni hivi vifuatavyo:
BAKITA
Hii ni taasisi ya serikali iliyoundwa kwa sheria ya Bunge Na.27 ya mwaka 1967 kwa madhumuni ya kukuza Kiswahili. Kutokana na sheria hii Baraza ndilo mratibu wa kusimamia asasi zote na mawakala wote wanaokuza Kiswahili katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
BAKITA imekuwa na mchango mkubwa sana katika ukuzaji na uenezaji wa lugha ya Kiswahili kupitia majukumu yake. Majukumu ya Baraza kama yalivyofafanuliwa katika sheria hiyo ni haya yfuatayo:
  • Kuratibu na kusimamia maendeleo na matumizi ya Kiswahili nchini kote. Katika kufanya hivi Baraza lina jukumu la kuhakikisha Kiswahili kinaendelea na kuhakikisha kuwa matumizi ya Kiswahili yanakuwa sahihi.
  • Kushirikiana na vyombo vingine nchini vinavyojihusisha na maendeleo ya Kiswahili na kuratibu shughuli zao. Vyama vya Kiswahili kama vile CHAKAMA, CHAWAKAMA vina mchango mkubwa wa kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili kwa kushirikiana na BAKITA. Ushirikiano wa BAKITA na vyama hivi waweza kuwa ni wa kuto ushauri, au msaada wa kifedha, kwa mfano BAKITA imekuwa ikiwasaidia CHAWAKAMA pale wanapokuwa wanataka kufanya makongamano nap engine wanahitaji msaada wa kifedha, kwa hiyo BAKITA imekuwa ikiwasaidia kifedha.
  • Kuhimiza matumizi ya Kiswahili katika shughuli rasmi na za kawaida. BAKITA imekuwa ikiandaa vipindi mbalimbli redioni ili kuhimiza matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili.
  • Kushirikiana na mamlaka zinazohusika kuthibitisha tafsiri sanifu za istilahi. Katiaka uundaji wa istilahi, BAKITA imekuwa ikichapisha vitabu mbalimbali ikionesha istilahi sanifu zilizoingizwa katika lugha ya Kiswahili. kwa hiyo kupitia jukumu hili Kiswahili kimekuwa kinakua.
  • Kutoa huduma za tafsiri na ukalimani kwa serikali, mashirika ya serikali na yasiyo yaserikali na asasi nyingine. Kupitia tafsiri zinazofanywa na BAKITA Kiswahili kimekuwa kikikuwa na kuenea.
  • Kuchapisha jarida au toleo linalohusu lugha na fasihi ya Kiswahili. Machapisho haya ya BAKITA yanaendelea kukifanya Kiswahili kukua kwa kuongeza msamiati mpya na hivyo watu wanaposoma machapisho hayo wanajifunza msamiati mpya na hivyo kufanya Kiswahili kukua.
  • Kushirikiana na mashirika ya kitaifa, asasi na watu binafsi, kufuatilia, kushauri na kusimamia shughuli zinazolenga kukuza Kiswahili nchini Tanzania.
  • Kutoa ushauri kwa waandishi na wachapishaji ili watumie Kiswahili fasaha. Kwa kufanya hivi matumizi bora ya Kiswahili yanakuwa yanaimarika.
  • Kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuthibitisha vitabu vya Kiswahili vitakavyotumika shuleni na vyuoni kabla havijachapishwa. Hili pia ni jamabo linaloimarisha matumizi ya Kiswahili sanifu.

TAKILUKI
Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI) ilianzishwa mwaka 1979 kwa lengo la kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Zanzibar, ili kutimiza lengo hilo TAKILUKI inajishughulisha na kazi zifuatazo:
  • Kuratibu na kuendesha mafunzo ya lugha ya Kiswahili visiwani Zanzibar, kuendesha mafunzo ya lugha ya Kiswahili kwa wazawa na wageni, kuhariri miswada mbalimbali ili kuthibitisha ufasaha wa Kiswahili na kufanya tafiti za Kiswahili katika Nyanja zake zote, hususani katika uwanja wa sarufi na fasihi.
  • Pia TAKILUKI wana kazi ya kuandaa istilahi za taaluma mbalimbali, kutoa huduma za taaluma mbalimbali, kutoa huduma za tafsiri na ukalimani kwa lugha mabalimbali kwa mashirika, idara, wizara, taasisi, kampuni na watu binafsi, kufundisha lugha za kigeni na kuandika vitabu mbalimbali vya Kiswahili.
  • Pia hujishughulisha na utoaji wa ushauri wa kitaaluma kwa watunzi wa vitabu ili waweze kuandika kazi zenye ubora, na kushirikiana na wadau wengine wa Kiswahili kama vile, mashirika, wizara, taasisi, vyuo na watu binafsi katika kuendesha shuguli za ukuzaji wa Kiswahili, mathalani kuandaa na kuendesha semina, warsha na kozi fupifupi za Kiswahili.
  • Vilevile hujishugulisha na usimamizi na ufuatiliaji wa matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili katika vyombo vya habari na katika shughuli mbalimbali za serikali na za kawaida.

TUKI/TATAKI
Majukumu ya TUKI ni pamoja na kuunda sera muafaka za kustawisha Kiswahili na pia kufanya utafiti katika lugha ya Kiswahili.
Majukumu mengine ya TUKI ni kuhariri, kuchapisha vitabu na kutawanya vitabu na majarida ya kitaaluma katika Kiswahili.
Kwa sasa TATAKI inatoa shahada ya awali na uzamili katika lugha ya Kiswahili, kwa njia hii inawaandaa wataalamu wa lugha ya Kiswahili ambao watatumika sehemu mbalimbali za ulimwengu kufundisha lugha ya Kiswahili.

CHAUKIDU
CHAUKIDU ni kifupi cha Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani, makao makuu ya chama hiki kwa sasa yapo chuo kikuu cha Wisconsin-Madison, Marekani.
Madhumuni makuu ya CHAUKIDU ni: Kuwajumuisha pamoja wakuzaji wa Kiswahili duniani kote kwa lengo la kuchochea kasi ya malengo mahususi yafuatayo:
  • Kukuza Kiswahili katika nyanja zote ambamo lugha hii inatumika au inaweza kutumika na kuongeza ufanisi wa mawasiliano katika ufundishaji na utafiti wa maarifa ya aina zote, uandishi/utangazaji wa habari, uandishi wa vitabu, uchapishaji vitabu na majarida, utayarishaji wa safari za mafunzo katika Afrika ya Mashariki na Kati, n.k.
  • Kusambaza habari na matokeo ya utafiti kwa kutumia machapisho mbalimbali na teknolojia ya mtandao wa kompyuta juu ya vipengele mbalimbali vya Kiswahili na masuala yanayohusiana na Kiswahili.
  • Kuwajumuisha wanachama kwa ajili ya kubadilishana mawazo na tajiriba zao katika masuala mbalimbali yanayohusu Kiswahili (k.v. uboreshaji wa ufundishaji, utangazaji, utafiti, uandishi, nk.) kwa njia ya mkutano wa kila mwaka, warsha au semina au kongamano maalumu, na hata kwa njia ya mtandao.
  • Kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kujivunia, kuendeleza, na kuheshimu Kiswahili.
  • Kushauri ama kushinikiza serikali za nchi ambamo Kiswahili kinazungumzwa kutambua thamani iliyobebwa na maliasili hii ili kuunda sera muafaka za kukiendeleza kadri ya uwezo wake kwa manufaa ya maendeleo ya serikali na watu wake kijamii, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni, kielimu, n.k
Powered by Blogger.