RIWAYA YA KISWAHILI


RIWAYA    YA    KISWAHILI
   MAANA   YA   RIWAYA    NA    AINA ZA RIWAYA:

Riwaya imefasiliwa na wataalamu mbalimbali miongoni mwao nikama vile,

Encyclopedia Americana (EA), Jz. 20 (1982:510f) wakinukuliwa naMulokozi (1996) wanasema, riwaya kuwa ni hadithi ya kubuni inayotosha kuwa kitabu.

Udhaifu; Maelezo haya yanaibua utata kwani hayafafanui kitabu kinapaswa kuwa na urefu kiasi gani. Matharani kwa mujibu wa UNESCO katika Mulokozi (1996) kitabu ni chapisho lolote lenye kurasa 48 au zaidi. Ama urefu wa kitabu hautegemei idadi ya kurasa tu pia unategemea ukubwa wa kurasa (upana na kina) ukubwa wa maandishi na mpangilio wake.


Encyclopedia Britanica EB, Jz.8, (1985:810) wakinukuliwa naMulokozi (1996) wanaeleza kuwa, riwaya ni masimulizi marefu yakinathari yaliyochangamana kiasi, yenye kuzungumzia tajriba yamaisha ya binadamu kwa ubunifu.

Udhaifu: Udhaifu wa hoja hii ni kwambawamejikita katika kigezo cha urefu, lakini hatujui urefu huo wapaswa kuwa kiasi gani.


Wamitila (2002) Senkoro(2011) na hawakubaliani na kigezo cha kufasili riwaya kwa kutumia

kigezo cha urefu. Mfano Senkoro anaeleza kuwa ,“Ikiwa tutakichukua kipimo cha jumla ya maneno(75,000)kuwa kielelezo cha riwaya basi itaonekana kuwatunariwaya chache mno katika fasihi kwa hali hiinadhani sifa ya mchangamano ni nzuri zaidikuelezeamaana ya riwaya” (uk. 56)Naye Wamitila anendelea kuelezea kuhusiana na suala urefu kuwa,“Kigezo hiki cha urefu hakifaitunapoziangalia kaziza fasihi ya Kiswahili...Mfano kazi mbili zaE. Kezilahabi,“Nagona naMizingile” hazina idadi kubwa yamaneno lakinini riwaya”.


Wamitila (2002) na Senkoro (2011) wanasema riwaya nikisa mchangamano ambacho huweza kuchambuliwa kupimwa kwamapana na marefu kifani na kimaudhui.

>> Riwaya ni kisa aumkusanyiko wa visa, nyenye urefu unaoviruhusu vitambe nakutambaa mahali pengi na kuambaa vizingiti vingi vya maisha kamaapendavyo mwandishi wake.

>> Riwaya basi ni hadithi ndefu ya kubuni,yenye visa vingi, wahusika zaidi ya mmoja, na yenye mazungumzona maelezo yanayozingatia kwa undani na upana, maisha ya jamii.Riwaya hutoa picha ya jumla ya maisha ya mtu toka nyumbani hadikatika kiwango cha taifa na dunia nzima.


Madumula (2009), Riwaya ni masimulizi marefu ya kubuni yaliyo katika mtindo wa kubuni yakisawili mtindo maalumu na madhumuni maalumu. Mhusika katika Riwaya anakuwa ni kipaza sauti cha mwandishi.

KWA UJUMLA;riwaya ni masimulizi ya kubuni ya kinathari yenye msuko au mpangilio fulani wa matukio au ploti inayofungamana na wakati au kusawili wakati na yenye visa vingi vivavyotendeka katika wakati fulani na yenye mawanda mapana yenye mchangamano wa dhamira, visa na wahusika.


MAANA YA RIWAYA KISWAHILI:

Riwaya ya Kiswahili ni ile ambayo inafungamana na utamaduni wa jamii ya waswahili katika lugha ya kiswahili ambao hupatikanakatika nchi ya Afrika mashariki. Pia ni ile riwaya ambayo inawahusu waswahili wenyewe.


VIPENGERE VYA MSINGI KATIKA RIWAYA;

Inaonyesha kuwa ili kujua maana ya riwaya ni vyemakuzingatia mambo kadhaa ambayo ndiyo ya msingi, na mambohayo ni;

 1) Lazima riwaya iwe na lugha ya kinathari,

2)  Isawiri maisha ya jamii,

3) Iwe na masimulizi ya kubuni na visa virefu,

4) Wahusika zaidi ya mmoja,

5) Iwe na mpangilio na msuko wa matukio,

6)  Lazima na maneno kuanzia elfu thelathini na tano na kuendelea, na

7) Riwaya ni lazima ifungamane na wakati yaani visa na matukio ni lazima viendane na matukio.



HISTORIA FUPI YA RIWAYA:

Riwaya ilizuka kutokana na maendeleo ya mageuzi ya kiutamaduni. Suala la ukoloni na uvumbuzi pia liliumba hali ambazo zilihitaji kuelezwa kwa mawanda zaidi ya yale ya ngano na hadithi fupi. Hapo hapo kuzuka kwa miji na viwanda pamoja na maendeleo ya wasomaji yalifanya riwaya nyingi ziandikwe.

Uchangamano wa maisha ya jamii kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni wenyewe ulizusha haja ya kuwa na utanzu wa fasihi ulio na uchangamano kifani na kimaudhui.

Kupanuka kwa usomaji, hasa wakati wa mapinduzi ya viwanda huko Ulaya, kuliwafanya waandishi waandike waandiko marefu kwani sasa walikuwapo wasomaji hasa wanawake waliobaki majumbani wakati waume zao walipokwenda viwandani, wasomaji ambao muda wao uliwaruhusu kusoma maandiko marefu marefu ijapokuwa hii lilikuwa jambo la baadaye sana wakati wa kina Charles Dickens. Hii historia fupi ya chimbuko. Senkoro (2011:55).


HISTORIYA KATIKA RIWAYA YA KISWAHILI;

Tanzu za asili zinaonyesha kuwa ndio zilichangia kwa kiasi kikubwa sana katika kuibua riwaya za Kiswahili.Na yafuatayo ni mawazo ya wataalamu mbalimbali juu ya chimbuko la riwaya ya Kiswahili.


Madumulla (2009), ameeleza kuwa riwaya ilitokana na nathari bunifu simulizi kama vile hadithi, hekaya, na ngano inayosimuliwa kwa mdomo. Anaendelea kusema kuwa fasihi ilitokana na maandiko ya fani ya ushairi hususan ni tendi za Kiswahili katika hati za kiarabu kwa sababu ndiyo maandishi yaliyotamba katika pwani ya afrika mashariki. Wazungu na waarabu hawakubadilishana maarifa kwa urahisi na hivyo pakapelekea kuwa na majilio ya taratibu za maandiko ya kinathari. Mwanzoni riwaya zilitafsiriwa kwa Kiswahili toka katika lugha za ulaya na kufanya riwaya za Kiswahili kutokea. Mfano wa riwaya hizo ni kama vile; Habari za mlima iliyoandikwa na Sheikh Ali Bin Hemed (1980).


Senkoro (2011) anaeleza kuwa riwaya zilizuka kutokana na maendeleo na mageuzi ya kiutamaduni, uchangamano wa maisha ya kijamii, kisiasa, kiuchumi, na kiutamaduni yaliyopelekea haja ya kimaudhui zaidi ya ngano na hadithi fupi. Anaendelea kusema kuwa riwaya za kwanza zilitafsiriwa toka riwaya za kizungu mpaka za Kiswahili, Anasema riwaya mojawapo ni ile ya James Mbotela ya Uhuru wa Watumwa. Ndiyo riwaya ya kwanza kutafsiriwa kwa Kiswahili. Pia anaeleza kuwa riwaya ni utanzu uliozuka kutokana na hali mahususi za kijamii. Riwaya kama ile ya kiingereza ya Robinson

Crusoe iliyoandikwa naDaniel Defoe ni miongoni mwa riwaya za mwanzo.


Mulokozi (1996) anaeleza kuwa chimbuko la riwaya ya Kiswahililipo katika mambo makuu mawili ambayo; nifani za kijadi za fasihipamoja na mazingira ya kijamii.Fani za kijadi za fasihi, Mulokozi anaeleza kuwa riwaya haikuzukahivihivi tu bali ilitokana na fani za masimulizi yaani hadithi, na ndipozikapatwa kuigwa na watunzi wa riwaya wa mwanzo. Fani hizozilizopata kuchipuza riwaya za mwanzo ni kama vile; riwaya zakingano, tendi, hekaya, visakale, historia, sira, masimulizi ya wasafiri,insha na tafsiri.


Ngano, Mulokozi anasema, kuwa ni hadithi fupi simulizi pia huwa nihadithi za kubuni na nyingi hasa zinawahusu wanyama wakali, piazinahusu malaika, binadamu, mazimwi na majini. Anasema kuwamara nyingi ngano huwa na msuko sahihi na wahusika wake ni bapana wahusika hao ni mchanganyiko wa wanyama, mazimwi nabinadamu. Anatolea mfano wa ngano zilizo chukua visa vya kinganokuwa ni kama vile riwaya ya Adili na Nduguze ya Shaaban Robart(1952), Lila na Fila ya Kiimbila (1966), Kusadikika ya Shaaban Robart(1951).


Hekaya,ni hadithi za kusisimua kuhusu masaibu na matukio ya ajabuyaani yasiyokuwa ya kawaida. Mara nyingi masaibu hayohufungamanishwa na mapenzi. Hekaya hizo zimepelekea riwaya zaKiswahili kama vile; Hekaya ya Adili na Nduguze ya Sharban Robart(1952), hekaya ya Ubeberu Utashindwa ya Kiimbila (1971), na Hekayaya A.J.Amiri, ya Nahodha Fikirini, (1972).

Tendi (utendi), ni hadithi ya kishairi kuhusu mashujaa wa kihistoria na wa kubuni, ambao waweza kuwa ni wa kijamii au kitaifa. Kwa kawaida baadhi ya tendi zina sifa za kiriwaya ila tu badala ya kuwa na umbo la kinathari zenyewe zina umbo la kishairi. Kuna tendi za aina mbili ambazo ni tendi andishi na tendi simulizi. Riwaya pevu kama tendi husawiri mawanda mapana ya kijamii na kihistoria. Huwa na wahusika wababe yaani mashujaa wenye kuwakilisha pande zinazopingana. Mfano wa tendi ni kama vile; Utendi wa Vita vyaWadachi Kutamalaki Mlima ya Hemedi Abdallah, (1895), Utendi war as (Ghuli), utenzi wa Fumo liyongo wa Mohamed Kijumwa K.(1913).Tendi katika riwaya za Kiswahili imetumia wahusika wawili tuambao ni wahusika wa kubuni na wale wa kijadi wa kiafrika.


Visasili, hizi ni hadithi zinazohusu asili na hatima ya watu, vitu,viumbe, ulimwengu na mataifa, na pia huangalia uhusiano wawanadamu na mizimwi pamoja na miungu. Hadithi za kivisasilizinapoonyeswa huaminika kuwa yakweli tupu hasa kwa kusimuliamatukio mengi ya kiulumwengu.Mfano wa visasili; Lila na Fila ya Kiimbila (1966) ambayo imekopamotifu ya asili ya ziwa ikimba huko Bukoba. Hadithi ya Mungu waKikuyu huko Kenya. Roza Mistika ya Kezilahabi (1971), Nagona(1987) naMzingile (1991), Siku ya Watenzi Wote ya Sharban Robart.


Visakale, ni hadithi ya kale kuhusu mashujaa wa taifa,kabila au dini. Mara nyingi visa kale huchanganya historia na masimulizi ya kubuni, na hadithi hizi hupatikana karibu katika kila kabila kila lugha.Baadhi ya visakale vya Kiswahili masimulizi huhusu chimbuko la miji ya pwani, mijikenda, mwinyi mkuu huko Zanzibar.Visa kama hivi ndivyo vinavyopelekea kuandikwa kwa riwaya za kiswahili. Mfano wake ni riwaya ya Abdalla Bin Hemed bin Ali Ajjemy (1972) katika kitabu cha Habari za Wakilindi, Kisima cha na Giningi ya M.S.Abdulla (1968) na ile Hadithi ya Myombekela na Bibi Bugonoka na Ntulanalwo naBuhliwali (1980) ya A. Kitereza.

Masimulizi ya kihistoria, haya ni masimulizi ya matendo ya, mwanadamu katika muktadha wa wakati, na ni fani muhimu sana katika jamii yeyote ile. Masimulizi halisi ya kihistoria yaweza kuwa ni ya mdomo au hata maandishi na yote huwa ni chemichemi nzuri ya riwaya. Mfano wa riwya hizo ni; Habari za pate za Fumo Omari Nabhany (1913) ambayo yalikuwa ni maandishi ya masimulizi na uchambuzi. Riwaya zingine zilizoathiriwa na matukio ya kihistoria ni;Uhuru wa Watumwa ya J. Mbotela (1934), Kifo cha Ugenini ya O. Msewa (1977), Kwa Heri Iselamagazi ya B. Mapalala (1992) na Miradi Bubu ya Wazalendo ya G. Ruhumbika (1992).


Sira, ni masimulizi ya kweli kuhusu maisha ya mtu au watu. Sira iliathirikuchipuka kwa riwaya hasa kwa kuonyesha masilimulizi ya maishaya mtu toka utotoni mpaka uzeeni. Masimuliza ya riwaya hiziyalikuwa katika masimulizi na hata katika maandishi pia kwa maanakabla ya ukoloni yalikuwepo maandishi yaliyohusu maisha ya mitumena masahaba.Mifano ya hadithi hizi ni; Kurwa na Doto ya M. S.Farsy(1960),Rosa Mistika ya Kezilahabi (1971),Kichwa Maji ya Kezilahabi(1974) pamoja na Dunia Uwanja wa Fujo (1975),Mzimu wa Baba waKale ya Nkwera (1967),na riwaya ya Maisha Yangu baada ya MiakaHamsini ya Sharban Robart (1951).

SIFA ZA RIWAYA;

Kwa mujibu wa Wamitila (2002) sifa hizo ni kama zifuatazo;

i)                    Uwazi na uangavu,

ii)                  kazi husika ya fasihi isiwasumbue nakuwatatiza wasomaji kuzielewa,

iii)                muwala na muumano,

iv)                 kazi yariwaya lazima iwe na mshikamano au mtiririko mzuri wa visa aumatukio kuijenga kazi ya kifasihi,

v)                  uchangamano wa visa yaanikutokea kisa zaidi kimoja,

vi)                Wingiwa maana kuhusiana na sifa yauchangamano na ukamilifu ni kule kuwako kwa elemeti zotemuhumiu na za kimsingi katika kazi ya fasihi.

SIFA NYINGINE NI:

vii)               Riwaya haifungwi na sheria wala kanuni.

viii)            Riwaya ina matumizi ya lugha ya kinathali. Ni lugha ya mjazo wa maneno  na mtiririko wa mawazo.

ix)                Riwaya ina urefu na upana wa kutosha,,,,,, urefu  na upana wa kimaudhui unapelekea kubeba vijitanzu vingine vidogovidogo ndani ya Riwaya.

x)                  Riwaya zao la kibepari: Riwaya ilizuka katika mfumo wa kibepari huko Ulaya , Riwaya ina sifa ya ubinafsi, ina uhitaji mkubwa wa viwanda nah ii ilianza ktk kipindi cha mapinduzi ya viwanda hivyo inahitji uchumi madhubuti kama vile uandishi na uchapaji.

xi)                Riwaya iko karibu na uhalisia, inahusisha masimulizi ambayo yalikuwepo,,,,, yapo,,,,,au yanatazamiwa yatokee na whusika hujengwa katika mazingira hayo.

xii)              Riwa inahitaji ujuzi wa kusoma na kuandika.

xiii)            Riwaya inahitaji maisha tulivu,,,,, maisha anbayo yatamfanya mtunzi awe katika hali ya kutunga Riwaya.


AINA ZA RIWAYA:

RIWAYA ZINAGAWANYIKA KATIKA MAKUNDI MAKUU MAWILIAMBAYO NI

(A) RIWAYA DHATI; Hizi ni Riwaya ambazo zina mambo dhati, wasaha na manbo ambayo ni adili kwa binadamu. Hutumia lugha fasaha, nyofu na hakuna matusi. Mfano ‘Kosa la Bwana Mussa’, ‘Mzimu wa Watu wa Kale’, ‘Utengano’ na ‘Almasi za Bandia’.


(B)  RIWAYA PENDWA;Hizi huzungumzia maswala ya upelelezi, mapenzi na mambo mengine ambayo ni pendwa. Riwaya pendwa huchomaza zaidi vipengere vya fani kuliko maudhui. Mara nyingi hutumia methali, misemo na mbinu nyingine ambazo humfanya msomaji asitafakari zaidi maudhui. Mfano: Pendo la Kifo, Njama, Kikosi cha Kisasi, Nyuma ya Pazia na Mfadhili.


AINA ZA RIWAYA KWA KUZINGATIA VIGEZO


I)                   KIGEZO CHA FANI:

Riwaya sahili; ni dhana inayotumiwa kuelezea aina za riwaya ambayo ina muundo rahisi na inaweza kueleweka kwa urahisi. Kwa mfano; riwaya ya “Kaburi Bila Msalaba” ya P . Kureithi.


Riwaya changamano; Ni riwaya ambayo ina muundo mgumu na inayohitaji umakini kuielewa. Kwa kawaida msuko wa riwaya hii huwatata. Inawezekana pakawepo na matumizi mapana ya mbinu rejeshi,upana mkubwa wa wahusika na mandhari, matumizi mengi ya lughaya kitamathali, mfano; “Mzingile” ya E. kezilahabi, “Zirail na Zirani” yaW.E Mkufya.


Riwaya ya majaribio, Ni riwaya inayojadili mkondo wa nafasi na riwaya kweli. Riwaya ya mjadara nafsi hutungwa bila kuzingatia kanuni za kawaida za uandishi wa riwaya, watunzi wa riwaya hii hudai kuwa kumbo la kawaida ya riwaya hii haitoshelezi mahitaji ya karne hii huwakilisha ukweli wa maisha.Riwaya hizi hutumia nafsi ya pili na wakati mwingine hutumia nafsi mimi kiasi kwa mwandishi ndiye mhusika. nafsi ya pili humfanya msomaji kuonekana kuwa ndiye katenda jambo. Mfano, “Mtunzi wa Hukumu” ya Kasri na “Bina-Adamu” na Musaleo” za Wamitila vilevile Nagona na Mzingire zake E, Kezilahabi.




II)                USIMULIZI:

Riwaya barua ni riwaya ambayo huwa na muundo wa barua kuanzia mwanzo hadi mwisho, au ni majibizano ya barua. mfano “Pamela” ya S.Richardson na “ Barua Ndefu kama Hii.


Riwaya ya kimonolojia ni riwaya ambayo sauti inayotawala ni moja. Sauti hiyo ni ya mwandishi. Wahusika wanaopatikana katika riwaya hii hudhibitiwa kwa kiasi kikubwa na sauti ya mwandishi. Mfano “Walenesi” na “Mafula” za Katama Mkangi.



III)             UPEO WA KIJIOGRAFIA:

Riwaya ya kiambo; ni riwaya ambayo inatilia mkazo kwenye mandhari, usemi au muundo wa kijamii na desturi za mahali maalumu. Mandhari na mahali huathiri njia mbalimbali za kuhisi na kuwaza kwa wahusika wanaopatikana kazi ya aina hii. Huelezea mambo ya tamaduni mfano, ‘Bwana Myombokera na Bi Bugonoka’, watu wa Ukerewe na ‘Kisiwa Cha Giningi’.


Riwaya ya kidastopia hii husawili jamii isiyokuwa ya kawaida na isiyokuako kwa wakati maalumu bali inafikirika tu. Katika jamii hiyo sheria za kawaida za kijamii zimebadilishwa kwa namna inayowafanya watu wengi waishie kutaabika na kuteseka sana. Mfano wa riwaya hizi ni kama vile “ Kusadikika” ya Shabani Robert na “Walenisi” ya Katama Mkangi.


Riwaya Kitaifa; hizi hujikita katika upeo wa kijiografia ambapo haivuki mipaka ya nchi. Maudhui na mawanda huwa ni yamambo yanayojiri katika taifa husika,


Riwaya za Kimataifa; Hi ni Riwaya ambazo ni kinyume cha zile za kitaifa kwa hujadili mambo ya nchi zaidi ya moja, mfano wan chi zinazoendelea na zilizoendelea.


IV)             MAUDHUI:

Riwaya historia ni aina ya riwaya ambayo msingi wake kuhusu matukio fulani katika jamii ya mwandishi, tukio hili huwa ni kubwa na la muhimu kijamii, laweza kuwa la kikabila au la kitaifa mfano “Uhuru wa Watumwa” ya J. Mbotela, “Miradi Bubu ya Wazalendo” ya Luhumbika na “Zawadi ya Ushindi” ya B. Mtombwa.


Riwaya ya kimaadili ni riwaya ambayo ina nia ya kufundisha maadili fulani mfano “Kufikirika” ya S Robert. Ni riwaya inayotoa maadili kwa jamii. Riwaya hizi huelezea mambo ya dini, mafunzo na maonyo ya maisha. Hujengwa katika nguzo tatu ambazo


a)      Mathema (kosa): Kosa analolifanya mhusika mkuu linafanya jamii ipate shida. Kosa hilo humfanya mhusika ajifunze na jamii ijifunze.

b)      Pathema (Funzo):Mafunzo anayoyapata mhusika juu ya kosa alilolifanya,

c)      Cathersis (utakaso): Utakaso unapatikana baada ya funzo na kubadilika.


Riwaya ya kimapinduzi ni riwaya ambayo inajadili migogoro namaisha ya binadamu kwa kutafakari kwa mantiki na kina kuhusumambo ambayo urazini wake hauonekani kwa urahisi.Hudodosa mapambano, mikinzano na matabaka katika jamii Mfano“Umleavyo” ya Haji na Kichwa Maji” ya E.Kezilahabi, vilevile na Dunia mti mkavu na Kusadikika.


Riwaya ya kisosholojia au jamiini riwaya ambayo inasawiri maisha ya kawaida ya jamii kwa kuchunguza matatizo yake, yawe kifamilia kitabaka, kiuchumi, kisiasa au hata kiutamaduni mfano “Titi la Mkwe” ya A. Banzi, “Kurwa na Doto” ya M.S. Farsi na “Rosa Mistika” ya E. Kezilahabi.

Riwaya saikolojiani aina ya riwaya inayododosa nafsi ya mhusika, fikra, hisia mawazo, imani, hofu, mashaka, matumaini na athari ya mambo hayo kwake binafsi na labda kwa jamii mfano “Kichwa Maji” ya E.Kezilahabi, “Kipimo cha Mianzi” ya Feud na “Kiu” ya M.S. Mohammed.


Riwaya ya kifalsafa, ni riwaya ambayo inashughulikia masuala ya kifalsafa. Mada ya kifalsafa huchukua sehemu muhimu katika riwaya ya aina hii kuliko wahusika, mandhari, msuko au mtukio.Mtunzi hutaka wasomaji wafikirie kifalsafa mambo Kama vile kuwepo au kutokuwepo kwa MUNGU, Baadhi ya viumbe, kufa na kuishi ni nini? Utu na mtu nini? Mfano, “Nagona na Mzingile” ya E kezilahabi na “Umleavyo” ya Haji Gorra Haji.


Riwaya ya mapenzi ni riwaya yenye kusawiri uhusiano wa kimapenzi kati mvulana na msichana. Huchomoza zaidi fani kuliko maudhui, Mfano “Kweli Unanipenda” “Mwisho wa Mapenzi” za Simbamwene.


Riwaya ya kitawasifu, ni riwaya ambayo ina muundo unafanana na muundo wa tawasifu kwa kuyachunguza maisha ya mtu fulani na kwa nafsi ya kwanza. Mfano riwaya ya “Uhuru wa watumwa” J. Mbotela na “Maisha Yangu baada ya Miaka Hamsini” ya S.Robert.


Riwaya ya wasifu, ni riwaya ambayo mwandishi huandika kwa lengo la kumhusu mtu fulani, mfano “Wasifu wa Siti Binti Saad” ya S. Robert.



KUNA MAKUNDI MENGINE YA RIWA AMBAYO HAYAKUAINISHWA HAPO JUU NAYO NI:


Riwaya ya ujasusi ni wa upelelezi wa kimataifa. Majasusi ni wapelelezi wanaotumwa na; nchi, serikali au waajiri wao kwenda katika nchi nyingine kuchunguza siri zao hasa siri za kijeshi, kiuchumi na kisayansi ili taarifa hizo ziwanufaishe wale waliotumwa mfano “The thirty nine steps” ya E. Msiba. “Mzimu wa Watu wa Kale”.


Riwaya ya kisayansi ni riwaya inayotumia taaluma ya sayansikama msingi wa matukio, masahibu na maudhui, mathalani riwaya hiihubashiri namna sayansi itakavyo athiri maendeeo ya mwanadamukatika karne zijazo. Mfano “Safari Kiini cha Dunia” ya Jules Vernes.


Riwaya tendi ni riwaya yenye mawanda mapana kama tendiaghalabu riwaya hii husawili matendo ya ushujaa na masuala mazitoya kijamii yenye kuathiri historia ya taifa husika. Mfano “Vita naAmani” ya Leo Tolstoi na “Chaka Mtemi wa Wazuru” ya Thomas M.


Riwaya istiara ni riwaya mafumbo ambayo umbo lake la nje niishara au kiwakilishi tu cha jambo jingine. Mfano “Kusadikika” yaS.Robert ambayo inasawili utwala wa mabavu na “Shamba laWanyama” ya Kawegere


Riwaya chuku ni riwaya ambayo hueleza vituko na masahibuyasiyo kuwa ya kawaida, ni riwaya ambayo haizingatii uhalisia namara nyingi masahibu yake huambatanana mapenzi.Mfano “Alfu lela

Ulela” ya G. Bocci ccio na “Kusadikika” ya S.Robert”


Riwaya ya kingano, ni riwaya yenye umbo na mtindo wa nganomathalani huweza kuwa na wahusika wanyama,visa vyenyekutendeka nje ya wakati wa kihistoriA.Mfano “Lila na Fila” yaLongman na “Adili na Nduguze” ya S.Robert


Riwaya kinzani ni riwaya inayotumiwa kuelezea ambayo imekwendakinyume na matarajio au kaida za uandishi wa riwaya. Mfano, kuwana muundo wa kimajaribio wahusika kukosa motisha, kuwako kwamatendo yasiyoweza kuungwa kimantiki.


Riwaya ya utetezi hii hutumiwa kuielezea riwaya ambayo inahusumatatizo ya kijami, kiuchumi pamoja na dhuluma inayowapatawanyonge au wasiokuwa na uwezo katika jamii fulani. Hivyo riwayahii hukusudia kurekebisha hali iliyopo katika jamii. Mfano “Walenisi”na “Mafuta” ya Katama Mkangi na “Kuli’ na “Vuta n’kuvute” za ShafiA.Shafi.


Riwaya ya kipolifoni; ni riwaya ambayo inahusishwa na urejeleaji ambapo kila wahusika wanapozungumza au kuongea sauti zaombalimbali zinawakilisha mikabala mbalimbali kiitikadi. Mfano “Duniamti mkavu” ya S.A Mohamed.


Riwaya ya kisasa; ni riwaya inayohusu wanasiasa na maisha yaowanasiasa. Hudhamiria kuyafichua mambo yanayotendeka kinyumena picha inayoonekakana waziwazi. Mfano; “Nyota ya Huzuni” yaGeorge Liwenga na “Njozi Iliyopotea” ya C.G. Mng’ong’o.


Riwaya ya kitarihi ni riwaya ambayo inajihusisha na mawanda makubwa ya kiwakati na kimandhari.Wahusika wengi walioteuliwakuakisi hali mbalimbali za kijamii na kiuchumi za wakati maalumu.Mfano;Riwaya ya “Habari za Wakilindi”


Riwaya ya kiutopia hii ni riwaya ambayo inasawiri jamii anayoionamwandishi kama jamii kielelezo na aghalabu huhusisha sifa zaKifantasia au kinjozi. Mfano wa riwaya hii ni kama, “Siku ya WatenziWote” ya Shaaban Robert.


Riwaya ya kiurejelevu hii ni riwaya inayojirejelea. Aghalabu katikausimulizi wake, riwaya ya aina hii huishia kutoa maoni kuhusuusimulizi wake na njia za kubuni na kutunga riwaya.Tunawezakusema hii ni riwaya inayofichua mbinu zake za kiutunzi. Mfano“Musaleo” ya K.W.Wamitila.


Riwaya tatizo; ni riwaya ambayo inajishughulisha na tatizo aumgogoro fulani katika jamii. Huweza pia kuelezea aina ya riwayaambayo inachunguza tasnifu au swala fulani la kisaikolojia. Mfano;“Kuli” ya Shafi A.shafi na “Mafuta” ya K. Mkangi.


Riwaya kampasi; ni riwaya ambayo mandhari yake ni chuo kikuu. Hata hivyo hii imepanuliwa nakuhusishwa na kazi za kuchekesha auzenye mwelemeo wa kitashititi. Kazi za aina hii hukusudia kufichuaudhaifu uliopo katika tabia za wanachuo.Mfano; “Small world” yaDavid Lorge.



NADHARIA ZA UCHAMBUZI WA FASIHI

Wataalamu mbalimbali wameainisha nadharia mbalimbali za uchambuzi wa kazi yoyote ya fasihi. Miongoni mwa nadharia hizo ni pamoja na;


(i)                 Nadharia ya umuundo (structuralism)

Umuundo ni nadharia inayojibainisha kwa kuangalia Ujumla wa uhusiano wa sehemu moja kwa nyingine katika kufanya kitu kizima. Kwa mfano muungano wa maneno hufanya sentensi na sentensi zikiungana zinaunda aya au onesho na onesho kuunda tamthiliya. Ntarangwi (2004) anasema kuwa umuundo waweza kuelezwa kama mtizamo wa kitathimini ambao huzingatia zaidi miundo inayojenga kazi binafsi.


 Mwasisi anayetajwa sana katika nadharia hii ni Ferdinard De saussure aliyependekeza mtizamo mpya kuhusu lugha. Kinyume na wataalamu wengine walioshughulikia historia na sura maalum za lugha fulani, Saussure alivutiwa na miundo inayohimili lugha zote, huku akijaribu kuonyesha kwamba lugha zote za ulimwengu zaweza kutathiminiwa kwa kaida maalum za umuundo. Alizua istilahi `parole' na `langue' kueleza maoni yake: `Parole' au uzungumzi ni lughakatika matumizi na hiki ndicho walichokizingatia wanaisimu wa awali,


Mkondo huu wa mawazo ya umuundo kuhusu sayansi za jamii ulianzia ulaya na kuathiri mtazamo wa elimu mbalimbali (duniani) kama vile: Falsafa, Anthropolojia, Historia, Uhakiki wa kifasihi naSasiolojia. Kwa hivyo twaweza kuangalia jamii katika muundo wake wa kijuu juu na kuielewa lakini tukitaka kupata maana mwafaka lazima tuchunguze muundo wake wa ndani ambao hupatikana katika kila jamii ya wanadamu. Kwa hiyo hata katika kuielewa fasihi lazima tuifahamu lugha yake.

UMUUNDO NA FASIHI

Kama vile muundo wa lugha ulivyo mfumo, muundo wa fasihi pia una vipengele vinavyotegemeana na vinavyoelezwa katika muktadha wa vipengele vingine. Katika kazi ya fasihi kuna kitengo cha kisanaa kama vile maudhui, ploti, wahusika, muktadha na lugha. Hakuna kipengele cha fasihi kati ya hivi kitakachoelezwa katika upekee wake. Lazima kielezwe kwa kuzingatia kuwepo kwa jukumu la vipengele vingine. Kwa mfano katika kueleza au kuzungumzia ploti, wahusika watashirikishwa na lugha yao kuzingatiwa. Kwa hiyo nadharia ya umuundo husisitiza vipengele vya kazi ya sanaa, jinsi vinavyohusiana hadi kuikamilisha kazi hiyo. Huangalia namna sehemu mbalimbali za kazi za sanaa zilivyofungamana. Yaani Neno halihitaji urejelezi ili lipate maana, na Kazi yenyewe ilivyoundwa ndivyo hutoa maana. Yaani maana inavyoumbwa ina dhima kubwa kuliko maana yenyewe.

(ii)               Nadharia ya umarx (marxism)

Kwa maana rahisi kabisa, tunapoongelea kuhusu nadharia ya UMarxtuna maana ya kurejelea mikabala mbalimbali ambayo misingiyake mikuu ni mawazo yanayohusishwa na Carl Marx na FriedrichEngels. Katika kitabu cha The Germany Ideology, Marx na Engelswalisema kuwa kitu cha msingi katika maisha ya binadamu ni kula nakunywa, kupata malazi na mavazi na mambo mengine. Tendo lakwanza la kihistoria kwa hiyo ni kutafuta njia ya kuyakidhi mahitajihaya ya msingi. Ili kufanikiwa katika lengo hilo, binadamu hulazimikakujiunga pamoja au kuunda umoja ili kuimarisha umoja na wepesi wakuizalisha mali ya kukidhi mahitaji hayo. Muungano huo huwa naugawaji wa majukumu au kazi ambayo ndiyo msingi wa kuundwakwa matabaka katika jamii.

Umarx katika Fasihi

>Usanii ni uumbaji wa Ukweli katika maisha.

> Ukweli unaooneshwa katika kazi za fasihi hiyo ni usahihi wa mambo katika jamii? Kama niRiwaya, Tamthilia, Ushairi na kadhalika inawakilishaje ukweli?

> Kazi za kisanaa zinatakiwa kuonesha mivutano iliyopo katika jamii hasa kati ya wanyonyaji na manyonywaji.

(iii) Nadharia ya urasimi

Kwa mujibu wa Njogu na Wafula (2007) Urasimi ni wakati maalumuambapo misingi ya kazi za sanaa huwekwa na kukubalika kuwavipimo bora kwa kazi nyingine. Hii ina maana kwamba kila jamii inaurasimi wake. Urasimi katika Kiswahili ulikuwepo kati ya karne ya 18na karne ya 18. Nao urasimi wa Kigiriki ulikuwepo baina ya karne yanne (KK) na takriban karne ya nne (BK).

Sifa za urasimi kwa ujumla

Pamoja na kwamba imeshatajwa hapo mwanzo kuwa kila jamii ina urasimi wake, lakini bado tunaweza kutoa sifa za jumla za urasimi mahali popote ulipo. Kwa mfano:


>Kazi ya kirasimi huwasilishwa katika lugha inayoeleweka kwa urahisi. Hii ina maana kuwa wazo linaelezwa moja kwa moja. Mitindo ya Kinjozi (mf.Nagona, Mzingile, Bina-Adamu, Walenisi) haitumiwi.Uhalisia unasisitizwa.


·>Kazi nyingi za kirasimi hazichoshi kusoma. Hii ni kwa sababu kazi hizi ni kazi bora. Husomwa mara nyingi na watu wengi na kila unapoisoma wazo jipya hupatikana.


>Fani na maudhui katika kazi za kirasimi ni mambo yaliyofinyangwa kwa kutumia mbinu kamilifu na teule. Daima kuna ufungamano uliokamilika kati ya kinachoelezwa na jinsi kinachoelezwa.




(IV) JE ONTOLOJIA YA KIAFRIKA INAWEZA KUTUMIKA KAMA

NADHARIA YA KUCHAMBULIA KAZI ZA FASIHI ZA KIAFRIKA?.

( fuatiliya makala hii katika mtandao ili kupata nukuu zaidi )


JE UNGEPENDA KUJUA MAANA AU FASILI YA FALSAFA

Wikipedia kamusi elezo huru wanasema,falsafa ni neno linalotokana na neno la kigiriki lenye maana ya upendo na hekima,wanaendelea kusema kuwa falsafa ni jaribio la kuelewa na kueleza ulimwengu kwa kutumia akili inayafuata njia ya mantiki . Falsafa huchunguza mambo kama vile kuweko,au kutokuweko,ukweli,ujuzi ,uzuri,mema, na mabaya,lugha na haki.


Kwa mujibu wa Wamitila (2003 ) anasema, falsafa ni mawazo anayoyaamini mtu au mwandishi kuwa yana ukweli unaotawala misingi ya maisha.

Hivyo, Falsafa ni taaluma au mtazamo unaochunguza matumizi ya dhana,kupima hoja,mbinu za ujengaji hoja,kufanya uhakiki au tathimini,kuthibitisha au kutoa ushahidi wa hoja zinazozungumzwananadharia mbalimbali zinazohusu maisha.Mfano,kuua ni tendo zuri au sio zuri?

BASI IMANI NA MTAZAMO WAKO VIKUONGOZE KATIKA KUSOMA NA KUTAFAKARI NUKUU HIZI:

NAKUTAKIA USOMAJI MWEMA WA KISWAHILI (RIWAYA KISWAHILI);

Nukuu hizi ni baadhi zimekusanywa kutoka wataalamu mbalimbali, Vitabu na mitandao ya kijamii; na

MWLIMU   ALLY  ABDUL MKINDI

NA AISHA ALLY ABDUL MKINDI






MALEJEO.

Madumulla, S.J. (2009) Riwaya yaKiswahili: Nadharia Historia na Misingi yaUchambuzi.Dar

es Salaam: MtureEducational Publishers Ltd.


Mulokozi, M.M. (1996) Utangulizi wa Fasihiya Kiswahili. Dar es Salaam: TUKI.


Senkoro, F.E.M.K. (2011) Fasihi. Dar esSalaam: KAUTTU.


Wamitila, K.W. (2002) Uhakiki wa Fasihi:Misingi na Vipengele Vyake. Nairobi:Phoenix

Publishers Ltd.

Wamitila, K.W. (2003) Kamusi ya Fasihi:Istilahi na Nadharia. Nairobi: FocusPublicatins Ltd.


Madumulla, J.S. (2009), Riwaya ya Kiswahili, Historian a Misingi ya Uchambuzi. Nairobi:

Sitima Printer andstations L.td.


Mulokozi, M.M. (1996), Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam. TUKI.


Mhando, P. na Balisidya, (1976), Fasihi na Sanaa za Maonyesho. Dar es Salaam: Tanzania

Publishing House.


Nkwera, F.V. (1978), Sarufi na Fasihi Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam: Tanzani Publishing

House.


TUKI,(2004),Kamusi ya Kiswahili Sanifu.Nairobi.Kenya:Oxford University Press.


Senkoro,F.E.M.K.(2011), Fasihi Andishi.Dar es Salaam.Kauttu L.t.d.


Wamitila,K.W.(2003),Kamusi ya Fasihi, Istilahi na Nadharia. Nairobi:Focus Publication.


Mihanjo A,(2010)Falsafa na ufunuo wa maarifa.Toriam.MorogoroTanzania.


Mohamed S.k (1988)Fungate ya uhuru.Dar-es-salaam universityplace(DUP).


Muhando p (1982) Nguzo mama. Dar-es-salaam universityplace(DUP).


Njogu na Chimera R(1999)Ufundishaji wa fasihi,Nadharia naMbinu.Jomo Kenyatta.Nairobi


Tuki(2004)Kamusi ya Kiswahili sanifu.Taasisi ya Uchunguzi waKiswahili.Dar-es-salaam.


Wamitila K.W (1996) Utangulizi wa Kiswahili.Chuo kikuu cha Dares-salaam.Dar-es-salaam
Powered by Blogger.