SURA YA PILI - Maendeleo ya Wahusika Katika Riwaya ya Kiswahili Tanzania



Katika uhakiki wa kipengele cha mhusika katika riwaya ya Kiswahili, mtindo wa uhakiki wa 'kijadi' umetokea kutumika zaidi na wahakiki wa fasihi. Uhakiki wa 'kijadi' tukiwa na maana ya kuwa wahakiki wamemtazama mhusika kwa kutumia vigezo na istilahi zilizozoewazoewa kama vile, uhusikabapa, uhusika halisi, uhusika shinda, uchorwaji wa mhusika, kufaulu kwa msanii katika kuwachora wahusika wake, na rnengine kama hayo. Mtindo huu wa kijadi wa kumwangalia mhusika unajitokeza katika majarida, vitabu na makala kadhaa ya fasihi (rejea majuzuu kadhaa ya Mulika, Kiswahili, Kioo cha Lugha, Zinduko, magazeti ya mashule na vyuo, n.k.). Mchango wa mkabala huo wa kijadi katika fasihi ya Kiswahili ni kwamba umejenga msingi wa uhakiki.
Tunaweza kusema kuwa mhusika alianza kutazamwa kwa namna nyingine kidogo mhakiki alipojaribu kuingia ndani zaidi ya maarifa ya uhakiki katika Aggressive Prose (1982:82) akapata kugundua aina ya namna yake ya mhusika aliyejitokeza katika uandishi wa riwaya ya Kiswahili kama itakavyogusiwa mwishoni mwa sura hii.
Makala mengine yanayostahili kutajwa ambayo yamemjadili mhusika kwa namna isiyo ya 'kijadi' ni yale ya Mlacha (Kiswahili, Vol. 53/1-2, 1986:146-167) ambamo anajadili mahusiano ya wahusika kwa vigezo vya kiujumi, akitumia nadharia ya kimuundo. Mlacha akiutumia mkabala unaofanana na ule wa V. Propp anaona kuwa wahusika wakuu katika riwaya ya Kiswahili wanapita katika hatua nne: 1. Mwanzo (Beginning); 2. Kuanza Upya (New Development); 3. Kujirudi/kujikosoa (Return); 4. Mwisho (End). Kati ya kilahatua, asemavyo Mlacha, kuna 'mkanganyiko' (confusion) (M1-3)) ambao unachukuliwa kama ni kipindi cha mpito kutoka hatua moja hadi nyingine.

M1

M2

M3

(1)
®
(2)
®
(3)
®
(4)
Aidha katika kustaamali mahusiano ya wahusika katika riwaya ya Kiswahili, Mlacha anaturejesha kwa mtaalam huyo wa nadharia ya kimuundo, Propp, akisema:
A fundamental analysis in this section can be based on Vladimir Propp's (1928) work where the roles assumed by the characters in the folk tale (sic) were reduced to seven ... A character in Vladimir Propp could either be a villain, the sought-for-person, the doner (sic), the helper, the dispatcher, the hero or false hero. One character can have more than one quality. With this approach in mind, we can identify the qualities of different characters in Kiswahili prose fiction.
(Uhakiki wa msingi wa sehemu hii unaweza kujigeza katika kazi ya Vladimir Propp (1928) ambamo nafasi za wahusika katika hadithi zilibainishwa kuwa saba;... Mhusika kufuatana na Vladimir Propp angeweza kuwa mkinzani, anayetafutwa/nguli, mtoakinga, msaidiaji, mtumaji, mbabe au mbabe asiye halisi. Mhusika mmoja anaweza kuwa na sifa zaidi ya moja. Kwa kuuzingatia mkabala huu, tunaweza kubainisha sifa za wahusika mbalimbali katika riwaya ya Kiswahili). (Kiswahili, Vol. 53 uk. 148)
Mkabala huu ulipigiwa hatua nyingine mpya na Greimas (1962-3) mwanaisimu, alipoamua kuutumia muundo huo wa uhusika si kwenye hadithi nzima tu, bali hadi kufikia kiwango chasentensi (Culler, 1975:233):
destinateur
®
objet
®
destinair
(mtumaji-addresser)

(anayetafutwa)

(mbabe-addressee)
adjuvant
®
sujet
¬
opposant
(-saidizi)

(sababu)

(-kinzani)
Kuhusu mkabala wa Propp, Jonathan Culler (1975:233), mtaalam mwingine wa nadharia ya kimuundo alitahadharisha kuwa:
“He (Propp - JM) made no claims for the universality of this set of roles,...''
(Yeye Propp hakudai kuwa seti hiyo ya dhima za uhusika ina kaida za kijumla...)
Tahadhari hii inaweza kupewa uzito ikitiwa maanani kuwa Propp aliijenga fomula yake kutokana na utafiti na uchambuzi wa hadithi 100 za kifasihi-simulizi. Fomula hiyo inayasadifu mazingira hayo ya kifasihi-simulizi kutokana na kawaida za kijumla za hadithi ya kifasihi-simulizi kama tutakavyoona mbele katika sura hii ambapo tutaonyeshwa kuwa mhusika wa hadithi ya namna hii ameundwa kwa namna maalum inayoyasadifu mazingira ya kijumla ili awe kielelezo kisichobadilika cha wakati.wote. Kwa jinsi hiyo tunapokabiliwa na riwaya ya kisasa ambayo muundo wake, hususan kifani, unazidi kujitofautisha na ule wa hadithi ya kifasihi-simulizi, fumula ya Propp inatakiwa ipokelewe na kutumiwa kwa tahadhari katika mazingira mapya ambayo yana visalia vya hapa na pale tu vya kaida za kijumla. Fomula ya Propp imeondokea kuwavutia wataalam kadhaa wa nadharia ya kimuundo ambao wameiendeleza na kuzidi kuifanyia marekebisho (k.m. Greimas, Todorov, Frye, Barthes, n.k.) katika kuueleza uhusika. Marekebisho hayo yanaendelea ili kukifikia kielelezo kitakachoyaziba mapengo yaliyozushwa na majaribio ambayo yamekuwepo hadi sasa, kama Culler (1975:237-8) anavyohitimisha:
Here, as elsewhere, structuralism does not offer a full-fledged model of a literary system, but by the problems it has posed and the formulations it has attempted it does at least provide a framework within which thought about the novel as a semiotic form can take place.
(Hapa, kama penginepo pote, nadharia ya kimuundo haitoi kielelezo kipana cha mfumo wa kifasihi; lakini kwa njia ya maswali yaliyoibuliwa, na vielezo vilivyojaribu kutolewa nadharia hii imetoa angalau njia ambayo kwayo wazo juu ya riwaya kama umbo la kisemiotiki litajengwa).
Vinginevyo, nadharia hiyo ya kimuundo ambayo imejitanua kuifikia riwaya ya Kiswahili ni namna nyingine mpya inayoibua changamoto ya namna yake katika kumchunguza mhusika wa riwaya ya Kiswahili. Pamoja na maendeleo hayo mapya ya kumtazama mhusika, katika sura hii, maendeleo ya wahusika katika riwaya ya Kiswahili (Tanzania) yanatazama jinsi mhusika 'alivyokuwa' kutoka masimulizi ya kinathari ya kifasihi-simulizi mpaka kufikia riwaya ya kisasa.
Riwaya ya Kiswahili imekuwa ikitazamwa na wanafasihi mbalimbali kwa namna za kuachana. Kuna wale ambao hawaoni kama kuna maendeleo katika uandishi wake, hususan wakiilinganisha na riwaya za mataifa ya Ulaya na hata zile riwaya zilizoandikwa na Waafrika katika lugha za kigeni. Hata hivyo kuna wachache wanaokubali kuwa riwaya ya Kiswahili imepiga hatua.
Ili kuipa riwaya ya Kiswahili, au riwaya yoyote ile, uamuzi unaostahili hatuna budi kuyapima maendeleo yake bila kuisahau historia yake fupi, tena ngumu. Hatuna budi kuvizamia vipengele vyake mbalimbali vinavyoiumba riwaya na kuona jinsi vilivyoathiriwa au kutoathiriwa na mabadiliko ya kihistoria. Pindi ikibainika kuwa mwenendo wa kijamii na kihistoria umeshindwa kuviathiri, na hivyo kutovibadili vipengele vya riwaya, hatutakuwa na budi tukubaliane na wale wanaodai kuwa riwaya ya Kiswahili haijaonyesha maendeleo. Katika kulistaamali suala hili, sura hii imeamua kukizamia kipengele cha wahusika waliotumika katika riwaya ya Kiswahili.
Tukichunguza kwa makini wahusika waliotumika katika riwaya ya Kiswahili, na hasa tukiwafuatilia wahusika wakuu, tunaweza kubaini kwa mshangao jinsi mhusika mkuu wa zamani alivyobadilika taratibu, lakini kwa kiasi kikubwa. Mhusika huyo alikuwa na nguvu za ajabu na ujasiri usio wa kawaida, na alitambuliwa kwa urahisi kutokana na sifa za uadilifu, nguvu na akili ambazo hazikuwa na mpaka; mhusika ambaye alikuwa na hali ya ajabu, nguvu za kimungu, majaribu magumu na aghalabu, hamu isiyovia ya kutimiza lengo lake. Mhusika huyu sasa nafasi yake inachukuliwa taratibu na mhusika mkuu mpya wa kisasa ambaye matendo yake na wasifu wake vinachukuana na hali ya kawaida (ya kila siku) ya maisha ya jamii, na ambaye matakwa yake na malengo yake, kwa namna fulani, yanaoana na kilio cha wakati huu cha walio wengi na kudhihirisha hofu na matumaini yao. Matakwa haya na malengo haya yanabainishwa kwa ufundi na mitindo ya kuachana ya kisanii na kwa itikadi mbalimbali. Mfano mzuri kabisa wa mhusika wa namna hii ni Fumo Liyongo.
Mhusika mkuu wa zamani alikuwa si halisi, mwenye sifa zisizo za kawaida, ambaye alisanifiwa na msanii kwa makusudi mazima ya kuumba mfano bora wa kuigwa, na aidha kumfanya awe kielelezo cha ukweli na ukamilifu wa maisha, na mwenye kupigania na kutetea mambo hayo pasipokuwa na dosari. Mhusika mkuu huyu wa zamani aliyatafakari maisha ya jamii kwa njia ya matendo makubwa na lugha teule. Mhusika huyu, ijapokuwa alijitokeza kuwa mtendaji mkuu kiasi hicho, lakini hakuwa na saikolojia wala hisia. Sifa hizi za upungufu wa saikolojia na hisia katika mhusika mkuu wa zamani ndizo zmazomtofautisha na mhusika mkuu wa kisasa. Mhusika huyo wa zamani anaweza kuitwa 'mhusika wa kitenzi' kwa sababu alijitokeza zaidi katika tenzi, ijapokuwa yumo pia katika hadithi za Fasihi-Simulizi.
Tofauti nyingine ya msingi ni ile inayohusu uhusiano kati ya mhusika mkuu huyo na wakati. Mhusika mkuu wa zamani, kama vile wa kwenye hadithi ya kifasihi-simulizi, alijitokeza kama mhusika mkuu wa wakati wote kutokana na jinsi alivyoumbwa na msanii wake ili kuuwakilisha ukweli mkamilifu, ukweli wa wakati wote. Kwa msanii wa namna hiyo ya wahusika, dhana za wakati na ukweli uliokamilika zilikuwa katika hali ya kutobadilikabadilika; wakati na ukweli vilikuwa ni vitu vilivyotulia pamoja. Kwa jinsi hiyo maandishi ya kisanii yaliyopewa jukumu la kuzibeba sifa hizo yalilengwa kuwa ni ya wakati wote, yasizeeke. Lakini, kinyume chake mhusika mkuu wa kisasa anayaona masuala ya wakati na ukweli uliokamilika kama ni masuala yasiyotulia, bali ni masuala ambayo yanabadilika pamoja na jamii. Na baadhi ya wasanii wa kisasa wanaona kuwa suala la ukweli uliokamilika, kwa kiasi kikubwa, ni ndoto iliyomo katika vichwa vya watu tu, na wala si katika maisha halisi. Mhusika rnkuu wa kisasa yuko katika wakati maalum wa kihistoria ambapo anayazamia maisha kwa undani na kuyatafakari.
Kufutika taratibu kwa mhusika mkuu wa zamani, au tuseme mabadiliko ya mhusika mkuu kutoka wa zamani kuelekea wa kisasa hayaanzi katika riwaya ya Kiswahili. Fox (1975:22) aliandika juu ya riwaya ya Ulaya akisema, “Kufutika kwa Mhusika Mkuu wa zamani kulimalizika katika karne ya 20... Lililobaki kwa msanii ni kumleta mtu (mhusika) katika nafsi hiyo ya riwayani ambaye atatoa picha kamilifu ya mtu, akionyesha kila hatua ya maendeleo ya mtu katika wakati wake maalum...”
Majaribu magumu ya Adili pamoja na mikasa yake ya ajabu katika Adili na Nduguze na masaibu ya kusikitisha ya mashahidi wa Karama katika Kufikirika ni mifano mizuri ya mhusika mkuu wa zamani katika riwaya ya Kiswahili. Ubapa wao unawafanya wawe ni vinyago au alama tu za mawazo. Lakini kadiri Shaaban Robert alivyozidi kuandika (k.m. Maisha Yangu, Siti binti Saad, Siku ya Watenzi Wote)ndivyo alivyozidi kuwapa wahusika wake sifa zinazokaribia au zinazoelekea katika hali halisi ya maisha. Hii ina maana kwamba mkabala wake ulizidi kuelekea katika hali ya kueleza ukweli kwa kutumia mbinu za kisanii ambazo hazikuitenga kazi ya sanaa kwa kiasi kikubwa na uyakinifu wa maisha. Hata hivyo, suala la msingi kwa Shaaban Robert pamoja na waandishi wengine waliotumia mtindo huo wa mhusika mkuu wa zamani ni kwamba ijapokuwa wahusika wanaojitokeza katika kazi zao wana sifa hiyo ya uzamani kifani, malengo yao na wajibu wao ni vipya, vikiakisi ukweli wa maisha ya wakati wa wasanii hao na kubainisha mfumo wa fikra zao pia. Hii inatokana na hali ya mabadiliko ya maisha pamoja na njia za kulitazama suala zima la mwanadamu na mazingira yake.
Katika wahusika wa Abdulla tunashuhudia tayari maendeleo makubwa katika uumbaji wa wahusika. Majaribio ya Shaaban Robert ya kuwaleta wahusika wake katika maisha ya kila siku yanapata kufikia hatua ya mwanzo ya kuridhisha kwa Mohammed S. Abdulla. Wahusika wa Abdulla wamechorwa vizuri kiasi kwamba picha yao inaingia barabara katika kichwa cha msomaji. Ni wahusika halisi, ijapokuwa bado wangali wakibainisha sifa mbili za mhusika wa zamani. Mosi, mhusika mkuu, Bwana Musa, ameumbwa juu ya wahusika wengine wote. Anawatawala, ijapokuwa si kwa wazi au si moja kwa moja. Hivyo Bwana Musa ana sifa ya ubabe, sifa ya kuwa kielelezo chenye ukamilifu, yaani kisicho na dosari. Pili, wahusika wengi wanabainisha mwenendo wa mlalo na si wima. Wamenyimwa na msanii kuendelea, hususan kiakili au kisaikilojia; sifa ambazo zingewawezesha kubadili mifumo yao ya fikra na utendaji wao. Hiyo inaonyesha jinsi wasivyopewa nafasi ya kutafakari. Wahusika wamefungiwa minyororo ya wajibu usiobadilika na kufanywa kuwa kama sehemu ya mashine inayofanya kazi ya aina moja tu daima dawamu. Wanabaki jinsi walivyo kutoka mwanzo wa riwaya hadi mwisho. Hii ina maana kuwa mpaka wakati wa Abdulla tunashuhudia, kwa kiasi kikubwa, mabadiliko ya jumlajumla tu ya wahusika, k.m. mabadiliko ya umbo, mavazi, chakula, 'sauti', n.k., lakini bila mabadiliko ya ndani, k.m. yale yanayohusu akili na maendeleo ya kisaikolojia. Hii ina maana kuwa mpaka wakati wa Abdulla hususan, kabla ya miaka ya sabini, riwaya ya Kiswahili ilikuwa bado haijaweza kumchora mhusika kisanii na kuweza kubainisha hali yake ya urudufu, yaani hali yake halisi.
Mabadiliko ya ndani ya mhusika katika riwaya ya Kiswahili yalianza hasa katika riwaya ya kwanza ya Kezilahabi, yaani Rosa Mistika na kuendelezwa na Mohammed Suleiman na yalifikia kiwango kikubwa katika kazi za S.A. Mohammed, na hasa katika Dunia Mti Mkavuna Nuru Katika Kiza. Riwaya ya Safari (Kabwela) na Shafi (Kuli) zinaelemea katika kiwango hiki kizuri. Na katika miaka ya themanini riwaya ya Nagona ya Kezilahabi imefanya jaribio la namna yake katika kuumba aina yake ya mhusika ambaye tutamwita mhusika jumui, yaani 'wengi' katika mmoja. Tukijaribu kuchunguza sifa za ndani za wahusika hawa, kama vile, maendeleo yao yakisaikolojia, kihisia, migogoro na mapambano yao katika wakati wao wa kihistoria na mahali pao walipo, ndipo tunaweza kugundua tofauti yao, upekee wao na umuhimu wao. Katika tafakuri zao za kibinafsi na katika miingiliano yao katikajamii wanadhihirisha maisha yenye ufahamu wa kupokea mawazo ya wengine, kuyakubali au kuyakataa kufuatana na uzito au wepesi wayo, wakitumia mwamko wao ambao uko katika viwango mbalimbali, kutokea kiwango cha chini hadi chajuu kabisa. Hii ina maana kuwa wahusika wanakua na kuongezeka (au kuendelea) wakiwa katikajamii zao; na katika akilizao unakua uwezo wa kufikiri na kuchagua, na kwa njia hii pia panastawi mantiki zao ambazo wanazitumia katika kuyatafakari masuala yanayohusu mazingira yao ya karibu na ya mbali. Uwezo wa mhusika wa kufikiri na kuchagua unaweza kuonyeshwa na hata kupimwa kwa hisia na fikra zake pamoja na matendo yake. Hisia, fikra na matendo kwa pamoja huweza kubainisha hali ya urudufu ya mhusika, kama vile nafasi yake katikajamii au masuala anayopendelea na kuyatetea. Ni katika hali hii ambapo wahusika hawa hawajitokezi kama masanamu tu yanayotenda kama mashine au vinyago visivyo na uhai ambavyo vimewekwa pale kama vipaza sauti vya mawazo yasiyochekechwa wala kuhakikiwa. Bali wahusika hawa ni wachunguzi, wenye hisia, wachaguzi, tena wanatumia mantiki. Baadhi yao ni wahakiki wakubwa wenye makini.
Sifa hizi ambazo zinawapa wahusika hawa wasifu wa binadamu halisi, zikiwaleta karibu kabisa na ukweli wa maisha katika mazingira, zinawavua kabisa lile joho la wahusika wa zamani. Hali ya sasa ya mazingira katika dunia imembana mhusika wa zamani na kumsukumia nje, na badala yake imemleta mhusika mpya. Kwa maneno mengine, hali ya riwaya ya kisasa imetengeneza maskani ambayo hayasadifu sifa za mhusika wa zamani. Riwaya ya sasa ya Kiswahili, ikiyakubali kwa utii madai ya janui ya sasa katika mazingira ya kisasa, inazidi kujitoa kutoka katika ile hali ya kuuchunguza ukweli wa maisha bila makini ya kutosha, yaani bila uyakinifu. Inajitahidi kupunguza masafa kati ya hali halisi katika jamii na msanii. Jitihada hii haikuifanya riwaya iwe na makini tu katika uchunguzi wake, bali pia kuwa mwamuzi bora wa yale yachunguzwayo. Kwa jinsi hii inawezekana hata kudai kuwa riwaya ya kisasa ya Kiswahili ina dalili ya kufumbata sifa za kisayansi.
Majadiliano haya, hata hivyo, yasifikiriwe kwamba yanadai kuwa mhusika mkuu wa zamani ametokomea kabisa. Mhusika huyo bado anajitokeza katika baadhi ya riwaya za kisasa za Kiswahili, na hasa katika riwaya zinazoitwa 'fasihi-pendwa' ambazo idadi yao kubwa ni kazi ya sanaa ya hali ya chini, hususan kimaudhui. Kwa yakini mtindo huu wa riwaya ni namna yenye upungufu wa kuutazama ukweli wa maisha, kwa sababu lengo lake ni kumfurahisha msomaji tu na kumstawisha msanii kiuchumi. Aidha ni mtindo unaosaidia kwa kiasi fulani kustawisha uhalifu kwa njia ya kuwafunulia wahalifu mbinu mpya za kufanyia shughuli zao. Idadi kubwa ya riwaya hizi inaweza kusemekana kuwa ni uigaji au uendelezaji wa mtindo wa kimagharibi wa riwaya za upelelezi za akina lan Flemming na Hadley Chase. Mtindo huu umekwisha kujijenga sana katika riwaya ya Kiswahili. Musiba akiwa ni mmoja wa waandishi wake bora. Na inaelekea kwamba mtindo huu tutazidi kuwa nao katika Fasihi ya Kiswahili kwa muda mrefu ujao kutokana na kuenea kwake kwa urahisi, na hasa miongoni mwa vijana. Aidha katika miaka ya themanini mtindo huu wa riwaya umetokea kuselelea. Kwa nini? Sababu kuu ni ya kiuchumi. Hata hivyo, suala hili linastahili sura ya pekee.
Sasa tutajaribu kuwaainisha wahusika wakuu kwa kadiri wanavyojitokeza katika riwaya ya Kiswahili. Hadi sasa kuna aina kama nne au tano hivi za wahusika wakuu katika riwaya ya Kiswahili tangu nyakati za Shaaban Robert hadi miaka ya themanini. Aina ya kwanza ni ile ambayo tunapenda kuiita 'mhusika mkwezwa' ambaye anapatikana katika riwaya za Shaaban Robert k.m. Kusadikika na Adili na Nduguze; katika riwaya ya Mhina ya Mtu ni Utu; katika riwaya za Abdulla na Musiba au katika riwaya pendwa kwa jumla. Sifa muhimu ni ile ya uwezo usio wa kawaida wa mhusika mkuu. Mhusika ameumbwa kama mfano bora wa kuigwa, mfano ulio mkamilifu. Katika harakati za kumwumba mhusika huyu msanii anaweza kuwa na lengo la kupigania jamii mpya kwa njia ya mhusika huyu. Hata hivyo wasanii wa mhusika huyu wana upungufu mmoja mkubwa. Wamejawa na taswira kubwa la kijamii lenye wasifu huo wa kijumla. Hawatambui kuwa mhusika hapaswi kuwa na wasifu wa jumla tu, kwa sababu mhusika huyo anawakilisha mtu halisi, na mtu halisi ana wasifu wa upekee usioweza kurudiwa, wasifu wa kijamii (wa kijumla) kwa sababu yeye ni kiumbejamii na wasifu wa kitabaka kwa kuwa yeye yuko katika kundi maalum la jamii, kwa hiari au kwa kulazimishwa.
Aina ya pili ya mhusika mkuu ni ile tunayoiita “mhusika wa kimapinduzi” ambaye anapatikana katika Ubeberu Utashindwa, Dunia Mti Mkavu, Kuli, na katika Mzalendo n.k. Mhusika huyu ambaye katika utu na utenzi wake anadhihirisha kuwa na mwamko mkubwa juu ya utu wake na utu wa jamii na ambaye kutokana na ufahamu mpana wa maisha anapigania mabadiliko ya kijamii, kiuchumi, kiutamadum na kisiasa katika kiwango cha kitaifa na kimataifa. Ni aina mpya ya mhusika katika riwaya ya Kiswahili ambayo imejitokeza hasa hasa katika muwongo wa katikati wa miaka ya sabini. Dalili hafifu za mhusika huyu zilianza kuonekana katika mhusika mkuu wa Shaaban Robert, k.m. katika Kusadikika ambamo maudhui yake yanalenga kulijenga taifa kwa njia ya mahusiano ya kimataifa. Wale mashahidi sita wa Karama wanasafiri katika nchi mbalimbali za dunia ili kupata maarifa mapya yatakayosaidia kuijenga na kuiendeleza nchi yao. Na katika Siku ya Watenzi Wote maudhui yanahimiza kuanzishwa kwa fungamano la kidini la ulimwengu mzima ambalo kwalo watu watajisikia kuwa kitu kimoja. Ijapokuwa imekwishaelezwa kuwa wahusika wa Shaaban Robert kimsingi ni wakwezwa, lakini kuna mwingiliano baina ya aina za wahusika kama ilivyogusiwa mwishoni mwa sura hii.
Mhusika mkuu wa kimapinduzi ana itikadi inayowaelekea watu wengi, asiye na hamasa inayozidi kiasi na ana mbinu zinazokubalika katika kulikabili tatizo. Katika utu wao wasifu wa 'utatu' (urudufu) unajionyesha vema katika migogoro yao ya binafsi na ya kijamii katika maisha ya kila siku. Ni hali hii ya utatu katika wasifu wa utu wao ndiyo inayowatofautisha na aina ya kwanza ya wahusika. Na hali hii ya utatu katika utu wa mhusika ndiyo inayompambanua mhusika aliyechorwa vizuri. Kwa maneno mengine tunataka kusema kwamba kuchorwa vizuri kwa mhusika siyo tu maelezo mazuri na fasaha ya umbo la nje la mhusika au pamoja na vitabia vyake fulani kama ilivyo katika Mzimu wa Watu wa Kale au Duniani Kuna Watu. Kwa sababu pamoja na ufundi huo wa uchoraji, mhusika anaweza kuwa amejitokeza sehemu moja au mbili tu za utatu wa sifa, na hivyo akawa si mwakilishi aliyekamilika wa hali halisi katika maisha halisi.
Lakini hebu tujiulize, kwa nini 'mhusika wa kimapinduzi' anajitokeza kwa nguvu katika miaka ya sabini? Jibu linaloshawishi ni kwamba mhusika huyu ni matokeo ya hali halisi ya kimapinduzi (kifikra) ambayo imejitokeza katika miaka ya sabini katika karibu eneo zima la kusini mwa Afrika, na hasa katika uga wa kisiasa. Kuchanuka na kupamba moto kwa vyama vya wapigania; uhuru na mapambano ya msituni vilifikia kilele cha mwanzo cha ushindi wakati Msumbiji (1975), Angola (1975) na Zimbabwe (1980) zilipojinyakulia uhuru wao wa kisiasa. Mapambano dhidi ya siasa ya kibaguzi ya Afrika Kusini na mapambano ya kupigania uhuru huko Namibia yaliingia katika hatua mpya, huku yakiwatia hamasa mpya wapiganaji na wale wanaowaunga mkono. Hali hii ilisababishwa kwa kiasi kikubwa na fikra za ki-Marx ambazo zinaweza kusemwa kuwa zilifikia hali yajuu katika eneo hili la kusini mwa Afrika katika muwongo wa katikati wa miaka ya sabini. U-Marx, likiwa kama somo mojawapo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pamoja na maandishi mengine yaliyokuwa na mwelekeo huo (U-mao, U-Kim Il Sung, Nkrumah, Nyerere, Ujamaa, n.k.) viliiathiri moja kwa moja Fasihi ya Kiswahili na matokeo yake ya mwanzo katika kazi za nathari yakawa kama vile Ubeberu Utashindwa na baadaye kazi za Shafi, Senkoro, Mohamed, Kezilahabi, Saffari na wengineo. Na uhakiki wa Fasihi ya Kiswahili ulilazimika kuchukua mwelekeo huu mpya. Kwa jinsi hiyo 'mhusika wa kimapinduzi' katika riwaya ya Kiswahili ya miaka ya sabini si tokeo la bahati nasibu, bali ni tokeo lililokuja na kimbunga cha mabadiliko ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni cha wakati huo katika kusini mwa Afrika. Riwaya hii ya kimapinduzi, ilikuwa imefanguliwa, na hata kutiwa ari, na mashairi ya kimapinduzi (k.m. katika Mashairi ya Kisasa: 1973 na Malenga wa Bara: 1976 yaliyoandikwa na Mulokozi na Kahigi) na ilijaribu kumchora mhusika wa kimapinduzi ambaye aliwahurumia wanyonge wa ulimwengu na kutafuta mbinu za kuwasaidia. Hii ilifanywa hasa kwa kutumia mbinu za kisiasa. Lugha pamoja na tamathali zilizotumika zilielekea katika siasa. Mkondo huu wa riwaya 'ya kisiasa' ulizidi sana katika miaka ya sabini hata kufikia kiasi cha kuwachusha wasomaji. Hicho kikawa ni kisingizio cha pili kikitanguliwa na sababu ya kiuchumi kuukaribisha mkondo wa riwaya pendwa katika mawanda ya upelelezi uliotanguliwa na uhalifu wa hali ya kuachana na mapenzi. Lakini kwa vyovyote vile hali halisi ya miaka ya sabini inatetewa kuwa iliisadifu riwaya ya kisiasa iliyojitokeza hata kama riwaya hiyo ilikuwa na upungufu wa kifani na kimaudhui.
Papo hapo ni muhimu kufahamu kuwa haya mawazo ya ki-Marx pamoja na mwamko wake wa kimapinduzi katika miaka ya sabini katika Tanzania yalimilikiwa hasa na vyuo, sekondari (hasa vidato vya V na VI) na taasisi za juu za taaluma. Hii inamaanisha kuwa mhusika mkuu huyu mpya wa kimapinduzi hajajifunua na kueleweka na idadi kubwa ya wasomaji, na hasa nje ya taasisi hizo za kitaalam.
Riwaya ya mkondo wa 'kidhanaishi' ambayo mwakilishi wake mkuu ni Kezilahabi ina mhusika ambaye nanma yake inakuwa kama ya mhusika wa kimapinduzi, lakini tofauti yao ya msingi ni namna mhusika wa kidhanaishi asivyo na suluhu sahihi za kupambana dhidi ya matatizo ya maisha. Hata hivyo mkabala wake tata dhidi ya matatizo haumwondolei moja kwa moja sifa yake ya kimaendeleo ambayo ni namna anavyofaulu kuyaweka wazi matatizo ya jamii, licha ya utata katika kutafuta suluhisho bayana. Kwa jinsi hii, mhusika huyu angeweza kuitwa ni mhusika wa 'kimaendeleo' ijapokuwa jina hili lingekuwa ni la jumla mno.
Hali kadhalika katika miaka ya sabini pametokea tena aina nyingine ya mhusika mkuu aliye na sifa ya kipekeepekee ya unyonge na kukata tamaa kwa upande nunoja; na kwa upande mwingine ni mhusika anayetia huruma kutokana na masaibu mbalimbali ya mazingira yanayomfika. Mhusika huyu tutamwita “mhusika wa kisaikolojia”. Mhusika wa aina hii ameletwa katika Fasihi ya Kiswahili ya kisasa na Mohammed Suleiman katika riwaya zake za Kiu na Nyota ya Rehema. Mhusika huyu mkuu ni mnyonge kimwili, na kiakili ana ufahamu usio mpana ambao haumsaidii vya kutosha. Aidha amenyimwa hata upendo kutoka kwa jamii yake na hapati matunzo muwafaka kutoka kwa jamaa zake. Kwa maneno mengine, katika sehemu kubwa ya maisha yake, amezongomezwa katika lindi la ukiwa na kutojitegemea. Na ijapokuwa yuko katika hali hii duni ya kiutu, anaonyesha hali hafifu ya kujitetea dhidi ya wakandamiziwake. Lakini tukimchunguza kihistoria, tunaona kwamba ni mhusika anayebeba funzo zito kwa msomaji; anaonyesha matatizo ya kihistoria ya jamii ya Zanzibar wakati wa umwinyi na usultani, wa wakati wa majilio ya ubepari wa mijini. Kwa hakika msanii (Mohammed Suleiman) hakumwumba kwa bahati nasibu tu mhusika mkuu huyu na hasa akiwa mwanamke kama ndiyo alama ya unyonge na unyenyekevu katika kipindi hicho cha umwinyi, kwa sababu kipindi hicho kilikuwa ni cha giza, mateso na maonevu kwa wenyeji wa Unguja kwajumla, na mwanamke ndiye aliyebeba uzito mkubwa zaidi wa matatizo hayo. Ni kwa sababu hii pia riwaya za Mohamed Suleiman ni mifano mizuriya riwaya ya istiara (allegorical novel).
Wahusika hawa wa Mohamed Suleiman wanadhihirisha hali ya kuendelea kubadilika kw'a mhusika mkuu na wahusika wengine kwa jumla katika riwaya ya Kiswahili, iwe ya visiwani au bara. Jambo gani linaweza kueleza mabadiliko haya (na hata ya fam, tanzu, muundo, n.k.)? Mwanafasihi mmoja, Lichatschow (1975:158) aliandika kwamba sababu hasa ya msingi ni ile inayotokana na kupatikana kwa wajibu mpya wa Fasihi kutoka kipindi hadi kipindi ambao unasababishwa na mabadiliko ya ukweli wa maisha na hasa mahusiano ya kijamii.
Katika miaka ya themanini amejitokeza mhusika mwingine wa namna yake ambaye tumemgusia hapo nyuma. Huyu ni wa aina ya mhusika jumui, yaani ni wahusika wengi katika mmoja. Tunaweza kumwita pia ni mhusika 'mwakilishi' ijapokuwa dhana hii haitabainisha uwingi uliomo katika 'mhusika' huyu. Mhusika huyu ameletwa na Kezilahabi katika riwaya yake ya Nagona. Riwaya hii fupi lakini tata kuliko riwaya zote ambazo ziko katika Fasihi ya Kiswahili mpaka sasa ni zao la kifasihi ambalo linaweza kusemekana kuwa linatokana na 'visasili' mamboleo ambavyo vinaonyesha kifalsafa maendeleo ya mzunguko ambao mwanadamu anafanya pasipo kuweza kufika katikati ya mzunguko huo ambapo pana ukweli wa maisha, kwani kufika hapo katikati kunakomesha kufikiri. Na riwaya hii ni jaribio la nadharia ya msanii ya kutaka kuiangalia falsafa ya Mwafrika katika dunia ya leo katika jicho la kifasihi. Nadharia ya (au za) msanii juu ya falsafa ya Kiafrika ina lengo la kuiumba fasihi mpya ya Kiafrika ambayo inajitoa kutoka katika mstari wa fikra wa kimagharibi. Lakini jaribio hilo huenda likawezekana katika mawazo ya mtu kichwani mwake tu, kwaai katika hali halisi jaribio hilo ni gumu, na yaelekea haliwezekani. Riwaya ya Nagona haionyeshi upekee wowote wa falsafa ya Kiafrika wala upya wowote katika Fasihiya kisasa kwa sababu inaeleza matatizo ya dunia yaliyozushwa na mchangamano wa mataifa ulimwenguni; elimu ya kweli ya utatuzi wake haijapatikana bado, na pengine haitapatikana kwa muda mrefu ujao kama ambavyo riwaya ya Nagona inavyoelekea kusisitiza. Kwa namna fulani riwaya hii ina mhusika wa 'kidhanaishi', na riwaya yenyewe ni hatua ya juu kabisa ya riwaya ya kidhanaishi. Katika Fasihi ya Kiswahili mwanzilishi wa riwaya ya kidhanaishi ni Kezilahabi na ni yeye aliyeihitimisha, kwa sababu inaelekea mkondo huu wa riwaya hautapata kilele kingine tena zaidi ya Nagona. Nagona si riwaya ya pekee katika fasihi ya kisasa kwani inalingana sana kimtindo na kimuundo na riwaya ya Christa Wolf iitwayo Cassandra inayotumia 'visasili' mamboleo kuelezea maangamizi ya maendeleo ya mwanadamu kwa njia ya mwanadamu, na tamathali yake kuu inajijenga katika maendeleo yaliyoangamizwa ya kiyunani.
Mjadala huu kuhusu wahusika na aina zao na jinsi walivyotokea na namna wanavyoendelea kubadilika katika riwaya ya Kiswahili unaweza kutazamwa vingine na wataalam wengine wa fasihi ya Kiswahili. Ohly (1982:82) anadai kuwa uumbaji wa wahusika katika hwaya ya Kiswahili umeathiriwa na uhusiano wa waandishi na watu wa chini (au tabaka la chini) na umeleteleza mtu wa aina ya pekee aitwaye “African Homo Luden” pamoja na upungufu wake, kama vile mtu aliyetaka kucheza kamari ijapokuwa hajui vizuri kucheza kamari. Lakini mtazamo huo wenye bezo na kejeli ambao unaitazama liwaya ya Kiswahili kama kitu kilichotuama mahali pamoja katika uduni na 'ushenzi' ni mtazamo wa mhakiki anayeitazama fasihi hii kutoka mbali na bila makini, akiwa nje ya mipaka, hasa ya kihistoria na kiujumi ya fasihi hh.
Hata hivyo lazima ikubalike kuwa mjadala huu wa kuainisha wahusika unawezekana zaidi kinadharia tu, kwani katika hali halisi aina hizi za wahusika, kama vile aina za mikondo, zipo katika hali ya kuingiliana na kuchangamana. Na inahitaji uchunguzi wa makini ili kuona tofauti zao na mabadiliko yao. Na panahitajika muda mrefu hadi aina moja ya mhusika kufutika kutoka katika jamii. Riwaya ya Kiswahili ilianza kupata mashiko baada ya kazi za Shaaban Robert kujitokeza hasa kwenye miaka ya hamsini. Hii ni baada ya yeye kuandika kitabu chake cha Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini na kama alivyosema Ohly (1981:13) kazi hii ilionyesha maendeleo ya riwaya ya Kiswahili kuelekea kwenye uandishi wa kisasa wa riwaya. Riwaya zake nyingine kama vile Kusadikika (1951), Kufikirika (1957) na Adili na Nduguze (1952) zilikuwa na mchango mkubwa sana na baadaye kuzaa riwaya zenye kuusogelea zaidi uandishi wa kisasa wa riwaya. Riwaya zake kama vile Siku ya Watenzi Wote (1968) na Utubora Mkulima (1968) zilionyesha mabadiliko makubwa katika historia ya uandishi wa riwaya ya Kiswahili. Badala ya kuwa ni hadithi za kinjozi Shaaban Robert, na baadaye waandishi wengine kama vile Nkwera na Mhina, walianza kutunga hadithi ambazo ziliisogelea jamii zaidi na kutoa taswira ya maisha ya watu halisi. Wahusika katika liwaya walianza kuonekana zaidi kuwa ni watu badala ya wanyama au majini. Dhamira za riwaya za Kiswahili zilianza kujengwa kutokana na maisha halisi ya jamii na zikawa na maudhui, visa na miundo ambayo ilionyesha kupevuka kwa riwaya.
Kati ya mwaka 1960 na 1970 historia ya riwaya ya Kiswahili ilikuwa katika hali ya kusimama. Wakati ushairi ulikuwa ukiendelea waandishi wa riwaya hawakujitokeza sana katika kipindi hiki. Riwaya chache zilizoandikwa zilikuwa ni Alipanda Upepo na Kuvuna Tufani (1969), Kuishi Kwingi ni Kuona Mengi. (1968), Mzimu wa Watu wa Kale (1960), Kurwa na Doto (1960), Ufunguo Wenye Hazina(1969), Lila na Fila (1966), Simu ya Kifo (1965), Mzishi wa Baba ana Radhi (1971), na riwaya zingine fupi. Sababu kubwa inaweza kuwa msisitizo mkubwa uliowekwa kwenye fasihi ya Kiingereza. Katika mashule Kiswahili hakikupewa nafasi ya kutosha kuweza kuwahamasisha waandishi wachanga katika Afrika Mashariki.
Riwaya zilizoandikwa kwa lugha nyingine na kisha kutafsiriwa kwa Kiswahili zilikuwa na nafasi kubwa katika historia na maendeleo ya riwaya ya Kiswahili Kama vile fasihi simulizi ilivyokuwa muhimu katika kuiendeleza historia hiyo, riwaya ambazo zilitafsiriwa zilikuwa na nafasi kubwa katika kuwahamasisha waandishi wachanga na vile vile wasomaji wa riwaya. Mkusanyiko wa fasihi-simulizi na hadithi kama vile Mashimo ya Mfalme Suleiaman, Mazungumzo ya Alfu Lela-U-lela, Kisima Chenye Hazina, Hekaya za Abunuasi na nyingine zilikuwa maarufu sana. Kama vile hadithi za Kiswahili zilizokusanywa kutoka kwenye simulizi za wenyeji riwaya hizi hazikuwa zimekitwa kwenye maisha halisi ya wenyeji. Hizi zilikuwa hadithi za kigeni ambazo zilikuwa na wahusika ambao mara nyingi hawakushabihiana kwa dhati na wale ambao wangeitwa 'wahusika halisi', wale ambao wametokana na jamii yenyewe. Zilikuwa ni riwaya zenye mandhari ya kigeni (ya Kiarabu/Kizungu) lakini maadili yake yalielekea kukubalika katikajamii. Hata hivyo, tofauti na hadithi fupi za Kiswahili ambazo zilitokana na masimulizi ya jamii, riwaya hizi za tafsiri zilikuwa zimezingatia misingi mingi ya riwaya za kisasa kama vile wahusika, dhamira, visa na kadhalika. Hivyo basi, riwaya za tafsiri zilikuwa zimepevuka zaidi na zilikuwa ni mfano bora wa kuigwa na waandishi wachanga wa mwanzo kama vile akina Shaaban Robert.
Kipindi cha mwaka 1960-1970 kilikuwa ndicho kipindi cha msingi baada ya uhuru. Kilikuwa ni kipindi cha msingi hasa kwa vile waandishi wengi wa wakati huu walikuwa wameishi maisha ya aina mbili. Moja ikiwa ni maisha wakati wa ukoloni ambapo waliweza kushuhudia madhila ya wakoloni na wazalendo waliotayarishwa ili kushika hatamu baada ya uhuru. Aina ya pili ilikuwa ni kushuhudia maisha baada ya uhuru ambapo shughuli nyingi ziliendeshwa na wazalendo. Kwa hali hii waliweza kuwa wawakilishi na waelezaji wa mwisho wa kipindi kimoja na mwanzo wa kipindi kingine. Hali hii ilikuwa ni matayarisho mazuri kwenye maendeleo ya historia ya Kiswahili baada ya mwaka 1970.
Baada ya mwaka 1970 historia ya riwaya ya Kiswahili ilisemekana kuwa moja ya fasihi maarufu katika bara la Afrika ya Tropiki. Sheglov (1976) aliyasema maneno haya akizingatia ukuaji wa fasihi hiyo. Katika kipindi hiki riwaya ya Kiswahili ilijitokeza sana katika ulimwengu wa fasihi kwa sababu zifuatazo. Sababu ya kwanza ilikuwa ni kukua kwa idadi ya watu wanaojua kusoma na kuandika katika Afrika Mashariki. Baada ya uhuru idadi kubwa ya kizazi kipya ilikuwa imepata nafasi ya kwenda shule na hivyo kuwa ni wateja wa kutarajiwa wa kusoma riwaya. Sababu ya pili ilikuwa kwamba Kiswahili, hasa katika Tanzania baada ya Uhuru, kilitiliwa mkazo sana katika shule na kikawa somo muhimu. Hali hh ilichangia zaidi katika kuikuza sababu ya kwanza. Sababu ya tatu na ambayo imejengwa zaidi na sababu ya kwanza na ya pili, ni kwamba waandishi wachanga walijawa na nia na shauku ya kuyaelezea matatizo ya wanajamii kwajinsi walivyoyaona.
Kipindi hiki, ambacho kimeonyesha kwa undani migongano na fujo zilizokuwepo katika jamii, kilitofautiana sana na vipindi vingine vya awali. Mojawapo ya tofauti hizo ni kwamba waandishi wengi wa kipindi hiki walikuwa watu ambao walizaliwa wakati wa ukoloni na hivyo kuwa mashahidi wa kipindi cha mwisho cha utawala dhalimu. Vilevile waandishi hao walikua wakati nchi nyingi za Afrika zinapata uhuru na hivyo kuona mafanikio na kasoro za uhuru kwa kipindi cha miaka kumi hivi. Ujuzi na mlinganisho wa yale waliyoyaona katika pande zote hizi tofauti ulikuwa ni amali na mchango mkubwa sana kwa fasihi ya Kiswahili. Zaidi ya yote hayo kipindi hiki kilionyesha mabadiliko katika mtazamo wa maisha na utamaduni wa jamii za Afrika Mashariki. Badala ya kujikita katika mila na desturi za kigeni au mawazo ya kinjozi, riwaya ya Kiswahili ilizingatia maisha halisi na kukosoa mila na desturi za kigeni wakati msisitizo wa mila na desturi za wenyeji ulijitokeza zaidi. Kazi nyingi zilizotoka wakati huu zilikuwa na mawanda mapana zaidi, ziliangalia maisha kwa jicho la nchi na sio sehemu au kabila. Mandhari, wahusika na mtiririko wa hadithi vilikwenda kutoka sehemu moja ya nchi hadi nyingine na kuhusisha watu wa makabila tofauti. Nyanja na aina tofauti za maisha ya binadamu zilitumika katika kujenga visa na dhamira kuu.
Kipindi cha mwaka 1970-1980 ndicho tunachoweza kusema kilionyesha kukomaa kwa riwaya ya Kiswahili. Riwaya zilizopevuka na makini zilijitokeza. Waandishi mashuhuri kama vile Kezilahabi, Said Ahmed Mohamed, Shafi Adam Shafi na wengine wengi waliandika riwaya ambazo zilivutia wahakiki wengi nje na ndani ya Afrika Mashariki. Aghalabu kazi nyingi zilijizatiti na kuzingatia kikamilifu nafasi ya vijana katika dunia ya wakati huo pamoja na uhusiano wao na kizazi kilichowatangulia. Kwa ujumla kilikuwa ni kipindi cha kuielimishajamii kuhusu utamaduni na siasa yao. Kama itakavyojitokeza katika kuzingatia dhamira na wahusika huko mbele kipindi hiki kilidhihirisha utajiri wa riwaya ya Kiswahili kuliko kipindi kingine kile katika historia ya riwaya ya Kiswahili.
Powered by Blogger.