HISTORIA YA MUZIKI WA HIP HOP NA BONGO FLEVA NA JINSI UNAVYOONEKANA KUATHIRIWA ZAIDI NA WASHAIRI WA KIMAPOKEO KULIKO WANAUSASA
Suala lingine ambalo
linasisitizwa na wanajadi ni uwepo wa kituo katika shairi. Abedi (kashatajwa
uk.4) anatueleza kuwa, kituo ni mstari wa mwisho wa kila ubeti. Anaendelea
kufafanua kuwa, kutuo huweza kuwa ama kiini cha habari au kimalizio. Maana hii
ya kituo haipishani sana na maana inayotolewa na Wamitila (2003:93) isipokuwa
anaongezea kuwa, wahakiki wengi hukiita kitua kuwa ni kibwagizo. Wasanii wa Hip
Hop na Bongo Fleva hupenda kutumia istilahi ya kiitikio. Kwa wanajadi kila
baada ya ubeti kama ubeti utakuwa na mistari mine basi mstari wanne ndiyo huwa
kiitikio/kituo, na kwa upande wa mashairi ya Hip Hop na Bongo Fleva huwa na
kituo yaani kiitikio isipokuwa wao hawana mstari maalumu ambao unapaswa kituo
kiwepo isipokuwa kituo/kiitikio huwekwa mara baada ya kukamilika kwa kila
ubeti. Hebu rejea mfano wa wimbo wa Profesa Jay wa Kubwa Kuliko anatumia
kiitikio kifuatacho kila baada ya kukamilika kwa ubeti.
Ninaposema jay kubwa
kuliko,
Siko niliko ndiko liko
zinduko,
Ninaposema jay kubwa
kuliko
Wakati
mwingine kiitikio si lazima kifuate kila baada ya ubeti kwisha, wapo wasanii
wengine ambao hutumia fomula ya kuanza na kiitikio kikifuatiwa na ubeti,
kiitikio ubeti kiitikio, rejea mfano wa Diamond Platznum wimbo wa Kesho,
msanii ameanza na kiitikio ndiyo ubeti unafuata (rejea mfano wetu wa wimbo huo
tulioutoa hapo awali, pia rejea shairi la Joh Makini Najiona Mimi naye kiitikio
kinajitokeza kila baada ya ubeti).
Abeid
(keshatajwa) anatueleza kuwa katika mashairi ya wanajadi, kituo/kiitikio
kinaweza kubadilika badilika, hali hii pia hujitokeza katika mashairi ya
wanamuziki wa Hip Hop na Bongo Fleva, mfano katika shairi la wimbo wa Profesa
Jay Ndiyo Mzee tunaona kiitikio cha ubeti wa kwanza
kinatofautiana na kiitikio cha ubeti wa pili. Kwa mfano ubeti wa kwanza
anatumia kiitikio kifuatacho;
Si
mtafurahi Watanzania jamani? (ndiyo mzee)
Si ni
kweli nakubalika jamani? (ndiyo mzee)
Basi
mimi ni mkombozi wenu jamani (ndiyo mzee)...
Wakati
katika ubeti wa mwisho anatumia kiitikio kingine na kinaimbwa na mtu mwingine
(Juma Nature) anasema;
Je
wananchi mmenisikia? (ndiyo mzee)
Kuwa
huyu jamaa hatufai (ndiyo mzee)
Na
inafaa kumchukia (ndiyo mzee)
Hatumtaki
aondoke zake (ndiyo mzee)
Jambo
lingine linalosisitizwa na mwanajadi katika mashairi ya kimapokeo ni
kujitosheleza kwa kila ubeti. Abedi (kashatajwa,uk.4) anaona utoshelevu ni
kipengele cha msingi katika shairi, anasema kuwa, kila ubeti ujitosheleze
kadiri iwezekanavyo, yaani, uwe na maana kamili, na usingoje kutimizwa na ubeti
mwingine. Jambo hili pia linajitokeza katika mashairi ya wasanii wa Hip Hop
na Bongo Fleva kila ubeti katika nyimbo zao huwa na maana
inayojitosheleza. Ukiangalia mifano ya nyimbo tulizozitumia hapo juu
ukichunguza kila ubeti utaona kuwa ubeti unajitosheleza na unatoa maana kamili.
Labda kwa mfano mzuri tutumie wimbo wa msanii Jay Mo unaoitwa Story
tatu Tofauti, katika wimbo huu kila ubeti umebeba kisa chake tofauti
ambacho kimekamilika na unatoa maana, hebu hapa tuangalia ubeti wa tatu.
Mariam alikuwa mtoto
aliyekuwa na uzuri wa peke yake,
Mi mwenyewe mmojawapo
kati ya waliotaka ajiweke,
Ili anione mchumba wake,
Alisimama peke yake,
alilinga kwa uzuri wake,
Tajiri familia yake, kama
hanyi au hali,
Kwa jinsi alivyojisikia,
na vile home kuna mali,
Kiburi alijijengea, hali
iliyofanya wengi waliomjua kumchukia,
Tuliosoma naye hiyo tabia
tulishaizoea,
Wazazi walisoma ndiyo
maana maisha yao ya juu,
Yeye hilo hakuliona cha
maana alichoona ni usister duu,
Pesa zikamtia udhaifu, za
nyumbani akaona hazitoshi,
Shuleni akacheza rafu,
masomo akashindwa pasi,
Alipata zero kitu ambacho
wazazi hawakuamini,
Angekuwa mtoto wa kiume
wangeshamfukuza nyumbani,
Wakaona siyo mbaya kama
atarudia mtihani,
Kitu ambacho mariam
hakikumuingia akilini,
Wakamuuliza anachotaka,
akajibu computer,
Cheti akapata kwenye
stashahada akachemsha,
Baada ya kupewa ujauzito,
inasemekana na kizito,
Ambaye ana mke na pia
nyumbani ana watoto,
Cha moto kikaanza
nyumbani alipofukuzwa,
Kumbe yule kizito ana
ngoma anafanya kuusambaza,
Hakumsikiliza Jose Mtambo
alipoimba kizaazaa,
Yamemwaribikia mambo na
mtoto bado hajazaa.
Katika
ubeti huu, utaona kuwa umebeba kisa kizima kinachojitosheleza na ukisikiliza
ubeti wa kwanza na wa tatu utaona kuwa kila ubeti una kisa chake
kinachojitosheleza na kinachotoa maana iliyokamilika wala ahitaji ubeti
mwingine ukamilishe wazo au maana ya shairi. Katika ubeti huu wa tatu msanii
anaelezea tabia za Mariam, kutowasikiliza wazazi wake, kutozingatia elimu na
kujikuta akipewa mimba na kuambukizwa virusi vya ukimwi.
Hitimisho.
Wasanii wa muziki wa
kizazi kipya yaani Bongo Fleva na Hip Hop kama wamechota baadhi ya sifa katika
ushairi wa kimapokeo katika kutunga mashairi. Kipengele kikubwa ambacho
wana-Hip Hop na Bongo Fleva wanaonekana kuathiriwa nacho ni kipengele cha
matumizi ya vina katika tungo zao ambacho hasa wanajadi ndiyo wanaona kuwa ni
roho ya ushairi. Lakini pamoja na hayo, pia usasa katika mashairi yao
unajitokeza kwa kiasi fulani, kwa mfano yapo mashairi ya wasanii wa muziki huu
ambayo hayazingatii vina lakini yanaimbika. Pia kutokuwa na idadi maalumu ya
mistari katika beti za mashairi yao pia ni sifa za usasa katika utungaji wa
mashairi.. Kwa ujumla hatuweza kusema wazi kuwa wanajadi ndiyo wamewaathiri
wasanii wa Hip Hop na Bongo Fleva au la kwani ni jambo linalohitaji utafiti wa
kina na mjadala mpana, tukiangalia hata namna muziki huu ulivyoingia nchini kwa
kuiga nyimbo za wasanii wa Marekani na Ulaya ambazo nazo zinaonekana kuzingatia
matumizi ya vina, vituo, kujitosheleza n.k. huenda wasanii hao ndiyo
waliowaathiri zaidi. Lakini kwa mujibu wa mjadala wetu tunasema uwepo wa nduni
za kijadi katika mashairi ya Hip Hop na Bongo Fleva hususani kipengele cha vina
washairi hawa inaonekana na hapa tunasisitiza kuwa inaonekana kama wameathiriwa
na wana jadi kwa kuwa jambo kubwa linalosisitizwa na wanajadi ni matumizi ya
vina na mizani ambayo hata wana Hip Hop na Bongo Fleva nao husisitiza matumizi
hayo kama tulivyoona hapo awali.
>>>>>>>>INAENDELEA>>>>>>>>>>>>