Riwaya mpya ya Kiswahili


 Kuhusu suala hili Mohamed, katika Babu Alipofufuka (uk.10) anatuambia: [S]iku hizi K, kinyinginya changu, anaweza kuketi meza moja na watu ambao miaka michache iliyopita ilikuwa mwiko kukaa nao. Mazimwi, aliwaita. Akatangaza vita nao kwa kusaidiwa na nyuki... Kwa waandishi hawa, kuwakaribisha mabeberu, bila au kwa viwango vilivyopo vya malipo ya uwekezaji ili kuchukua rasilimali za nchi zetu na kutumia jasho la watu wetu, ni ujinga usiokuwa na mfano. Mohamed katika Babu Alipofufuka (uk.13-14) akiwaelezea wahusika wake wa kigeni anathibitisha tena ujinga huu kwa maneno haya: [I]nasemekana Delpiero karibuni amemeza eneo zima la ardhi la pahala fulani tumboni mwake. Wavuvi waliposimama kidete kupuliza cheche zao za uchungu, K alikuja juu kuwaambia wastarehee neema zao... Miyazawa aliyetoka kwao juzijuzi na kuwa mwenyeji kuliko wenyeji, haonekani na mtu yeyote kuwa na kazi ya maana nchini humo ila sifa zake za mkonowazi... Naye Von Heim, ana nia kubwa ya kusaidia kumfufua maiti kwa kummiminia bia kutokana na tangi lake kubwa... Tena kulikuwa na Di Livio ambaye kaja huku kucheza kamari. Halali mchana wala usiku; yumo mbioni vilabuni, mabasini, mandarini, hotelini... Kusema kweli, ujinga wetu hauko katika kukubali kuibiwa tu rasilimali zetu, bali pia kukubali kupokea vibovu na vichafu kwa thamani kubwa. Wamitila (keshatajwa) anaiendeleza fikra hii kwa maneno haya: “Hiki ni kiwanda.” “Cha nini?” “Reconditioned cars.” “Mnazitumia?” “Ahh, deki masen! Haiwezekani asilani. Sheria zetu zinakataza matumizi ya magari hayo.” “Basi mnayetengenezea nini?” “Kuna soko kubwa huko upande wa chini. Huko ndiko tunakotupa tusivyovihitaji.” “Mnavitupa ehh?” “Mmm, ni hivi tuseme, wanakubali wenyewe; ...” Kauli kali kabisa ya uhakiki na mkemeo wa waandishi hawa kuhusu ujinga wetu unapatikana katika mswada wa riwaya ya Mohamed, Dunia Yao (38), kauli ambayo inathibitisha jinsi gani tulivyotoa nafasi kutawaliwa, kwa kuogopa kutopata ruzuku au kwa kutarajia uokovu kutokana na utandawazi: Wamechukua kila kitu: niliendelea; wao wamekuwa ndio wafikiri wetu, wasemaji wetu, wanaohisi kwa ajili yetu, wanaoona njaa na kiu zetu, walimu, madakitari, wanafalsafa, wanauchumi, mashehe, mapadre, walinzi wetu ... kwa ujumla waendesha maisha yetu yote; sehemu ya viwiliwili na akili zetu ... kwa ufupi wao ni kila kitu! Sisi wengine ni mapipa matupu. Hatuna rojo la uhai: Hatuna supu ya maisha wala nyama ya ubinadamu wetu. Hatuna sehemu ya utu. Hatuna rai. Hatuna maoni. Hatuna chetu. Hatuwezi kufikiri kama wao au zaidi ya wao. Hatutarajiwi kusema. Hatutarajiwi kushiriki hata mambo yanayohusu nafsi zetu. Chambilecho Fowles... Kuna mtazamo fulani wa kisasa katika dunia yetu kwamba falsafa waachiwe wanafalsafa, elimujamii iwe bahari ya kuogelewa na wanaelimujamii na kifo kwa maiti. Lugha hii ya uhakiki na mkemeo kwa utandawazi inakita katika kauli, picha na jazanda zinazojenga kejeli au tashititi. Katika matumizi ya lugha ya namna hii waandishi hawa wanatoa dalili ya ujinga wa jamii na uongozi wao na uchungu walionao kwa ujinga huo unaotendeka –dalili ambazo zinaweza kupewa tafsiri tofauti miongoni mwa wasomaji. Kwa mfano, haifahamiki nani kaelekezwa nalo dondoo hilo hapo juu: utawala wetu wa ndani? Makuadi wa soko huria? Ukoloni mamboleo? Wakoloni mamboleo wenyewe? Utandawazi au waasisi wa utandawazi na vyombo vyao? Utandawizi ambao unajidhihirisha katika mshuko wa kiwango cha chini kabisa katika heshima ya dunia? Uelezaji huu unalingana na unakwenda sanjari na utata na mkinzano wa mambo mengi jinsi yanavyokwenda katika dunia yetu ya leo. Fikiria utata na mkinzano wa utawala au uongozi wetu wa ndani na haki za raia zinazovunjwa ovyoovyo. Fikiria ukoloni mamboleo na utandawazi wenyewe unavyovunjavunja kila kitu na jinsi matokeo yake yanavyoafikiana sana na matumizi ya lugha katika riwaya hii. 3.3. Ujengaji Fantasia na Uhalisia Mazingaombwe Sifa iliyo dhahiri sana katika riwaya hii ni namna gani lugha inavyotumiwa kujenga kwa makusudi fantasia na uhalisia mazingaombwe. Katika makala haya tunatofautisha fantasia na uhalisia kwa sababu fantasia ni dhana inayoelezea njia ya kutumia lugha kwa kutia chumvi mno, hadi kufikia kuvuka mstari wa uhalisia na mantiki. Kwa maneno mengine, fantasia ni dhana pana inayohusiana na chochote kinachoelezewa kwa kutiwa chumvi na kusimama nje ya uhalisia na mantiki. Uhalisia mazingaombwe ni aina fulani ya fantasia, lakini ni mbinu inayozileta dunia mbili pamoja za ‘ukale’ na ‘usasa’ –ukale wenye misingi ya mazingaombwe au ukweli ambao hauwezi kuelezeka katika mantiki ya nchi za Ulaya. Na usasa unaojaa taathira za kitamaduni, sayansi na teknolojia iliyoletwa na wakati wa ukoloni na wakati baada ya ukoloni. Tunaweza kusema kwamba Shaaban Robert ni mwanzilishi wa riwaya ya fantasia katika fasihi ya Kiswahili, hasa katika Kusadikika (1951), Adili na Nduguze (1952) na Kufikirika (1967). Lakini ingawa riwaya hizi zina uhalisia wa aina fulani, fantasia yake ni tofauti na ile ya riwaya mpya, kwa vile zimejikita mno katika ubunifudhanifu wa kila kipengele chake: ‘simulizi’, ‘hadithi’, ‘uhusika’, ‘mandhari’ na hata ‘uhalisia’ wa baadhi ya miketo7 ya matini yake. Fantasia ya riwaya mpya ni ya kuuelezea ukweli kama ulivyo hivi sasa na kwa hivyo uko karibu na kinachotokea katika mandhari, karibu na simulizi na wahusika wa riwaya yenyewe. Ingawa huu ni uhalisia mazingaombwe una mnato zaidi kuliko fantasia ya Shaaban Robert. Fantasia na uhalisia mazingaombwe ni pumzi za riwaya mpya. Huwezi kusoma ukurasa mmoja au hata pengine aya moja bila ya kujikuta unatoka katika uhalisia na kuingia katika mazingaombwe au kutoka mazingaombwe na kuingia katika uhalisia. Mpaka baina ya matukio au dunia hizi mbili ni mfinyu mno kiasi kwamba ni sawa na 7 Tafsiri ya Chunks kusema haupo. Mbinu hii imetawala katika riwaya zote za mwelekeo huu –mbinu ya uhalisia usio uhalisia, mazingaombwe yasiyo mazingaombwe, fantasia isiyo fantasia. Katika Nagona kuna mto unaonguruma usioonekana, ukohozi wa watu wasiokuwepo, miti inayocheka, hali ya mhusika kuchapwa na watu usiowaona, ukimya unaokatwa ghafla na sauti za watu wanaosoma wasioonekana (yote katika uk. 1 tu), maiti aliyefumbatwa katika kiza ambaye anashika Biblia mkono mmoja na Koran mkono mwingine, paka wa ajabu anayetarajiwa kuwa mlinzi wa mauti (uk.2-3), bustani yenye maua meupe yanayoteleza na kutoa mwangaza, maua na matunda ambayo hayawezekani kuvunwa (uk.13), kikundi cha wafu cha wanafalsafa mashuhuri, wanabiolojia, wanasosiolojia na wanasaikolojia wanaofufuka ... (uk.15). Katika Babu Alipofufuka kuna dhana nzima ya fikira kwamba hatufi, tunapita tu katika dunia nyingine ya kutoonekana tukiwa mizuka, dhana nzima ya ndoto anayoiota binadamu katika dunia yetu ya leo, ndoto ambamo ndani yake binadamu anajiona hana hakika kama yupo au hayupo, anaishi au amekufa. Pia katika riwaya hii kuna miujiza ya aliye hai kuweza kujiua na kujifufua tena au kujigeuza mchwa na kurejea tena katika umbo la kibinaadamu au kuzama chini ya ardhi na kuibuka baharini na tena ghafla kukanyaga nchi kavu. Katika Bina-Adamu kuna miujiza ya kutumika chakula na kinywaji kisichokwisha na ambacho kinashibisha mara moja. Au ya mhusika kuweza kusafiri dunia nzima kifikira au ndoto, kupitia nchi kavu na mtoni na baharini. Kuna hali ya mtu mzima kurudi utoto kimaumbile. Mna viumbe wa miujiza kama lile jitu lenye miguu mirefu kupita kiasi ambalo linaitwa beberu au UMERO-JAPA. Au aina ya kiumbe mwingine anayeitwa Wotan, Mungu wa vita na mfalme wa mashujaa. Au mahuntha watatu ambao wanatafutwa lakini hawaonekani kwa sababu ni viumbe wa miujiza. Kuna P.P (Peter Pan /Yanguis??) mwenyewe ambaye ana miujiza ya kinanga8 na kuzongwa na visaasili ambaye pia anatafutwa na mhusika mkuu ili iwe ni sababu ya kukikomboa kijiji kilichotengwa mno duniani. Viumbe wengine wa miujiza ni wale watu waliofufuliwa, akina Fyura (yaani Fuehrer, lakabu aliyopewa kiongozi wa kiimla Adolf Hitler), Dkt. Joseph Mengele, Hiro (Hirohito, aliyekuwa mfalme wa Japan), Osagyefo (yaani marehemu Kwame Nkrumah), Churchill na Stalin. Mwalimu au Mussa anayeishi vileleni mwa miti na ambaye anapenda sifa na kuimbiwa nyimbo (labda marehemu mwalimu Nyerere). Katika Ziraili na Zirani kuna mpaka mdogo sana wa maisha ya duniani na mbinguni. Kuna mchanganyiko wa watu, malaika na Uungu. Kuna roho kusimama na kusema au ufufuzi wa watu wanaosema na majini, mashetani
>>>>>>>INAENDELEA>>>>>>>>>
Powered by Blogger.