Riwaya mpya ya Kiswahili




na malaika. Pia katika riwaya hii maisha ya mbinguni yanachorwa kisitiari na kufananishwa na maisha yetu tuliyonayo leo: maisha yaliyojaa suitafahamu za kiitikadi za kidini na siasa, uonevu, mabavu, unyonyaji, uongo, unafiki, ufisadi, njama, ugomvi na vita. Mlinganisho huu ni wa uhusiano wa karibu mno mpaka msomaji anajiuliza kama mwandishi anazungumza kwa njia ya ishara na fumbo, ahera au dunia tunayoishi leo. Katika Dunia Yao, mazingaombwe yamo katika ile hali ya mhusika kuikimbia nafsi yake, familia yake, marafiki, majirani na jamii kwa jumla; ile hali ya mporomoko wake unaomrusha akili na kumfanya aishi kwenye chumba kidogo mfano wa jela ambamo anazurura katika dunia pana bila ya kuzurura. Anamozurura katika ndoto. Katika dunia hii mhusika mkuu anapanga udugu na kompyuta, mtu-mashine pekee 8 Tafsiri ya Epic aliyebaki katika maisha yake anayeweza kumwamini, kuzungumza naye, kushauriana naye, kumtumia kama kiwango cha kuandikia historia na hadithi yake na hadithi za watu wengine na kiwambo cha kuweza kuzungumza na binti yake ambaye anaishi London kama mkimbizi-njaa. Kuna wahusika-picha wanaosimama kutoka katika albamu na kuwa viumbe vyenye ngozi, nyama, damu na mifupa –viumbe vyenye urazini kamili. Ndani ya riwaya hii pia kuna mtoto mkombozi9 ambaye tokea siku yake ya kuja duniani anaonyesha miujiza ya kusema, kula, kutembea na kutoa rai kama vile mtu mzima. Pia katika riwaya hii kuna matambiko yanayohusishwa na Miungu ya Kiafrika kama ile ya kosmolojia ya Waibo wa Nigeria. Jambo muhimu hapa ni kukumbuka kwamba fantasia na uhalisia mazingaombwe hayapo kwa ajili ya kuwepo tu au kwa ajili ya mchezo wa lugha na sanaa. Ni mbinu muhimu ya kumfanya msomaji autupie jicho kali uhalisia mpya ambao una ukweli wa aina nyingine kabisa, uhalisia wenye mkanganyo na utata. Ni mbinu ya kukemea kile kinachoonekana na waandishi hawa kuwa ni utandawizi badala ya utandawazi. Ni mbinu ya kuonyesha mporomoko wa kila kitu katika jamii zetu –uchumi, utamaduni, uhusiano baina ya mtu na mtu, uhusiano wa raia, umakinifu wa ukoo na mtu binafsi kama Mtanzania na Mkenya, utambulisho wa mtu binafsi ambao umesambaratika na kuteremka chini kwa kiwango kikubwa mno, au kuporomoka kwa huduma za kijamii, kunajisika kwa heshima ya Mwafrika, Mtanzania, Mkenya na mpopote-pale-alipo ulimwenguni. Ushahidi mzuri wa fantasia na uhalisia mazingaombwe umo katika dondoo hili la Mohamed katika Dunia Yao (uk.172-173) – dondoo ambalo linaelezea dhana ya utandawazi katika picha za kimiujiza kabisa: Sasa hivi ndiyo kile kitu kimeshakaribia. Karibu mno kuweza kutambulikana. Kitu gani? Ilikuwa vigumu hata kubahatisha kukiagua au kukitaja kwa asahi. Kitu au jitu? Utata wa jitukitu labda. Umbo lake limekas’mika nusu bin nusu, kushoto na kulia, katikati ya jimwili lake. Pandikizi la jitukitu jinsi lilivyoumbika. Kushoto, linamemetuka anga la ki- Ungu linaloumiza macho na kuogofya. Kushoto pia linachanua uzuri wa ajabu. Uzuri wa kike ndani ya uzuri wa kiume. Uzuri unaokanganya. Sijapata kuona kiumbe duniani chenye uzuri namna hii. Useme hao huru-l-ayen wa peponi watajikanao. Na kulia, jimwili lake limekumbatiwa na giza zito la maangamizi ambalo kila mara lilikuwa likiripuka moto kuunguza kila kitu kilichosimama kwenye njia yake. Lilikuwa likipita kwa kasi ya umeme, lakini bado lilionekana lipo papo hapo daima – haliondoki! Linapiga kasi katika njia yake inayojiandika yenyewe – mara Globalization mara Americanization. Na lilipotimka lilitifua kila kitu katika kasi na mikiki yake. Kila kitu kilipojaribu kufukuzana nalo, kilijikuta kinaachwa nyuma milioni ya kilomita. Likapita kwa kasi na pepo zake za dhoruba likiripuka mandimi ya moto yaliyounguza na kukausha kila kitu: watu, wanyama, barabara, majumba, miji, maji, hewa, pwani, bahari, nchi kavu, madini, umeme, mafuta, hospitali, madawa, benki, viwanda, biashara, raslimali zote ... shule, vyuo, desturi, mila, tamaduni na hata uhai, heshima na mustakabali wa watu – hata roho zao. Lilipenya hata ndani ya nyumba na vibanda vya watu kusasambura na kupekua kila kitu kukashifu na kufedhehi na kisha kuangamiza lilivyopenda. Liliingia humo na kutawala na kuamrisha na kulazimisha mambo katika nyumba yake mwenyewe mtu ... Ingawa huu si mkemeo kamili (labda ni maombolezo), bado lakini tunaona hasira za mwandishi na kutokubaliana kwake na dhana ya utandawazi iliyoingia katika vichwa vya 9 Katika riwaya hii mpya ‘mkombozi’ ni neno muhimu sana linalorejelewa katika nyingi ya matini ya riwaya zenyewe viongozi na watu wetu. Ni dondoo linaloonyesha aina ya kuwezwa vibaya sana ukilinganisha na zile siasa za miaka ya 1960 hadi 1970 zilizotupa tamaa ya kukwamuka na kuwa na ufahari wa kuwa sisi ni watu pia. 3.4 Lugha ya Mchanganyondimi10 Gromov (2004:6) anapiga ndipo anaposema kwamba sifa moja muhimu ya riwaya hii mpya ya Kiswahili ni ile ya mchanganyondimi. Lakini Gromov haishii hapo, anafafanua mchanganyondimi kama unavyotumika katika riwaya hii kwa kuuita mchanganyondimi wa mbambizoviraka11. Kwa mfano, hadithi ya Babu Alipofufuka inaanza kama hadithi ya mzuka, kisha inaingia katika maelezo ya matukio ya uhalisia katika jiji mojawapo la nchi za Kiafrika na baadaye inamwongoza msomaji katika ukweli wa kifantasia ambao umo katika dunia nyingine. Tena tunaelezewa kuporomoka kwa Pate ya Al-ikishafi. Kisha inakuja habari ya UKIMWI ikifuatiwa na uharibifu wa tabaka ozoni. Halafu tunakutana na Visaasili vya Wagiriki na Mungu wao wa pwani, yaani Proteus ambaye anahusishwa na utandawizi wenyewe au kiongozi mkuu wa nchi za Kiafrika ambaye anautumikia utandawizi huku akienda dhidi ya nchi yake na watu wake. Wamitila katika Bina-Adamu, pia anatumia mchanganyondimi usio mipaka ya urejeleshi12 kuhusu ‘matokeo ya historia za dunia’, ‘fasihi’, mchanganyo wa ‘visaasili’, ‘matini za kidini’, ‘falsafa’ na mambo muhimu ya uhalisia wa maisha ya kisasa. Riwaya hii pia inaingiza wababe kama Wotan, Pandora, Joseph Mengele, Emperor Hirohito, Che Guevara na maandishi ya Heike Monogatari na William Dubois’ The Soul of Black Folk. Katika riwaya mbili za Kezilahabi, Nagona na Mzingile kuna mchanganyondimi wa aina hiyohiyo, ingawa kwa mtindo na nyenzo tofauti. Kwa mfano, matini inajengwa kwa lugha faragha ya mwandishi mwenyewe anayejificha nyuma ya wahusika wake, lugha ambayo imo katika mkondo simulizi, lakini kila mara inaingiliwa kati na miketo ya kifilosofia, dini, saikolojia, maneno ya mitume waliofufuka na wahusika wengine wenye uwezo wa kuishi maelfu ya miaka. Hivi ndivyo miketo hiyo inavyopachikwa kimbambizoviraka juu ya matini kuu ya riwaya ya Nagona (uk.15): Uwaonao katika duara hii ni kikundi kidogo tu cha waliokuwa wabishi katika usakaji wa njia. Yule pale ni Plato, na yule ni Socrates. Huyu hapa ni Aristotle. Yule ni Hegel huyu ni Darwin na waliokaribiana na Marx ni Freud na huyu ni Nietzsche ... Na si kama wafu hawa wanatajwa majina tu – lakini pia wanaonyeshwa kushiriki katika historia yao ya mapambano ya kifalfasa na kiitikadi kama pale tunapoambiwa: [S]asa hivi wametulia kidogo. Zamani wakianza majadiliano na roho zao ilikuwa vurugu tupu. Na wakianza majadiliano ya wao kwa wao basi hapo duara iliwaka moto ...(uk.15) 3.5 Lugha na Falsafa Kwa kawaida matukio makuu yote yanayokuja kuwaelemea watu vibaya sana, huzusha mijadala ya kifalsafa. Kuzuka kwa neno utandawazi na taathira ya neno hili katika maisha ya watu katika ubinafsi wao, ujamii wao, utamaduni wao, imani zao za kijadi na 10 Tunalitumia neno hili kwa maana ya ‘collage’, yaani mbandikizo wa picha mbalimbali ambazo si lazima ziwe na uhusiano wa moja kwa moja juu ya mji wa sanaa ya uandishi 11 Tunalitumia neno hili kwa maana ya ‘collage’, yaani mbandikizo wa picha mbalimbali ambazo si lazima ziwe na uhusiano wa moja kwa moja juu ya mji wa sanaa ya uandishi 12 Tafsiri ya Allusion kidini, kuwepo kwao duniani kiujumla, kuwepo kwao duniani kama kikundi cha watu wa jinsi fulani, kuangamia kwao, mwelekeo wao wa maisha ya baadaye, utambulisho wao, heshima yao kama binadamu ni mambo kadha ambayo bila ya shaka yanazua masuala ya kifalsafa kama vile: nini mtu? Nini utu? Nini ubinadamu? Nini uraia? Nini uzalendo? Nini ukweli na nini uwongo? Nini uhuru? Nini siasa? Ipi siasa bora? Nini historia? Nini dini? Kwa nini mtu alazimishwe kugeuza imani yake? Kwa nini mtu alazimishwe kuishi wanavyotaka watu wengine? Nini raha na...
>>>>>>INAENDELEA>>>>>>> 
Powered by Blogger.