UTANDAWAZI AU
UTANDAWIZI? JINSI LUGHA YA RIWAYA MPYA YA KISWAHILI INAVYODAI Said A.M. Khamis
1.0 Utangulizi Kuzuka kwa riwaya mpya ya Kiswahili katika miaka ya 1990
kunaelezwa kwa viwango mbalimbali na wahakiki kama vile Wamitila (1991, 1997),
Gromov (1998, 2004), Khamis (1999, 2001, 2003, 2004), Bertoncini (2002), Topan
(2002), King’ei (2002), Dittemer (2002/2003) na Rettová (2004). Hapa, hatuna
nafasi ya kurejelea tabia za ‘kimaumbo’, ‘kimiundo’ na ‘kimaudhui’
zinazoitofautisha riwaya hii ya Kiswahili na nyingine, ila tutajishughulisha na
kipengele kimoja tu cha msingi, nacho ni kipengele cha lugha kama alama
mojawapo ya mtindo1 au mwelekeo wa riwaya hii – lugha katika uhusiano wake na
utandawazi au utandawizi. Katika makala haya tunatilia mkazo kwamba aina ya
lugha inayotumika katika kazi fulani ya fasihi huathiriwa na nini kinachotokea
katika jamii yenyewe ambamo mwandishi huchota fikira, maudhui, falsafa,
itikadi, jazanda, mitindo, maumbo na miundo-lugha –hasa inapokuwa jamii yenyewe
imo katika kasi ya mabadiliko makubwa kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia
kuanzia wakati riwaya hii ilipoibuka katika miaka ya 1990 hadi leo. 2.0 Riwaya
Mpya na Utandawazi Riwaya ya Kiswahili tunayoizungumzia imezaliwa mwanzoni mwa
miaka ya 1990, muda mfupi tu baada ya neno utandawazi kuingia masikioni na
kuzama akilini mwetu kuanzia miaka 1980. Utandawazi ni neno dhahania mno, lenye
maana nyingi zenye utata kutegemea msisitizo wa anayelitumia. Pamoja na tofauti
za maana na matumizi ya neno hili, wataalamu wanakubaliana kwamba ni neno
linaloelezea mfungamano na uhusiano uliojitokeza katika miaka 30 iliyopita;
hasa katika biashara na uchumi, lakini pia katika utamaduni, miongoni mwa jamii
tofauti za dunia. Mfungamano na uhusianao huu unatofautishwa na mfungamano na
mahusiano mengine ya aina hii yaliyojitokeza hapo awali, kwa sababu utandawazi
umepata kasi kubwa ya kuwekeza mitaji na kuvuna bamvua la faida kiuchumi na
kiutamaduni; ukisaidiwa na maendeleo makubwa ya kiteknolojia yaliyopatikana
karibuni, hasa ya vyombo vya mawasiliano ambavyo vimefupisha au kuondoa vikwazo
vya masafa na wakati (Jauch 2001, Offiong 2001). Kiutamaduni, utandawazi
unahusishwa na kuenea kwa tamaduni za ki-Magharibi kwa njia ya kibiashara (k.m
vinywaji vya Coca Cola, bia na pombe kali ambazo hapo zamani zilikuwa
hazijulikani au zilijulikana kwa watu wachache tu wa Dunia ya Tatu na vyakula
vya Kentucky na Mcdonald) au mtiririko wa muziki na taswira kupitia video,
televisheni, mitandao ya kompyuta na simu, CD, DVD na VCD. Lakini kwa hakika si
sahihi kuuchukulia utandawazi kijuujuu tu, au jinsi unavyofasiliwa na watetezi
wake. Kwa hivyo, ipo haja hapa kuelezea, ingawa kwa ufupi, asili ya kuibuka
kwake. Historia ya utandawazi haiwezi kuepushwa na misingi ya mikakati ya G7,
Benki ya Dunia, IMF na WTO, vyombo vinavyosimamiwa, kuimarishwa na kuendelezwa
na itikadi ya uliberali-mpya2 (Jauch 2001; 3-15; Offiong, 2001: 1-19). Kwa
kweli, 1 Tunapenda kukumbusha kwamba hii ni maana moja tu ya mtindo – yaani
mbinu ya pamoja inayotofautisha kundi la 2 Tafsiri ya ’neo-liberalism’
kinadharia, mfungamano na uhusiano huu wa utandawazi unafasiliwa kwa namna
tofauti baina ya kambi mbili. Kambi ya kwanza inauchukulia utandawazi kuwa ni
‘baraka’ kwa nchi zote duniani, kwa sababu hatimaye utaboresha maisha ya watu
wote duniani kote (Ruigrok & Van Tulder 1995:169). Kambi hii inadai kwamba
utandawazi una faida kubwa hasa kwa nchi zinazoendelea3, na kwamba kufungua
milango ya biashara, masoko huria ya bidhaa na kuufanya utamaduni wa taifa moja
ukutane uso kwa uso na utamaduni wa mataifa mengine (sifa moja kubwa ya
utandawazi), kunaleta fanaka kila pahala (Jauch, keshatajwa: 3). Kambi ya pili,
ikitumia ithibati jarabati, inakanusha kabisa uhalali wa madai ya kambi ya
kwanza, kwa kusema kwamba utandawazi si dhana mpya kamwe, bali ni upeo wa dhana
kongwe yenye sifa mpya ya kutumia maendeleo makubwa yaliyopatikana
kiteknolojia, kunyonya, kwa mapana na marefu, utajiri wa dunia na kuwaacha watu
wa nchi masikini kuwa masikini zaidi kuliko walivyokuwa zamani. Na si kuwaacha
masikini zaidi tu, bali pia kuchafua uchumi, tamaduni, mazingira na maisha yao
vibayavibaya, hadi kufikia nchi hizo kudharauliwa na kuonekana si lolote si
chochote katika fikra ya dunia hivi leo. Mabadiliko haya, kwa sehemu kubwa,
yanatokana na upeo wa matatizo ya kiuchumi ya kimataifa yaliyotokea mwanzoni
mwa miaka ya 1970, ambayo yalisababishwa na maslahi ya kibiashara na utashi wa
mataifa makubwa yanayolenga kila siku kupata faida kubwa kupita kiasi (Murray
2000:7-8; ILRIG 1998). Jumla ya riwaya za Kiswahili tunazoita mpya ni zile za
Euphrase Kezilahabi za Nagona (1990) na Mzingile (1990), riwaya moja ya Katama
Mkangi ya Walenisi (1995), riwaya ya W. E. Mkufya ya Ziraili na Zirani (1999),
riwaya moja ya Mohamed ya Babu Alipofufuka (2001) na miswada yake miwili4 ya
Dunia Yao na Mkamandume, riwaya moja ya Wamitila ya Bina-Adamu (2002) na, kwa
namna na kiwango fulani, riwaya ya Chachage ya Makuadi wa Soko Huria (2002).
Sifa moja kubwa ya kimaudhui, miongoni mwa sifa kadha za riwaya hii, ni ile ya
kushughulikia kwa kina matatizo ambayo yanaukabili ulimwengu wetu leo. Kwa
namna nyingine tunaweza kusema, ingawa bado riwaya hii inajishughulisha kwa
kiwango fulani, na matatizo ya ndani ya nchi na jamii husika, kwa kiasi kikubwa
imekiuka mipaka ya kitaifa na kieneo. Kwenye jalada la nyuma la Bina-Adamu,
tunaambiwa wazi kwamba… [n]i riwaya inayotumia sitiari ya kijiji kuangalia hali
ya mataifa ya ulimwengu. Katika kuhitimisha makala yake Postmodernistic
Elements in Recent Kiswahili Novels, Gromov (2004:13) anatuambia: [t]unaweza
kusema kwamba fasihi ya Kiswahili inaendelea kuchukua dhima ya uchunguzi wa
jamii –lakini, huku ikibeba silaha mpya za njia ya utunzi na fikra za
majadiliano, inajishughulisha na matatizo mapya, na inachunguza, si jamii ya
Afrika Mashariki tu, bali dunia yote kubwa (na) pumbavu, isiyoishika tena,
lakini ndiyo pekee tuliyonayo– dunia yetu ya leo ... (tafsiri yangu). 3 Sina
hakika kwamba neno hili tunaweza kuendelea kulitumia kurejelea nchi zetu za
Kiafrika, lakini nitalitumia kwa kukosa neno linalofaa zaidi. 4 Dunia Yao ni
mswada uliopelekwa Jomo Kenyatta Foundation tangu 2001 na kukubaliwa
kuchapishwa lakini mwandishi aliuondoa huko, kwa kuchelewa kuchapishwa,
akaupeleka OUP ambako nako umekaa tangu Julai, 2004. Ms wa Mkamandume
ulimalizwa kuandikwa mwaka 2004 na bado haujawasilishwa kwa watoa vitabu
wowote. Ingawa riwaya hii mpya, kama tulivyosema, inajishughulisha na mada
mbalimbali za kimaudhui kuhusu matatizo yanayoikabili dunia yetu ya leo –hapa
tumechagua kuzungumzia, kwa mujibu wa maoni yetu, tatizo kubwa na sugu kabisa
la utandawazi– tatizo ambalo riwaya kama Nagona, Mzingile, Babu Alipofufuka,
Dunia Yao, Bina- Adamu na Mkamandume, zinalijadili waziwazi. Kwa mfano, katika
kuthibitisha namna gani dhamira ya utandawazi inavyotawala katika Bina-Adamu,
Gromov (2004:8), akiteua kwa uangalifu lugha na picha zinazoelezea dhana ya
utandawazi, anatambia hivi: Wakati wa safari yake ndefu, mbabe, akisaidiwa na
sauti ya ajabu ya mwanamke mwenye sifa zisizo za kibinamu anayeitwa Hanna,
anazuru Ulaya ambayo ‘inaishi jana’, Asia ya viwanda ambayo ‘inaishi kwa
matumaini’ na Afrika, ambayo ‘inaishi mwishoni mwa kijiji cha utandawazi na
imeharibiwaharibiwa na njaa na vita. Anapokuwa njiani, kila pahala anakutana na
mambo yanayoonekana hayana mantiki, mambo ambayo hayaelezeki yanayofanywa na P.
P mwenye miujiza –Ulaya P. P ameushinda ufashisti, lakini bado unaishi imara
miongoni mwa wafuasi wake. Huko Asia ametupa bomu la Atomiki Hiroshima. Afrika,
akitumia jiwe, amevigonga vichwa vya wanasiasa kuvitoa akili. Huko Urusi,
ambako P. P anazuru kwa muda mfupi, hatuambii anafanya nini kwa vile anamwogopa
Stalin. P. P anaiuza Afrika kwa watalii wa kigeni, anaharibu bahari kwa mafuta
na mabaki machafu ya ‘radioactive’: Mwishoni mwa safari yake mbabe anaigundua
Amerika –Bustani ya Adeni ya pili, ambamo wakazi wake, mapapa wa biashara za
kimataifa, wanaishi (vizuri) kutokana na umasikini wa Nchi za Dunia ya Tatu,
wakidai kwamba wanaishi leo na tena wanaishi katika uhalisia wa mambo ...
(tafsiri yangu)
>>>>>INAENDELEA>>>>>