CHAWAKAMA


CHAWAKAMA husimama badala ya Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili vyuo vikuu Afrika Mashariki. Chama hiki kilianzishwa mwaka 2004 kwa lengo la kukuza na kueneza Kiswahili katika eneo lote la Afrika Mashariki kupitia wanafunzi wanaosoma Kiswahili vyuoni. Wanachama wa chama hiki ni wale wanosoma Kiswahili na hata wale wenye mapenzi ya lugha ya Kiswahili pia wanaweza kujiunga na chama hiki.
Chama hiki kina utaratibu wa kuandaa makongamano ambapo wanachama wake kutoka nchi zote za Afrika Mashariki hupata fursa ya kukutana mara moja kila mwaka. Pamoja na utaratibu wa chama kuandaa makongamano pia uanzishwaji wake umeambatana na malengo kadhaa ambayo ndiyo dira inayoiongoza chama kwa mujibu wa katiba, malengo hayo ni haya yafuatayo:
  1. Kuwapa wanachama nafasi ya kujadili, kuimarisha, kuendeleza na kukuza vipawa vyao vya lugha na fasihi ya Kiswahili.
  2. Kuamsha ari ya mapinduzi ya utamaduni wa lugha ya kiswahili.
  3. Kueneza lugha ya kiswahili ndani na nje ya nchi.
  4. Kushirikiana na vyama vingine katika juhudi za kuendeleza na kuimarisha lugha ya kiswahili ndani na nje ya nchi wanachama.
  5. Kuwaunganisha wanafunzi wa kiswahili Afrika Mashariki na kati katika kukikuza kiswahili.
  6. Kushirikiana na asasi mbalimbali zinazojihusisha na ukuzaji na uenezaji wa kiswahili ndani na nje ya nchi kama vile BAKITA, TATAKI, TAKILUKI, UWAVITA, CHAKAMA, BAKIZA n.k.
  7. Kuchapisha kijarida cha chama na machapisho mengine ili kusaidia kueneza taaluma ya kiswahili.
  8. Kuweka kumbukumbu ya wataalamu wa kiswahili kwa nia ya kuwatumia katika kufanikisha malengo ya chama na wadau wa Kiswahili.
  9. Kuratibu makongamano na mijadala mbalimbali inayohusiana na taaluma ya kiswahili.
Pamoja na malengo hayo, lengo kuu la chama hiki ni kueneza Kiswahili lakini sasa wanakienezaje? Wanachama wa chama hiki ambao ni nchi wanachama wa jumuia ya Afrika mashariki wanakawaida ya kuandaa makongamano kwa ngazi ya kitaifa na ngazi ya kimataifa.
Kwa ngazi ya kitaifa kila nchi huandaa kongamano kila mwaka ambalo linawakutanisha wanachama wote kutoka vyuo mbalimbali katika nchi husika. Katika kongamano hilo mada mbalimbali zinazohusu lugha ya Kiswahili na mustakabali wake hujadiliwa lakini pia maazimio mbalimbali huchukuliwa juu ya maendeleo ya chama. Sasa katika mijadala kama hii inatoa nafasi ya Kiswahili kukua kwani makala mbalimbali huandikwa ambazo pia husomwa na watu mbalimbali. Makala hizi pia zimekuwa zikichapishwa katika majarida ya chuo husika na pia zimekua zikichapishwa mtandaoni ambapo hutoa fursa kubwa kwa watu wengi zaidi kuzifikia na kusoma, hivyo kwa njia hiyo Kiswahili kinakua kimeenea.

MAFANIKIO NA CHANGAMOTO ZINAZOVIKABILI VYOMBO VYA UKUZAJI WA KISWAHILI
Mafanikio
  • Vyombo vya ukuzaji wa Kiswahili vimejitahidi sana kukuza lugha ya Kiswahili, kwa hali ya Kiswahili ilivyo sasa ni matokeo ya juhudi za vyombo hivyo. Mafanikio ya vyombo hivyo ni pamoja na haya yafuatayo:
  • Machapisho ya lugha ya Kiswahili ni mengi sana nchini na nje ya nchi, kufanya mafunzo ya Kiswahili, kukua kwa matumizi ya Kiswahili na kuongezeka kwa idadi ya watumiaji wa Kiswahili nchini.
  • Matumizi ya lugha ya Kiswahili katika sehemu rasmi hasa katika ofisi za serikali na ofisi za watu binafsi inadhihirisha mafanikio ya jitihada za vyombo hivi kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili.
  • Kufundshwa kwa lugha ya Kiswahili kama taaluma kwa ngazi ya shahada ya awali, uzamili na uzamivu. Hizi ni jitihada za TATAKI katika kuhakikisha kunapatikana wataalamu wa lugha ya Kiswahili, hivi sasa TATAKI wanafundisha lugha ya Kiswahili kwa ngazi ya shahada ya awali, uzamili na uzamivu.
  • Matumizi ya lugha ya Kiswahili katika vyombo mabalimbali vya kimataifa, matumizi ya lugha ya Kiswahili katika vikao vya Umoja wa Afrika na pia ufundishwaji wa lugha ya Kiswahili katika vyo mabalimbali Duniani ni ishara tosha ya kuonesha mafanikio ya jitihada za vyombo vya ukuzaji na uenezaji wa Kiswahili.

Changamoto
Licha ya mafanikio hayo lakini pia kuna changamoto zinazovikabili vyombo hivi vya ukuzaji wa Kiswahili.
  • Vyombo hivi vinakabiliwa na upungufu wa wataalam. Wataalamu wengi waliobobea katika taaluma za Kiswahili wanakimbilia nje ya nchi wakidhani huko ndiko kuna maslahi mazuri zaidi.
  • Upungufu wa fedha za kuendeshea shughuli za ukuzaji wa Kiswahili katika vyombo hivi pia limekuwa ni tatizo sugu. Kwa hiyo shughuli za ukuzaji wa Kiswahili zinakuwa zinakwenda taratibu.
  • Taasisi hizi pia zinashindwa kujitangaza vizuri kutokana na kwamba hazina vyombo vya habari binafsi ambavyo vingeweza kutumika kutangaza shughuli zao. Jambo hili limesababisha vyombo hivi kushindwa kutoa elimu ya Kiswahili kwa kutumia vyombo vya habari kutokana na kwamba gharama za kufanya hivyo ni kubwa.
  • Vyombo hivi baadhi havina ofisi za kudumu, na hivyo kuhamahama jambo ambalo linaathiri utendaji kazi wa vyombo hivyo.
Powered by Blogger.