SURA YA SITA - Uchambuzi wa Kifani Katika Riwaya
Uchambuzi wa kifani katika kazi ya fasihi ni njia moja ya kuielewa kazi ya fasihi. Fani ni aina ya uchambuzi ambao hujumuisha sehemu zote zinazoiunda kazi ya fasihi na kutokea kuwa mkusanyiko ambao unaweza kuonyesha upekee wa maandishi ya mwandishi mmoja. Kujua fani husaidia kujifunza na kuifahamu kazi moja ikihusiana au kufananishwa na nyingine hasa kwa vile huzingatia lugha, dhamira, wahusika, umbo la kazi hiyo na sehemu nyingine. Kwa sababu hii pia, fani husaidia kuielewa kazi moja kwa undani zaidi. Sehemu hizo tofauti za kazi ya fasihi huchunguzwa kwa mwingiliano unaokubaliana kulingana na kazi hiyo ilivyoundwa.
Sura hii itazingatia uchambuzi wa kifani wa riwaya na tutajikita hasa katika riwaya ya Bwana Myomhekere na Bibi Bugonoka.Tutazingatia fani ya kifasihi, ambayo kwa kiasi kikubwa ni upanuzi wa uchambuzi na uhakiki wa kazi yote ukizingatia dhamira, wahusika na muundo. Aidha hapa tutaangalia fani ya lugha ambayo itazingatia miundo ya lugha na uhusiano wa maneno yaliyounda lugha ya mwandishi, jinsi maneno hayo na lugha iliyotumika inavyokidhi haja za fani ya kifasihi na sehemu zake.
Katika uchambuzi wa fani kifasihi ni muhimu tuelewe kwamba fasihi huvuka mipaka ya wakati na mahalt ili kutoa kauli zinazohusu binadamu na matendo yake, tabia na maisha yake. Riwaya ya Bwana Myombekere na Bibi Bugonoka (kuanzia sasa BMBB), kama kazi ya fasihi, inatupatia ujuzi mpana unaohusu watu wengine, utamaduhi mwingine na pia kutupatia uwezekano wa kufikiria kuhusu sisi wenyewe na shughuli zetu. Kama kazi nyingine ya fasihi, riwaya hii inatupa nafasi ya kuweza kuwa mahali pamoja kimawazo na binadamu wengine. Kwa hali hiyo basi, uchambuzi wa kifani wa riwaya hii utazingatia wakati uliopita, uliopo na hata ujao na vilevile kuangalia riwaya hiyo ndani na nje ya mipaka ya utamaduni au jamii iliyozingatiwa. Ili kwenda nje ya mipaka hiyo miwili tunaweza kuiangalia dhamira kuu inayojitokeza kwenye riwaya ya BMBB kuona ni vipi uchambuzi wa kifani wa dhamira unaweza kutupatia mwanga zaidi.
Dhamira, ikiwa ndilo wazo kuu linalotenda au kujitokeza katika riwaya nzima, huashiriwa na mfululizo wa vijiwazo vinavyoweza kuoanishwa na kuunganishwa kutoa wazo moja. Vijiwazo hivyo hujitokeza katika kila sehemu inayoikamilisha riwaya; iwe ni wahusika, muktadha, maneno au hata mazingira. Ni uhusiano baina ya dhamira na sehemu zingine ambao huashiria fani iliyotumika na pia nafasi ya fani hiyo katika kuikamilisha kazi hiyo. Kama asemavyo Geoffrey Leech (1970:125) kunakuwa na “uhusiano wa kimshikamano unaotoa kidokezo cha ufafanuzi wa kazi hiyo.” Kwa maneno mengine ni kama wavu uliojengwa kwa sehemu tofauti za kazi ya fasihi (kwa mfano riwaya). Katika riwaya ya BMBB dhamira kuu inayojitokeza ni unyumba. Riwaya hii imeliangalia swala la unyumba kwa kutumia mila na desturi za Wakerewe (Mlacha:1988). Riwaya nyingi za Kiswahili zimeligusia swala la unyumba kwa namna tofauti lakini tofauti kubwa baina ya riwaya hizo na hii ya BMBB ni ile ya kifani kuliko kimaudhui au muktadha. Hata hivyo, tofauti kubwa zaidi ambayo imejumuisha fani, maudhui na muundo ni ile aliyoitumia mwandishi wa riwaya hii kwa kuitumia familia moja (ya mke na mume) ambayo imo ndani ya jamii. Familia hii, katika ufinyu na upana wake imezingwa na jamii ambayo imehusishwa kikamilifu katika maisha ya Myombekere na Bugonoka na swala hilo la unyumba. Ni kutokana na muundo huu ambapo tunaiona riwaya ikiwa katika mshikamano wa kimkufu. Hii ina maana ya kwamba tukio moja linahusiana na jingine na kutegemea tukio jingine ili kukamilika. Wahusika vile vile wapo kwenye uhusiano wa kutegemeana na kukamilishana kulingana na dhamira kuu ya hadithi hii.
Katika uchambuzi wa kifani lugha huchukua nafasi kubwa. Hii inatokana na kufahamu kuwa lugha ndiyo inayotumika kuiunda kazi hiyo na kuwajenga wahusika ambao ndio wabebaji wakuu wa mawazo ya mwandishi. Nafasi ya lugha katika uchambuzi wa kifani inaweza kuonekana katika pande mbili. Upande wa kwanza ni ule ambapo lugha hutumiwa ili kuifanya kazi ya fasihi ivutie zaidi na iwe ndio chombo cha kuifanya kazi hiyo iwe nzuri. Upande wa pili ni pale ambapo fasihi nayo huchangia kuikuza lugha ingawa fasihi hiyo imetokana na lugha. Uhusiano huu wa kutegemeana tutauangalia kwa makini katika uchambuzi wetu hapo baadaye.
Lugha hutumiwa ili kuifanya kazi ya fasihi ivutie, ikiwa ni pamoja na kuifanya kazi hiyo iweze kueleweka, kwa msomaji. Malengo haya huandamana na lengo la kuburudisha, kigezo ambacho kimeonekana ni muhimu pia kwa wasomaji. Malengo haya yote yanaweza kufikiwa kutokana na mpangilio wa maneno na uundaji wa sentensi. Aidha uteuzi wa maneno na kauli na pia namna wazo lilivyojengwa ni njia nyingine. Katika riwaya hii Aniceti Kitereza ameweza kutunga hadithi ndefu ambayo imejengwa kutokana na lugha inayoweza kuchambuliwa chini ya misingi hiyo. Kazi hii inaweza kueleweka vizuri iwapo msomaji anaweza kuzingatia maisha ya Bwana Myombekcre yanavyokwenda siku baada ya siku na matukio yote yanayotokea. Lugha iliyotumika m nyepesi na inayoeleweka. Paleambapo anatumia maneno ambayo siyo ya Kiswahili amejitahidi kuyaelezea kwa Kiswahili sanifu ili kumpa msomaji picha karnili ya wazo lililofumbatwa katika neno hilo. Kwa mfano:
Kwa kuwa yeye alikuwa Omugimba, yaani mletamvua na alikuwa anataka mbuzi mweusi yule wa kutoa sadaka kwa sababu ya mvua .... (uk. 417)
Hapa mwandishi amefafanuamaana ya neno omugimba na kumfanya msomaji asiyejua lugha hiyo aipate picha kamili. Kwa wale wanaolifahamu neno hilo kifungu hiki kinawapeleka kwenye picha kamili zaidi na hivyo kuyakaribia mazmgiraya hadithi. Maneno mengine mwandishi ameyaacha kwenye mabano au bila kuyafafanua ndani ya hadithi. Badala yake ameyachukua maneno haya na kuyapa ufafanuzi mwishoni mwa kitabu kwa mfano:
lakini huyu ni mnyama mkali (ekikaka) haliwi kamwe na Abakerebe (uk. 487)
Nerio ekikaka limetafsiriwa mwishoni (uk. 597) kama dude, mnyama mkali anayetisha; nduli nk. Matumizi ya maneno ya Kikerewe katika hadithi hii yamekuwa na umuhimu sana katika kuielewa hadithi. Ni maneno ambayo yanaelezea vitu ambavyo vinaelezea utamaduni wa Wakerewe na ambavyo vinaweza kueleweka na kuvutia wasomaji wa jamii hiyo na pia kuwaelimisha waleambao wanatoka kwenye jamii zingine. Huu ni uandishi Pekee kifani katika uandishi wa Kiswahili lakini si uandishi mgeni katika fasihi. Waandishi mashuhuri kutoka Afrika Magharibi kama vile Chinua Achebe, Wole Soyinka na wengine wameutumia vile vile na kufanikiwa kuufikisha ujumbe kwa undani zaidi.
Matumizi ya fani ya aina hii katika uandishi wa riwaya yanaweza kurahisisha kufuatilia wazo na kuona namna lilivyojengwa. Hatari yake ni kuwa na maneno au kauli zinazojenga wazo hilo lakini zinaonekana kama zinapingana. Nitafafanua zaidi hapa. Maneno hayo ambayo sio ya Kiswahili yanaweza kuchukuliwa kama yalivyo na kueleweka hasa kama yamerudiwarudiwa baada ya kufafanuliwa, kwa mfano:
Pale tena ndipo pakawa kivumbi, wale walaji wa nyama mbichi, iitwayo obubisi, wakafuata wakiwa na uchu mwingi, hata watu wazima na wazee pia wakajongea karibu wapate kula obubisi (uk. 37.)
Katika ukurasa huo wa 37 neno obubisi limerudiwa sana (mara nane) licha ya kuwa limetumiwa tena baadaye. Hata hivyo, maana yake hasa sio nyama rnbichi tu ba1i ni nyama inayoliwa ikiwa mbichi. Kwa hali hii mtunzi ametumia neno obubisi kuweza kumfanya msomaji aweze kufuatilia wazo kirahisi hata pale ambapo sentensi yenye neno hilo imeundwa visivyo kama vile:
Mke wa pili aliwaletea majt ya kuoshea utumbo, na vingine villvyobaki, yaani visivyoliwa obubisi katika nchi ya Bukerebe. (uk. 38.)
Hali iliyokuwa inasisitizwa hapa ni ya nyama za aina fulani ambazo haziliwi zikiwa mbichi na sio kila kitu. Hata hivyo, jambo muhimu hapa ni kwamba uteuzi wa neno hilo na mpangilio wa sentensi zake ambazo zina neno hilo kifani huashiria msisitizo wa kile anachokizungumzia. Wakati mwingine, kama ilivyoonyeshwa awali, uteuzi na mpangilio huo wa maneno unaweza kuachana na miundo na hata matumizi ya kawaida katika lugha. Mtindo huo huwa na umuhimu sana katika kuichambua fani ya kazi ya fasihi au kazi za mwandishi mmoja.
Jambo moja la kusisitiza hapa ni kwamba mara nyingi maneno yote ambayo si ya Kiswahili yamepewa nafasi maalum katika sentensi. Mara nyingi maneno hayo hujitokeza kabla ya kituo kikubwa au kidogo au karibu sana na vituo hivyo. Hii kifani inaweza kuangaliwa kama sehemu ya 'mapumziko', baada ya wazo kuu kujengwa na kumaliziwa na neno hili na hivyo kurahisisha kueleweka neno hilo. Kwa mfano:
Munegera akarudi kule kwa Kalibata pamoja na vipande vya miti ya migazu alivyoviweka kwa wakati ule walipokuwa maarusi wanafukiziwa manukato ya Omugazu, ... (uk. 519)
Pamoja na hayo itaonekana kwamba maneno yote yaliyotumiwa arnbayo sio ya Kiswahili yanaweza kuepukika na wala yasiathiri kuielewa hadithi. Ni wazi picha kamili haitapatikana bila kuipata picha inayowakilishwa na neno hilo lililobeba utamaduni huo. Kifani haya ni mafanikio makubwa hasa kwa vile maneno haya yanachukua nafasi ya msisitizo pamoja na malengo ya msingi aliyotaja Mulokozi (1985:213) ya
Kuhifadhi lugha, desturi, practices na utamaduni wa Bakerebe.
Kwa kuangalia lugha aliyoitumia Kitcreza tunaona kwamba lengo la kuelekeza limejitokeza sana. Ufundi wa kifani aliotumia mwandishi kukidhi lengo hili umejitokeza kwenye kutumia maneno fulani fulani na vile vile maneno hayo kurudiwarudiwa. Maneno haya ni maneno ambayo yanalumika sana kwenye lugha ya mazungumzo. Luglia ya mazungumzo imeweza kuifanikisha riwaya hii kwa kuwaangalia wasomaji kama wasikilizaji wa hadithi na hivyo kuwahusisha kikamilifu kufuata matendo yanayoelezewa.
1. Pite pite Kahwagizi mweleka mmoja chini; Puu! mgnu wake ukavunjika, loo? Masalale. (uk. 408.)2. Myombekere akayadaka maneno hayo akamjibu mke wa Kanwakefa hivi, “kumbe, kweli! ndivyo hivyo! Kazi zenu zinawapa wasiwasi nyingi hivyo, shemeji. (uk. 368.)
Wakati mwingine mwandishi anatumia lugha isiyo sanifu na hali ya msisitizo inajitokeza.
1. Mimi huwa ninakwambia kila siku hivi: litoto hili ni lyehu, wewe unakataa, sasa vipi? (uk. 157)2. Ee! hili ni litu la ovyo kama mama yake (uk. 158)
Hapa katika lugha ya mazungumzo badala ya litoto ingekuwa toto, litu ingekuwa jitu na lyehu ingekuwa jehu. Mabadiliko hayo yangeweza kuifanya lugha ikawa ya mazungumzo na pia sanifu ukilinganisha na hiyo aliyoitumia mwandishi. Kitereza ametumia muundo huo kwa kuathiriwa na lugha yake ya asili na hivyo kuongezea msisitizo wa mhemuko na hasira iliyosababishwa na matendo ya mtoto huyo.
Muundo wa sentensi za mwandishi wa BMBB ni wa pekee katika sehemu kubwa ya hadithi hh. Ni muundo ambao haukubaliki katika Kiswahili sanifu lakini unatoa picha kamili ya kile mwandishi anachotaka kukielezea. Uandishi wa aina hii umeweza kuwapa sifa waandishi kadhaa Afrika ambao wameivunja lugha ya Kiingereza ili kukamilisha mawazo yao kulingana na jamii wanamoishi. Waandishi kama Ken Sora-Wiwa (1985) aliyeandika Sozaboy: A Novel in Rotten English aliweza kutajwa kwa heshima kwenye zawadi ya Noma mwaka 1987. Mifano michache itatuonyeshajinsi Kitereza alivyotumia Kiswahili kibaya ili kufikisha ujumbe muhimu kwa wasomaji wake:
Akakaa penye mchana wa asubuhi pamoja na wengine aliwakuta wamekwisha fikapo. (uk. 158)
Hapa yaelekea mwandishi, alikuwa anataka kuelezea muda maalum bila kutumiasaa. 'Mchana wa asubuhi' inaweza kuwa mnamo saa tano hivi kwani sio alfajiri au asubuhi na mapema. Ni asubuhi ambayo inaelekea mchana. Muda umechukuliwa kama mahali - akakaa penye -. Hata hivyo inaelezwa kwamba wote walikuwa wamekaa nje ya nyumba. Hii inaonyesha kuwa mwandishi alitaka kuweka msisitizo wa hali katika wakati huo. Namna yake ya kuandika ni tofauti na waandishi wengine kwani anatumia Kiswahili ambacho katika undani wake kina mantiki ingawa kwa juu juu kinaonekana kama Kiswahili kibovu. Mfano uliopo hapo chini unadhihirisha haya:
Akose leo na kesho, keshokutwa aende kumleta mwanamke atakayesindikiza binti wao kwa maarusi hayo; tena siku ile atakapolala amekwisha kutoka kumleta mwanamke msindikizaji yule apumzike miguu, tena atakapokucha ndipo atume mtu wa kwenda kujulishwa wakati gani wa kwenda kuoa. (uk. 494)
Aidha kipengele hiki ni mfano mzuri wa hadithi nzima inavyokwenda. Kuna mfululizo wa vitendo ambavyo viko huru lakini vile vile vimeunganishwa kimantiki. Hadithi yenyewe imejengwa na mfululizo wa visa ambavyo ingawa vipo huru vina uhusiano wa kutegemeana na visa vingine. Mtindo wa kimkufu (Mlacha: 1988) unajitokeza sana. Huu ni mtindo unaotumika sana kwenye simulizi. Aghalabu mtindo huu huifanya hadithi ieleweke zaidi pale unapozingatiwa na msomaji.
Muundo wa riwaya ni sehemu mojawapo katika kujadili fani ya sanaa. Katika riwaya hii itaonekana kwamba familia ya Bwana Myombekere na Bibi Bugonoka ndiyo inayofungua hadithi. Mwandishi anaanza kwa kuyahadithia matatizo ya familia hii na kisha hadithi inaanza kukua na kuwaingiza ndugu za mume na mke. Hapa ndipo tatizo walilokuwa nalo watu hawa wawili linaonekana kwamba ni kubwa na linaihusisha jamii nzima ya Wakerebe. Kwamba kutokuwa na mtoto sio kitu kidogo kwani kinahusu hata vizazi vinavyofuata. Myombekere anajitahidi amrudishe mkewe ili aweze kuimarisha farnilia yake. Pamoja na matatizo mengine ya maisha hadithi inakwisha baada ya kuonyesha mafanikio ya Myombekere na Bugonoka kupata watoto.
Wahusika wote wamehusishwa na mhusika mkuu, Bwana Myombekere. Mtindo huu wa uandishi unaonyesha upevu kisanii. Kwa vile wahusika wameshikamana na wamejengwa katika hali ya uhalisi wameweza kuchangia sana katika kukuza dhamira kuu. Myombekere na Bugonoka ndio wahusika wakuu katika kulikuza swala la unyumba na kulitoa kwa uwazi katika kazi hii. Wazazi wa Myombekere ndio wachochezi wakuu ambao wanasababisha watu hawa waachane wakati wazazi wa Bugonoka wamehusishwa zaidi kwenye masikitiko ya Bugonoka. Vivyo hivyo wahusika wote vvamekuwa na michango tofauti katika kuyakamilisha maisha ya kina Myombekere kwenye raha na matatizo. Nafasi walizopewa wahusika zinalingana na nafasi yao katika kuikamilisha hadithi. Kwa mfano Myombekere anaonekana ni mtu mwenye shida baada ya kuachana na mkewe. Akiwa katika hali hiyo anaonekana akiitegemeajamii nzima ili kumpata mkewe na kuweza kupata watoto.
Riwaya ya BMBB ni riwaya ambayo ina methali nyingi. Methali zilizotumika ni za Kikerewe ambazo zmaweza kupata rnethali za Kiswahili zinazoelezea falsafa ya aina hiyo hiyo. Kwa mfano methali ya 'Mgongo hauna macho' (uk. 5) imelinganishwa kwa kiasi fulani na methali isemayo 'mshika mbili moja humponyoka! Mlinganisho huo unafafanuliwa zaidi na maelezo yafuatayo: Walipozidi kuzungumza na baba mkwe wake, Bwana Myombekere akageuka asikie vizuri maneno kumtazama asikilize kwa makini' (uk. 5.) Kitereza hutumia methali kuhitimisha maelezo yake na kuyapa maelezo hayo nguvu zaidi pia huwatumia wahenga. Kwa mfano Myombekere anapokwenda kwa baba mkwe wake kuomba arudishiwe mkewe anahitimisha maombi yake kwa methali; anasema: Sababu wahenga walisema: 'Mzazi hatapiki ila huchukizwa tu' (uk. 49.)
Pamoja na mbinu zote hizo kifani, Aniceti Kitereza ametumia fani mbali mbali kuijenga riwaya yake. Ametumia nyimbo (uk. 101, 115, 116, nk.,) lugha ya mazungumzo, misemo tofauti na kurudia maneno ili kuweka msisitizo. Hata hivyo, lugha ya Kikerewe imejitokeza sana katika riwaya hii kiasi ambacho mara nyingi inabidi msomaji aende kwenye maelezo ya maneno ya Kikerewe ili kuielewa hadithi kikamilifu.
Hitimisho
Kitabu hiki kimeiangalia riwaya ya Kiswahili kwa ujumla na wala hakikunuia kuichambua kazi moja au nyingine. Lengo lake ni kumpa mwalimu na mwanafunzi ujuzi zaidi kuhusu uhakiki wa riwaya na pia kumpa nyenzo za kuweza kuielewa riwaya ya Kiswahili. Kama ilivyoonekana katika sura zote zilizotangulia uhakiki wa kijadi ulikuwa finyu mno na uliwafanya wanafunzi wasiwe na ustadi wa kuitambua riwaya wanayoijadili darasani na badala yake kuishughulikia juu juu tu. Ni wazi baada ya kuzingatia tuliyoyajadili hapo juu itaonekana kuwa riwaya ni ngumu zaidi kuliko wengi wetu tulivyodhani hapo awali, lakini ni katika ugumu huo ambapo tunaweza kuielewa. Ugumu wa riwaya ni kweli unatokana na kuiangalia riwaya kwa jicho la uhakiki.
Kwa mhakiki na msbmaji makini wa riwaya jambo la muhimu zaidi ni kuelewa ni wakati gani riwaya fulani ilipotokea na ilikuwa inazungukwa na vitu gani katika maisha halisi. Inabidi kuangalia siasa za wakati huo, elimu ya wanajamii na ya kijamii, hali ya kiuchumi na kadhalika; kwani vyote hivi huhusika sana katika kuiunda riwaya. Kadhalika inahitajika kuwaangalia waandishi wenyewe wanavyohusiana na wakati pamoja na hayo yote tuliyogusia awali. Kwa hali hii sura ya pili imekuwa ni muhimu sana kutangulia sura zingine ili kuitoa picha kamili ya kihistoria kuhusu riwaya ya Kiswahili. Wakati ni muhimu sana katika uundaji wa riwaya. Waandishi wa wakati mmoja wanaweza kuwa na uandishi unaofananafanana au wenye kutofautiana. La muhimu hapa ni kwamba kunaweza kuwa na mikondo tofauti ambayo inaweza kujitokeza katika nyakati tofauti. Mikondo hiyo inaweza kutambulika baada ya kuisoma riwaya na kuangalia wahusika, dhamira na hata maudhui na lugha iliyotumika. Kwa kuangalia inaendeleo na mabadiliko ya wahusika tumeweza kuonyesha jinsi historia na mikondo tofauti iliyojitokeza vilivyoweza kuathiri wahusika na uundaji wao. Muundo wa riwaya ni nadharia mpya ambayo imetumiwa hapa kuonyesha mabadiliko katika uhakikl. Mtindo uliokuwa ukitumiwa sana, ule wa kijadi kama ilivyoelezwa katika sura hii, ni mtindo ambao hauipi riwaya na uhakiki wake nafasi ya kutosha. Unafanya riwaya iwe inaelezwa upya badala ya kuonekana na kuweza kujengwa, kubomolewa na kujengwa upya. Hapa tumewaelewesha wanafasihi namna mpya ya kuichambua riwaya ambayo tunadhani itawasaidia zaidi na kuwapa nafasi pana zaidi ya kujibu maswali ya fasihi na hasa riwaya. Sura ya riwaya pendwa imetoa mwangaza kuhusu upande mwingine wa riwaya ambao haujapewa nafasi na kupata mashiko katika uhakiki wa riwaya. Hata hivyo, tumedokezea sababu zilizosababisha hali hiyo kwa kuonyesha tofauti ya riwaya pendwa na riwaya dhati. Hivyo kitabu hiki kinaweza kuwa cha manufaa sana kwa kumtambulisha mwanafasihi riwaya ya Kiswahili, kumwelimisha kuhusu uchambuzi wake na hali ya hivi sasa.
Kitabu hiki hakidai kuwa ndicho chenyewe tu ambacho kimekidhi malengo muhimu ya uhakiki wa riwaya au kuitoa picha nzima ya riwaya hiyo bila kasoro. Hata hivyo ni kitabu ambacho ni msaada mkubwa kwa wanafunzi, waalimu, wasomaji wa riwaya kwa jumla na hata waandishi. Ni kitabu ambacho kinatoa vidokezo maridhawa na wala sio sheria za kuweza kufurahia na/au kuielewa riwaya ya Kiswahili.
Ni vema pia kugusia kuwa pamoja na uhakiki wa kijadi, kumekuwa na ule wa Kisosholojia ambao ulikuja Afrika pamoja na kuko la Umarx. Uhakiki huo umekuwa na mkabala wa upembuzi na uyakinifu wa kihistoria, na kilele chake katika Fasihi ya Kiswahili kilikuwa katikati ya miaka ya sabini. Kati ya wafuasi wake wenye makini na walioumudu vizuri ni Mulokozi na, kwa kiasi fulani, Senkoro. Mkabala huu uliondokewa kusemwa kuwa ama ulielekea kutia uzito mkubwa upande wa maudhui na kuisahau fani, ama ulielekea kuingiza siasa (kidogo au sana) katika Fasihi, iwe katika kazi za sanaa au za uhakiki. Hata hivyo, ni uhakiki uliochangia kwa kiasi kikubwa katika kuipigisha hatua mbele Fasihi ya Kiswahili. Umuhimu wa uhakiki huu kifasihi na kijamii ni suala linalohusu majadiliano kama vile tu namna nyingine za uhakiki zinavyohitaji majadiliano juu ya usadifu wao na mafao yao.
Hali kadhalika, katika uhakiki 'mpya' uliojitokeza katika Fasihi ya Kiswahili sambamba na ule wa kimuundo ni ule wa kihemetiki na, kwa namna fulani, kukawa na dalili za ule tunaouita wa kimjenguo. Uhakiki wa kihemetiki umeletwa katika Fasihi ya Kiswahili na Kezilahabi katika joho la falsafa ya kidhanaishi.
Riwaya fupi ya Nagona ya mhakiki huyu, pindi ikichunguzwa kwa makini, inajitokeza kama ni jaribio la kuuthibitisha mkabala huo wa kihemetiki unaoonyesha mahusiano kati ya msanii, maudhui ya kazi yake na msomaji, na hatimaye kudai kuwa mwandishi ndiyo mdhibiti, ndiye kitovu, cha hayo yote. Na kwa nmi iwe hivyo? Kwa sababu inadaiwa kuwa maana halisi ya kazi ya fasihi (au sanaa) imo ndani ya msanii mwenyewe. Msimamo huu usingekubaliwa na Wanauyakinifu wa Ki-Marx.
Kuhusu uhakiki wa kiudadisi dalili zake zimejionyesha vizuri hadi sasa katika kazi mbili ndogo za J. Mbele (1988) (1989). Aina ya uhakiki huu ambao misingi yake imejengwa na wataalam kama vile Nietzsche na, baadaye, Jacques Derrida, kwa kiasi fulani inadhani, na hata kudai kuwa jadi au mikabala inayofuatwa na wengi katika jamii au taaluma si lazima iwe ndiyo sahihi. Ndiyo maana katika mifano miwili ya tahakiki za mkabala huo, Mbele anajaribu kuidadisi na kuisaili mikabala mitangulizi iliyozitazama hizo mada; anajitokeza na fikra zake mwenyewe zinazojaribu kuchochea udadisi ambao ama unathibitisha kinyume cha mikabala mitangulizi ama inaibua hoja zilizokuwa zimejificha hapo awali. Upungufu unaojitokeza haraka katika uhakiki huu ni ule wa mhakiki kuweza kupinga kwa ajili ya kupinga tu au kwa ajili ya kutaka kuchokoza hoja zaidi. Huku kupinga kunaweza kuwa kumewekwa kwa namna ambayo inaweza kupotosha. Mfano mzuri ni ule wa 'Mhakiki, Uandishi na Jamii', makala ambayo yanadai, kwa lugha nzuri tena inayoshawishi, kuwa mhakiki si muhimu katikajamii, ni mtu aliyejipachika tu. Lakini katika hali halisi hii si kweli, na mwandishi wa makala haya anajua kuwa anachokoza tu mawazo ya wasomaji ili waweze kumchunguza mhakiki kwa undani zaidi. Je matokeo yatakuwaje kwa wale wasiopenda kujifikirisha zaidi?
Fasihi ya Kiswahili, hususan kipehgele cha riwaya, kingali kikijitanua na kuzidi kulidhoofisha dai la Ortega Y. Gasset (1948) kwamba ni makosa kufikiri kuwa riwaya ni uwanja utakaoendelea kutoa namna mpya za riwaya pasipo kukoma. Riwaya ya Kiswahili inazidi kustawi kimaudhui, kifani na kinadharia; inazidi kubainisha kuwa waandishi wake wanazidi kuyapanua mawanda yao kwa njia ya kusoma riwaya zingine pamoja na tahakiki na, hali kadhalika, wahakiki wanazidi kutononoka katika uwanja wao kwa kusoma tahakiki na riwaya mbalimbali. Kwa jinsi hiyo riwaya ya Kiswahili inaendelea kwa kasi kubwa katika mbinu za uandishi na uhakiki wake.