MADA YA KWANZA: MAWASILIANO
KIDATO CHA KWANZA
MADA YA KWANZA: MAWASILIANO
Katika mada hii unatarajiwa kuelewa
fasili ya mawasiliano na jinsi mchakato wa mawasiliano unavyofanyika. Utaelewa
dhana ya lugha na vipengele muhimu vinavyokamilisha fasili ya lugha. Utaelewa
dhima kuu za lugha, matumizi na umuhimu wake. Vilevile katika mada hii
utajifunza juu ya lafudhi na matamshi mbalimbali ya watumiaji wa lugha ya
Kiswahili.
Lugha kama Chombo cha Mawasiliano
Mawasiliano ni mchakato wa
kuhawilisha taarifa kwa njia ya ubadilishanaji wa mawazo, hisia, malengo,
tabia, matarajio, mitazamo kupitia mazungumzo, ishara na maandishi. Ni
ubadilishanaji wa taarifa unaoleta maana baina ya pande mbili au zaidi ambazo
zinaweza kuwa viumbe hai au kinyume chake. Sasa hapa sisi tutajikita katika
mawasiliano yanayofanywa baina ya viumbe wanaotumia lugha (ambao kimsingi ni
binadamu).
Maana
ya Mawasiliano
Lugha ni nyenzo muhimu sana katika
mawasiliano ya binadamu. Ulishawahi kujiuliza kwamba mwasiliano yangekuwaje
pasipokuwepo lugha? Mwalimu angekua anatumia mtindo gani kukufundisha darasani
au wewe ungemwombaje kalamu rafiki yako? (Unasema ungewasiliana kama wanavyowsiliana
watu wasiosikia au kuzungumza?) Hao pia wanawasiliana hivyo kwa sababu wana
maarifa ya lugha.
Mafumbuzi ya kisayansi na
teknolojia, yote haya yasingewezekana pasipo kutumia lugha, usingeweza kusogoa
(kuchat) na marafiki zako kwenye facebook, usingeweza kumwandikia ujumbe rafiki
yako kupitia simu yako na kadhalika.
Umeona sasa jinsi lugha ilivyo
muhimu katika mwasiliano? Kabla hatujaona umuhimu huu hebu tuangalie
fasili/maana ya lugha.
Kuna mitazamo mbalimbali juu ya
fasili ya lugha lakini kwa ujumla lugha inaweza kufasiliwa kama mfumo wa
sauti za nasibu zilizokubaliwa na watu au jamii ili zitumike katika mawasiliano
yao ya kila siku ili kuelezea hisia, mawazo, matakwa na mahitaji yao.
Kulingana na fasili hii tunaweza
kubainisha maneno ya msingi yanayojitokeza katika fasili ya lugha, maneno hayo
ni pamoja na haya yafuatayo:
Lugha
ni mfumo
Kila lugha ya mwanadamu imeundwa
katika mifumo miwili mikuu; mfumo wa sauti na mfumo wa maana. Lugha huundwa kwa
sauti ambazo huunganishwa kuunda neno au sehemu ya neno, maneno nayo huungana
kuunda miundo mikubwa zaidi yenye maana kama virai, vishazi, sentensi na aya.
Mfano; k+u+k+u – kuku
Mtoto + anatembea – mtoto anatembea
Katika muunganiko huu wa maneno na
miundo mbali mbali, huwa kuna kanuni na sheria zinazodhibiti mfuatano wa kila
kipashio. Kuna kanuni zinazodhibiti mfuatano wa sauti, mfuatano wa mofimu,
mfuatano wa maneno na hata mfuatano wa sentensi. Kwa maana hiyo, lugha ya
mwanadamu ni mfumo wenye kanuni, sheria na taratibu maalumu ambazo zikikiukwa
basi kunakuwa hakuna utimilifu wa lugha husika. Sheria hizi zinazotawala
mpangilio wa viunzi vya lugha hiyo ndizo zinazowawezesha watumiaji wa lugha
fulani kuelewana.
Lugha
ni mfumo wa sauti nasibu
Lugha ni ya nasibu kwa maana kwamba,
hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya neno (kwa mfano jiwe) na kitu chenyewe
tunachotumia katika ujenzi na matumizi mengine (maana na kirejelewa). Hii ina
maana kwamba, maumbo ya ishara za kiisimu hayana uhusiano wowote au mfanano
wowote na maana ambazo tunayapa. Kwa mfano neno “jiwe” hakuna watu waliokaa na
kusema kuanzia leo hili litaitwa jiwe. Vile vile hakuna uhusiano wowote kati ya
neno “jiwe” na umbo linalorejelewa. Uhusiano wake ni wa nasibu tu na
hutofautiana kutokana na lugha moja na nyingine. Jiwe mnaliitaje katika lugha
yenu? Basi huo ndio unasibu wa lugha.
Lugha
ni maalumu kwa mwanadamu
Lugha ni chombo cha mawasiliano
ambacho amejaliwa binadamu tu na kwamba hakuna kiumbe mwingine ambaye si
binadamu mwenye uwezo wa kuzungumza na kutumia lugha. Hii ina maana kuwa kuna sifa
fulani za lugha za binadamu ambazo hazipatikani kwa kiumbe mwingine yeyote yule
isipokuwa mwanadamu. Ingawa ndege, mbwa, nyuki, tumbili wanaweza kuwasiliana,
mawasiliano yao huwa ni ya sauti au ishara ambazo kimsingi siyo lugha, pia huwa
yanadhibitiwa na hisia tu kama hofu, njaa, na ishara za kutoa taarifa. Binadamu
ana uwezo wa kujifunza lugha mbalimbali na kuitumia katika mazingira yake na
kitu ambacho wanyama hawawezi. Kwa mfano, ukimchukua paka wa china na kumleta
Tanzania atatoa sauti ile ile sawa na paka wa Tanzania kwa kueleza shida ile
ile au kutoa ishara ile ile.
Lugha
ni mfumo wa ishara
Uishara wa lugha unamaanisha kuwa
maneno huambatanishwa/huhusishwa na vitu, matendo,mawazo au hisia kwa
makubaliano ya unasibu tu. Vile vile, yale tunayoyasoma katika maandishi ni
ishara tu, maana zake lazima zipatikane katika muktadha wa mawasiliano. Hivyo
basi, tunapojifunza lugha lazima tufahamu mfumo wa alama za lugha hiyo na
kuelewa uhusiano uliopo kati ya ishara na vitu vinavyowakilishwa.
Lugha
hutumia sauti
Sifa kuu ya lugha ni kutumia sauti
ambazo hutengenezwa na ala za sauti. Pamoja na maendeleo ambayo mwanadamu
ameyafikia kwa sasa katika uandishi na uwasilishaji wa taarifa kwa kutumia
lugha sauti ndiyo msingi wa kila kitu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba:
- Mtoto hujifunza kuzungumza kabla hajajifunza kusoma na
kuandika.
- Mtoto hujifunza lugha moja kwa moja bila kufikiri
kadiri anavyokuwa
- Maandishi yalikuja baada ya mazungumzo
- Maandishi huwasilisha yale yanayozungumzwa
- Watu kwa kawaida hutumia muda mwingi kuzungumza kuliko
kuandika
Kuna mambo mengi ya muhimu katika
sauti za lugha ambayo hayawezi kuwasilishwa vema kwa kutumia maandishi. Mambo
hayo ni kama, kiimbo, toni, mkazo, kidatu; haya ni muhimu katika mawasiliano
lakini hayawezi kuwasilishwa kisawasawa kwa kutumia maandishi