MWINGILIANO WA MAANA KATI YA MANENO YA KISWAHILI YENYE UMBO SAWA
MWINGILIANO WA MAANA KATI YA MANENO YA KISWAHILI YENYE UMBO SAWA
Kwa Mukhtasari
HOMONIMIA ni hali ya maneno mawili au zaidi kuwa na umbo moja lakini maana zake zikawa tofauti. Mfano ni 'Barabara’ (likiwa na maana ya njia pana ipitiwayo na watu, wanyama na magari) na 'Barabara’ (likiwa na maana ya sawasawa kabisa au hali shwari) Massamba, 2004:17.
Ni dhana inayorejelea maumbo tofauti ya lugha yenye umbo sawa kifonetiki na maandishi sambamba.
Kwa mujibu wa Mgullu (1999:2), Homonimia ni maneno ambayo kimofolojia yanaonekana kuwa ni neno moja lakini kimaana ni maneno tofauti kabisa. Maana za maneno hayo hujulikana tu yanapotumiwa katika tungo.
Wakati ambapo polisemia inarejelea maana halisi ya kimsingi, homonimia inarejelea maana ya ziada kwa kuchunguza tofauti iliyopo kihistoria.
Ingawa hivyo, aghalabu huwa ni vigumu kubainisha iwapo tunashughulikia polisemia au homonimia.
Kamusi hutofautisha kati ya polisemia na homonimia kwa kuchunguza chimbuko na historia ya neno, iwapo inajulikana japo kwa mara nyingi huwa ni vigumu kuziwekea mipaka dhana hizo.
Homonimia za Kiswahili zinaweza katika misingi ya misingi homografu na homofonia.
HOMOGRAFU
Ni maneno mawili au zaidi yanayofanana kimaandishi lakini ni tofauti kimatamshi.
Katika Kiswahili, kuna homografu kisinkronia (kiwakati wa sasa) na homografu kidayakronia (kihistoria).
Homografu kisinkronia ni maneno mawili au zaidi yaliyokuwa homografu lakini yenye historia tofauti.
Hayawezi kufafanuliwa kietimolojia kwa kuwa hujitokeza kibahati nasibu tu.
Mfano:
(a) Mbuni (nomino 1) Ndege mkubwa wa mbugani asiyeweza kuruka lakini ana mbio sana.
(nomino 2) Mti uzaao matunda madogo ya kijani ambapo yakiiva huwa mekundu na hukobolewa na kusagwa ili kutengeneza kahawa.
(b) Mbu (nomino 1) Mdudu mdogo mwembamba ambaye huuma na kufyonza damu kutoka kwa mtu na kuambukiza magonjwa kama vile matende na malaria.
Shida za kuyapambanua maneno haya zinatokana na tofauti za mpumuo (aspiration) na shadda (stress) lakini Kiswahili hakitilii mkazo suala la mpumuo katika maandishi.
Mpumuo ungekuwapo, tofauti katika maneno kama vile 'mto’, 'basi’, 'mwiko’, 'chungu’, 'kaa’, 'panda’, 'ganda’, nk zingekuwa rahisi kutolewa.
Homografu kidayakronia ni zile ambazo uchunguzi wa kihistoria utaonyesha kuwa maneno hayo yalikuwa na uhusiano wa kipolisemia wakati mmoja.
Mfano:
(a) Mbaazi (nomino 1) Mmea uzaao vitumba vyenye mbegu ndogo zifananazo na fiwi, kunde, nk.
(nomino 2) Mbegu ndogo zinazotokana na mmea huo
(b) Mvinyo (nomino 1) Mti utambaao na huzaa matunda
(nomino 2) Kileo kinachotengenezwa kwa maji ya matunda yanayotokana na mvuke.
HOMOFONIA
Ni hali ya kutamka maneno sawa lakini yenye kutofautiana kimaana au kitahajia. Ni hali ya maneno kulandana kimatamshi lakini kutofautiana kimaandishi, kimaana na kihistoria kwa mfano katika Kiingereza 'one’ (nambari) na 'won’ (shinda), 'flower’ (ua) na 'flour’ (unga).
Baadhi ya homofonia za Kiswahili hubainika kwa njia ya Akronimu. Akronimuni ni neno linaloundwa kutokana na ufupisho wa herufi au silabi za mwanzo za majina kama vile, TATAKI - Taasisi ya Taaluma za Kiswahili .
(a) Ukuta – Ua wa mawe, udongo, nk, kiambaza
UKUTA – Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania
(b) Tapa – Enda huku na huko baada ya kufikwa na jambo fulani au kuwa na haja; hangaika
TAPA – Tanganyika African Parents’ Association
(c) Kamata – Shika
KAMATA – Kampuni ya Mabasi Tanzania.
(d) Kanu – Mnyama kama paka mwitu mwenye mkia mweupe, huiba na kula kuku sana.
KANU – Kenya African National Union. (Chama cha kisiasa nchini Kenya).
Upo ugumu katika kutofautisha polisemia na homonimia. Hii ni kwa sababu wakati mwingine homonimia hupata kugeuka na kuwa polisemia na polisemia pia aghalabu huweza kugeuka na kuwa homonimia.
Ingawa hivyo, homonimia hujitokeza tu inapokuwa kwamba maana husika hazina uhusiano wa aina yoyote katika wakati uliopo.
Kwa mfano, katika Kiingereza neno “mole” lina maana mbili: aina ya mnyama aitwaye 'fuko’ na pili ni baka jeusi kwenye ngozi.
Maana hizo zatokana na maneno mawili ambayo kutokana na mabadiliko ya kihistoria, yametokea kuwa neno moja ama kimatamshi, (mfano katika Kiingereza 'I’ na 'eye’) au kimaandishi, (mfano katika Kiingereza neno 'desert’ ambalo lina maana ya 'jangwa’ na 'kuacha au kuondoka mahali’)