Katika makala hii tutajadili maana ya fonolojia na maana ya isimumuundo kasha usuli wa nadharia ya isimumuundo. Katika kiini cha makala hiii ni Ubainishaji wa vipengele vya kifonojia na Ubainishaji wa mbinu za kimuundo pamoja na ufafanuzi wa mbinu hizo katika vipengele vya kifonolojia. Kisha tutahitimisha mjadala wetu.
Kwa mujibu wa Mugulu (1999) akimrejelea Fudge (1973) anasema kwamba fonolojia ni kiwango kimojawapo cha lugha fulani kilicho na vipashio vidogo zaidi kuliko vipashio vingine vyote vya lugha. Vipashio vya kifonolojiani fonimu na alofoni zake.
Dosari ya fasili hii ni kwamba haijafafanua kiwango kipi cha lugha ambacho kinahusika na fonolojia kwani lugha inaviwango mbalimbali.
Massamba (2010) anasema kuwa fonolojia ni tawi la isimu linalojishughulisha na mfumo wa sauti (asilia) za lugha. Hii inamaana kwamba, kila lugha mahususi inamfumo wake wa sauti ambamo maneno hujengwa. Ki ukweli fonolojia hujihusisha na namna sauti zinavyotumika katika maneno ya lugha mahususi katika kuleta maana.
Massamba na wenzake (2004) wanafafanua kuwa, fonolojia ni tawi la isimu ambalo hujishughusha na uchunguzi, uchambuzi na uainishaji wa sauti pambanuzi ambazo hutumika katika mifumo mbalimbali ya sauti za lugha za binadamu.
Massamba (2010), pamoja naMassamba na wenzake (2004), wanaonekana kufanana katika fasili zao juu ya fonolojia isipokuwa, Massamba na wenzake (2004), wameonesha kuwa fonolojia si tawi linalojihusisha na mfumo wa sauti tu, bali huzichunguza, huzichambua pamoja na kuziainisha sauti hizo.
TUKI (1990) wanasema kuwa, fonolojia ni tawi la isimu ambalo hushughulikia uchambuzi wa mfumo wa sauti zinazotumiwa katika lugha fulani.
Vilevile dosari ya fasili hii ni kwamba, imeegemea upande mmoja tu yaani uchambuzi wa mfumo wa sauti za lugha fulani na kusahau kuwa taaluma hii ya fonolojia haijikiti tu katika uchambuzi bali huzingatia uchambuzi, uchunguzi pamoja na uainishaji wa sauti hizo kama asemavyo Massamba na wenzake (2004). “fonolojia ni tawi la isimu ambalo hujishughusha na uchunguzi, uchambuzi na uainishaji wa sauti pambanuzi ambazo hutumika katika mifumo mbalimbali ya sauti za lugha za binadamu.”
Kwa mujibu waMatthews (2001)anafafanua kwamba, Isimumuundo ni tawi la isimu ambalo hutumika kama kihuzi cha kinadharia kinachochunguza au kuchambua na kuelezea muundo wa lugha kwa kuzingatia vipengele vya lugha pamoja na uhusiano wake katika kuunda kitu kikubwa zaidi.
Pia isimumuundo ni mkabala unaochambua na kufafanua mfumo wa lugha kama unavyojibainisha ukilinganisha na kipindi maalum katika historia.
Baada ya kuangalia fasili hizo ufuatao ni usuli wa nadharia ya isimumuundo kwa mujibu waMatthews (kishatajwa). Nadharia ya umuundo ilianzia Ufaransa miaka ya 1900 na mwanzilishi wake ni Ferdinand de Saussure katika dhana yake ya langue (umilisi) na parole (utendi).
Nadharia ya isimumuundo imejadiliwa na matapo makuu mawili yaani tapo la Ulaya na tapo la Marekani
Awali ya yote wanasimu wa awali walijaribu kuchunguza lugha kwa kulinganisha zaidi na historia. Ferdinand hakuridhika na ulinganishaji huo kwani aliona kwamba ulikuwa unajibu swali kuwa asili ya lugha hiyo ni wapi, lakini haikujibu swali kuwa hiyo lugha inamfumo gani.
Tapo la Ulaya lilitoa hoja kuu zifuatazo katika nadharia hii:
Lugha inamfumo, yaani lugha ni mfumo ambao una elemeti zinazotagusana.
Lugha ni mfumo wa alama: kwa mfano kelele ni lugha endapo tu zitawasilisha au kuelezea mawazo fulani, mfano dhana (dhahania), kiashiria na kiashiriwa.
Lugha hushughulika katika viwango viwili ambavyo ni langue (umilisi) na parole (utendi)
Baada ya tapo la Ulaya lilifuata tapo la Marekani ambalo nalo lilifafanua dhana ya umuundo au nadharia hii ya isimu muundo kama ifuatavyo: Hapo awali watu walijishughulisha na uchunguzi wa lugha za Marekani yenye asili ya kihindi, walikuwa wanaanthropolojia, lakini ilionekana kuwa hawakuwa na mbinu mahususi ambazo wangezifuata ili kuweza kufafanua lugha hizo.
Kutokana na mapungufu hayo wakatokea wanaumuundo wa kimarekani walioongozwa na Bloomfield ambaye yeye aliona kuwa uchunguzi wa lugha unapaswa kujikita katika kile watu wanachokisema. Hivyo basi walipendekeza hoja kuu zifuatazo.
Isimu ni sayansi fafanuzi; yaani inafafanua kile watu wanachokisema na sio kile wanachotakiwa kusema.
Kila lugha ni mfumo ulio na taratibu zake: lugha haipaswi kuchambuliwa kwa kutumia lugha nyingine, bali inapaswa kuchambuliwa kwa kutumia mfumo wake wenyewe.
Lugha ni mfumo ambao vipashio vidogovidogo zaidi huunganika kimpangilio ili kuunda vipashio vikubwa zaidi. Wanamuundo hawa walipendekeza taratibu ambazo walianza kuzitumia kwa kuchambua vipashio vidogo kabisa na kuviainisha na kuvipambanua katika ruwaza ambazo zilitumika kuunganisha ilikuunda vipashio vikubwa zaidi.
Maana haipaswi kuwa sehemu ya ufafanuzi wa kiisimu. Bloomfield na wafuasi wengine wa tapo hili waliona kuwa maana ni dhana ya kinasibu ambayo haiwezi kuchunguzika, kwa hiyo si ya kisayansi.
Taratibu za kutambua vipashio katika lugha ni lazima ziwe halisi na zenye kufuata taratibu maalum.
Baada ya usuli wa nadharia ya isimumuundo, vifuatavyo ni vipengele vya kifonolojia pamoja na mbinu za kimuundo katikaufafanuzi wa vipengele hivyo(kifonolojia) kwa mifano. Vipengele hivyo ni sauti (foni), alofoni, fonimu na silabi. Pia mbinu zitumikazo na wanaisimumuundo katika ufafanuzi wa vipengele hivyo ni mbinu ya uainishaji, sintagmatiki, paradigmatiki, moza, jozi pekee, mpishano huru, mgawanyo kamilishani, mgawanyo wa kiutoano, na ubadala.
Kwa kuanza na mbinu ya uainishaji. Kwa mujibu wa Kamusi ya Karne ya 21(2011), uainishaji ni “upangaji wa vitu au viumbe katika makundi kwa mujibu wa jinsi vinavyohusiana.”
Hivyo basi, katika muktadha wa kifolonojia tunaweza kusema kuwa, uanishaji ni upangaji wa vipashio katika makundi kulingana na nduni zake bainifu au uhusiano wake. Kwa mfano: kosonanti za Kiswahili ziliainishwa kulingana na namna zinavyotamkwa, mahali pa matamshi na hali ya nyuzi sauti.
Kwa mfano: konsonanti “m”, “n”, “g” waliziainisha kama nazali pamoja na kuzipa sifa zake kama vile; [m] [n]
+kons +kons
+nazali +nazali
+midomo +ufizi
+ghuna +ghuna
Hivyo kila sauti waliipa nduni za ziada na nduni bainifu, zilizotofautisha fonimu moja na nyingine. Kwa mfano fonimu; “s” na “l”
[s]=kikwamizi [l]= kitambaza
+kons +kons
+kikwa +kitambaza
+ufizi +ufizi
-unazali -unazali
-ghuna +ughuna
Mbinu ya pili sintagmatiki; sintagmatiki ni ubadilishanaji wa nafasi ya vipashio vya kifonolojia (fonimu) kwa njia ya mlalo. Hivyo katika lugha ya Kiswahili vipashio kwa kawaida hupangwa katika mfuatano maalum wenye mahusiano, ambao ni;
K+I – b+a = ba mfano katika neno “baba”
K+K+I – c+h+a = cha mfano katika neno “chama”
K+K+K+I – m+b+w+a = mbwa mfano katika neno “mbwa”
Hivyo basi mbinu hii ya sintagmatiki imejikita zaidi katika kuangalia mpangilio sahihi wa sauti katika lugha husika kiulalo. Na kamwe huwezi kukuta neno “ngoma”limeandikwa ngmoa, au kata – ktaa.
Vilevile hata muundo wa silabi za Kiswahili hubainishwa idadi yake kwa kufuata mbinu ya kisintagmatiki, yaani kuhesabu kwa ulalo kuanzia kushoto kuelekea kulia. Mfano neno “Anajichekelesha” neno hili lina silabi 7 ambazo ni $$ A$$ na $$ ji $$ che $$ ke $$ le $$ sha $$ 1 2 3 4 5 6
7
Mbinu ya tatu ni mbini ya paradigmatiki, neno paradigmatiki limetokana na neno paradigm likiwa na maana ya kundi la vitu vinavyoweza kukaa pamoja kutokana na mahusiano yao.
Hivyo paradigmatiki kwa mujibu wa The New American Dictionary paradigmatiki ni mahusiano wima baina ya vipengele vya kiisimu vinavyounda muundo mkubwa zaidi kama vile sentensi. Kwa hiyo, nadharia hii hubainisha vipashio kiuwima zaidi. Kwa mfano;
m
mw nafasi iliyokaliwa na /m/ inaweza kukaliwa na mu pia mw
w
Pia katika muundo wa lugha ya Kiswahili sauti huweza kubadilishana nafasi kiparadigmatiki (wima) na kuunda neno jingine lenye maana tofauti na lile la awali. Kwa mfano katika neno “pata” tunaweza kupata maneno yafuatayo kwa kubadilisha fonimu (konsonanti) kiuwima;
/p/+/a/+/t/+/a/ = (pata)
/b/+/a/+/t/+/a/ = (bata)
/k/+/a/+/t/+/a/ = (kata)
MAREJEO:
Jewell, E. J and A. Frank. (2005). The New Oxford American Dictionary. (2nd Edit).Oxford University Press. New York.
Mdee, J. S. na wenzake (2011). Kamusi ya Karne ya 21.Longhorn Publishers (K) Ltd. Nairobi.
Massamba, D.P.B na wenzake. (2009).Fonolojia ya Kiswahili Sanifu (Fokisa): Sekondari na Vyuo.Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Massamba, D.P.B. (2010). Phonological Theory: History and Development. Institute of Kiswahili Studies (IKS). Dar es Salaam.
Metthews, P. (2001). A short History of Structural Linguistics. Cambridge University Press. British.
McCarthy, J.J. (1989). “Linear Order in Phonological Representation.”Linguistics Department Faculty Publication Series Paper 45.http:// scholarworks.umass.ed/linguist_faculty_pubs/45
Mgullu, R.S. (1999).Mtalaa wa isimu: Fonetiki, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Longhornpublishers.Ltd. Nairobi.
TUKI, (1990).Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.