NADHARIA ZA MAANA

Udhaifu wa nadharia hii ya kichocheo-mwitiko ni kwamba, kichocheo kimoja kinaweza kusababisha utokeaji wa viitikio viwili au zaidi. Kwa mfano mvua imeanza kunyesha, mama anawaamrisha watoto waingie ndani. Watoto wanaitikia kwa kukimbia kwenda ndani ya nyumba.
           Kichocheo……………………mvua
           Tamko………………….ingia ndani
           Kiitikio ……………….watoto kuingia ndani ya nyumba upesi.
Katika mfano wetu huu viitikio vinaweza kuwa; watoto kuchukua ndoo na sufuria na kuanza kuteka maji, kuingia ndani na kuchukua miavuli, kuingia ndani na kukoka moto (Matinde, 2012:259).

Maneno mengi katika lugha hayataji vitu vinavyoonekana, kwa hiyo basi maneno hayo hayawezi kusababisha mwitikio wa msikilizaji. Mfano wa maneno hayo ni kama vile njaa, busara, upendo, uchoyo na huruma (Alston, 1967). Hii ni kwa sababu maneno dhahania hayawezi kuelezwa kwa kutumia nadharia hii.

Pia wakati mwingine wanalugha hawaitiki maneno kwa vitu vinavyowakilisha maneno hayo (Holm na Karlgren, 1995:4). Hii ina maana kuwa kujenga maana ya kinyambo kwa kutumia nadharia ya kichocheo mwitiko inalazimisha upekee wa vinyambo au maneno husika. Ukweli ni kwamba wanajamii huitikia vitu vinavyowakilisha maneno hayo.

Aidha semi nyingi sana katika lugha hazidhibitiwi na kichocheo katika muktadha peke yake. Kwa mantiki hii nadharia ya kichocheo mwitiko inakosa mashiko kwani wakati mwingine mtu anaweza kuulizwa swali na asijibu au akajibu kinyume kabisa na swali. Kwa mfano ni kawaida kwa Mtanzania kusema nakuja wakati anaonekana anakwenda.

Nadharia ya masharti – ukweli husisitiza dhana ya ukweli katika ujasiri wa maana, hivi kwamba maana sharti iwe ya kweli na ukweli huo ubainishwe bayana. Nadharia hii iliasisiwa na wanamantiki na wanafalsafa, kisha ikafafanuliwa na wanaisimu.
Mfano (a) Ukweli wa kihistria
i/ Muungano wa Tanzania na Zanzibar 1964
           ii/ Rais wa kwanza wa Tanzania ni J. K.Nyerere
          (b) Ukweli wa maarifa ya kiulimwengu
Ukweli huu hutokana na uhalisia wa kiulimwengu ambao kila mwanajamii anakuwa nao. Mfano shairi huundwa na beti, mistari, vina na mizani au mwanamke hujifungua.
       
(a)ukweli wa kiisimu
Ukweli huu hubainishwa kupitia mfuatano wa maneno katika sentensi na usahihi wa mfuatano huo.
      i ) Hadija aliolewa na Kanyansa (sahihi)
      ii) Kanyansa aliolewa na Hadija ( si sahihi)

Nadharia hii hushughulikia sentensi arifu tu, kwa kuwa ndizo hutoa kauli ambazo zinaweza kuwa kweli au si kweli. Hivyo ni vigumu kubashiri maana ya sentensi swalifu na amrishi kwa maswali na amri haviwezi kubainisha ukweli au si kweli. Vilevile ni vigumu nadharia hii kutumiwa kubainisha ukweli au wigo wa sentensi tendezi, kwani sentensi tendezi hazielezi matukio. Kwa mfano; Ninakubali kuwa yeye si jambazi. Katika sentensi hiyo ni vigumu kuamini au kutoamini ukweli wa kauli hiyo. Sentensi moja au zaidi huweza kuibua seti nyingi za masharti ukweli hali ambayo huifanya nadharia hii kuwa na mzunguko usiokikomo katika ufasiri na ufafanuzi wa maana.

Nadharia hii hutegemea zaidi maarifa ya kiulimwengu imani, mielekeo na tajiriba pana kuhusu kila tungo. Sentensi inayodokeza maarifa ya kiulimwengu ni ya kijumla kuhusu taaluma mbalimbali kama vile; maji hayana rangi- itakuwa kweli endapo tu maji hayatakuwa na rangi. Hivyo basi ukweli huu ni wa kiulimwengu kwa sababu kila mwanajamii anakuwa nao.

Nadharia ya masharti-ukweli hujikita zaidi katika maswala ya taaluma ya mantiki na kuvuka upeo wa taaluma ya isimu maana. Hii ni kwa sababu tu nadharia hii inajikita zaidi katika kujua maana ya neno. Kwa mfano nini maana ya kifo na ukweli ni nini. Hivyo basi kutokana na mifano hiyo hapo juu nadharia hii huenda mbele zaidi na kuvuka upeo wa taaluma ya isimu maana.

Nadharia ya utendaji au matumizi ilianzishwa ili kutatua upungufu uliojitokeza katika nadharia zilizotangulia. Nadharia hii inasema kwamba si sahihi kuangalia maana ya neno au kisemo kuwa si kitu ambacho kinajitosheleza. Msisitizo upo wa maana ya neno hupatikana katika utumizi uliotumika, kwani neno halina maana moja. Mwasisi wa nadharia hii ni Ludwing Wittgenstein, yeye aliona nadharia hii itatoa upungufu ulijitokeza katika nadharia zilizopita (Matinde, 2012:260). Katika kitabu cha Philosophical Investigation (1963) anasema ni kosa kubwa kuangalia kama kitu au kiumbile kamili. Hivyo alipendekeza kuwa maana ya neno iangaliwe kwa kuzingatia muktadha wa neno au kisemo jinsi kilivyotumika. Kwa maana hiyo maana au kisemo ni matokeo au athari inayopatikana.

Neno moja huweza kuwa na maana nyingi kutokana na muktadha au kutokana na matumizi yake. Kwa kuangalia muktadha wa jamii kuna baadhi ya maneno ambayo huwa na maana katika jamii fulani. Kwa mfano matumizi ya tumsifu Yesu kristo huendana na muktadha wa ibada au waumini wawili hasa wa kikatoriki. Usemi huu utakapotumiwa msikitini utazua utata wa imani za kidini.

Pamoja na  ugumu uliopo katika kufasili maana ya maana kwa kutumia nadharia mbalimbali zilizojadiliwa na wataalamu wengi, kila nadharia ina ubora na mapungufu yake katika kufasili maana ya maana katika kiwango cha neno na sentensi. Kwa hiyo maaana ya maana inabaki kuwa dhana telezi kutokana na utata wa kufasili dhana hii. Ni vema tafiti mbalimbali ziendelee kufanyika ili kuziba pengo la  ugumu wa kufasili maana ya maana.

                                                   MAREJEO
Alston, W. P. (1967) Meaning The Encyclopedia of philosophy, vol 5 Macmillan  and  Free press,
                                PaulEdwards, Editor in Chief, (pp.233-241), imesomwa tarehe 11/04/2014 saa 22:00
                                kutoka www.sciencedirect.com/science/article.

Baron, J. (1972) Semantic Components and Conceptual development, Elsevier imesomwa tarehe 11/04/2014
                                saa 22:15 kutoka www.sciencedirect.com/science/article.

Bloomfield, W. L. P. (1983) LanguageLondon –New york.

Filp, H (2008) What is Semantics, What is Meaning, imesomwa tarehe 11/04/2014, saa 20:00 kutoka
                                www.sciencedirect.com/science/article.

Habwe, J. na Karanja, P. (2007) Misingi ya Sarufi ya Kiswahili, phoenix publishers LTD, Nairobi.

Holm, P. and Karlgrey, K. (1995) The Theory of meaning and Different perspective on information System,
                                Stockholm UniversityMarburg.

Lyons, J. (1981) Language; Meaning and ContextFontana Paperbacks.

Matinde, R. S. (2012) Dafina ya Lugha Isimu na Nadharia, kwa Sekondari, Vyuo vya Kati na Vyuo Vikuu,
                               Serengeti Education publishers (T) LTD, Mwanza.

Mdee, S. J. na wenzake (2011) Kamusi ya Karne ya 21: Kamusi ya Kiswahili yenye Uketo zaidi Katika Karne
                               Hii, Longhorn publishers LTD, Nairobi.

Sengo, T. S. Y.M (2009) Fasihi za Kinchi, The Regestered Trustees of Al Amin Education and Research
                               Academy, Dar es Salaam.

Wamitila, K. W, (2003) Kamusi: Istilahi na Nadharia, Kenya Focus Publications LTD, Nairobi.

Powered by Blogger.