Uandishi wa hotuba na risala

Uandishi wa hotuba na risala

Risala ni hotuba fupi inayosomwa mbele ya kiongozi kwa niaba ya kundi fulani la watu hasa hasa wanafunzi, wafanyakazi, washiriki, wanachama, mafundi; na Hotuba ni insha ambayo hutoa maneno halisi ya mzungumzaji/kiongozi anapozungumzia hadhira, kuhusu jambo fulani. Katika mada hii utajifunza jinsi ya kuandaa risala au hotuba kwa kuzingatia muundo unaohusika kwa kila kipengele.
UANDISHI WA HOTUBA

Hotuba ni insha ambayo hutoa maneno halisi ya mzungumzaji/kiongozi anapozungumzia hadhira, kuhusu jambo fulani. Insha ya hotuba huandikwa katika hali ya usemi halisi na mwandishi hatakiwi kuweka alama za kunukuu anapoanza insha yake.

Hotuba inaweza kutolewa na kiongozi wa kisiasa, utawala, kidini, kikundi, shirika fulani, daktari, n.k. Hadhira katika hotuba husheheni wageni waalikwa, wanachama, wafuasi, wananchi, n.k ambao wanahusishwa katika mada inayorejelewa katika hotuba hiyo.

Mundo wa hotuba
Hutuba inakuwa na muundo ufuatao:

Anwani
Anwani, mada au kichwa cha hotuba hurejelea mada ya hotuba.  Pia mada inaweza kutaja hadhira.
  • Hotuba ya Waziri wa Afya kuhusu madhara ya ukimwi kwa wananchi.
  • Hotuba ya Mwalimu Mkuu kwa Wazazi

Utangulizi
  • Anza hotuba yako kwa kuwatambua waliohudhuria mkutano (hadhira).
  • Wataje kwa majina/vyeo vyao kuanzia yule wa cheo cha juu hadi wa chini, mabibi na mabwana. Kumbuka kwamba hauhitajiki kuwasalimia. Kuwatambua kwa majina pekee kunatosha.
  • Jitambulishe kwa hadhira yako hasa ikiwa unazungumzia hadhira isiyokujua au wageni.
  • Tanguliza mada yako. Kwa mfano:

Waziri wa Kilimo, Mkuu wa Wilaya, Mhe. Mbunge, wanachama wa kikundi hiki cha Mazingira, mabibi na mabwana. Ni matumaini yangu kwamba nyote mu buheri wa afya. Mimi ni mwakilishi wa Kikundi cha Mazingira na jioni ya leo kuna jambo muhimu ambalo ningependa sote tulifahamu ili kuboresha mazingira yetu kwa …

Kiini
  • Hakikisha kuna mtiririko wa hoja kuanzia mwanzo hadi mwisho
  • Ujumbe wako wote unapaswa kuwa katika usemi halisia wala si wa taarifa.

Tamati
  • Hakikisha kwamba mwisho wa hotuba yako unatambulika.
  • Unaweza kumaliza kwa shukurani

UANDISHI WA RISALA

Maana ya risala
Risala ni hotuba fupi inayosomwa mbele ya kiongozi kwa niaba ya kundi fulani la watu hasa hasa wanafunzi, wafanyakazi, washiriki, wanachama, mafundi n.k ili kutoa maelezo ya haja zao mbalimbali na mahitaji yao au kuonyesha msimamo wa kundi hilo kwa kiongozi.

Mambo muhimu Katika utungaji wa risala
  • Utanguizi

  • Cheo cha kiongozi anayehusika
  • Kundi linalowakilishwa

  • Kiini
  • Maelezo ya hali halisi ya maswala na msimamo wa kundi linalowakilishwa.
  • Mapendekezso na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa.

  • Hitimisho
  • Shukrani

Tanbihi: Kama vilivyosemwa awali risala ni hotuba fupi lakini inachukua mambo muhimu tu na kuyaeleza. Hivyo risala yenyewe huwa ni maelezo ya muhtasari kwa jambo linalohitaji maelezo marefu Katika hotuba. Utungaji wa risala unahitaji uangalifu sana na lugha ya heshima iliyo wazi kueleweka kwa kiongozi.

Mfano wa risala:

Ndugu Mgeni rasmi, Walimu, Wanafunzi wenzetu, Wazazi, Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana.

Kwa niaba ya wanafunzi wa kidato cha nne, tunayo heshima na furaha kubwa , kukukaribisha ili ushiriki nasi katika siku hii muhimu na kusikia mafanikio mbalimbali kwa kipindi chote cha masomo yetu hapa shuleni.

Shukrani zetu za pekee na za dhati ziende kwa uongozi mzima wa Shule na walimu wetu wote kwa jinsi walivyojitoa kwa moyo  wa kutufundisha, hivyo tumefundishika vyema; kwasababu tupo tofauti sana na  tulivyokuja hapa mwezi januari 2009.

Ndugu mgeni rasmi, tulianza kidato cha kwanza tukiwa wanafunzi 120; wasichana 60 na wavulana 60. Mpaka leo tunapohitimu tupo wanafunzi 90; kati yao wavulana ni 43, na wasichana 47. Wengine wameshindwa kuhitimu nasi siku ya leo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo utoro, ujauzito na kuhama shule. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema wa Baraka kwa ulinzi wake kwetu hadi leo hii tunahitimu  kidato cha nne.

Ndugu mgeni rasmi,  elimu hii ya kidato cha nne imetupatia  msingi mzuri wa kujiunga na Elimu ya juu, pia imetujengea uwezo mzuri wa kujitambua na kufikiri, kufanya kazi vizuri na kufanya maamuzi sahihi; pia imetuwezesha sisi wanafunzi kupata elimu ya mambo mbalimbali  kupitia masomo tunayo fundishwa hapa shuleni, mfano; tumepata elimu ya uraia, historia ya mambo mbalimbali katika nchi yetu na dunia kwa ujumla, pia tumeweza kupata uelewa kuhusu  afya na magonjwa, usalama katika mazingira yetu, Kilimo, Maumbile ya nchi, hali ya hewa, misitu, na viwanda. Vilevile  tumeelewa umuhimu wa kusoma vitabu mbalimbali kwa lengo la kupata ujuzi wa kuinua uchumi wetu wa taifa.

Ndugu mgeni rasmi, mafanikio hayo yamepatikana kwasababu ya ushirikiano mzuri kati yetu na walimu wetu. Tangu tujiunge na shule hii tukiwa kidato cha kwanza tumefanya majaribio na mitihani ya mara kwa mara jambo lililo tusaidia kuinua taaluma yetu.Tunawashukuru sana  walimu wetu, tuna waahidi kufanya vizuri katika mitihani yetu ya Taifa ya kidato cha nne mwaka huu, na Mungu awabariki sana.

Ndugu mgeni rasmi, tumepata changamoto mbalimbali wakati wa maisha yetu ya kielimu hapa shuleni, kama ifuatavyo;

Ndugu mgeni rasmi, tuna changamoto ya upungufu wa vitabu vya kiada na ziada; hii imepelekea kushindwa kujisomea vizuri, kwani kitabu kimoja kinatumiwa na wanafunzi zaidi ya ishirini (20).

Ndugu mgeni rasmi, changamoto nyingine ni upungufu wa vifaa vya maabara, hii inapelekea  kuchangia kifaa kimoja, hivyo tuna tumia muda mwingi sana kujifunza na kumuelewa mwalimu.

Ndugu mgeni rasmi, pia kuna changamoto ya upungufu wa walimu, hasa wa masomo ya sayansi; hii imepelekea  kutomaliza ‘syllabus’ kwa wakati.

Ndugu mgeni rasmi, pia kuna changamoto ya upungufu wa samani za shule, kama vile; madawati kwa ajili ya wanafunzi, viti na meza kwa ajili ya walimu; hii imepelekea baadhi ya wanafunzi wenzetu kukaa wawili kwenye dawati moja.

Ndugu mgeni rasmi,  maji ni changamoto hapa shuleni, kwani shule haina kisima cha maji, hii imepelekea shule kununua maji kwa gharama kubwa, ambayo hayatoshelezi mahitaji ya shule, kama vile usafi; hususani kwa upande wa vyoo, bila kuwa na maji ya kutosha tutapata magonjwa ya mlipuko, kama vile kipindupindu.

Ndugu mgeni rasmi, changamoto ya vifaa vya michezo; kama unavyojua kuwa michezo ni afya, shule yetu ina upungufu mkubwa wa vifaa vya michezo kama vile; mipira ya miguu, pete na mikono, pia hatuna milingoti ya chuma kwaajili ya magoli ya viwanja vya michezo yote tunayocheza hapa shuleni.

Ndugu mgeni rasmi, tunashukuru uongozi wa shule hii, walimu na wazazi ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya shule yetu; kwa upande wa masomo ya sayansi; shule imeweza kutenga chumba kimoja cha darasa kitumike kama maabara japo kuwa kuna upungufu mkubwa wa vifaa.

Ndugu mgeni rasmi, tunayo matumaini kwamba maombi yetu umeyasikiliza na utayaatekeleza, maana tunajua kwamba wewe unaweza kupitia Hlimashauri unayo isimamia, asante sana.

Mwisho tunaomba msamaha wa dhati toka moyoni mwetu kwa Walimu, Wanafunzi wenzetu na Wazazi pale tulipoenda kinyume na matazamio yenu, kwani watu wakiishi pamoja tofauti lazima ziwepo, tunatumaini mtapokea msamaha wetu, nasi hatuna jambo lolote baya kwenu.

Ndugu mgeni rasmi, tuna kushukuru sana kwa kufika katika Mahafali yetu, kwani tunatambua kuwa unamajukumu mengi ambayo umeyaacha na kuwepo hapa kwaajili yetu.
Powered by Blogger.