Historia ya sintaksia kwa ujumla ulimwenguni pamoja na mwendelezo wake katika kushikamana na Sintaksia ya Kiswahili.














































Historia ya sintaksia kwa ujumla ulimwenguni pamoja na mwendelezo wake katika kushikamana na Sintaksia ya Kiswahili.






 Suali hili litajikita katika kuangalia historia ya sintaksia kwa ujumla ulimwenguni pamoja na mwendelezo wake katika kushikamana na Sintaksia ya Kiswahili.
 Hivyo vipengele mbali mbali vitaangaliwa katika kukamilisha historia hiyo, kama: maana za istilahi mbali mbali zilizojitokeza katika suali hili, asili na chimbuko, waasisi wa taaaluma hii, mikabala pamoja na hitimisho juu ya muendelezo wake katika kushikama na sintaksia ya Kiswahili mpaka kufikia miaka ya sasa.
Kwa kuanzia na maana;
Kwa mujibu wa BAKIZA (2010: 117) neno historia lina maana ya taarifa za mtu, jambo au eneo katika wakati uliopita.
Kwa upande wa TUKI (2004: 115) wao wanalifasiri neno historia kuwa ni elimu maalum inayohusiana na mambo yaliyopita.
Kwa uapnde wa neno asili:-
Kwa mujibu wa BAKIZA (2010: 12) neno  asili lina maana ya chimbuko la mtu, kitu au jambo.
Kwa upande wa TUKI (2004:14) wao wanalifasiri neno asili kuwa ni mwanzo wa mtu au kitu.
Kwa mujibu wa Bakressa (1992) asili ni mwanzo wa kitu au mtu.
Massamba na wenzake, (1999) wameeleza juu ya neno asili kuwa ni jinsi kitu ama jambo lilivyotokea ama lilivyoanza.
 Hivyo asili ya neno Sintaksia limetoholewa kutoka lugha ya Kingereza “Syntax” ambapo asili ya neno hilo linatokana na maneno mawili ya Kigiriki ambayo ni “Syn” likiwa na maana ya mjumuiko au kuweka pamoja na “taxis”  likiwa na maana ya mpangilio au utaratibu au muundo. Hivyo maneno haya yanapoungana pamoja tunapta neno moja likiwa na maana ya taaluma ya kuchanganya maneno. Awali taaluma hii ilijulikana kama tawi la sarufi lilozungumzia jinsi maneno yanavyopangika ili kuonesha muambatano wa maana.
Maana ya chimbuko limeelezewa na wataalmu mbali mbali kama hivi ifuatavyo:-
Kwa mujibu wa BAKIZA (2010: 51) inaeleza kuwa chimbuko ni pahala jambo lilipoanzia na baadaye kuenea.
Kwa upande wa TUKI (2004:48) wao wanalifasiri neno chimbuko kuwa ni mwanzo au asili.
Kwa mujibu wa Bakhressa (1992) anasema chimbuko ni mwanzo, asili au chanzo.
Massamba na wenzake, (1999) chimbuko lina maana ya sehemu au mahali ambapo kitu kimeanzia.
Hivyo, chimbuko la taaluma ya sintaksia ni Ugiriki ambako ndiko ilikoanzia katika lugha ya Kigiriki kisha kuhamahama na likaendelea katika sehemu nyengine kama vile Rome katika lugha ya Kilatini kisha Kisanskriti na Kisha kuenea sehemu nyengine kama vile Ulaya na Marekani (Malmkjaer, 2009).
Kwa upande wa maana ya Sintaksia wataalamu wengi wameizungumzia dhana hii kama hivi:-
Maana ya Sintaksia kwa mujibu wa TUKI (2004: 377) ni tawi la isimu linalojihusisha na uchanganuzi wa taratibu na kanuni za mahusiano baina ya maneno katika tungo.
Kwa mujibu wa BAKIZA (2010: 371) wanasema sintaksia ni tawi la isimu linaloshughulikia ufafanuzi wa kanuni zinazoongoza uhusiano wa maneno katika sentensi.
Kwa mujibu wa Khamis (2011) anasema Sintksia ni tawi la lughawiya fafanuzi linalohusu taaluma ya uchambuzi na uchanganuzi wa muundo wa matumizi ya sentensi na vijenzi vyake katika lugha mahsusi. 
Baada ya kuangalia maana ya sintaksia kwa mujibu wa wataalam tafauti, kuna sababu mbali mbali zilizopelekea taaluma hii kuibuka. Miongoni mwa sababu hizo ni kama hizi zifuatazo
Sababu kubwa iliyopelekea kuanzishwa kwa taaluma hii ni wanalughawiya wa mwanzo kutaka kujua asili ya lugha kama lugha ni tukio la maumbile au tukio la unasibu (nature or nuture). Katika mjadala huu Plato alikuwa na msimamo kuwa lugha ni tukio la maumbile kwa sababu miongoni mwa hoja zake ni kwamba binadamu anazaliwa na viungo ambavyo vinamuezesha kuweza kuzungumza lugha ambavyo hujulikana kama ala za sauti, viungo hivyo vilivyowekwa vinamuezesha binadamu huyo kuweza kuwa na lugha mfano namna meno, ulimi, midomo miwili (lower lip and upper lip) nakadhalika. Kwa upande mwengine mwanafunzi wa Plato ambae ni Aristotle yeye anamsimamo wa kuwa lugha ni tukio la unasibu (nurture). Hoja zake ni kuwa binadamu anazaliwa na akili ambapo akili hiyo humuwezesha kujifunza  mambo kutokana na uzoefu na maingiliano na watu mbali mbali pia kuizoeya dunia yake hali hii inamuezesha binadamu huyo kupata lugha.(  Sleeper, 2006).
Habwe na Karanja (2004) wanaeleza kwamba sababu nyengine zilizopelekea kuibuka kwa sintaksia ni kuainisha miundo ya sentensi iliyomo katika lugha.
Mfano katika lugha yakiswahili
 “Mama anapika chakula”.
Miundo: sentensi hii inaundwa kwa maneno matatu:
mama,anapika na chakula na kwamba kila neno lina kategoria yake.
Kategoria za maneno yanayounda sentensi : mama na chakula ni nomino za umoja,na anapika ni kitenzi kilicho katika wakati uliopo.
Sentensi hii ina kiima na kiarifu.
Mama ni kiima na anapika chakula ni kiarifu.
Sababu nyengine nikwamba, Ili kuonyesha uhusiano wa maneno uliomo katika sentensi.
 Mfano.  Anakula    maji
Pamoja na ukweli kuwa kitenzi kula  ni elekezi( kinaweza kubeba nomino lakini sababu za kisemantiki zinakataa) huwezi kula maji.
Sababu nyengine ni kwamba kujaribu kuonyesha jinsi sintaksia za lugha mbalimbali zinavyoweza kuchangia nadharia ya lugha kwa ujumla
Hivyo, kwa mujibu wa  Malmkjaer (2009) sintaksia baada ya kuanzia huko Ugiriki ambako inaaminika kuwa muanzilishi wa taaluma hii ni Plato ambapo alifuatwa ni wanalughawiya wengine kama vile Aristotle, Panin na Protagoras, Varro, Donatus and Priscian. Taaluma hii iliendelea kukua na kuenea ambapo kama ilivyoelezwa kwamba ilianzia katika lugha ya Kigiriki na kufuatia lugha nyengine kama vile Kilatini, Kisanskriti ambapo pia badae iliweza kuenea katika sehemu mbali mbali za dunia ambapo iliweza kufika katika sehemu za Ulaya, Marekani na Ufaransa ambako katika maeneo yote hayo kuliibuka wanalughawiya mbali mbali kama vile Ferdinand de Saussure wa Mswidi, Chomsky wa Marekani, Bloomfield na wengineo.
Hivyo kutokana na ukuaji na ueneaji huo wa sintaksia imepelekea kupatikana kwa mikabala tafauti ya sintaksia ambapo mikabala mikubwa mashuhuri inayojulikana ni ule mkabala wa kimapokeo au wa zamani au wa kale na ule mkabala wa kisasa au kimamboleo. Hivyo, mikabala hii tunaweza kuiona wakati, wafuasi na hata sifa za mikabala hii na namna inavyotafautiana kama hivi inavyofuata:-
Kwa kuanzia na mkabala wa kimapokeo, mkabala huu ina sadikika kuwa, kwa mujibu Matinde (2012:211) ananeleza kuwa sarufi mapokeo ni mkabala wa awali ulioshughulikia sarufi ya lugha. Waasisi wake walikuwa wanafalsafa wa ugiriki. Habwe na karanja (2004:129), anataja wanafalsafa hao kuwa ni Plato, Aristotle, Protagoras, Dionysius Thrax, na Priscian. Katika kipindi hiki Sarufi ilishughulikiwa sambamba na falsafa, dini,fasihi,balagha na mantiki. Pia, mwanaeleza kuwa Plato ailiuwa wa mwanzo kugawa sentensi katika sehemu kuu mbili mtenda (subject) na prediketa (predicate). Hatimaye Aristotle akaendeleza kazi ya mwalimu wake kwa kusema sentensi inaweza kuundwa na aina za maneno mbali mbali, yeye ametaja aina tano ambazo ni; nomino, kitenzi, kivumishi, kiunganishi na kielezi.
Miaka ya 100 K K, mwanasarufi myunani Dionysus Thrax aliandika kitabu cha sarufi ambacho ni cha awali kilichoitwa “Techne Grammatike (The art of grammar)”. Mwansarufi huyu alianisha aina saba za maneno ambazo ni nomino, kitenzi, kivumishi, kiwakilishi, kiunganishi, kielezi na kiingizi (Kihisishi). ( Malmkjaer, 2009).
Pia, Massamba na wenzake (1999) wanaeleza kwamba sarufi mapokeo zilikuwa ni sarufi elekezi ambazo zilisisitiza kanuni na nini cha kusema na wajua lugha. Watu wasiojua kanuni za lugha wanapaswa kujifunza kutoka kwa wanaojua sarufi ya lugha. Wanaendelea kusema kuwa, wanaojua lugha hupaswa kutunga kanuni za sarufi.
Sarufi za kwanza zijulikanazo hii leo ni za lugha ya Kigiriki, ambayo ilikuja kufuatwa utaratibu wake na lugha ya Kilatini. Kilatini kilichukua utaratibu wa Kigiriki katika kuichunguza na kuielezea lugha hiyo, ikafatia lugha ya Kisanskriti ambayo nayo ilifuata mfumo huu wa Kigiriki na kufuatia lugha nyengine za Ulaya. Na hatimaye lugha zote kufuata mfumo mzima wa lugha ya Kigirki au Kilatini, na ilisemekana kuwa lugha yoyote isiyofuata mfumo wa Kilatini ilichukuliwa kama ni lugha iliyopotoka. Kwani wanalughwawiya mapokeo waliamini kuwa lugha zote duniani zinafata msingi mmoja wa sarufi ya Kilatini.
Baada ya kupita miaka kadhaa utaratibu uliokuwa ukitumika katika kuichambua na kuielezea Sarufi ya Kigiriki ukatumika pia katika kuichambua na kuielezea sarufi ya Kilatini, lugha ambayo kwa muda wa karne nyingi zilizofuatia ndiyo iliyokuwa lugha ya taaluma na utawala katika jamii nyingi za Ulaya. Kwa kuwa lugha za Kigiriki na Kilatini zilikuwa na mnasaba mmoja, yaani zilikuwa na asili moja, haikiuwa vigumu kutumia utaratibu uliotumika kuchambua na kuielezea sarufi ya Kigiriki katika kuichambua na kuielezea sarufi ya Kilatini. 
Aidha, kwa sababu lugha ya Kilatini hapo zamani ilikuwa maarufu sana waandishi wengi wa mambo ya sarufi waliamini kwamba taratibu zilizokuwa zikitumika katika kuianisha au kuichambua sarufi ya lugha hiyo ndizo zilizokuwa sahihi na ndizo zilizostahili kutumiwa katika uchambuzi na uainishaji wa lugha yoyote ile. Hii ndiyo sababu sarufi za lugha nyengine zilizoandikwa hapo zamani zilifuata taratibu na muundo wa sarufi ya Kilatini.
Mkabala huu wa kimapokeo una sifa mbali mbali ambazo zimeijenga sintaksia ya wanasarufi wa kale ambazo ni hizi zifuatazo:-
Sifa kubwa ya mkabala huu ni kuwa ni elekezi (Strazny, 2013).  yaani zikisisitiza usahihi wa lugha kwa kuonyesha sheria ambazo hazina budi kufuatwa ili mathalani kufanya muundo fulani wa sentensi usemekane kuwa ni sahihi. Kwa maneno mengine hii ni sawa na kusema kuwa sarufi hizo za kimapokeo zilikuwa zikisisitiza jinsi ambavyo lugha ilipaswa kuwa na kuonyesha jinsi ambavyo lugha haikupaswa kuwa. Massamba na wenzake (1999)  pia wanaizunguimzia hoja hiyo kwa mfano sentensi “kitabu kimeibiwa”,Kwa mujibu wa sarufi mapokeo sentensi hii si sahihi Kwani kitabu ni kitu kisicho na uhai iweje kipewe sifa ya ubinadamu ambayo ni kuibiwa pia wao wanaamini kuwa kauli ya kutendwa inawakilishwa kwa kutumia mofimu “w” iweje leo itumie kiambishi “iw”  kikiwa bado kinaonesha hali ya kutendwa. Hivyo, Usahihi wa sentensi hii kwa mujibu wa sarufi mapokeo ni “kitabu kimeibwa” mifano mengine “Mtoto aliyepotea ameonekanwa” na si “ameonekana” nakadhalika.
Sifa nyengine ni kuwa sarufi mapokeo iliweza kuelezea kategoria kwa misingi ya maana ya sentensi. Kwa kueleza kuwa sentensi ni utungo wenye maana kamili. Kwa mfano; “Mwanamke yule mzuri kweli kweli” kwa mujibu wa mkabala huu tungo hii inahesabiwa kama ni sentensi yenye kuleta maana kamili. Na sentensi haikuwa na lazima ya kwamba kuwepo kwa tendo au utendaji ndani yake. Pia,  walieleza kitenzi kuwa ni neno linaloashiria kitendo fulani, na nomino ni majina yanayotaja vitu, watu na mahala, kivumishi ni neno linaloelezea au kutoa maelezo juu ya nomino na halkadhalika aina nyengine za maneno zilielezwa kwa mnasaba kama huo.
Pia, mkabala huu ulitilia maanani suala zima la ujinsia. Kutokana na kuwa lugha ya Kilatini ilikuwa na sifa ya ujinsia wa baadhi ya maneno kama vile uke, ume na kati, hivyo kila lugha ili lazimika kufuata sifa hiyo. Kwa mfano Kingereza cha zamani kiliweza kufuata hali hii kwani zipo nomino ambazo zilikuwa na sifa ya uke nyengine sifa ya ume na nyengine kati (neutral), ambapo hadi sasa athatri hiyo kwenye Kingereza ipo kwa kiasi kidogo hasa kwa maneno yenye ujinsia wa kike na ume. Kwa mfano; kiwakilishi “she” kinatumika kuashiria jinsia ya kike na kiwakilishi “he” kilitumika kuashiria jinsia ya kiume.
 Mfano wa sentensi “she is cooking” ikiwa na maana ya yeye mwanamke anapika.
“He is playing football” ikiwa na maana ya yeye mwanamme anacheza mpira wa miguu.
Mifano mengine ni kwamba yapo majina katika Kingereza ambayo yanonesha ujinsia wa uke au ume mfano wa majina hayo ni kama vile actor (muigizaji kiume) na actress (muigizaji wa kike), hero (shujaa wa kiume) na heroine (shujaa wa kike), fiancé (mchumba wa kiume) na fiancée (mchumba wa kike).
Vilevile, mkabala huu ulijikita zaidi katika lugha ya maandishi na ndio maana watu walikuwa wanaelekezwa namna ya kutumia lugha na si watu ambao wakiiongoza sarufi ya lugha
Udhaifu wa mkabala huu mkubwa ni kwamba, taratibu za uchanganuzi wa lugha hazikuzingatia lugha ya kuzungumza kama ilivyo leo hapa ina maana yakuwa wao hawakuwaangalia watu (jamii) wanazungumza kitu gani ili wapate sheria za lugha badala yake walikaa na kuandika sheria ambazo zinatakiwa zitumike na jamii nah ii ndo sababu ikasemekana kuwa waliangalia zaidi lugha ya maandishi kuliko ya mazungumzo. Wanasarufi mapokeo walienzi na kuchunguza lugha ya maandishi. Hivyo basi ni dhahiri kwamba mkabala huu unaangukia katika mitazamo ya kifalsafa. Hivyo kiujumla mkabala wa kimapokeo ulijikita zaidi katika maandishi pamoja na kumuelekeza mtumiaji lugha sheria za lugha, na namna ya kutumia sheria hizo pasi na kuenda kinyume.  (Malmkjaer, 2009).
 Hivyo basi ni wazi kuwa katika sarufi hii ya mapokeo tunakutana na mikabala miwili inayoangukia katika mkabala huu ambayo ni sarufi ubongo na sarufi kama kaida za kiisimu.
Kadri utafiti katika lugha mbali mbali ulivyozidi kusonga mbele ikadhihirika kwamba vigezo vya uchambuazi na uainishaji wa sarufi za lugha nyengine, hasa zile ambazo hazikuwa na uhusiano wowote wa kimnasaba na lugha ya Kilatini. Kutokana na ukweli huo wanalughawiya wa sarufi za lugha nyengine wakaamua kuachana na kigezo hicho cha lugha ya Kilatini na kuanza kuichunguza kila lugha kwa upeke wake wakizingatia na kuongozwa na vigezo vya muundo wa lugha inayohusika.
Pamoja na ukweli huo lakini kulikuwa na  athari  zilizotokana na sarufi za lugha na sarufi za lugha za Kigiriki na Kilatini amabzo ziliendelea kutumika katika uchambuzi wa lugha mbali mbali, athari ambazo baadhi zinajitokeza hadi hii leo.  Moja wapo ya athari hizo ni istilahi zilizotumika kama mitajo ya maumbo au dhana mbali mbali katika sentensi, kama vile; nomino, vivumishi, kielezi nakadhalika. Matumizi ya istilahi hizo yalibakia kutokana na umuhimu wake; sababu ni kwamba baadhi ya istilahi hizo zinahusu dhana ambazo hujitokeza takribani katika lugha zote za ulimwengu zijulikanazo.  Mkabala huu wa kimapokeo inasemekana ulifikia kilele chake kwenye karne ya 18 na 19 (Massamba na wenzake, 1999).
Kutokana na udhaifu ambao ulijitokeza katika mkabala huu kama ulivyoelezwa hapo juu ni kwamba wanalughawiya wapya waliofuata wakati huo walikuja na mkabala mpya ambao ni mkabala wa kimamboleo au wa kisasa au kileo.
Kwa kawaida mkabala huu  wa kimamboleo huhusishwa na  mwanalughawiya mashuhuri wa mwanzo ambaye ni Ferdinand De Saussure ambaye ni Mswidi anayetambulika kama ni muanzilishi wa mkabala huu wa kimamboleo uliyoibuka mnamo karne ya kumi nane (18) na kumi na tisa (19). Mkabala huu ulianza kuibuka huko Ulaya na Marekani. Wafuasi wa mwanalughawiya huyo katka mkabala huu ni kama vile Noam Chomsky, Bloomfield, Edward Sapir na wengineo.
Mkabala huu umekuja kuleta marekebisho juu ya uchambuzi na ufafanuzi wa lugha na wa sarufi ya lugha pamoja na kupinga kuwa sarufi ya lugha moja na lugha nyengine haziwezi kufanana isipokuwa zile lugha zenye asili moja kwa mfano kama vile ilivyokuwa kwa sarufi ya Kigiriki na Kilatini kuwa na srufi moja kwa sababu asili yao ni moja.
Hivyo, mkabala huu ulijikita zaidi na lugha kiufafanuzi; yaani sarufi katika mtazamo wa kisasa hujishughulisha na kuchambua vipengele vya sarufi kama vinavyojitokeza katika lugha ya wasemaji na jamii Fulani ya watu bila ya kujali kama utaratibu wa wasemaji katika jamii hiyo unakubalika katika jamii nyengine au haukubaliki. Hii ina maana kwamba katika mtazamo huu si kazi ya mwanalughawiya kuhukumu usahihi wa lugha  (Malmkjaer, 2009) na (Massmba na wenzake, 1999).
Katika mkabala huu una maana kwamba sarufi za kileo hujishughulisha na kila aina ya lugha yaani hazijibani katika aina moja tu ya lugha kama ilivyokuwa katika sarufi mapokeo.
Sifa kuu ya  mkabala huu ni kwamba umejikita zaidi na lugha kiufafanuzi  (Malmkjaer, 2009). Hapa ina maana ya kuwa kile kinachosemwa na jamii ndicho ambacho mwanalughawiya anapaswakukifafanua katika maandishi yake hivyo umejikita zaidi katika lugha ya mzungumzo.
Pia, mkabala huu haujikiti na uchambuzi wa sarufi ya lugha moja kuweza kutumika kwa lugha zote. Hapa ina maana ya kuwa kila lugha inachambuliwa peke bila ya kuhusishwa na lugha nyengine isipokuwa zile zenye asili moja.
Katika kuzungumziwa na wanalughawiya mbali mbali kutokana na kukua kwake, kuenea na kupita kwa wakati katika makbala huu tunapata mikabala mengine kama vile sarufi miundo na sarufi geuza
Mwanzoni mwa mkabala huu ulianza mkabala wa sarufi muundo au miundo ambao ndio haswa unaoshikamanishwa na mwanalughawiya wa mwanzo wa mkabala wa kimamboleo ambaye ni Ferdinand De Saussure ambapo kazi yake ya mwanzo inayojuilikana kama “Course de Linguistique Ge͂neral ( A  Course in general linguistics).  Iliyochapishwa mnamo miaka ya 1916/1915 kazi hii hakuiandika yeye isipokuwa baada ya kufariki wanafunzi wake walizikusanya notes zake ambazio aliziacha kwenye maandishi (Script) na kuandika kitabu hicho wakati yeye ameshafariki  (Malmkjaer, 2009)..
Desaussure alikuja na nadharia hii ya kimamboleo huku akitoa hoja yakwamba:-
Uelezaji wa elementi za kisarufi kwa misingi ya kimaana inasababisha utata. Hivyo akaja na nadhria ya sarufi miundo ili kupunguza matatizo hayo. Kwa mfano dhana ya sentensi kwa wanalughawiya mapokeo ni utungo wenye maana kamili hivyo kupitia maana hii tunaweza kupata maana katika hata neno au kirai ambapo kiuhalisia si sentensi. Hivyo yeye akazungumzia dhana kama hii kimuundo kuwa lazima iwe na utendaji ndani yake.
Pia, kuondosha dhana ya kuwa lugha Fulani ni bora kuliko lugha nyengine.
Vilevele, sarufi ya kale ilikuwa haingalii mahusiano ya sentensi moja na nyengine. Hivyo, sarufi miundo imekuja kutatua tatizo hili.
Sababu nyengine ya  kuibuka nadharia hii ni kuja kueleza lugha badala ya kuelekeza  (Malmkjaer, 2009)..
Katika mkabala huu wa kimapokeo baada ya mwanalughawiya De Saussure kuja na nadharia ya sarufi miundo mwanalughawiya mwengine mashuhuri ambaye ni Noam Chomsky alikuja na nadharia nyengine ambayo ni nadharia geuzi au sarufi geuzi au sarufi umbo mnamo miaka ya (1957) ni Mmarekani ambaye ameshiriki kwa kina katika uchambuzi wa lugha.
Sababu zilizopelekea mwanalughawiya huyu kuleta nadharia hii ni kwamba:-
Sarufi mapokeo na sarufi miundo zilichambua sentensi kijujuu bila ya kutathmini mahusiano yake ya ndani ( Chomsky, 1957).
Sarufi mapokeo hazikuwa na tabia ya kuonesha kuwa sentensi ya kauli ya kutenda na kutendwa zinatokana na na muundo mmoja wa ndani.
Sarufi mapokeo zilitawaliwa zaidi na nadharia elezi na hivyo ilishindikana kupatikana kwa nadharia fafanuzi. Chomsky anaamini ya kwamba msemaji mzawa wa lugha ana ujuzi unaomuwezesha kutumia lugha na sio taratibu ambazo zimewekwa ili zimuongoze mtu katika kutumia lugha. Kwani nadharia ya kimapokeo  ilijikita zaidi kuangalia katika kuweka sheria , namna gani mtu aitumie lugha yake (Prescriptive) ila nadharia yakimamboleo imekuja zaidi kuelezea  ni namna gani watu wanavyoitumia lugha  yaani (Descriptive)  hivyo iliichunguza lugha kwa wajibu wa wazawa wa lugha hiyo wanavyoitumia.
Nadharia elezi inachunguuza sentensi katika hali mbili; yaani katika muundo wa nje (sheria za kisarufi) na muundo wa ndani (maana ya sentensi).


Muendelezo wake katika kushikamana na sintaksia ya Kiswahili.
Sintaksia imeweza kufika Afrika Mashariki kutokana na wageni mbalimbali ambao walikuja katika bara hili kutoka nchi za Ulaya na kwengineko duniani  watu wa kwanza kujishughulisha na sarufi za Kibantu ni Wamisionari, na Wazungu ambao walihitaji kuzielewa vizuri lugha hizo ili wazitumie kwa mahitaji yao. Kwa mfano, katika shughili zao za kidini.
Baadaye wakoloni nao, wakajishughulisha nazo kwa madhumuni ya kuzitumia katika shughuli zao za utawala. Kutokana na athari za sarufi za lugha zao, ambazo zilikuwa na athari nyingi za sarufi ya Kilatini, walipoanza kuandika juu ya sarufi ya lugha ya Kiswahili Wamisionari hao wakawa wanatumia utaratibu waliouzoea katika lugha zao.
Baadaye ilidhihirika wazi kuwa utaratibu huo ulikuwa haufai kutumika katika kuzichambua au kuziainisha sarufi za lugha za Kibantu. Kwa mfano, lugha zao zilikuwa zinatumia utaratibu wa kuonyesha jinsia katika maneno; yaani baadhi ya maneno yalikuwa katika jinsi ya kike, mengine katika jinsia ya kiume, na mengine katika jinsia ya kati. Utaratibu huu haumo kabisa katika lugha za Kibantu ikiwemo lugha ya Kiswahili.
Kuibuika kwa waandishi wa lugha ya kiswahili na sarufi yake.
Waandishi wa mwanzo walioibuka juu ya lugha ya Kiswahili na saufi yake walikuwa kama ni wageni kama ilvyoelezwa hapo awali kwamba ndio walionza kujishughulisha na sarufi ya Kiswahili yaani ya lugha za Kibantu.
Kuna wataalamu mbali mbali ambao waliandika vitabu mbali mbali. Kwa mujibu wa Massamba na wenzake (1999) ametaja wataalamu wa mwanzo waliojishughulisha na sarufi ya Kiswahili na vitabu vyao ambao ni hawa wafuatao:-
Kwa mfano, Reichat, A. na M. Kuesters, ambao waliandika kitabu cha Elementary Swahili Grammar (1926), Ashton, E.O. ambaye aliandika kitabu cha Swahili Grammar (Including Intonation) (1940), Kapoka, E.B. ambaye aliandika Sarufi ya Ufasaha, I. Vihusiano, II. Miao (1959), Loogman, A. ambaye aliandika kitabu cha Swahili Grammar and Syntax (1965), Maw, J. ambaye aliandika kitabu cha Sentences in Swahili: A Study in their International Relationships (1969),  Askofu Edward Steere, ambaye aliandika kitabu cha Handbook of Swahili Language (1980), Broomfield, G. W,ambaye aliandika kitabu cha sarufi Kiswahili (1990), na wengine waliofuati
Miaka ya sitini hadi miaka ya sabini mwishoni mwishoni (1969 – 1977) kulikuwa hakuna vitabu au maandishi mengine yoyote muhimu juu ya sarufi ya Kiswahili.

Mnamo mwaka (1978) waafrika walianza kujishughulisha na uchambuzi wa lugha kwa mfano  Nkwera, F.M.V aliandika kitabu kinachitwa “ Sarufi na Fasihi katika Sekondari na Vyuo”  (1978). Baada ya kitabu hicho cha Nkwera kuchapishwa kukawa hakuna kitabu kingine cha sarufi ya Kiswahili kilichochapishwa bali kuna makala chache ambazo ziliandikwa kwa mfano  wataalamu waliondakia ni Mkude, D (1983) pia Khamis, A. M., Wesana-Chomi na wengineo.
Mnamo mwaka (1983) Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) ilichapisha Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu, pia Mgulu (1999) aliandika kitabu cha Mtalaa wa Isimu, manamo mwaka (1999) Massmba na wenzake waliandika Sarufi miundo ya Kiswahili Sanifu (SAMIKSA). Na wengineo.
Pia, mnamo miaka ya elfu mbili hadi sasa kuna vitabu kadhaa ambavyo vimechapishwa, vitabu hivyo ni kama vile;  Mgullu, (2001), Massmba na wenzake walitoa matoleo mengine ya  Sarufi miundo ya Kiswahili Sanifu (SAMIKSA) mnamo 2004,  Khamis, A. A. (2003),  kitabu kinachitwa Kiswahili sekondari na vyuo,  Habwe na Karanja (2004), ambao waliandika kitabu cha Misingi ya sarufi, Khamis, A. A, (2011), ameandika kitabu cha Uchambuzi wa Kiswahili Fasaha na Matinde, R. (2012), ameandika kitabu cha Dafina ya Lugha, Isimu na Lughawiya.
Hii hiyo ndio historia ya Sintaksia ulimwenguni na mshikamano wake na lugha ya Kiswahili na hadi sasa jitahada kubwa katika skuli na vyuo mbali mbali vianendeleza sintaksia ya Kiswahili kwa kufundishwa shuleni pia kuwa ni miongoni mwa kozi katika vyuo vikuu pia na wanalughawiya mbali mbali wanaendelea kujishughulisha na sintksia ulimwenguni kwa ujumla na hata katika tamthilia ya Kiswahili.
Hivyo, Licha ya kuwa historia ya taaluma ya sintaksia imepitia katika vipindi tafauti na kuonesha ubora wa kila kipindi pamoja na kushikamana na taluma ya sintaksia ya kiswahili, bado jitihada kubwa za utafiti  zinahitajika kufanywa ili kuondoa kasoro zinazojitokeza juu ya taaluma hii ya sintaksia kwa mfano, hadi sasa katika kuzichanganua sentensi, inafika pahali kunakuwa na mvutano kwamba ni upi mtazamo sahihi wa kufuata kama ni ule wa kimapokeo au wa kimamboleo kutokana na nafasi zinavojitokeza




MAREJEO
Bakhressa, S. K. (1992). Kamusi ya maana na matumizi. Nairobi: Oxford University Press.
 Chomsky, N. (1957). Syntactic structures. United States: Mouton

Khamis, A. A. (2011). Uchambuzi wa Kiswahili Fasaha.(Sarufi na Lughawiya).Zanzibar:                                  Kiwanda Cha Uchapaji Cha Chuo Kikuu Cha Elimu Chukwani, Zanzibar
Khamis, M. A na Kiango, G. J. (2002).Uchanganuzi wa Sarufi ya Kiswahili. Dar es    salaam: TUKUHabwe na Karanja. (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers.
 Malmkjaer, K. (2004). Linguistics Encyclopedia 2nd  ed. London and New York:                                   outledge
 Malmkjaer, K. (2009). The Routledge Linguistics Encyclopedia 3rd ed.UK: Routledge

Massamba, D.P.B na wenzake. (1999). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu:                                                           Sekondari na Vyuo. Dar es salaam:TUKI. 
Matinde, R.S. (2012). Dafina ya Lugha, Isimu Na Nadharia; Kwa Sekondari, vyuo                             vya Kati na vyuo vikuu. Mwanza: Serngeti Educational Publishers (T)                     LTD.
 Sleeper, A.  A. (2006). Speech and Language. United States: Infobase Publishing

TUKI, (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es salam: Oxford University Press.
Powered by Blogger.