KUKITANDAWAZISHA KISWAHILI KUPITIA SIMU ZA KIGANJANI: TAFAKARI KUHUSU ISIMUJAMII ALDIN MUTEMBEI










KUKITANDAWAZISHA KISWAHILI KUPITIA SIMU ZA KIGANJANI: TAFAKARI KUHUSU ISIMUJAMII ALDIN MUTEMBEI Utangulizi Mojawapo ya matokeo ya utandawazi ni kuwapo kwa simu za kiganjani1 na matumizi yake. Siku hizi nchini Tanzania mawasiliano ya simu yamekuwako kwa wingi kuliko ilivyokuwa tangu wakati wa uhuru hadi katikati ya miaka ya tisini. Mahali ambapo hakukuwa na mawasiliano kabisa, kama sehemu nyingi za vijiji vya Tanzania, siku hizi kuna mawasiliano kwa njia ya simu hizi za kiganjani na lugha inayotumika katika mawasiliano haya ni Kiswahili. Lugha ya Kiswahili inayotumika katika simu hizi ni ya kiutandawazi na pengine si rahisi kuiona nje ya wigo huu wa kiutandawazi ambao pia unajumuisha mawasiliano kwa barua pepe, na maongezi katika tovuti. Katika lugha hii ya kiutandawazi, watu huwasiliana kwa kutumiana matini fupi fupi zenye mchanganyiko wa maneno na namba, na hivyo kuunda lugha tofauti na iliyozoeleka katika jamii nyingine
Mbali na lugha hii katika simu, barua pepe, na Tovuti, Kiswahili kimeshuhudia pia matumizi ya Sheng hasa miongoni mwa vijana. Lugha hii ipo kwa wingi nchini Kenya ambapo wataalamu wa isimu na lugha wamekwisha kuiandikia Kamusi (Mbaabu 2003), na hata makala (Mokaya 2006; Momanyi 2009). Lugha hii pia inatumika hasa katika programupendwa za vijana katika stesheni za radio na TV katika Afrika mashariki. Ingawa lugha kama 1 Simu ya Kiganjani pengine inaitwa ‘simu ya mkononi’, au ‘rununu’
KUKITANDAWAZISHA KISWAHILI KUPITIA SIMU ZA KIGANJANI 199 Sheng imefanyiwa utafiti na imeandikwa, lugha hii ya kiutandawazi inayojichomoza sasa kupitia katika barua pepe, simu za kiganjani na maongezi katika Tovuti, bado haijavuta – kwa kiasi kikubwa, shauku ya wataalamu na wapenzi wa lugha hata kuifanyia utafiti. Makala chache kuhusu suala hili zimeongelea lugha hii katika mawanda tofauti. Kwa mfano, Butts na Cockburn (2001) wameandika wakitathmini utumaji wa matini (texting) kama mbinu ya mawasiliano. Waligundua kwamba, utumaji wa matini fupi fupi ni desturi inayokuwa haraka hasa miongoni mwa vijana. Na kuwa kati ya Januari na Disemba 2000 matini fupi fupi (SMS) zilizotumwa ziliongezeka kwa haraka kutoka matini bilioni nne na kufikia bilioni kumi na tano kwa mwezi. Waliona kuwa matini kama hizo zitakuwa zimeongezeka na kuwa bilioni 200 kwa mwaka ifikapo Disemba 2001. Mtaalamu aliyeandika kuhusu aina ya ujumbe na uundwaji wa lugha mpya ni Crystal (2008a; 2008b). Katika makala yake, aliyoiita Texting (hapa ninaiita ‘Umatinishaji’), anasema kuwa umatinishaji ni jambo jipya kabisa ambalo sasa linaelekea kupata lugha yake. Anaelezea kuwa katika umatinishaji, lugha mpya aliyoiita textspeak inakua kwa haraka hasa miongoni mwa vijana. Makala yake hii ni ya msingi sana katika mjadala wetu. Hata hivyo, makala ya Crystal iliongelea umatinishaji katika lugha moja tu ya Kiingereza, na wala haikuonesha athari ya lugha hii “textspeak” au lugha tandawazi katika nadharia za isimujamii. Suala kubwa tunalolijadili katika makala hii ni changamoto zinazoletwa na lugha hii katika Isimujamii, hasa kuchanganya msimbo (lugha) na kubadili misimbo (lugha) (code mixing and code switching) au kama asemavyo King’ei “kuchanganya ndimi na kubadilisha ndimi” (2010: 24). Tangu maandishi ya akina Blom na Gumperz (1972), suala hili la kuchanganya msimbo na kubadili msimbo, limeshughulikiwa sana na wanaisimujamii. Waliolieleza kwa kina ni pamoja na Labov (1973), Trudgill (2000), Meyerhoff (2006), na Nilep (2006) na hasa zaidi utafiti na machapisho mbalimbali ya Myers-Scotton (1990, 1993a/1997, 1993b, 1993c, 2002). Hata hivyo, kwa wote hao ukimtoa Crystal (keshatajwa) hakuna aliyeshughulikia kwa upana lugha ya simu za kiganjani; lugha ambayo hapa tumeiita ‘lugha tandawazi’. Kwahiyo mwelekeo wa makala hii ni utafiti wa matumizi ya lugha hii tandawazi kwa kuangalia simu za viganjani na athari yake katika nadharia za isimujamii. Madhumuni yetu ni kuangalia matumizi ya lugha ya Kiswahili katika simu za viganjani. Kwa vyovyote vile, matumizi ya Kiswahili cha leo katika simu yanafungua nafasi kwa matumizi ya lugha-pendwa yanayosababishwa na utandawazi. Je Kiswahili cha kesho, tunaweza kubashiri kitakavyokuwa na hivyo kukiandaa ili jamii ikipokee na kuendelea kukitumia? Ingawa Crystal hadhani kuwa lugha hii ya simu itaathiri lugha ya kawaida ya Kiingereza, inawezekana matokeo yakawa tofauti kwa lugha ya Kiswahili. Tukiangalia nyuma na kuitalii historia ya makuzi ya lugha ya Kiswahili, tunaona kuwa Waswahili wa miaka iliyopita walifanya kazi kubwa kukiandaa Kiswahili cha leo. Misingi iliyojengwa miaka ya nyuma ndiyo iliyosimamisha nguzo za Kiswahili cha leo. Changamoto kubwa katika kukua kwa kasi kwa lugha inaletwa na sayansi na matumizi ya teknolojia: vipengele viwili vinavyosukumwa mbele na utandawazi. Kwahiyo, ili kujiandaa na ukuaji huo wa kasi, na ALDIN MUTEMBEI 200 mwelekeo wa lugha na kuutawala, hatuna budi kuihakiki ‘lugha tandawazi’ kama hivi vinavyoibuliwa leo na simu za kiganjani hasa miongoni mwa vijana. Tutafanya hivyo kwa kuangalia mawasiliano miongoni mwa jamii za Tanzania tukijadili nafasi ya Kiswahili katika mawasiliano hayo. Aidha tutaibua changamoto katika vipengele vya isimujamii ambapo katika lugha tandawazi, tunaona upya unaotutaka tuziangalie tena tafsiri na maana ya kubadili au kuchanganya msimbo. Utandawazi na Mawanda ya matumizi ya simu Jamii nyingi za Kitanzania kama zilivyo nyingi katika Afrika, bado zinaishi vijijini ambako hakuna umeme. Aidha katika vijiji kama hivyo, hakukuwa na mawasiliano ya ‘simu za mezani’. Kwahiyo, ilikuwa haiyumkiniki kuwa na mawasiliano kwa njia rahisi bila kuwepo kwa miundombinu hasa umeme na simu. Upatikanaji wa simu za viganjani, na kukua kwa matumizi yake kumeleta mabadiliko makubwa na kurahisisha mawasiliano. Matumizi ya simu hizi mijini na vijijini ni mojawapo ya matokeo chanya ya utandawazi. Simu hizi za viganjani zinatumika kwa wingi miongoni mwa wanajamii bila kujali umri, jinsia, elimu au mahali mtu atokako. Wanajamii hawa huwasiliana kwa hutumia ‘lugha tandawazi’, yaani lugha ya maandishi iliyochanganywa na namba huku ikifupishwa na pengine kuchanganywa zaidi ya lugha mbili tofauti. Kutokana na ukweli huu swali letu la kwanza ni je lugha tandawazi inayotumika katika mawasiliano ya simu inatumiwa na nani hasa katika jamii? Je inatumiwa na wote (kama walivyotajwa hapa juu) au matumizi yake yanajipambanua kutokana na umri, jinsia, elimu au mahali pa watumiaji? Swali jingine ni je, tunaweza kuwa na sheria za lugha hii katika mawasiliano? Je mawasiliano haya yanaingia katika mundo wa isimujamii uliokwisha kuwapo au yanaanzisha muundo mpya? Maswali yote haya yanahitaji utafiti wa kina wa uwandani ili kuweza kujibiwa kiuyakinifu; makala hii ni ya kiuchokozi kuanzisha mjadala kama huo. Utafiti wa awali wa watumiaji wa lugha tandawazi kwa jiji la Dar es Salaam (Mutembei 2010), ulihusisha vijana wenye umri wa kati ya miaka 14 na 18 toka shule za Jangwani, Azania, Tambaza, Makongo, Jitegemee na Mbezi. Mawasiliano ya vijana hao wa shule yalilinganishwa na mawasiliano ya wafanyakazi wenye umri kati ya miaka 40 na 55 ambao walichaguliwa toka Ofisi mbalimbali katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo cha Ardhi, Chuo Kikuu kishiriki cha Chang'ombe na Chuo Kikuu cha Sayansi za Tiba – Muhimbili. Sehemu zote mbili, ile ya shuleni na ile ya Vyuoni zilifanana kwa kuwa zote ni sehemu za utoaji elimu. Wote walichukuliwa kuwa ni watu wenye uelewa na wanajitahidi kwenda na wakati wakiathiriwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Katika utafiti huo, tuligundua kuwa wengi wa watumaji wa lugha tandawazi ni vijana kutoka shule za sekondari. Katika jumla ya vijana 60 ambao walikubali kutupatia mawasiliano mbalimbali waliyoyafanya na vijana wenzao, ni kijana 1 tu ambaye hakuwa na wingi wa mchanganyiko wa namba, maneno, ufupishaji na mchanganyiko wa lugha mbili KUKITANDAWAZISHA KISWAHILI KUPITIA SIMU ZA KIGANJANI 201 hasa za namba. Na kati ya wafanyakazi 60 ambao walikubali mawasiliano yao yaangaliwe kama data ya utafiti, ni 4 tu ambao walikuwa wamechanganya namba, maneno na ufupishaji, lakini hata hawa hawakuchanganya lugha mbili. Bila shaka utafiti kama huo ukiweza kufanyika ukihusisha watu wengi zaidi na wa kada mbalimbali unaweza kutupa majibu sio tu kuhusiana na vipengele vya isimujamii, bali hata athari za lugha tandawazi hasa kwa mustakabali wa lugha ya Kiswahili. Ni kweli kwamba kuenea kwa simu mahali pengi na kuongezeka kwa matumizi yake kumerahisisha sana mawasiliano. Aidha ni kweli kuwa matumizi hayo yanakuza Kiswahili – lugha inayotumika katika mawasiliano hayo. Tukiukubali ukweli huu, hatuna budi pia kuuangalia ukweli mwingine unaojitokeza. Matumizi ya lugha tandawazi kwa njia ya simu na barua pepe yanaweza kuwa na athari kubwa katika lugha ya Kiswahili nje ya miktadha ya mawasiliano haya ya simu na barua pepe. Kabla hatujaangalia athari za lugha tandawazi nje ya wigo wa simu na barua pepe, napendekeza tukubaliane kuhusu muundo wa mabadiliko ya kiisimujamii katika lugha. Mabadiliko na Uchanganyaji msimbo katika Isimujamii Kwa mujibu wa Wanaisimujamii, kuna miundo miwili ya lugha katika Isimujamii. Moja ni muundo wa kubadili misimbo na wa pili ni muundo wa kuchanganya misimbo. Kwa mujibu wa Weinreich (1953), aliyenukiliwa Naseh (1997: 202), ubadilishaji misimbo hutokea katika mazingira ya mazungumzo pale “watu wenye zaidi ya lugha moja wanapobadili msimbo kutoka lugha moja kwenda nyingine kwa mujibu wa taratibu za mabadiliko katika lugha.” Naye Hymes (1974) anaeleza ubadilishaji msimbo kuwa ni matumizi ya lugha mbili au zaidi zinazogusa sentensi zaidi ya moja, au hata mitindo tofauti ya lugha. Ufafanuzi wa Bokamba (1989) unatupeleka mbele kidogo pale anapoelezea ubadilishaji msibo kuwa ni “uchanganyaji wa maneno, makundi ya maneno au sentensi kutoka katika mifumo miwili tofauti ya ki ALDIN MUTEMBEI 202 na L2) havikiuki kaida za kisintaksia za lugha mojawapo. Ingawa ukweli umekuwa ni huu katika maandishi ya kiisimujamii, zipo tofauti kidogo katika kubadili msimbo au hata kuchanganya misimbo kupitia simu za kiganjani hasa pale kunapotokea matumizi ya namba. Kama ilivyo kwa kubadilisha misimbo, kuchanganya misimbo kunagusa tu maneno katika lugha zinazoshughulikiwa na sio namba. Ujio wa lugha tandawazi inayotumika kwa simu za viganjani, barua pepe na maongezi katika tovuti, umeleta mabadiliko katika lugha ambapo miundo ya uchanganyaji na ile ya mabadiliko huingiza pia namba. Kabla hatujaanza kuijadili lugha tandawazi kwa undani, tuangalie sifa bainifu za lugha hii. Sifa za lugha tandawazi Kimsingi, kuna sifa bainifu moja katika lugha tandawazi ambayo ni ‘ufupishaji’. Ufupishaji huu unatokea kutokana na ‘udondoshaji’, ‘unambaishaji’ na ‘umatamshi’. Sifa hizi ingawa zinaweza kuangaliwa kama zinazojitegemea, ni vijitawi tu vya sifa moja kuu yaani ufupishaji. Kama nitakavyoonesha hivi punde, lengo la sifa hizi tatu: ‘udondoshaji’, ‘unambaishaji’ na ‘umatamshi’ hulenga kufupisha neno, sentensi au kifungu cha sentensi ili mhusika aweze kutuma maneno mengi iwezekanavyo kwa kutumia nafasi ndogo. Kwa maneno mengine anafanya mawasiliano ‘marefu’ kwa kutumia maneno machache. Sifa hizi zimeelezwa kwa undani na wataalamu kama vile Crystal (2001, 2004, 2008a, 2008b). Inawezekana kadri utafiti katika eneo hili unavyozidi kuongezeka, ndivyo tutakavyogundua sifa bainifu nyingine zaidi ya hii ya ufupishaji, na hata kupata mawazo mapya kutokana na tafiti hizo. Sifa hii ya ufupishaji ni matokeo ya utandawazi. Utandawazi umefafanuliwa na watu mbalimbali kwa mitazamo tofauti. Katika makala hii ninatumia neno ‘utandawazi’ nikikubaliana na Sullivan na Kymlick (2007: 1) waliofafanua kuwa: Kuongezeka kwa maingiliano ya watu nje ya mipaka ya mataifa yao, hususan katika nyanja za biashara na uwekezaji, lakini pia ni utoaji wa teknolojia, safari za watu na mtawanyiko wa mitindo ya maisha ya kimagharibi inayosukumwa ulimwenguni kupitia bidhaa kama vile sinema na filamu za Hollywood na vyakula vya McDonald (Tafsiri ya mwandishi) Katika maana hii ya Sullivan na Kymlick, suala la utolewaji wa teknolojia halijawa wazi kama hayo mengine. Nchi nyingi zinazoongea Kiswahili kwa mfano, zimepokea zaidi bidhaa zilizokwisha kuundwa kuliko zilivyopokea teknolojia. Kwa mfano, nchi hizi zimepokea simu za kiganjani bila kupokea teknolojia ya utengenezaji simu hizo. Aidha, watumiaji wa simu wamepokea simu hizo pamoja na namna fulani ya utamaduni katika matumizi ya simu. Matumizi ya lugha ya mawasiliano katika simu hizi yamekuwa yakifanana kwa watumiaji wa lugha ya Kiswahili mahali pengi wanapokuwa. Lugha hii tandawazi ina sifa kama nilivyozieleza na inasukumwa mbele na utandawazi kama nilivyoueleza. Hata hivyo kuna sifa ya ziada katika utandawazi popote ulimwenguni. Sifa hiyo ni watu kutaka kutumia zaidi huku wakilipia kidogo. Sifa hii ndiyo tunayoiona katika matumizi ya simu: watumiaji wanataka kuwa na maneno mengi kadri inavyowezekana, lakini wana nafasi ndogo katika simu zao, na KUKITANDAWAZISHA KISWAHILI KUPITIA SIMU ZA KIGANJANI 203 wangelipenda kutokutumia fedha zaidi kama ikiwezekana. Ufupishaji wa mawasiliano unaoletwa na lugha tandawazi unaweza kuonekana kuwa unamwelekeo huu. Ikiwa tunakubaliana kuhusu sifa hii bainifu na vijitawi vyake, tutafakari sasa changamoto zinazotolewa na lugha hii, katika nadharia za isimujamii. Nadharia tunayoijadili hapa ni ile inayohusiana na kuchanganya msimbo na kubadili msimbo (code mixing na code switching). Katika isimujamii, mbinu hii ya matumizi ya lugha hutokeza hali mbili ambazo zote uhusisha maneno. Kwa mujibu wa King’ei (keshatajwa) kuchanganya msimbo hutokea pale ambapo mzungumzaji huamua kuwa na misimbo au ‘ndimi’ zaidi ya moja katika usemi mmoja. King’ei ametumia mifano ya misimbo ya Kiswahili na Kiingereza. Aidha ameelezea kuwa mazingira ya uchanganyaji misimbo unaweza kuhusiaha lahaja za lugha moja, na hapo amaonesha mifano ya uchanganyaji misimbo inayohusisha Kiswahili, Kiingereza na Sheng (2010: 25). Katika mifano yote miwili, amefafanua uchanganyaji huo unaohusisha maneno tu. Kubadili msimbo kunaelezwa kuwa ni “kuchanganya lugha mbili tofauti lakini katika kauli tofauti badala ya kuwa katika usemi mmoja” (kama hapa juu). Na hata katika mfano huu, maelezo yake yanahusisha maneno tu. Jambo hili ni tofauti katika lugha tandawazi; lugha inayoletwa na matumizi ya simu za viganjani, barua pepe na maongezi katika tovuti. Utafiti wa Crystal katika lugha hii ya simu za viganjani, umehusisha lugha ya Kiingereza tu. Ingawa vitabu na makala zake zimesaidia sana kutoa mwanga katika makala hii, hazikujadili changamoto zinazojitokeza kama lugha mbili au zaidi zikiwa pamoja. Mifano inayotolewa toka kwa wazungumzaji wa Kiswahili na lugha nyingine ni ya kipekee ambayo hatuna budi kuijadili kwa kina kama sehemu inayofuata inavyoanzisha mjadala huu. Masuala ya Isimujamii katika lughatandawazi Maelezo yanayotolewa na wataalamu wa isimujamii kuhusu kuchanganya msimbo na kubadili msimbo yanahusu lugha ya maneno. Hebu tuangalie data ifuatayo iliyochukuliwa toka mazungumzo ya simu za kiganjani baina ya wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili. Mfano wa 1 (kutoka mwanafunzi kidato cha 5, Tambaza, Dar es Salaam) Lugha tandawazi Maana fafanuzi 2o8 ksh mch Tuonane kesho mchana Katika mfano huu, kuna mbinu tatu. Kuchanganya namba na maneno, kuchanganya lugha mbili ambapo moja ni Kiingereza na nyingine ni Kiswahili, na kuchanganya matamshi ya namba katika lugha mbili tofauti. Kwa hiyo katika mfano huu, tunaona kuwa namba mbili (2) inaitwa two, ambayo inatamkika ‘tu’ kwa matamshi ya Kiswahili. Namba ya Kiswahili ‘nane’ (8) haikubadilika matamshi, na hivyo imeambatanishwa katika herufi ‘o’ ya Kiswahili ili kufanya neno liwe ‘tuonane’. Ndani ya neno hilo pia tunaona mbinu nyingine ya udondoshaji, ambapo mbinu hii ina sura mbili tofauti. ALDIN MUTEMBEI 204 Udondoshaji katika mfano huu una sura mbili. Sura moja ni kudondosha maneno na kutumia namba pekee kama ilivyoelezwa hapa juu: 2o8. Hapa maneno ‘tu’ na ‘nane’ yamedondoshwa na katika nafasi yake kuna namba ambazo huchukua nafasi ndogo zaidi na hivyo kutoa nafasi kuandika ujumbe mrefu ukitumia nafasi finyu. Suala jingine ni lile liliyokwisha andikwa na wataalamu wengine, ambapo irabu hudondoshwa na kubakiza konsonati tu. Hapa neno ‘kesho’ linakuwa ksh na ‘mchana’ linakuwa mch. Kwa mfano tulioutoa: 2o8 ksh mch, maana ya kuchanganya msimbo inabadilika kidogo ambapo sasa tunaona kuwa uchanganyaji unakuwa na hatua kadhaa zinazohusisha maneno na namba. Tuangalie mifano mingine inayojitokeza katika lugha tandawazi. Mfano wa 2 (Kutoka mwanafunzi Chuo cha Ustawi wa Jamii, Dar es Salaam) Lugha tandawazi Maana fafanuzi 2lizaliwa tumbo 1 Tulizaliwa tumbo moja Katika mfano wa 2, kuna kuchanganya misimbo ambako kunaendana na lugha mbili. Kiswahili na Kiingereza. Katika mfano huu kuna mfuatano huu: Kiingereza (namba)→Kiswahili (maneno) : Kiswahili (maneno) → Kiswahili (namba). Katika uchanganyaji huu, sio tu maneno (msimbo, au ndimi) bali pia kuna kuchanganya namba. Mfano wa 3 (Kutoka Mwanakwaya CCT, Chuo Kikuu Dar es Salaam) Lugha tandawazi Maana fafanuzi Cjui 2nyi atfka lni? Sijui Mbilinyi atafika lini? Katika mfano wa tatu, mbali na udondoshaji wa jumla, kuna kuchanganya ‘sauti’, maneno, na namba. Lugha inayotumika ni lugha ya Kiswahili kwahiyo, hatuwezi kusema kuna uchanganyaji msimbo au ndimi kwa maana iliyozoeleka katika simu jamii. Katika mfano huu, mfuatano ni Sauti ya Kiingereza→maneno (Kiswahili) : namba (Kiswahili)→maneno Kiswahili : maneno Kiswahili. Kwa kawaida, katika Kiswahili hakuna sauti ya c kama inavyotamkika kwa Kiingereza. Uchanganyaji huu, unaivuta sauti hii ili itamkike kwa Kiswahili cha ‘si’ ili kuleta maana. Katika mifano miwili ya kwanza, namba mbili ya Kiingereza (two) ilibadilishwa na kutamkika kwa Kiswahili ‘tu’ ili ilete maana. Lakini, katika mfano wa tatu, namba hiyo hiyo, imebaki ‘mbili’ jinsi ilivyo bila kubadilishwa ili kuleta maana. Kwa njia hii kuna lugha ya kiingereza inayotumika sambamba na lugha ya Kiswahili kwa kuangalia tafsiri ya namba, au mchanganyiko unaoletwa na sauti toka lugha hizi mbili. Tuangalie mfano mwingine ili kusisitiza hoja yetu katika kuchanganya misimbo ya mawasiliano ya lugha tandawazi. KUKITANDAWAZISHA KISWAHILI KUPITIA SIMU ZA KIGANJANI 205 Mfano 4 (Kutoka Katibu Muhtasi, Idara ya Kiswahili Chuo Kikuu Dar es Salaam) Lugha tandawazi Maana fafanuzi Znaita 2 zte 2! Zinaita tu zote mbili! Katika mfano huu, kuna namba za lugha mbili tofauti, ingawa zinaonekana sawa kimaandishi. Moja ni namba mbili ya Kiingereza two, inayotamkika kwa Kiswahili ‘tu’, na nyingine namba mbili ya Kiswahili na inayotamkika kwa Kiswahili ‘mbili’. Kuchanganya huku ingawa kunaendana na udondoshaji kwa maana kwamba ukubwa wa maneno unapungua na hivyo kufanya nafasi kubwa zaidi, ili kuweza kuandika maandishi mengi zaidi, hakuendani na maana ya kuchanganya msimbo ambayo imezoeleka katika uwanja wa isimujamii. Mjadala Kwanini wazungumzaji hutumia mbinu ya kuchanganya misimbo au kubadili misimbo? Maana zinazotolewa na wanaisimujamii wengi ni zile ambazo zinaendana na hadhi, kuonesha mahusiano, kuonesha nafasi ya mtu katika jamii kama vile kisomo n.k. Hata hivyo, katika kuchanganya huku kunakosukumwa na lughatandawazi, kuchanganya msimbo hutokea sio tu kuonesha mahusiano, hadhi, nafasi ya mtu au vipengele kama hivyo. Uchanganyaji msimbo katika lughatandawazi hutokea ili kuleta maana. Maana ndiyo kigezo kikubwa katika lugha tandawazi, kuliko mahusiano au kuonesha hadhi. Ni kweli kuwa, katika lughatandawazi, bado tunaona nadharia ya Myers-Scotton (1993a/1997) ya lugha-solo LS (au lugha-matriki, matrix language) inasimama kwamba, LS ndiyo huamua sarufi katika uchanganyaji msimo au kubadili msimo iweje. Sintaksia ya LS ndiyo hujitokeza kwa uwazi. Hata hivyo, katika maana ya sarufi au sintaksia ya MyersScotton hakuna popote tunapokutana na namba. Kwahiyo, changamoto inayoletwa na lughatandawazi kutoka simu za kiganjani, haina budi kutupatia upya wa mawazo kuhusu isimu jamii hasa vipengele vya maana za ubadilishaji au uchanganyaji msimbo. Aidha, suala jipya la pili katika lughatandawazi ni sheria au kaida zake ambazo hazina budi kufuatwa ili kuleta maana tarajiwa. Ni sheria kama hii pia ambayo inamlazimisha mtumiaji kuifuata ili kukubaliana na utumiaji huu. Kumbe, suala hili halijitokezi tu kiholela, ALDIN MUTEMBEI 206 kama ambavyo wataalamu wengine walivyodai, na kusema kuwa ni lugha ambayo haina maana na inalenga kuharibu lugha rasmi. Kwa mfano, pale ambapo namba mbili zinafuatana na zote zingaliweza kutumika kuleta maana, ni lazima namba moja tu ndiyo itumike na sio zote mbili. Hii humpa mtumiaji nafasi ya kuchagua. Tuangalie mfano huu. Mfano 5 (Kutoka Mwanafunzi, Mwaka wa 2 Chuo Kikuu Dar es Salaam) Lugha tandawazi Maana fafanuzi Ntku2mia zte ksh Nitakutumia zote kesho Nitakutu100 zte ksh Nitakutumia zote kesho Nitaku2100 - Maana inapotea Katika mfano wa 5, tunaona kuwa nafasi ya uchaguliwaji kati ya namba 2 na namba 100 ni ile ile. Zote zina nafasi sawa. Kutokana na hili, haiwezekani mtumiaji kutumia namba zote, ikiwa namba hizo zina nafasi sawa za utokeaji katika msimbo uliochanganywa. Sheria au kaida ya pili ni ile inayoruhusu matumizi ya ‘sauti ’ toka lugha moja katika mfumo wa sauti ya lugha nyingine. Matumizi haya yanaweza kuambatana na namba au bila namba na bado ikaleta maana. Kwa mfano, matumizi ya sauti c ambayo inatamkika ‘si’, na kuunda sentensi ya ukanushi inajitokeza katika uchanganyaji ufuatao. Mfano 6 (Kutoka Mwanafunzi kidato cha tano, Tambaza Dar es Salaam) Lughatandawazi. Sauti c ukanushi Maana fafanuzi - Ukanushi C2mii sgr Situmii sigara Katika mfano wa 6, uchanganyaji msimbo unahusu lugha ya Kiingereza na Kiswahili na wakati huo huo kuhusu namba na herufi. Kwa upande wa Kiingereza, tunaona kuwa sio sauti tu iliyochukuliwa toka lugha hiyo na kuwekwa katika kitenzi kanushi cha Kiswahili, bali hata namba ya Kiingereza two imewekwa katika sentensi hiyo na wale wanaowasiliana wanafahamu kuwa namba hiyo katika neno hili sio ‘mbili’, bali ni two ambayo itatamkika ‘tu’ ili kuleta maana ya kitenzi cha Kiswahili ‘situmii’ Kutokana na mchanganyiko huu, tunaona kuwa lughatandawazi inatupatia hatua mbalimbali katika kipengele cha uchanganyaji msimbo tofauti na hatua tulizozizoea katika isimujamii. Hoja ya tatu ambayo hatuna budi kuijadili inatokana na suala hili la namba. Suala linalojitokeza hapa ni je, namba ni tafsiri au zinajitokeza katika lugha ya asili? Swali hili linatuonesha kuwa hatua nyingine ambayo haina budi kufikiriwa katika lugha hii ni hatua ya tafsiri. Katika mifano tuliyoitoa hapo kabla, tuliona kuwa miongoni mwa lugha ya mawasiliano katika lughatandawazi ni neno ‘tuonane’ ambalo huandikwa 2o8. Tunaona kuwa neno hili lina hatua mbili za namba. Moja ni ile ya tafsiri ambapo Kiingereza two kimetumika, na nyingine imebaki katika Kiswahili ambapo ‘nane’ imetumika. Hapa tunaona umuhimu wa kuzingatia maana katika kutoa tafsiri. Watumiaji hawachagui kiholela, KUKITANDAWAZISHA KISWAHILI KUPITIA SIMU ZA KIGANJANI 207 wanachagua ama kutafsiri au kutotafsiri kutokana na ujitokezaji wa maana. Hapa katika uchanganyaji msimbo huu, sio suala la hadhi au mahusiano, bali zaidi suala la kuwapo kwa maana tarajiwa. Suala hili la tafsiri ili kujenga maana linaweza kueleweka vizuri zaidi kwa kuangalia uchaguzi katika mfano huu ufuatao: Mfano 7 (Kutoka mwanafunzi mwaka 2 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) Lughatandawazi. Maana fafanuzi - Ukanushi tu2 wa UDSM Tumbili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Jmaa km 2kimo! Jamaa kama mbilikimo! Katika mfano huu, sehemu ya kwanza imechanganya neno na namba na kuchukua nafasi tatu tu za herufi. Hapa neno ‘tu’ limebaki hivyo hivyo bila kutafsiriwa, kama tulivyoona kabla ambapo Kiingereza two > ‘tu’; na kumetokea mchanganyiko wa namba za Kiswahili (2) kumaanisha ‘mbili’. Mtumaji katika lughatandawazi, anajua kuwa kwa mujibu wa kaida za lugha hii, ya kwanza itabaki ni ‘tu’ na sio two ya pili itabadilika na kuwa 2 ili kuleta maana ya ‘mbili’. Katika sehemu ya kwanza, mtumiaji anajua kuwa neno ‘tu’, hapo haliwezi kubadilishwa (kunambaishwa) kuwa ni namba (2) ambapo namba ya pili (neno) linabadilishwa na kuwa ni namba (2) ili kufanya neno kuwa fupi na hivyo kuwa na nafasi zaidi kwa kuandika maneno mengi. Suala muhimu ni maana: Ubadilishaji huu wa neno unabakiza maana ya ‘tumbili’. Katika sehemu ya pili neno ‘mbili’ limebadilishwa na kuwa namba (2) ili kubakiza maana ya ‘mbilikimo’. Kutokana na kigezo hiki cha tafsiri, tunaona kuwa lughatandawazi inazo kaida zake ambazo hazina budi kufanyiwa utafiti na kuhakikiwa ili zijulikane wazi. Vilevile, suala hili la kutafsiri namba ambapo pia namba huwa zimefuatana linatuingiza katika kaida au sheria nyingine inayojitokeza katika mfano wetu wa 7 kama inavyojionesha. Kaida au sheria nyingine ambayo inajitokeza katika lughatandawazi ni ile ya inayosema kuwa, endapo itatokea kuwapo kwa namba mbili zinazofuatana (au maneno mawili yakifuatana na yanayomaanisha namba), basi moja kati ya hayo ibadilike kuwa ni namba na nyingine ibaki kuwa ni maneno. Neno ‘tumbili’ lina maneno mawili au namba mbili. two > ‘tu’ na ‘mbili’ (2). Kwa mujibu wa kaida hii, ingawa maneno yote mawili yanauwezo wa kubadilishwa kuwa namba, ni neno moja tu ambalo ndilo litachaguliwa kuwa namba na jingine litaachwa kubaki ni neno. Hivyo tunapata ama tu2 au 2mbili na mtumiaji anachagua lile ambalo linachukua nafasi ndogo zaidi na kumwachia nafasi kubwa ya maneno zaidi katika mawasiliano. Mawasiliano haya, sio tu hutumia namba ‘mbili’, pekee. Mifano mingine ambayo tumeipata japo kwa uchache imehusisha pia namba ‘moja’ (1) ambapo imetafsiriwa kwenda kwa Kiingereza. Katika mifano iliyotangulia, tumeona kuwa tafsiri zilikuwa zinatoka katika ALDIN MUTEMBEI 208 Kiingereza kwenda Kiswahili; mfano two > ‘tu’. Hata hivyo kuna wakati kuna tafsiri ya kutoka Kiswahili kwenda Kiingereza kama katika mfano ufuatao: ana1nia uongz (anawania, uongozi). Katika neno hili, neno la Kiingereza one liwekwa katika namba (1) ambapo limefanywa la Kiswahili kimatamshi ‘wani’. Hata hivyo matumizi ya ‘wani’ hayakuwa mengi katika data yetu. Namba nyingine ambayo tumekutana nayo katika mawasiliano ya lughatandawazi, ni namba ‘nne’ (4) ambapo pia tafsiri imetumika. Hii imeonekana kwa wingi katika mawasiliano kuhusu muziki wa kizazi kipya au bongo flava. Katika lughatandawazi, mawasiliano yalifupishwa hivi: mzk wa k4ka4ka (muziki wa kufokafoka). Herufi ‘fo’ za Kiswahili zimeangaliwa kama namba four ambayo inatoka lugha ya Kiingereza na kuandikwa 4. Kwa kufanya hivi, mtumiaji, ametumia namba, ametafsiri, amechanganya lugha na kufupisha urefu wa neno kwa wakati mmoja. Namba nyingine ambayo imetokea japo kwa uchache ni namba ‘tatu’ (3), ambapo sawasawa na ile ya ‘nne’, herufi imetokana na namba ya Kiingereza three kumaanisha neno la Kiswahili ‘thiri’ katika neno mw3ka (mwathirika/muathirika). Kama kawaida ya kaida za lughatandawazi, hapa pia tunaona kufupisha, namba, tafsiri na hata udondoshaji wa baadhi ya herufi. Kwa kuhitimisha, lughatandawazi inatoa changamoto katika tafsiri za vipengele vya isimujamii vya ubadilishaji msimbo na uchanganyi msimbo. Changamoto hizi hazina budi kufanyiwa utafiti zaidi ili kubaini mwelekeo wa lugha hii ambayo ni lugha pendwa katika mawasiliano ya simu za kiganjani. Hatua mbalimbali zinazohusika katika lugha hii, pamoja na ufupishaji, udondoshaji, tafsiri, unambaishaji na uchanganyaji lugha ni mambo ambayo wanaisimujamii na wana mawasiliano kwa ujumla hawana budi kuyaangalia na kutafiti kwa kina katika lugha hasa zidi ya moja kama ilivyo kwa watumiaji wa Kiswahili na Kiingereza. Marejeo Bokamba, E. 1989. Are there Syntactic Constraints on Code-mixing? World Englishes 8(3): 277-292. Blom, J. & Gumperz, J.J 1972. Social meaning in linguistic structures: code switching in Norway. Directions in Sociolinguistics: The Ethnography of Communication, ed. by J. Gumperz & D. H. Hymes New York: Holt Rinehart and Wiston. Pp: 407-434. Nilep, C. 2006. Code Switching in Sociocultural Linguistics Colorado Research in Linguistics 19. Boulder: University of Colorado. (http://nhlrc.ucla.edu/events/institute/2011/readings/He%20-%20Nilep.pdf) Crystal, D. 2001. Language and the Internet. Cambridge: Cambridge University Press Crystal, D. 2004. A Glossary of Netspeak and Textspeak. Edinburgh: Edinburgh University Press KUKITANDAWAZISHA KISWAHILI KUPITIA SIMU ZA KIGANJANI 209 Crystal, D. 2008a. Text Messages. ELT Journal 62(1): 77-83. Crystal, D. 2008b. Txting: the gr8 db8. Oxford: Oxford University Press Grosjean, F. 1982. Life with two Languages: An Introduction to Bilingualism. Cambridge MA: Harvard University Press. Ho, Judy Woon Yee. 2007. Code-mixing: Linguistic Form and Socio-Cultural Meaning. The International Journal of Language Society and Culture 21 (http://www.educ.utas.edu.au/users/tle/JOURNAL/issues/2007/21-2.pdf) Hymes, Dell H. 1974. Foundations in Sociolinguistics: An Ethnographic Approach. Philadelphia: University of Pennsylvania Press. Labov, W. 1973. Sociolinguistic Patterns (Conduct and Communication). Philadelphia: University of Pennsylvania Press Butts, L & A. Cockburn 2001. An Evaluation of Mobile Phone Text Input Methods. Australian Computer Society, Inc. This paper appeared at the Third Australasian User Interfaces Conference (AUIC2002), Melbourne, Australia. Conferences in Research and Practice in Information Technology, Vol. 7. John Grundy and Paul Calder, Eds. King’ei, K. 2010. Misingi ya Isimujamii. Dar es Salaam: Institute of Kiswahili Research. Mbaabu, I.G. 2003. Sheng-English Dictionary. Dar es Salaam: Institute of Kiswahili Research. Meyerhoff, M. 2006. Introducing Sociolinguistics. New York: Routledge. Mokaya, B. 2006. Hybrid Languages: The Case of Sheng. Selected Proceedings of the 36th Annual Conference on African Linguistics, ed. by Olaoba F. Arasanyin and Michael A. Pemberton. Somerville, MA: Cascadilla Proceedings Project. Pp: 185-193. Momanyi, C. 2009. The Effects of ‘Sheng’ in the Teaching of Kiswahili in Kenyan Schools. The Journal of Pan African Studies 2(8): 127-138. Mutembei, A.K. 2010. Lugha ya Vijana katika Mawasiliano ya Simu za Viganjani. Paper presented at the Semina ya Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Muysken, P. 2000. Bilingual speech. A typology of code-switching. Cambridge: Cambridge University Press Myers-Scotton, C. 1990. Codeswitching and Borrowing; Interpersonal and Macrolevel Meaning. Codeswitching as a Worldwide Phenomenon. ed. by Jacobson, R. Frankfurt: Peter Lang. Pp: 86-109. Myers-Scotton, C. 1993a/1997. Duelling Languages; Grammatical Constraints in Codeswitching. New York: Clarendon Press. ALDIN MUTEMBEI 210 Myers-Scotton, C. 1993b. Social Motivations for Codeswitching: Evidence from Africa. USA: Oxford University Press Myers-Scotton, C. 1993c. Common and uncommon ground: social and structural factors in codeswitching. Language in Society 22: 475-503. Myers-Scotton C. 2002. Contact Linguistics: Bilingual Encounters and Grammatical Outcomes. Oxford: Oxford University Press. Naseh, L. 1997. Codeswitching between Persian and Swedish, Eurosla 7 Proceedings: 201- 211. Poplack, S. 1980. Sometimes I’ll start a sentence in Spanish y termino espanol: Toward a Typology of Code-Switching. Linguistics 18: 581-618. Sullivan, W.M & W. Kymlicka 2007. The globalization of ethics: religious and secular perspectives. New York: Cambridge University Press Trudgill, P. 2000. Sociolinguistics: An Introduction to Language and Society. London: Penguin Books
Powered by Blogger.