SINTAKSIA NA SEMANTIKIA YA KISWAHILI
SINTAKSIA NA SEMANTIKIA YA KISWAHILI
MLINGANO NA MUACHANO KATI YA TAALUMA YA SINTAKSIA NA SEMANTIKI
Katika kujadili mada hili, kwanza tutatoa fasili ya sintaksia na sematikia kama zilivyotolewa na Wataalamu mbali mbali, kisha tutaelezea na kufafanua kwa kina namna taaluma hizi zinavyojengana au zinavyohusiana na kuachana, na mwisho tutatoa hitimisho juu ya mjadala huu.
Kwa kuanzia na taaluma ya sintaksia, wataalamu mbalimbali wameifasili dhana hii kama ifuatavyo:
Habwe na Karanja (2004) wamesema Sintaksia ni utanzu wa isimu unaoshughulikia muundo wa sentensi na elementi nyingine zinazounda sentensi kama vile kategoria za maneno, vikundi na vishazi.
Taaluma ya sintaksia ni tawi mojawapo la isimu linalojishughulisha na ushambuzi wa namna maneno katika lugha yanavyoweza kufumwa na kuunda vipande vikubwa zaidi tuviitavyo vishazi, virai na sentensi. (Kipacha, 2007).
Pia, Massamba na wenzake (1999) wamesema Sintaksia ni utanzu wa sarufi unaojihusishana uchunguzi wa mpangilio wa maneno katika sentensi na uhusiano wa vipashio vyake.
Hivyo basi, taaluma ya sintaksia ni tawi la isimu au lughawiya ambalo hujishughulisha na uchambuzi wa maneno mbali mbali katika lugha jinsi yanavyoungana na kuunda sentensi.
Kwa upande wa taaluma ya semantiki, pia kuna wataalamu mbalimbali ambao wameweza kufasili dhana hii, miongoni mwao ni:-
Habwe na Karanja (2004) wamesema Semankiti ni utanzu wa isimu unaochunguza maana katika lugha ya mwanadamu. Wanaendelea kusema kuwa, semantiki hushughulikia maana katika viwango vyote vya lugha, kama vile sauti, maneno na sentensi.
Crystal(1987) amesema Simantiki ni utanzu wa isimu unaochunguza maana katika lugha.
Hivyo basi, taaluma ya semantiki ni taaluma ambayo hujishughulisha na uchunguzi wa maana katika viwango vyote vya lugha.
Kimsingi taaluma hizi mbili yaani, taaluma ya sintaksia na semantiki zina uhusiano wa moja kwa moja, hivyo taaluma hizi hujengana na kutengemeana kwa kiasi kikubwa katika mfumo lugha. Zifuatazo ni hoja na mifano inayothibitisha na kuonesha mjengano kati ya taaluma ya sintaksia na semantiki:-
Kwanza, Mjengano hujitokeza katika uainishaji wa sentensi sahihi na sentensi zisizo sahihi, taaluma ya Sintaksia hutumia kigezo cha kimaana(semantiki) kama ni kigezo kimoja wapo katika uanishaji wa sentensi sahihi na sentensi zisizo sahihi. Hili linathibitishwa zaidi tunaporejelea maana mbali mbali zilizotolewa na Wataalamu kuhusu sentensi kuwa ni “ ni tungo yenye maana kamili na yenye kjitosheleza.”
Mfano: a.) Mwalimu anaandika vizuri ubaoni.
b.) *Yule aliyekuwepo usiku ule.
c.) *Ungelikuja.
d.) Ali na Juma wanasoma kitabu.
e.) Anakula.
Katika mifano hii tunaona kwamba tungo ya (a, d na e) ni sentensi sahihi kwa sababu zinatoa maana kamili na toshelevu, na tungo zilizobaki (b na c) si sentensi sahihi kwa sababu haitoi maana kamili. Kwa hiyo kupitia mifano hiyo tunaweza kuona kuwa taaluma ya sintaksia na semantikia ni taaluma ambazo huweza kujengana na kutegemeana na kukosekana kwa taaluma moja huweza kupelekea kasoro katika taaluma nyengine.
Pili, Uhusiano katika mfuatano na mpangili sahihi wa maneno na viambajengo katika sentensi, Mfuatano na mpangilio mzuri wa maneno au viambajengo katika uundaji wa sentensi ndio unaosababisha kupatikana kwa maana sahihi katika tungo, yaani taaluma hizi zote huzingatia uhusianao na mpangilio mzuri wa maneno katika tungo na kigezo hichi ndicho kinachosababisha kuundwa kwa sentensi mbali mbali zenye maama kamili.
Kwa mfano: a.) Mohamed mfupi anasoma Qur-an vizuri.
b.) *Vizuri anasoma mfupi Qur-an Mohamed.
Katika mifano ya hapo juu tungo(a) hii ni sentensi sahihi na yenye maana kamili kwa sababu ya mpangilio mzuri wa maneno katika sentensi hiyo, na tungo (b) hii si sentensi kwa sababu haijafuata mpangilio sahihi wa maneno na haina maana kamili. Kwa hiyo, tunapochunguza kwa makini zaidi mifano hiyo hapo juu tunaweza kuona wazi wazi namna ya taaluma hizi jinsi zinavyokamilishana na kujengana.
Vile vile, uundaji au uzalishaji wa sentensi mbali mbali katika taaluma ya sintaksia husababishwa na uwepo wa taaluma ya semankiti. Taaluma ya sintaksia ni taaluma ambayo hushughulika na uundaji wa miundo tafauti tafauti ya sentensi, lakini kwa kuwepo miundo hiyo imesababishwa na kuwepo kwa taaluma ya semantiki, yaani kwa kuzingatia kigezo cha maana tunaweza kuzalisha sentensi mbali mbali kwa kupitia sentensi yenye umbo moja kwa kuangalia maana ya nje na maana ya ndani ya sentensi.
Kwa mfano:
“Ali na Salma walizawadiwa na Hassan.”
Katika sentensi hii, tukitumia kigezo cha kimaana(semankiti) tunaweza kuzalisha sentensi mbili zenye maana tafauti, kama vile:-
i.) Ali, Salma na Hassan wote wamepatiwa zawadi.
ii.) Ali na Salma ndio waliozawadiwa na Hassan.
Kwa hiyo, mifano hiyo hapo juu, inatuonesha namna taaluma ya semantiki inavyosaidia katika kuzalisha sentensi mbali mbali katika taaluma ya sintaksia.
Mwisho, kanuni ya upatanishi wa kisarufi, taaluma ya sintaksia lazima izingatia kanuni ya upatanishi wa kisarufi katika kuunda sentensi yaani izingatia uhusiano au kuwiyana kati ya kiambishi awali katika jina na kiambishi awali katika kitenzi, hivyo kanuni hii huathiri taaluma ya semantiki kwa kusababisha kupatikana kwa maana kamili katika tungo. Na pindipo sentensi inapoundwa bila ya kuzingatia upatanishi wa kisarufi, vile vile huathiri maana, na huweza kusababisha utata katika tungo.
Mfano: a.) Mtoto anakula.
b.) *Mtoto wanakula.
Tunapoangalia mifano hii, tutagundua kwamba sentensi ya (a) imefuata kanuni ya upatanishi wa kisarufi kwani kiambishi awali “m-” cha jina kinawiyana na kiambishi awali cha kitenzi ambacho ni “a-” vyote vinaonesha hali ya umoja, hivyo basi imepelekea kupatikana kwa maana kamili katika sentensi. Lakini tungo(b) haijafuata kanuni ya upatanishi wa kisarufi kwani kiambichi awali “m-” cha jina hakiendani na kiambishi awali cha kitenzi ambacho ni “wa-”, hivyo basi imepelekea kuathiri maana katika tungo hiyo na kusababisha utata. Kwa hiyo tunapochunguza mifano hiyo, tunaona wazi wazi namna taaluma hizi zinavyotengemeana na kujengana.
Baada ya kuangalia namna taaluma hizi zinavyojengana, sasa tutaelezea na kufafanua namna taaluma hizi zinavyotafautiana yaani kuachana. Taaluma ya sintaksia na semantiki zinatafautiana katika vipengele vifuatavyo:
Kwanza, katika kigezo cha uamilifu/kikazi, taaluma ya sintaksia hujishughulisha na kanuni za uundaji wa sentensi katika lugha, yaani huchunguza namna vipashio vidogo jinsi vinavyoungana na kuunda kipashio vikubwa na hatimae kuunda sentensi.
Mfano: i.) neno + neno = kirai
Mwanafunzi + hodari = Mwanafunzi hodari
ii.)kikudi kirai(KR) + Kikundi tenzi(KT) = Sentensi
Mwanafunzi hodari + anasoma = Mwalimu hodari anasoma.
Kwa upande wa pili, taaluma ya semantiki hujishughulisha zaidi na uchunguzi wa maana katika lugha, yaani huchunguza maana katika vipengele vyote vya lugha; sauti, maumbo(maneno) na sentensi.
Mfano; neno “ota” katika taaluma ya semankiti linaweza kutolewa maana zaidi ya moja;
Ota – kuona picha usingizini
Ota – kuchipuka kwa mmea shambani
Ota – kujipasha, kama vile moto au jua.
Vile vile, taaluma ya semantiki ni taaluma inayochunguza maana, na dhana ya maana ni ya kidhahania kwa sababu maana haina muundo, yaani maana hutengemea zaidi namna ya matumizi katika jamii(kimazingira au kimuktadha), hivyo maana ya maneno katika lugha huweza kubadilika kutokana na athari za kimazingira au kimuktadha, isipokuwa maneno yenye maana ya msingi.
Lakini taaluma ya sintsksia si dhahania kwa sababu viambajengo vyake hujithihirisha katika miundo yanayoonekana na kanuni zake katika uundaji haziwezi kuathiriwa na kimazingira au kimuktadha.
MAREJEO:
Crstal, D.(1987). The Cambriage Encylopedia of Language.New York:Oxford University Press
Habwe & Karanja.(2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Kenya:Phoenix Publisher.
Kipacha, A.(2007). Utangulizi Wa Lugha Na Isimu. Dar es salaam: Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania.
Massamba, D. P. B na Wenzake(2001). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu(SAMIKISA). Sekondari na Vyuo. Dar es salaam:TUKI.
Matinde, S. R. (2012). Dafina Ya Lugha Isimu Na Nadharia. Serengeti Educational Publisher: Tanzania.