Simulizi; NABII WA UONGO *SEHEMU YA 11**










Simulizi; NABII WA UONGO
*SEHEMU YA 11**

Bila kutegemea, Hatimaye katika harakati za kunikomboa, na kunitoa katika utumwa wa kishetani. Mzimu wa Juliet unajikuta katika wakati mgumu baada ya kuishiwa nguvu na kisha kukamatwa na wakubwa wangu wa kazi.Nyoka wangu wa ajabu ndiye aliyemuimbia wimbo Juliet, wimbo ambao ulikua na siri kubwa kuhusu viumbe ambao walikufa na kisha kugeuka mizimu.

Wimbo wa kiasili ambao nyoka wangu aliuimba, kumbe ulikuwa na uwezo wa kudhoofisha nguvu za Juliet.Siri hii nyoka aliweza kuitambua kutokana na nguvu alizokuwa nazo, kwani mwanzoni nyoka wangu alikua ni sehemu ya Nyoka mkubwa ambaye alikuwa ndiye mkuu wa chama chetu. Hivyo alikuwa bado ana uwezo wa ajabu na kufahamu mambo mengi sana, ikiwemo namna ya kupambana na viumbe hatari waliokufa na kugeuka mzimu kama Juliet.

"Tumpeleke kuzimu , tukamfunge huko,naamini nguvu zake hazitarudi tena,na hataweza kutufuatilia" ,yalikuwa ni maneno ambayo nyoka mkubwa ,nyoka ambaye alikuwa na vichwa vingi sana,aliweza kuyaongea huku mzee Jabir pamoja na mganga wakimsikiliza.Kwa upande wangu nilikuwa nimepigwa tu na butwaa nikiwatazama,nikiwa sijui nini nifanye kwa wakati ule.

"Mchungaji wewe baki,na endelea na majukumu yako,hakuna atakaye weza kukudhuru na kukuharibia sifa zako",mganga alinipatia maelekezo,baada ya kunitazama usoni na kutambua fikra zangu.Aligundua kwamba nilikuwa nataka kuongozana nao,jambo ambalo lilikuwa sahihi kabisa.Nilitaka kwenda nao huko kuzimu niweze kupafahamu,na pia niweze kujua kitu ambacho walitaka kumfanyia Juliet.

"Sawa nitabaki ,lakini nilitaka kwenda na nyinyi" ,niliongea bila hofu,na kuonesha nia yangu ya kutaka kuongozana nao ,bila kutegemea nilijikuta nikipata nafasi ya kuongozana nao kuelekea kuzimu.

"Twende naye ,hajawahi kufika kuzimu tangu ajiunge na chama chetu,twende naye akaone jinsi chama chetu kilivyo na watu wengi",nyoka wa ajabu ,nyoka ambaye alikuwa na vichwa vingi sana,mwenye uwezo wa kuongea kama vile binadamu wa kawaida,aliweza kunikubalia ombi langu.Kwakuwa alikuwa ndiye mkuu,hakuna aliyeweza kumpinga,na hatimaye haraka sana safari ya kuelekea kuzimu iliweza kuanza.

Nilipewa maelekezo ,na kuyafuata kwa umakini. Sote kwa pamoja tuliweza kushikana mikono na kutengeneza duara,huku mzimu wa Juliet ukiwa umelala chini katikati yetu.

"Fumbeni machoo! asifumbue mtu yoyote yule mpaka nitakaposema" Nyoka yule alitoa amli, amli ambayo tulipaswa kuifuata ili tusije tukapata matatizo. Ghafla upepo mkali, upepo ambao sikujua ulitokea wapi, kwani madirisha na mlango wa chumba changu cha siri ilikua imefungwa.

Sehemu ya sakafu tuliyokuwa tumesimama ikafunguka, na shimo lenye usawa wa duara ambalo tulikuwa tumelitengeneza baada ya kushikana mikono likatokea. Upepo ule mkali, upepo ambao ulikua mithili ya kimbunga uliweza kutusafirisha kwa kasi ya ajabu kuelekea chini, ndani ya shimo lile.

Nilitamani nifumbue macho yangu niweze kushuhudia yaliyokuwa yakitokea, lakini nilishindwa kwani nilikuwa na hofu juu ya jambo baya kunitokea, baada ya kuonywa kabla ya safari kuanza.

Upepo mkali uliendelea kutusafirisha kwa kasi ya ajabu, kuelekea chini kabisa ya shimo. Shimo ambalo sikuweza kutambua urefu wake, lakini bila shaka lilikuwa na umbali mrefu sana.

"Puuuuh ……",ulikua ni mlio wa sauti nzito, sauti ya kishindo ambacho kilisababishwa na sisi kudondoka chini. Kishindo hicho kiliweza kuashiria kufika mwisho wa safari, safari ambayo ilichukua takribani muda wa kama masaa mawili.

"Karibuni sana katika dunia yetu, ",ulikua ni mlio wa sauti ya kiume, sauti ambayo bila shaka ilikua ni ya mtu mzima tena wa makamo. Alionekana kufurahia ujio wetu, na bila shaka alitambua lengo la sisi kuwepo katika nchi ile ya kuzimu.

"Fumbueni macho, tumefika, "nilifurahi sana baada ya kuruhusiwa kufumbua macho, kwani muda mrefu nilitamani kufumbua macho na kutazama kile ambacho kiliendelea, na isitoshe niweze kutazama kwa macho yangu jinsi kuzimu kulivyofanana.

"Waaaooh, kuzimu kuzuriii hivi, nilizani panatisha! ",nilifurahi sanaa, ni baada ya kufumbua macho na kutazama uzuri wa nchi hii ya kuzimu. Kulikua na maghorofa mazuri sana zaidi ya yale ya kariakoo, jijini Dar es salaam. Barabara nzuri za kila aina, zingine zilikua barabara za juu kwa juu huku zikipambwa kwa lami nzuri ambayo ilifanya magari kupita bila buguza yoyote ile.

Sikuamini kama hata kuzimu kulikua na magari, tena ya kifahari kiasi kile. Nilishangaa kuona watu wakipishana, na kuendelea na shughuli zao kama kawaida. Kuzimu kulifanana sana na duniani, lakini tofauti yake, watu walioishi kuzimu walionekana kuwa na maisha mazuri na tena matajiri wakubwa sana.

"Kijana usishangae, ukifanya kazi yako vizuri duniani, baada ya miaka kadhaa utakuja kuishi huku " ,sauti ya mzee, mzee ambaye alitukaribisha mala ya kwanza baada ya kufika. Akiwa amevalia mavazi ya kifalme, baada ya kuniona nikishangaa uzuri wa kuzimu, alinitamkia maneno yaliyonifanya nizidi kutamani kuendelea kukitumikia chama hiki cha kishetani na kumsahau Mungu.

"Sawa mkuu, nitafanya kazi kwa bidii nije kuishi huku, nimepapenda " ,niliongea huku nikitabasamu, lakini mzee yule aliyeonekana kuwa na madaraka makubwa kuzimu ,alionekana kama vile alikuwa akitaka kusema jambo, lakini alisita baada ya kuona nikitoa jibu haraka na kumfanya asubili kwanza nimalize kuongea.

"Mkuu wa chama changu duniani, naomba mchukueni huyo kiumbe mkafungie katika gereza, na huo ndio utakua mwisho wake, hataweza kuwasumbua " ,amli ilitoka kwa mkuu yule wa kuzimu, na haraka sana, mganga pamoja na mzee Jabir walitii amli, kwani wao ndio walikuwa na vyeo vidogo, na kisha kumchukua Juliet na kwenda kumfungia katika gereza ambalo lilizungukwa na nyoka wengi wa ajabu Nyoka hawa waliimba nyimbo za kiasili, nyimbo ambayo nyoka wangu aliweza kuimba na kumfanya Juliet aishiwe nguvu na kudondoka chini.

Hivyo basi, mzimu wa Juliet uliishiwa nguvu zote, na matumaini ya kunikomboa kutoka katika utumwa ule yakawa yamefifia, kwani nyoka wale waliomlinda Juliet, waliimba usiku na mchana na kumaliza nguvu zake zote, kiasi kwamba alishindwa hata kupata nguvu za kumfanya apambane.

"Tayali, tunaweza kurudi duniani, mzimu wa Juliet hauwezi kutufuatilia tena ",mkuu wetu nyoka, nyoka wa ajabu mwenye vichwa vingi sana, aliongea na kutoa amli ya kurudi duniani, baada ya kukamilisha kazi ya kumfungia Juliet na kumuwekea ulinzi mkali kuzimu. Kwa upande wangu, fikra zangu zote zilitekwa na sikuweza kujitambua hata kidogo. Jambo pekee ambalo nilianza kuliwaza, ni kutoa kafara nyingi ili baadaye nipande cheo na kuja kuishi kuzimu.

**ITAENDELEA *
Powered by Blogger.