Ijue falsafa ya kiafrika katika fasihi simulizi

        Kazi hii imegawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo ni utangulizi kiini na hitimisho.Katika utangulizi kuna maana ya falsafa fasihi simulizi na                          


FALSAFA YA KIAFRIKA
Maana ya falsafa
Falsafa ni dhana ambayo imefasiliwa na watu  tofautitofauti  kwa mitizamo ambayo hulenga katika kumaanisha kitu kimoja.Wataalamu mbalimbali wametoa mawazo yao kuhusu dhana hii ya falsafa kwa kutoa maana mbalimbali.Wafuatao ni wataalamu na maana za falsafa na falsafa za kiafrika.
Falsafa (kutoka Kigiriki  filosofia = pendo la hekima) ni jaribio la kuelewa na kueleza ulimwengu kwa kutumia akiliinayofuata njia ya mantiki. Wamitila, K.W. (2003).
Neno Falsafa  hutokana na maneno mawili ya kiyunani yaani philo lenye maana ya upendo na Sophia linalomaanishahekima.  Hivyo utaona kuwa falsafa ni Taaluma inayojishughulisha katika kutafuta ukweli wa jambo kwa njia ya kutafakari.

Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa falsafa ni taaluma inayo dadisi hali halisi ya maisha ya binadamu kwa kuzingatia imani, mila, desturi, pamoja na mienendo aliyonayo binadamu katika jamii yake, huku akitafakari njia sahihi na bora za kuweza kutatua changamoto mbalimbali anazo kabiliana nazo katika maisha yake ya kila siku.
Maana ya fasihi;
Ngure(2003) anasema kuwa fasihi ni aina ya sanaa ambayo wasanii wake huonyesha ustadi wao katika kutumia maneno kisanii ili kuwasilisha ujumbe kwa wasomaji au jamii lengwa
Mulokozi(1989)anasema kuwa fasihi ni sanaa itumiayo lugha ili kufikisha ujumbe kwa jamii bila kujali kuwa imeandikwa au haijaandikwa.
Kutoka na maana ya fasihi kwa wataalamu hao,tunaweza kusema kuwa fasihi ni aina ya sanaa ambayo hutumia lugha katika uwasilishaji wake kwa hadhira lengwa bila kujali kuwa imeandikwa au haijaandikwa ili kufikisha maudhui kwa hadhira lengwa au iliyokusudiwa.
Oruka (1990), na Mbiti (2011). Wameifafanua dhana hii ya falsafa  ya kiafrika kuwa ni fikra au mitazamo wanayoishughulikia  waafrika wenyewe au watuwengine ambao wanakubali mila na desturi za kiafrika.


Hivyo twaweza sema kuwa falsafa ya kiafrika ni dhana au mawazo ya waafrika wenyewe  juu ya mambo mbalimbali wanayoyafanya kama vile imani juu ya maisha, mila, desturi,jinsi ya kushirikiana katika katika jamii, na kutafuta suluhisho juu ya changamoto au matatizo yanayowakabili. Utambulisho wa falsafa ya kiafrika, sifa hizo ni kama vile; falsafa ya kiafrika imejikita katika tanzu za fasihi simulizi,
Mfano
a)      visasili;
b)      visakale.
c)      Sifo
d)     Ngano
e)      Mafumbo
f)       Vitendawili
g)      Miviga
h)      Ngomezi
i)        Tambiko
j)        ngoma.
Wamitila, (2004).Anaeleza kuwa  haipingiki  kuwa falsafa ya kiafrika hujidhihirisha katika tanzu za fasihi simulizi ya Kiswahli. Tanzu zifuatazo zinathibitisha uwepo  wa falsafa ya kiafrika miongoni mwa tanzu hizo ni kama zifuatazo;
Falsafa ya kiafrika inajidhihirisha katika
Hadithi;
hadithi simulizi ni masimulizi ambayo yanatumia lugha ya mjazo au nathari na mtiririko wake huwa mwepesi au sahili.
(Wamitila, 2003). Anaeleza aina za hadithi kama vile ngano, visasili, visakale, hekaya, na nyingine nyingi. Kwa kiasi kikubwa falsafa ya kiafrika inajidhihirisha katika hadithi. Kwa mfano katika hadithi ya Abunuasi’Katika hadithi hii Abunuasi alikufa kirahisi baada ya kutolewa nguvu uhai ambazo zilitolewa kwasababu ya ujinga wake kuto tumia akili zake.
Falsafa ya waafrika inajitokeza kupitia ushairi wa fasihi simulizi,Waafrika wana mfumo maalumu wa fikra na hujishughulisha na mila, desturi, tamaduni, na namna ya kutatua matatizo yao.

Msanii anadhihirisha waziwazi falsafa ya kiafrika anapozungumzia masuala ya
        i.            Ndoa
      ii.            saula
    iii.            dini
    iv.            suala la maadili
      v.            suala la malezi ya familia.
Haya ni mambo yaliyopo na yanayotokea katika jamii yetu ya kila siku. Mwanafalsafa wa kiafrika “ Tempeles” anasema falsafa ya kiafrika imejikita katika mila, desturi, na tamaduni za kiafrika. katika wimbo huu kutokana na tamaa mbaya vijana wanakiuka maadili na kutowajali wazazi wao, wamewaacha marafiki, ndugu, wake, na watoto pia. Sababu ya tamaa wamesahau amri za mungu kuwa usiue. Usiibe, usitamani vya watu, pia waheshimu baba na mama yako. Mwisho wa tamaa ni kifo na kupelekwa gerezani. Hivyo basi msanii anaamini na anaonya kuwa mwisho wa tamaa ni majuto tuache  tamaa.

Falsafa ya kiafrika katika semi, semi ni tanzu ya fasihi simulizi ambayo hujishughulisha na maneno yasiyokua na majibu ya moja kwa moja kwa msikilizaji ama hadhira. Katika utanzu huu kuna vipera vinavyo ambatana nacho, baadhi ya vipera hivyo ni misemo, nahau, mafumbo, na lakabu.
Semi ina dhima zake katika jamii inapotumika na baadhi ya dhima hizo ni kama vile kuelimisha jamii juu ya mambo mbalimbali mazuri ya kufanya, kama kusikiliza kauli njema za wakubwa wetu na wazazi, mfano msemo wa “asiyefunzwa na mamae hufunzwa na ulimwengu”.”asiye sikia la mkuu huvunjika guu”.
Kwa upande mwingine semi hizo kuonya na kuadabisha jamii juu ya mambo mbalimbali mabaya na yasiyofaa katika jamii, kama wizi, imani na tabia mbaya, mfano msemo usemao “za mwizi ni arobaini”. Semi ni miongoni mwa tanzu za fasihi simulizi inayoonesha falsafa ya jamii moja na nyingine. Wanafasihi wana dhihirisha kuwa falsafa ya kiafrika inaweza kujidhirisha katika utanzu huu wa semi kwa kupitia vipera mbalimbali vya utanzu huu.
Kwa  mfano, kupitia methali mbalimbali zinazotumika katika jamii ya waafrika dai hili linaweza kuthibitishwa,kwa kutumia mifano ya methali zifuatazo; asiye na mwana aeleke jiwe.”, “Mgaagaa na upwa hali wali mkavu”, na “Ndondondo si chururu”Aliye juu mngoje chini”. Falsafa ya Afrika inadhihirisha kuwa katika masuala ya utawala, waafrika walikuwa katika makundi madogo madogo kama vile koo au makabila, na mtu aliyekuwa anaaminika kuwa ni mwenye nguvu ndiye aliyekuwa anatawala katika jamii husika. Viongozi waliokuwa wanaaminika kuwa ni wenye nguvu ni kama vile; chifu Mkwawa, Kinjekitile Ngwale, na Chifu Mangungo wa Msovelo.

Falsafa ya kiafrika ikijidhihirisha katika sanaa za maonesho; katika kujadili vipengele vya ujidhihirishaji wa falsafa ya kiafrika, tumechagua vipera viwili katika utanzu huu ambavyo ni

a)      Kupitia matambiko.
b)      Kupitia ngoma za jadi.

Matambiko, ni miongoni mwa vipera vya sanaa za maonesho ambacho wahusika wake katika jamii hufanya shughuli mbalimbali za kutoa sadaka kwa miungu, wahenga, na mababu waliowatangulia, ambao wanaonekana wana nguvu asilia zinazosaidia kuepusha utokeaji wa majanga kama njaa, radi, ukame, mafuriko, kuvamiwa au kutekwa kwa utawala, pamoja na kushinda vita. Katika jamii ya wabena, matambiko mbalimbali hufanywa ikiwemo matambiko yanayofanyika mtu anapo kosa motto ama kukosa kutunza mali za urithi wa wazazi wake.
Shughuli mbalimbali wakati wa matambiko hufanywa mfano ngoma, nyimbo na sherehe zinazoambatana na wanyama kuchinjwa na damu zao kutumika kama sadaka kwa ajili ya matambiko hayo. Katika kuthibitisha hili Placide Temples anaeleza kuwa maisha ya jamii nyingi za wabantu wanategemea nguvu uhai (vital force) ili kujikinga na utokeajia wa majanga katika jamii hizo kama ilivyoneshwa katika jamii ya wasukuma.

Ngoma; hiki ni kipera kinachoonesha utokeaji wa falsafa ya kiafrika katika maisha halisi ya waafrika wenyewe. Ngoma katika jamii za kiafrika ni kiashiria cha mambo muhimu, mfano hutumika kama nembo ya utawala, kitumbuizi katika shughuli mbalimbali kama vile harusi au kupandishwa cheo.

Lengo kubwa ni kutumbuiza watu na kujua ubora wa .

Katika kujadili dhana ya falsafa ya kiafrika Temples anasema kuwa mwaafrika hawezi kuacha asili yake ambayo ndiyo utambulisho wa utamaduni wake. Kama ilivojidhihirisha  katika jamii ya wasukuma ngoma ni moja ya asili zinazotambulisha utamaduni wa jamii husika.
Baada ya kuangalia falsafa ya kiafrika inavyojidhihirisha katika tanzu za fasihi simulizi. Pia falsafa ya kiafrika inajidhihisha katika tanzu za fasihi andishi ya Kiswahili kama inavyoelezewa katika vipengele vifuatavyo;

Falsafa ya kiafrika inajidhihirisha katika ushairi; ushairi ni sanaa inayopambanuliwa kwa mpangilio maalumu wa maneno fasaha na yenye muwala, kwa lugha ya mkato, picha au sitiari au ishara katika usemi, maandishi au maadhi ya wimbo (Mulokozi na Kahigi, (1979). Kwa kutumia “Kunga za Ushairi na Diwani yetu” iliyoandikwa na Kahigi na Mulokozi falsafa ya kiafrika inajidhihirisha kama ifuatavyo;
Waafrika wanaamini katika suala la umoja; toka awali waafrika walikuwa na umoja waliishi kwa kushirikiana na hata kufa nya kazi pamoja kwa manufaa ya jamii nzima. Kwa kuumia shairi la “Msiba Uliotuangukia” suala la umoja kama imani ya waafrika linajidhihirisha;
                         “…Na mara shambulio tukalianza
                                  Huko sauti za chuki tunazipaza
                            Tobaa litumbo la nduli kafiri
                            Atakaye tumbole lituhasiri!
                                Tukalichoma tukalikata sana…”
Shairi hili linaonesha kuwa waafrika waliamini katika umoja kama nyezo ya kupinga ukoloni na unyanyasaji. Pia waafrika wanaamini kuwa wazee ni watu wenye busara, hekima, na mawazo mazuri ambapo ni vyema kuheshimu mawazo yao. Mfano katika shairi lifuatalo;

Ya Allahu ya Azizi, unifungulie njia, 
               “ Nienzi wangu wazazi, nisije kuwakosea, 
               Waniridhie wazazi, kila nitowatendea, 
                Katu siwezi kulipa, kwa mliyonifanyia’.

Suala la kifo; vilevile waafrika wanaamini kifo sio mwisho wa uhai bali ndio mwanzo wa maisha mengine. Waafrika wanaamini kuwa mtu akifa anaendelea kuishi kati yao ingawa hawamuoni. Hii injidhihirisha katika shairi la “kinjikitile Ngwale ” ambapo mtunzi anasema;

 ‘…shujaaa..ooooh shujaa..kwa mti wa shamba mkoloni twamtwanga oooohh,shujaa uishi                           
milele,uishi milele.
Waafrika wanaamini kuwa watu walio kufa wapo karibu na Mungu na wale walio hai humuomba Mungu kupitia wale waliokufa. Hili linajidhihirisha kupitia urithishaji wa majina pamoja na matambiko  au kuomba mizimu ya mababu inayofanywa na waafrika wengi katika maisha ya kila siku.
Dhana ya uzuri na ubaya pia imejidhihirisha kama falsafa ya kiafrika hasa katika shairi la ‘Pendo”. Mtunzi wa diwani hii anadokeza kuwa uzuri au ubaya upo katika macho ya muonaji au anayeangalia, anasema;
1 moyo wangu ume lizi, mimi kuku penda wewe,
   mwingine tena siwazi,sije nitia kiwewe
   nina muomba mwenyezi,maisha nikae nawe
       pendo langu mimi nawe halihitaji hirizi                           

2  haliihitaji hirizi,naomba sana welewe
    nikumbatie mpenzi,usi hofu wenginewe
    wabaki na simulizi,watuige wapagawa
        pendo langu mimi nawe halihitaji hirizi
Hii ni dhahili kuwa aghalabu uzuri au ubaya wa kitu kwa waafrika unategemea na mtazamo au mawazo ya muonaji. Hata katika jamii mtu anaweza kupenda au kukiona kitu fulani kizuri na mwingine kukiona kitu hicho ni kibaya.
Katika tamthiliya wandishi ameonyesha falsafa mbalimbali ambazo zimezoeleka na zinatumika sana na jamii ya kiafrika. Falsafa zinazojidhihirisha katika tamthiliya hii, ambazo ni kama vile;
a)      Dhana ya ngoma
b)      Dhana ya nyimbo,

N. Hussein na tamthiliya yake ya Mashetani, kuwa ni moja kati ya tamthiliya za mwanzo kabisa katika harakati za utumiaji wa kanuni za kijadi ndani ya kazi za kifasihi. Wafura anasema:
                            “Hussein alijitokeza tena uwanjani, akathibitisha ameidhibiti bahari ya tamthiliya kwa kutoa ‘Mashetani”
Katika tamthiliya hii mwandishi ameonyesha namna ngoma na nyimbo zinavyochukuliwa katika jamii nyingi za kiafrika. Ngoma na nyimbo huchukuliwa kama ni dhana ambazo zinazochochea umoja na ushirikiano kwa jamii wakati wa kufanya kazi na mara dhana hizi zinapokosekana kazi huzorota na hata watu huvunjika moyo na kushindwa kufanya kazi, na mwisho hutawanyika.

Mwandishi “Hussein”ametumia ngoma na nyimbo kama kichocheo cha kufanya kazi.Hivyo huu ni uhalisia uliopo katika jamii za kiafrika hususani kwenye makabila mbalimbali, ngoma na nyimbo huchukuliwa kama vichocheo na viashiria vya matukio ndani ya jamii.

Dhana ya mwanamke katika jamii, mwandishi Medical aid foundation  ameonyesha namna mwanamke anavyochukuliwa na jamii Mwanamke amechorwa kama mtu asiye na elimu juu ya mambo ya jinsia na ukimwi, katika kuilezea nafasi hii, mwandishi anamtumia muhusika Mama Suzi, ambaye anaoneka kutokuwa na ufahamu mzuri juu ya masuala ya UKIMWI, kwa mawazo yake anaamini kuwa ugonjwa wa UKIMWI ni ugonjwa unaowahusu watu wakubwa tu, na watoto hawawezi kuambukizwa jambo ambalo si sahihiVile vile, mwandishi amemchora mwanamke kama chombo cha starehe, anamtumia muhusika Joti ambaye anawatumia wanawake ili kujistarehesha kingono, lakini pia tunaona namna watu wanavyotumia pesa na vitu vya thamani ili kuwarubuni wasichana wapate kukidhi mahitaji yao ya kingono.

Jambo hili lipo miongoni mwa jamii za kiafrika ambapo mwanamke anachukuliwa kama kiumbe duni asiyeweza chochote mbele ya mwanaume na ndio mitazamo ya wanaume na wazee katika familia nyingi za kiafrika,kwa mfano mtoto wa kike mara nyingi hutengwa na mtoto wa kiume katika shughuli mbalimbali likiwemo suala la elimu.
Kwa hiyo mwandishi ameonyesha namna gani falsafa ya kiafrika inavyojidhihirisha juu ya anavyochukuliwa mwanamke, tofauti na Ulaya na Asia ambapo mwanamke amepewa nafasi kama mwanaume katika Nyanja zote  za kimaisha.

 Pia kupitia riwaya ya “Mirathi ya Hatari” iliyoandikwa na Mung’ong’o,G. tunashuhudia falsafa ya kiafrika inajidhihirisha katika vipengele vifuatavyo kama ifuatavyo;
Kifo,
waafrika walio wengi mbali na kuamini kuwa vifo vingi vinavyotokea katika jamii vina sababu zake ambazo huelekezwa katika Mungu na uchawi au ushirikina. Haya yamezungumzwa na wanafalsafa wa kiafrika kama vile Placide Temples na Samweli Mbiti. Katika riwaya hii hali hii inajidhihirisha kupitia kifo cha mzee Kazumbe.Cchanzo cha kifo ni kulogwa, mwandishi anasema “Mwanangu, leo asubuhi nilikwenda kwa mama Tumwene kuulizia kifo cha baba yake Uganga unasema kuwa kifo chake kimetokea si kwa mapenzi ya Mungu, ila kwa michezo ya binadamu wafaidio kuwaona watu wakifa!
Katika tamthiliya ya Lina Ubani tunaambiwa kuwa Talafa aliyekuwa msumbufu kwa wanakijiji walioktiwa wamelima fiwi badala ya pamba aligeuzwa shingo, uso umetazama mgongoni! Jambo hili ni la kutisha. Linaweza kubadilisha nia ya afisa yeyote mtendaji ambaye atakwenda kijijini hapo.

Pia suala la dini, kupitia mwanafalsafa John Samweli Mbiti ni dhahiri kuwa waafrika wana dini zao tangu mwanzo mbali na ujio wa wakoloni ambao walileta  ukristo pamoja na uislamu wao. Katika riwaya hii mwandishi kupitia wahusika kama Gusto na mama yake (Nyamidze) ni wakristo tena huwa wana kwenda kanisani katika (uk 29) baada ya Gusto kuoga na kuvaa ili aende kanisani anamuuliza Nandi, “Hivi mama amekwenda wapi?” Nandi anajibu “Amekwenda kanisani”. Ni usiku huo huo tu wa kucha jumapili Gusto alihudhuria kikao cha wachawi mapangoni.
Siku hiyo hiyo ya Jumapili mama yake Gusto (Nyamidze) anaenda kwa mganga (uk 37) kwa mama Tumwene. Huu ni uhalisia katika jamii zetu, matatizo yanapoikumba familia za watu mbalimbali miungu hukimbiliwa. Uamini kuwa mtu akifa hujiunga na miungu.

Suala la urithi, katika falsafa ya kiafrika tunaamini mzazi hasa baba anapofariki huwaachia urithi watoto wake hasa wa kiume. Katika “Mirathi ya Hatarianasema
‘Nakuachia dawa zote na milki yangu katika mizungu ya sihiri”. Mirathi hii anaipokea Gusto na baadaye inasababisha madhara makubwa ikiwa ni pamoja na vifo vya mama, dada, na hata kipenzi chake Dina ambapo vifo vimetokea kama kisasi baada ya Gusto kumtoa kafara mjomba wake Kapedzile. Suala hili la urithi lipo na linajidhihirisha katika jamii zetu za kiafrika.

Kwa kuhitimisha, tunaweza sema kuwa falsafa ya kiafrika imejikita hasa kuelezea mfumo mzima wa maisha anayoishi mwaafrika na ukweli kuhusu fikra, mila, utamaduni, na mienendo yake katika jamii. Kwa sasa falsafa ya kiafrika imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na falsafa ya kimagharibi hususani suala zima la utandawazi.Kuna  mambo  mbalimbali kama vile, mavazi, vyakula,dini, mfumo wa elimu na afya vyote vimebadilika kwa kiasi kikubwa kutokana na kuzuka kwa utandawazi. Pia maendeleo ya sayansi na teknolojia yamesababisha falsafa ya kiafrika kwa kiasi kikubwa kupotea, mfano ngoma za jadi katika kizazi hiki zinazidi kupotea kutokana na kuibuka kwa taaluma ya muziki kutoka katika iamii za kimagharibi.























   MAREJEO.
Kahigi, K.K., & Mulokozi, M.M. (1979). Kunga za Ushairi na Diwani Yetu. Dar es Salaam: Tanzani Publishing House.

Mbiti, J. (1990). African Religion and Philosophy. New York: Praeger Publisher

Muhando, P. (1982). Nguzo Mama. Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press

Mung’ong’o, C.G. (1977). Mirathi ya Hatari. Dar es Salaam: Tanzania publishing House

Wamitila, K.W. (2003). Kamusi ya Fasihi: Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus Publications

Mulokozi, M.M. (1989) Tanzu za Fasihi Simulizi Mulika 21:1-24, Dar es salaam: TUKI.

Mulokozi, M.M. (1996) Fasihi ya Kiswahili, Chuo Kikuu Huria cha Dar es salaam

Wamitila, K.W.(2002) Uhakiki wa Fasihi Misingi na Vipengele Vyake. Nairobi, Phoenix,
Publishers Ltd.




Powered by Blogger.