IJUWE HISTORIA YA KABILA LA WAHA

IJUWE HISTORIA YA KABILA LA WAHA 
MKOA WA KIGOMA
Takwimu ya wakazi mwaka 2014 jumla ya wakazi wa mkoa huu walikuwa zaidi ya milioni 2.1 Mkoa wa Kigoma umepakana na nchi ya Burundi , mkoa wa Kagera na Geita upande wa Kaskazini, Mashariki umepakana na mikoa ya Shinyanga na Tabora, Kusini umepakana na mkoa wa Rukwa na kwa upande wa Magharibi umepakana na Ziwa Tanganyika penye mpaka wa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo.
Wakazi wa asili wa mkoa huu ni wa Kabila la WAHA. Inazo wilaya 6, Tarafa 21, Kata 136, mitaa 176 na vitongoji 1,856 na kufanya jumla ya halmashauri za Wilaya kuwa 8; Kakonko, Kibondo, Kasulu mjini, Kasulu vijijini, Buhigwe , Uvinza, Kigoma vijijini na Manispaa ya Kigoma /Ujiji.
UKUBWA WA ENEO;
Ni KM2 45.066(sawa na 4.8) ya eneo lote la Tanzani ambapo KM2 8.029 ni maji na KM2 37.037 ni Nchi kavu. Kwa ujumla eneo la mkoa wa kigoma ni Tambarare ya juu inayoanza kwenye mita 800 juu ya UB Kribu na Ziwa Tanganyika na kupanda hadi mita 1,750.
MAKABILA;
Mkoa huu unayo pia makabila mengine kama, Wabembe, Wahutu, Watongwe,Wagoma , Wabwali , Wamanyema, Waholoholo na Watutsi.
Wapo pia makabila mengine kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania wanaoishi kama nyumbani kwa kuhamia ama kwa kufanyakazi tu kisha wakiwa na mipango ya kurudi katika mikoa yao.
KABILA LA WAHA;
KABILA LA Waha; Jina la Kabila ni WAHA. Watu wa kabila hili huitwa Waha au Abhaha katka wingi na katika umoja Umuha. Lugha yao ni miongoni mwa familia ya lugha za Kibantu iitwayo Kiha. Hapo zamani himaya yao kiutawala iliitwa Buha ambayo ilijumuisha mipaka yote ya eneo la mkoa wa Kigoma uliopo Kaskazini –Magharibi mwa Tanzania kwa jina maarufu Buha (Kigoma Mwisho wa reli).
Kwa mujibu wa Mchambuzi na Mwandishi wa masuala ya Kihistoria Bwana B.A Ogot, katika kitabu chake kiitwacho “A Survey of Two Thousand years of East Afrikan History “ katika ukurasa wa 76 -85 amejaribu kuorodhesha jumla ya makabila yaliyoishi katika eneo la Afrika Mashariki kwa kuzingatia lugha na maeneo yao. Hapa ni wazi kwamba jamii za watu wa zamani ziliishi kwa kuhamahama katika nyakati tofauti tofauti zikitokea sehemu za Afrika Magharibi kandokando mwa mto Niger na Kongo, na jamii nyinginezikitokea maeneo ya Afrika Kaskazini hivyo hadi kufikia miaka 1300 KK tayari jamii za Wabantu zilikuwa zimeshafika katika eneo hili la Afrika Mashariki. Nitaje tu baadhi ya makundi ya wabantu yaliyoishi pamoja katika koo zao na koo za Waha katika eneo waliloishi linalozunguka Ziwa Viktoria walikuwa ni; Wajita, Wakerewe, Wakara, Wazinza, Wahaya, Wahutu na Watwa, Wakiga, Watoro, Wanyoro, Wanyankole, Waganda, Wasoga, Wasese, Wakwere, Wakenyi, Wagisu, Wasiriani, Waluya, Wasubi, Waha, Wahangaza, Washubi na Wavinza.
Katika eneo hili ndipo walipofikia Wabantu hawa wa mwanzo na kuweka makao yao na hivyo hawakuwa katika makabila haya tuyaonayo sasa, bali ilikuwa katika makundi madogo madogo tunayoweza kuyaita koo.
Kadri walivyoendelea kuishi kwa muda mrefu waliongezeka kisha waliendelea kujigawa kwa kuhama na kwenda kuishi katika maeneo mbalimbali ya Afrika Mashariki hadi katika maeneo wanayoishi hadi hivi sasa.
Hadi kufikia karne ya 16 tayari koo za Waha zimeshafika katika eneo la Buha na kuishi pamoja katika maeneo tofauti toufauti. Waha hutambuliwa kwa koo zao ambazo zimesheheni utamaduni wao katika mila na desturi zao, misemo, hadithi, ngoma, mtindo wa mavazi, nyumba zao, vyakula vyao na mtindo wa kuabudu.
Aidha pia koo hizi katika kujitofautisha na koo zingine ziliweza kujiita majina tofauti tofauti na kutumia majina ya wanyama na ndege mbali mbali kama; Tumbili, Nguruwe, Nyati, Hondohondo, nk. Pia ilikuwa sio jambo geni kwa ukoo mmoja kujitenga na ukoo wake na kujiita aina nyingine ya mnyama tofauti na Yule wa awali kwenye ukoo huo ingawa ukoo uliweza kubakia uleule wa mwanzo na sababu ziliweza kubainishwa. Kwa mfano, Wakimbili Hondohondo na Wakimbili Mpongo na wakimbili Vinza .
Shabaha kuu ya kufanya hivyo ilikuwa ni kujitofautisha baina yao na koo zingine. Baadhi ya koo za kabila la Waha ni kama; Wajiji, Wakimbili, Watela, Walagane, wanyongozi, Watambo, Wasindi, Walima, Wasase, Waheza nk. Moja ya sifa maarufu ya kabila hili ni ile ya kuhama na nyumba na methali yao isemayo ” Ibhiharagi bhisumbinyama” yaani Mboga ya maharage ni bora kuliko nyama. Ikiwa na maana kwamba “Bora kutumia mboga ya maharage inayopatikana kwa urahisi kuliko kupenda nyama iliyo ya ghali na isiyopatikana kwa urahisi”
WAHA NA MFUMO WAO WA UTAWALA; Kuna usemi wa Wazungu usemao kwamba “Mwafrika hakuwa na maendeleo yoyote kabla ya ujio wa Wazungu” na Kuna pia msemo wa watu kwamba ” Waha hawakuwa na tawala zao kabla ya ujio wa Watutsi”.
Kauli hizi si za kweli, kwani binadamu amekuwa akipambana na mazingira yake kwa miaka milioni 30 iliyopita. Kwanza tuone dhana ya ” uongozi” ni mamlaka au karama ya kuonyesha njia kwa vitendo. Dhana ya “UTAWALA” Neno hili lina maana pana kulingana na aina zake, kwa kifupi Utawala ni “Mfumo unaotoa Mamlaka ya dola au serikali kwa kiongozi.”
Hivyo kutokana na dhana ya Uongozi na Utawala hapo juu, ni wazi kwamba kila palipo na watu kuanzia wawili na kuendelea kuna utawala au Uongozi. Kwa hali hii Waha waliishi mwanzoni katika koo mbalimbali zilizokuwa na mfumo wake wa uongozi. Mfumo maarufu uliotumika kutawala katika jamii ya Waha ilikuwa wa UKOO. Koo zilizoishi katika eneo moja ziliwpaswa kuchagua ukoo mmoja na kuusimika kuwa ukoo wa utawala wao , hivyo mtawala alitokea katika ukoo huo. Koo tawala ziliitwa kwa jina moja la WATEKO katika wingi na katika umoja UMTEKO. Mfano mmojawapo wa koo hizi za utawala ulikuwa ukoo wa Wajiji uliotawala katika eneo la NKalinzi au Kalinzi ya leo ikianzia sehemu za Mukigo.
Ili Mteko/Wateko aweze kutawala alipaswa kuwa na sifa mbalimbali kama; uwezo wa kutoa tiba, kuleta mvua, uwezo wa kuongoza watu kwa hekima , uwezo katika shughuli za ulinzi na usalama, uwezo wa kuleta neema miongoni mwa jamii yao na kulinda ardhi nk.
Mfano wa pili wa ukoo wa wateko ulikuwa ukoo wa Wakimbil wa Manyovu-Ibhugalama (Kibila) ukoo huu ndio ulikuwa ukiongoza katika sehemu hizo kwani tunaona kwamba hata wakati mfumo wa utawala wa Wami ukoo huu na maeneo yake ndiyo yaliyochukuliwa kuwa makao makuu ya viongozi (umtwale Munini/ watwale) na katika kipindi cha matambiko inasemekana shughuli zlikuwa hazifanyiki hadi ukoo wao umehudhuria .
Hivyo koo za Waha zimedumu na kuishi kwa zaidi ya miaka 1600 katika koo zao huku baadhi ya koo zikiwa ndio watawala( Wateko) wa koo zingine hadi mfumo wao ulipobadilika kutokana na ujio wa jamii ya Wahima/Watutsi ambao walifika na kuanzisha mfumo mwngine wa utawala katika karne 17 miaka 1700 BK iliyopita. Katika miaka hiyo eneo lote la Buha lilikuwa na kabila moja tu la Waha lililoishi hapa. Hivyo ujio wa Watutsi ndio uliopelekea mwingiliano wa kwanza wa jamii ya watu wasio Wabantu katka ukanda huu wa Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.
Kadhalika na katika sehemu zingine ambako Wabantu walihamia kama; Urundi, Rwanda, Karagwe, Bukoba na Ngara, Ukerewe, Wazinza nk. Waliendelea kuishi katika mifumo ya Tawala zao hadi pale walipoingia katika mabadiliko kadri ya historia yao. Kwa makabila niliyoyataja nitajaribu kuelezea jinsi walivyoathiriwa na ujio wa jamii nyingine katika maeneo yao.
MUUNDO WA UTAWALA;
Katika tawala za Wateko sikuweza kupata muundo wa uongozi ulliotumika katika kutawala. Sababu ni kwamba, mfumo wao ulitumika kwa muda mrefu na hakukuwa na Masimulizi au maandishi yaliyoweza kuandikwa kwa ajili ya kuweka kumbukumbu. Hata hivyo Historia ni somo linalokubali mabadiliko hivyo ni fursa kwa wasomaji na wachambuzi wengine wa mambo ya kihistoria kuichukulia kama mahali pengine pa kufanyia utafiti ilikuja na majibu ya uhakika kwa ajili ya kutoka elimu kwa kizazi kilichopo na kijacho.
8.KABILA LA WATUTSI.
Watutsi au Wahuma au Wahima au Wahinda au Imfure, Banyaruguru =Rwanda watu wa kaskazini), Wahima=Burundi, Banyamlenge=sehemu za Kivu kongo, Watutsi= Buha, Bahinda=Karagwe yote haya ni majina yao. Majina haya yametokana na mtindo wa jamii ya Wabantu kushindwa kuwaita kwa maneno yao mfn. “Wa’o’oruma’ kwa kibantu WAHIMA /WAHUMA, kutokana na kushindwa kutamka majina yao yanayotamkwa kutokea Puaani na kooni. Hili Ni kundi la jamii nyingine ya watu wa Afrika Mashariki lililotokea katika eneo la Afrika Kaskazini sehemu za Chari-Naili kandokando mwa mto Naili katika karne ya 17 au miaka 1700BK.
Tofauti na kundi lile lilotoka katika eneo la Afrika Magharibi la Wabantu. Kundi hili lipo katika jamii ya kundi linalozungumza lugha za Wamoru Madi, Waniloti au Waafroasia. Kundi hili kama yalivyo katika makundi ya kibantu yalijimega na kuhamahama. Kwa kuwa yalikuwa makundi ya wafugaji walisafiri katika makundi madogo madogo mno hasa ya mtu mmoja mmoja au familia.
Hii iliwezekana kutokana na mtindo wao wa ufugaji ambao uliwawezesha kufika mahali na kukaa kipindi kirefu wakichunga ng’ombe zao, tofauti na Wabantu ambao wengi wao walikuwa wakulima hivyo pindi walipoamua kuhama walihama na kuishi katika makundi makubwa ya ukoo na kuendeleza shughuli zao za kilimo.
Jamii hii ya watu ilifika katika makundi madogomagogo katika vipindi tofauti tofauti hadi maeneo ya Kaskazini Magharibi mwa Tanzania katika Bukoba,Ngara, Unyamwezi na Buha na katika tawala za Urundi na Rwanda kwenye nchi za Burundi na Rwanda wakitokea sehemu za Uganda.
Ushahidi unaonesha hivyo kutokana na baadhi ya jamii hizo kuonekana zaidi ukanda huu tofauti na ilivyo katika mikoa ya Mara, Shinyanga Mashariki na Kaskazini, Dodoma na ama katika mikoa ya kusini na pwani ya Tanzania. Pia jamii hii haina lugha yao maalumu wanayozungumza.
Kwa kuwa hawa sio jamii ya wabantu tungetarajia waongea Lugha kama za Kimasai ama Kijaruo na zinginezo zinazozungumzwa na jamii ya watu waliotokea Kaskazini. Badala yake huongea lugha za Kibantu.
Kabla ya kutazama utawala wao hebu kwanza tuone namna walivyoanza kuishi na jamii za Wabantu walizozikuta. Kama nilivyotambulisha hapo awali kwamba, wabantu waliendelea kuishi katika tawala zao za kiukoo, zikifanya shughuli zao. Walipofika hawa Watutsi kwanza walijitambulisha kwa Mteko aliyekuwa mtawala. Kisha walitambulishwa kwa ukoo wa Wateko na kwa baadaye kwa koo zote ziLIzoongowa na Mteko. Baada ya wenyeji kuridhika na kuwapokea katika himaya yao, Watutsi kwanza waliomba kuingia katika koo za Wateko kama watoto na ndugu wa Ukoo.
Ndio maana hadi leo huwezi kukuta ukoo ama kabila la Watutsi , bali wameendeleza koo za wateko pale wanapojitambulisha kwa koo za wenyeji kwa kuzingatia mahali walipo. Kisha sehemu ya mali zao (ng’ombe) zilitolewa kwa mtawala wakimaanisha kushukuru kukubaliwa kwao ndani ya ukoo husika. Katika kuishi kwa muda mrefu jamii hii iliendelea kuaminiwa na kukubalika katika koo, hivyo shughuli na michakato yote ya Kifamilia na kiukoo zilihusisha pia watutsi wakiwa sehemu ya ukoo .
lli kuhakikisha kwamba wanawateka wenyeji na kutwaa Utawala mbinu kadhaa zilitumika;mfn, Kuozesha watawala binti zao, Mvuto kutokana na maumbile yao (uzuri wa umbo), mfumo wa Ubugabile, Wanawake kuua waume zao hasa wale waliokuwa watawala ili watoto wa Kitutsi walithi utawala, tabia za kujifanya wanyenyekevu, heba za kuwa na malingo Fulani ambazo zote hizo ziliwavutia jamii za Watawala na wanaukoo kwa ujumla wao.
Katika masimulizi nimewahi kusikia kwamba ilifika mahali baada ya Watutsi kukaa na Jamii ya Wabantu Wanyamezi hadi leo wameweza kuziishi baadhi ya Tabia zao. Hasa za majivuno na malingo. Baada ya kuhakikisha kuwa wameweza kuaminiwa na jamii yote kwa wema waliokuwa wakiufanya na kwa sababu hizo ndipo jina la Mtutsi liliipata sifa likimanisha MTU MWEMA . Kumbuka maneno kama” Mtutsi wanje” Likimaanisha ; Mtu mwema kwangu. Ni msemo ambao hadi leo kwa baadhi ya maeneo ya Buha umekuwa ukitumika . Zoezi hili lilifanyika kimkakati, kwa makini na kwa kipindi kirefu .
Kama tunavyofahamu kwamba mtu wa hila huwa hakurupuki katika kutekeleza mipango yake.
MFUMO WA UTAWALA WA WAMI;
Utawala wa Watutsi ndipo ulipoanza Baada ya kufanikiwa kuuangusha utawala wa Wateko/ Umteko katika karne hiyo ya 17BK. yaani miaka 1750BK katika sehemu za Urundi na Rwanda na katika miaka ya 1700BK. katika eneo la Buha, kwa kumpa jina mtawala wao kuwa ni MWAMI. Mwami katika tofasili isiyo rasmi ya Kibantu ni mtawala /Kiongozi/ Mfalme mwenye hadhi ya juu kabisa.
Mfano wake ni Mungu “Umwami wachu wo Mwijuru” Hii ni nukuu ya baadhi ya maneno ya sara za Kanisa Katoliki katika lugha ya KIHA, ikimanisha “Mungu wetu uliye mbinguni”.
WAMI; Baada ya kuanguka kwa utawala wa WATEKO ndipo Wami waliposhika madaraka ya utawala . Shughuli kuu tatu na muhimu ndizo zlizobakia kwa Wateko. Shughuli hizo zilikuwa ni kumiliki na kugawa ARDHI, MATAMBIKO NA DINI.
Mambo ya ulinzi na usalama, utawala, mahusiano na nchi za nje na mambo ya ndani nk. yalikuwa chini ya utawala wa Watutsi. Hapa sababu zilizopelekea kuchukua utawala kwenye maeneo hayo, ilikuwa ni kwamba, wafugaji walizoea kuwa na jeshi linalolinda mifugo yao hivyo waliona ni muhimu wadhibiti masuala ya ulinzi na usalama wa mipaka yao.
Aidha pia kwa kuwa jamii zao ndiyo waliotawala karibu maeneo mengi baada ya mfumo wa utawala wa Wateko kuanguka wangependa kushirikishana masuala yanayohusu habari za nchi zao ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama wan chi zao hizo. Ikumbukwe kwamba katika kipindi hiki
Waha walianza kupoteza umaarufu wao wa Mfumo wa Utawala wa UKOO/ WATEKO.
Mfumo wa Watutsi ulichukua nafasi na Buha ikaangukia katika mikono ya watawala wa Mwami. Katika nyakati tofauti tofauti Tawala ziliundwa katika eneo lote la Buha. Tawala zilizoanzishwa katika eneneo lote la Buha zilikuwa 6 kwa majina yao ni;i;UTAWALA WA HERU=Ikulu yake HERU JUU pamoja na sehemu ya mipaka yote ya Manyovu, Kasulu vijijini na Kasulu Mjini,ii; MUHAMBWE=Ikulu yake KIBONDO na sehemu za Wilaya ya Kibondo,iii; BUYUNGU= Ikulu yake KAKONKO na sehemu za mipaka yote ya wilaya ya Kakonko na iv;UJIJI=Ikuu yake Nkalinzi na sehemu zote za mipaka ya wilaya za Kigoma vijijini, Manispaa ya Kigoma/ Ujiji na wilaya ya Uvinza .
Nyingine zilizomeguka kutoka kwenye utawala wa Heru ni; v;NKANDA-LUGURU=Ikulu yake NKANDA na maeneo yote ya mipaka yake na vi;HERU-USHINGO=Ikulu yake Heru Ushingo.
MUUNDO WA UTAWALA WA MWAMI;
1.Mwami-Mteko
2.Umtware Munini
3.Umtware Mtoyi
4. UMhamagazi
5.Katikiro
6.Abhintala
MUUNDO WA UTAWALA WA MTWALE MUNINI
1. Umutware Munini.
2. Umutware Mtoyi.
3.Umhamagazi(mtoa Taarifa).
4.Katikiro(askari).
5.Abhintala(wananchi).
UTAWALA WA HERU; mwaka 1750 – 1963;
1. MWAMI RUHINDA; Mtawala wa kufikilika anayedhaniwa kuwa ndiye mwanzilishi wa Himaya zote za Wahinda.
2. MWAMI KANYONI.
3. MWAMI NTARE I.
4. MWAMI BIGONDA.
A. MWAMI GWASA I === wa Nkanda-Luguru na Heru- Ushingo zilizojitenga kutoka Utawala wa HERU.
5. MWAMI NYAMIHONDO====GWASA I, aliyetawala HERU katika karne ya 18.
6. MWAMI KANYONI II.
7. MWAMI NTARE II ===Aliongoza vita dhidi ya Wangoni na Watemi wa Wavinza katika miaka 1850.
8. MWAMI GWASA II ===Aliongoza vita dhidi ya Wajerumani katika mwaka 1897.
9. MWAMI NTARE III ===Alifariki wakati wa mapigano baina ya Wami wa Buha 1918.
10. MWAMI KATONDWA ===alijisimika kuwa Mwami lakini aliondolewa na WATWALE na kumsimika MWAMI TUNDA.
11. MWAMI LUYAGWA ===Alitumia majina ya Gwasa, Ntale na Ruhinda.
12. MWAMI KANYONI III ===Alisimikwa na wakoloni wa Kiingereza kama kibaraka wao
13. MWAMI NTARE IV ( TERESIA JOSEPH NDALICHAKO)=== Ni Mwani mwanamke wa kwanza na wa mwisho kutawala HERU mwaka 1949 -1963. Ana sifa ya kuoa na kumtolea Mahali mume wake kutokana na MWAMI haolewi na kucha nchi yake.
Utawala huu ulichukua eneo lote linalopakana na Mto Malagarasi kuanzia mipaka yake ya Magharibi na Kaskazini na mipaka yake ukivuka Mto Maragalasi katika maeneo yanayopakana na wilaya za Kibondo, Kasulu na Uvinza. Aidha pia mipaka yake ya Kusini kwenye mipaka ya wilaya za Uvinza na Kigoma Vijijini.
Katika kipindi hicho idadi ya watu ilikuwa ndogo hivyo sehemu kubwa ya eneo lake ilikuwa pori. Mtawanyiko wa watu ulikuwa kama ifuatavyo; Heru, Manyovu, Ushingo na Nkanda. Pia tunapotaja sehemu ya utawala tusidhani kwamba sehemu yote ya eneo tulionalo hivi leo, au tunalosikia kwamba ilikuwa himaya ya utawala Fulani kwamba ilikuwa imeenea watu la hasha, kilichokuwa kinafahamika ni mipaka yake tu.
Tena katika enzi hizo isingelikuwa vyepesi kuchukua kipande cha ardhi ya mtawala fulani na kujimilikisha kama sehemu yako. Wateko walikuwa makini sana na wenye weredi mkubwa katika kuweka na kutunza kumbukumbu za mipaka ya eneo lao kwa kuzingatia uwenyeji katika eneo na mamlaka waliyokuwanayo ya umiliki wa ardhi.
Nadhani hata utaratibu wan chi yetu wa ardhi kumilikiwa na wananchi kwa kuiweka chini ya Raisi, ni utaratibu uliorithiwa kutoka kwa kabila la Waha. Pia ili kuhakikisha kwamba utawala unadumu na kuwa na nguvu, kulikuwa na desturi ya utawala mmoja kuvamia utawala jirani na kupigana vita. Utawala ulioonekana kushindwa katika vita hivyo ulitekwa na kutawaliwa. Hivyo tuseme kwamba tawala zote zilizokuwapo eneo lote la Buha tunaweza kusema ndizo jumla na nchi zilizokuwepo.
UTAWALA WA UJIJI;
Ujiji ni ukoo mmojawapo miongoni mwa koo nyingi za kabila la Waha. Koo hii ilikuwa moja ya Koo tawala la Wateko katika eneo la Kilemba(Mukigo). Mukigo kieneo ilijumuisha sehemu za nyakelela, NYanzali ,Kilemba na Shuza iliyopo katika bonde la mto shuza katika bonde la ufa la Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.
Kipindi cha ujio wa Watutsi eneo hili nalo lilikumbwa na athari ya ujio wao. Inasemekana kwamba eneo hili la Ujiji lilikuwa chini ya utawala wa HERU. Baadaye mtawala huyu aliamua kugawa sehemu ya utawala wake na kumpa mwanaye. Sehemu hii ya utawala mpya iliitwa Ujiji kutokana na jina la ukoo wa Wateko walioishi hapo. Mipaka ya eneo lake lilichua sehemu za wilaya za Kigoma vijijini, Kigoma Mjini na Uvinza.
Mtwale wa Tawala ya Ujiji wa Kilemba alipakana na Mtwale wa Tawala ya Heru kwa upande wa Mashariki aliyeishi eneo la Manyovu. Ikulu ya MWAMI WA UJIJI mwanzo ilikuwa MUKIGO, baadaye ilihamia NKALINZI/ KALINZI. Sehemu kubwa ya eneo lake lilikuwa pori na ilikuwa na wakazi wachache sana. Katika masimulizi sikupata kujua eneo lingine lililokuwa na Watwale zaidi ya Mtwale wa Kilemba.Watu waliishi katika maeneo ya Nyanda za juu tu tofauti na ilivyo sasa ambapo watu wamejaa mwambao wa ziwa Tanganyika pande za Kaskazini na Kusini. Aidha pia katika kipindi hiki hata Waarabu walikuwa bado hawajafika katika eneo la Ujiji. Kuna watu wanadhani kwamba KALINZI ni MANYOVU hapana, mwanzoni ilikuwa Manyovu chini ya Mtawala wa Heru.
Baadaye eneo la Ujiji kugawiwa kwa Mtawala mwingine ndipo jamii zilipoanza kutengana. Jamii ya Manyovu ikawa chini ya utawala wa Heru chini ya Mtwale wa Manyovu na Jamii ya Ujiji ikawa chini ya utawala wa Ujiji chini ya Mtwale wa Kilemba. Mtengano ulianzia hapo katika masuala ya kiutawala, hivyo tunaweza kusema tofauti za jamii hizi mbili zinatokana na mipaka ya utawala wakati wa Wateko na baada ya Wateko Wami.
BAADHI YA MAJINA YA WAMI WA UJIJI.
1.MWAMI RUSIMBI
2.MWAMI GWASA.
3.MWAMI George Bhatega
Powered by Blogger.