LIFAHAMU VIZURI KABILA LA WABENA

LIFAHAMU VIZURI KABILA LA WABENA
WABENA ni kabila la kibantu linalopatikana katika eneo la Nyanda za Juu Kusini
mwa Tanzania wilaya ya Njombe mkoa wa Iringa.
Lugha yao inaitwa Kibena na makao yao makuu yanaitwa Ubena. Makao makuu
ya Wabena ni Iringa katika eneo maarufu la Ubena, idadi kubwa ya Wabena
inapatikana pia katika wilaya jirani ikiwa ni pamoja na Ulanga mkoani Morogoro.
Kwa mujibu wa utafiti wa Profesa Sethi Nyagava kuhusu historia ya Wabena
hadi mwaka 1914, maeneo makuu ya Wabena yamegawanyika katika sehemu
tano ndani ya wilaya ya Njombe ambayo ni Ivanging’ombe, Usovi, Ikilavugi,
Nyikolwe na Mfirika.
Utafiti uliofanywa na Dk Kilemile wa miaka ya hivi karibuni unaonesha Kibena ni
lugha pana yenye utajiri wa maneno na lahaja kuu tano ambazo ni Ki-Kilavwugi
inayotumiwa na wakazi wa eneo ya Ilembula; Kisovi inayotumiwa na Wabena wa
eneo la Lusisi hadi Makambako. Lahaja nyingine ni Kimaswamu inayotumiwa na
wakazi wa Imalinyi, Njombe mjini na sehemu ya kata ya Mdandu, Ki-Lupembe
inayotumiwa na wakazi wa Lupembe na Kimavemba ambacho kutumiwa na
Wabena wa Uwemba na sehemu ya tarafa ya Igominyi.
Dk Joram Kilemile anafafanua kuwa lugha ni moja tu ila tofauti ni ndogondogo,
zinazotokana na matamshi. Mfano kukaza “dz”, kwa lahaja zote isipokuwa
Kikilavwugi ambacho ingawa inaandikwa “dzi” inatamkwa kama “dji” kama vile
‘umuhudji’. Watumiaji wa lahaja ya Kilupembe inaandikwa “dzi” lakini wanatamka
kama “chi” umuhuchi, achile - amekuja, wakati “adjile” (Kikilawugi)... Wengine
wote wanakaza adzile, umuhudzi. Tofauti nyingine ni ya kutumia herufi K na H.
Mfano katika maneno Kamwene wengine husema Hamwene, Kangi na hangi
pia ukukulima na uhulima. Ingawa historia ya Wabena haitoi jibu sahihi huu ya
jina la kabila, watafiti mbalimbali wanahisi kuwa limetokana na ama kazi ya
kuvuna ulezi yaani kubena au kutengeneza chumvi kwa kuwa majina ya eneo
yalitokana na majina ya watu maarufu au kazi muhimu yenye kuwaingizia
wananchi wengi kipato.
Kutokana na tofauti za kijiografia, shughuli za Wabena hutofautiana kutoka eneo
moja hadi jingine. Hata hivyo, kwa ujumla Wabena wote ambao hivi sasa
hupatikana wilaya za Njombe, Mufindi, Kilombero na Songea ni wakulima
hodari. Wabena wanaoshi sehemu zenye mito na mabonde hujishughulisha pia
na uvuvi, wakati wale wa ukanda wa juu wanajishughulisha na kilimo na ufugaji.
Wabena wana historia nzuri ya kudumisha ujamaa na ushirikiano kutokana na
mfumo wao wa wakibadilishana mazao na mali mbalimbali. Wabena, kabila
linalosifika kwa ukaribu pia lina sifa ya kipekee katika historia ya hatua za
maendeleo ya binadamu kwa kuwa lilikuwa hodari wa kufua chuma. Kwa mujibu
wa utafiti wa akiololojia uliofawanya na Profesa Paul Msemwa mwaka 2001
katika na maeneo yanayozunguka mji wa Njombe walikuwepo wakulima ambao
walifua chuma kuanzia kipindi cha kame ya tano au hata kabla ya hapo, jambo
linalodhihirisha kuwa Wabena walikuwa wakifua chuma.
Utafiti huo wa kisayansi umefanyika kwa kuchimbua ardhi kwa lengo la kutafuta
masalia ya zana mbalimbali zilizotumiwa na watu wa kale umeweza kuibua
masalia ya vipande vya vyungu na masalia ya viwanda vya chuma katika eneo
linalokaliwa na Wabena ikiwamno Mgala Isitu, tarafa ya Igominyi. Vipande vya
vyungu vilivyopatikana Mgala Isitu vina marembo yanayoshabihiana na
marembo ya vyungu vilivyowahi kupatikana nchi za Zimbabwe na Zambia,
jambo linalodhihirisha kuwa baadhi ya tamaduni za makabila ya kibantu zina
mwingiliano na zinashabihiana.
Utafiti huo umebaini kuwa Wabena wa kale walitunza mazingira kwa kuwa
walijenga viwanda vya chuma mbali na makazi ya watu na pia hakuna shughuli
ya kuichumi iliyofanyika karibu na vyanzo vya maji. Hata hivyo, kadri miaka
ilivyosonga mbele shughuli za viwandani zilisogezwa katika makazi ya watu na
kusababisha uharibifu wa mazingira ambayo matokeo yake ni kutoweka kwa
asilimia kubwa ya misitu ya asili na vyanzo vya maji.
Sehemu pekee ya Ubena ambayo bado ilikuwa maarufu katika uyeyushaji wa
chuma hadi mwanzoni mwa kame ya 20 ni Njombe Kusini (Umavemba) na
Mashariki ya Wilaya ya Njombe ambako bado kulikuwa na misitu ya asili. Hivi
sasa maeneo hayo nayo yamebakiwa na maeneo machache ya misitu ya asili
kwa kuwa sehemu kubwa ya misitu imetoweka kutokana na miti kukatwa kwa
ajili ya mkaa wa kuyeyusha na kutengenezea chuma.
Maeneo mengine ya Ubena ambayo bado yana misitu ya asili ni yale ambayo
yana umuhimu kimila kwa baadhi ya koo au kwa jamii ya Wabena kwa ujumla.
Umuhimu wa uyeyushaji chuma katika eneo la Ubena linadhihirishwa na
kupatikana kwa wingi mabaki ya viwanda. Pia, katika maonesho ya wakulima
yaliyofanyika Iringa mwaka 1951, Wabena walionesha jinsi ya kupata chuma
kutokana na udongo wenye madini ya chuma unaofahamika kwa jina la Mdapo
kwa Lugha ya Kibena.
Historia kwa njia ya simulizi inasema baadhi ya mila na desturi za Wabena
zinashabihiana na mila za jamii mbalimbali za Nyanda za Juu Kusini. Kwa
mujibu wa historia Wabena wana uhusiano wa karibu koo za watu wa makabila
ya Wahehe na Wanyakyusa ambao walihamia eneo linalojulikana kama
Nyumbanitu lililoko kati ya Njombe na Mdandu katika barabara ya Njombe na
Mbeya.
Kabla ya kuanza kwa mfumo wa kuhakikisha kuwa watoto wote wenye umri wa
kwenda shule wanaandikishwa na kuhudhuria masomo watoto wa Kibena
walitumia muda mingi katika michezo. Michezo hiyo ilichezwa kwa kuzingatia
rika na jinsia ambapo watoto wa kiume walicheza maporini wakati wa kuchunga
ng’ombe pia kulikuwa na michezo ya majumbani baada ya kazi.
Mchezo wa Pia maarufu kama Dila au Mbila kwa lugha ya Kibena huchezwa na
wavulana wenye umri wa miaka mitano hadi 16. Vijana wa kiume wenye umri
kati ya miaka 17 hadi 24 hupendelea mchezo wa mieleka na mshindi
hupongezwa na kuonekana mtu hodari na mwenye ujasiri. Mchezo wa
Mbingambinga huchezwa na watoto wa rika zote. Mchezo huo hutumia kamba
zenye rangi mbalimbali zinazofungwa kushoto na kulia kisha huchezwa kwa
kuzunguka kama na kutambua kama yenye rangi fulani kulingana na maelekezo
ya mtu anayeongoza mchezo.
Wabena wanasifika kwa kushika dini. Hata kabla ya kuingia kwa dini ya Kiislamu
na ya Kikristo waliamini katika mungu mmoja ambaye wanamwita Nguluvi au
Inguluvi. Kutoka na imani Wabena husema, “Nguluvi, Inguluvi, yeliya gavile ifinu
fyonde” ikiwa na maana Mungu aliyeumba vitu vyote. Huamini kwa kuwa Mungu
aliumba vitu vyote ndiye mwenye mamlaka juu ya viumbe vyote duniani, ana
uwezo, huruma, ujuzi na mwenye kutoa baraka kwa watu wanaotenda matendo
mema na kuwaadhibu wote wanaotenda uovu.
Falsafa hiyo ilitawala na kuwa mwongozo wa maisha yote ya Wabena halisi.
Kama ilivyo kwa makabila mengine yanayomwamini Mungu, Wabena wanaamini
kwamba kuna ulimwengu mwingine baada ya maisha ya hapa duniani.
Wanapokutana katika msiba hutumia salamu maalumu inayosema:
“Mumwamukile uyu nayu muyingo (akwadza)” ikiwa na maana kuwa mwezetu
ametangulia tutakakofika wote.
Hata hivyo, wanaamini kuwa sio kila mtu atafika katika ulimwengu mpya na
kuuona utukufu wa Mungu. Ili kufikia ulimwengu huo mpya ni lazima kila mtu
awe na matendo mema katika ulimwengu wa sasa.
Powered by Blogger.