Simulizi; NABII WA UONGO **SEHEMU YA 15**
Simulizi; NABII WA UONGO
**SEHEMU YA 15**
……FAINALI ……
Dar es salaam,
Juliet hakuweza kupumzika, alitaka kumaliza misheni iliyomrudisha duniani haraka iwezekanavyo, kwani siku hadi siku, nilizidi kupotosha jamii na kuwa na wafuasi wengi sana... Kwakuwa nilipanga kutoa kafara nyingine ya watu watatu, Juliet aliweza kulitambua hilo na hakua na sababu kuzuia lengo langu lisiweze kutimia.
Jioni ile ile, jioni ya siku ya ijumaa. Juliet alitoweka nyumbani kwao, baada ya kufanikiwa kutoka kuzimu. Hali aliyoikuta duniani, haikuwa ya kawaida, alishangaa sana kwani wazazi wake pamoja na wazazi wangu, walikosa furaha. Waliumia sana, kila walipoona nikiponya watu na kusifiwa, huku nikitumia nguvu za giza. Kitendo cha kupata wafuasi wengi sana kupita wale wa awali, kilimtisha sana na hakua na budi kujitoa kwa nguvu zote kupigana na watu wabaya, ambao walinitumikisha na kubadilisha fikra zangu. Fikra ambazo zilijali pesa, kuliko Mungu na binadamu alio waumba. Nilikua tayali kutoa uhai wa mtu yoyote yule, ilimradi nipate utajiri na sifa kubwa katika jamii.
………………………………
"Ninaondoka kwa mala nyingine tena, sina muda wa kupoteza, lakini kabla jua halijazama siku ya kesho, nitarudi hapa nikiwa na mchungaji, akiwa amebadilika na kuwa mtu mwema, na mimi nitawaaga kurudi kwetu…………", ilikuwa ni sauti nzuri, sauti ya msichana mrembo Juliet. Msichana ambaye nilimuua na kisha kumtoa kafara kwenye chama changu cha kishetani, katika hali ya kushangaza, Juliet alirudi duniani kama mzimu, kwa ajili ya kunikomboa kutoka katika utumwa wa kishetani. Utumwa wa kumtumikia shetani kama nabii wa uongo, na kufanya anasa mbalimbali za kidunia, ambazo hazikumpendeza Mungu. Kwahiyo basi, Juliet hakua na sababu kuaga ili akaweze kuikamilisha misheni yake, na kuahidi kurudi nyumbani kwao, na kunikabidhi kwa wazazi wangu nikiwa mtu mwema………
Wazazi wangu, pamoja na wazazi wake Juliet, walimtazama Juliet na kumsikiliza kwa makini, maneno ambayo aliweza kuyazungumza. Mwili wake uliyeyuka na kupotea kama upepo, hali iliyoashiria, alitoweka kuelekea kwenye mapambano ya kunikumbatia. Familia nzima waliketi sebuleni, walishindwa kwenda kujipumzisha mpaka Juliet atakapo rudi, akiwa amekamilisha misheni yake ya kunikomboa.
Waliamua kukaa palepale sebuleni, kusubili hatma ya maisha yangu. Kwani walikuwa wamechoshwa na taarifa zangu kila kukicha, taarifa ambazo zilizungumzia habari zangu za unabii,na kuwaponya watu matatizo yao, kwa kutumia nguvu za kishirikina, huku wengi wakiamini, nilitumia nguvu za Mungu jambo ambalo halikuwa la kweli. Pete yangu niliyoivaa mkononi, kitambaa pamoja na maji ajabu niliyowanyunyizia watu, na kudai yalikua ni maji ya baraka. Ndiyo siraha pekee nilizotumia kuwatibu watu, na kulifanya jina langu kufahamika duniani kote, kwa muda mfupi tu.
…………………………………
Bagamoyo;
Mzee Jabir aliamua kubakia Bagamoyo kwa siku kadhaa mala baada ya kutoka kuzimu, hakutaka kurudi Dar es salaam haraka sana bila kumaliza shughuli zote ambazo zilihusiana na chama chetu ……
Kama wasemavyo wahenga, siku ya kufa nyani miti yote huteleza. Ndivyo ilivyotokea katika kasri letu ambalo lilikua Bagamoyo, Nyoka ambaye alikuwa ndiye mkuu wa chama chetu, baada ya kazi nzito hakuwa na nguvu tena za kumfanya aweze kupambana. Kwani ni muda mrefu tangu apate chakula, siku ambapo meli iliyokuwa ikisafiri kutoka Dar es salaam kwenda Zanzibar kuzama. Tangu siku hiyo alipomeza wahanga wa ajari hiyo, alikuwa bado hajapata chakula chochote kile cha kumuongezea nguvu.
Nyoka alilala tu muda wote, bila hofu yoyote ile kwani aliamini Juliet asingeweza kutoroka kutoka kuzimu, na kusababisha matatizo yoyote yale. Mganga pia aliendelea kufurahia na kujiona mshindi, alilala fofofo huku mguu mmoja ukiwa huku, na mwingine kule. Uchovu aliokuwa nao baada ya shughuli nzito haukuwa wa kawaida, kwa takribani siku mbili tangu atoke kuzimu, uchovu wa safari ulikua bado haujamtoka katika mwili wake ………
Upepo mkali kutoka baharini ulivuma, na kufanya eneo lote la Bagamoyo kuwa na baridi kali siku ya ijumaa usiku wa manane. Baridi hii iliufanya usingizi wa mzee Jabir, mganga pamoja na nyoka kuwa mtamu sana na isitoshe walikuwa wana siku chache tangu watoke kuzimu, safari ndefu ambayo iliweza kuwachosha.
Hivyo basi, mzimu wa Juliet ulifika Bagamoyo, na kuikamilisha kazi yake kwa urahisi ambao haukua wa kawaida. Ukimya uliweza kutawala katika kasri letu, na kwa kutumia uwezo wa ajabu, aliweza kugundua kuwa hakuna kiumbe yoyote yule aliyekuwa macho.
Juliet aliamua kufanya jambo la ajabu sana, na kuonesha uwezo wake, alifumba na kisha kufumbua. Baada ya kufumbua, mapipa kadhaa ya petroli yalikua mbele yake. Alinyoosha kidole, mionzi mikali ilitoka na kutoboa mapipa yale ya mafuta. Hakuishia hapo, alipandisha kidole chake hewani, na kisha kuchora mduara hewani. Mapipa yale yalipanda hewani kufuata ishara ya kidole cha Juliet, na kisha kumwaga mafuta kulizunguka jengo lote, kufuata ishara ya duara ambalo Juliet alichora. Ndani ya sekunde chache tu, jengo lote la chama chetu, liliweza kulowa mafuta ya petroli.
"Puuuuuh ……puuuu ……,kila jambo linamwisho wake, haya ndiyo malipo ya dhambi zenu ",mzimu wa Juliet ulitema mate mala mbili, na kisha kuongea maneno ya kulaani vitendo vibaya ambavyo mzee Jabir, mganga pamoja na kiumbe wa ajabu nyoka, waliweza kuvitenda duniani.
Baada ya Juliet kutema mate tu, mate ambayo yalimtoka mdomoni kama cheche za moto, na kusababisha jengo letu lote kulipuka na kusambaratika kabisa. Baada ya kitendo hicho, Juliet aliweza kupotea na kurejea Dar es salaam kama umeme.
………………………………
"Aiiiiiih………aaaaii…ii…ih ",ulikua ni mlio wa huzuni, mlio ambao niliusikia usiku wa manane siku ya ijumaa. Nilishtuka sana kwani niliona mabadiliko makubwa sana ndani ya mwili na fikra zangu. Haraka haraka niliamka, na kisha kuelekea chumba changu cha siri, chumba ambacho kuliweza kutokea kelele.
"Mungu wangu, nini hiki! ……",nilishangaa sana kwani nilikuta nyoka wangu mdogo aliyekuwa akinilinda, na kulinda chumba changu cha siri akiwa amekufa huku akionekana kubabuka na moto. Kitambaa changu, pete yangu pamoja na maji ya ajabu, na yenyewe yalionekana kuteketea kwa moto. Kumbe baada ya jengo la Bagamoyo kuungua, jengo ambalo lilikuwa na kila kitu, siri pamoja na nguvu zetu, ndipo vifaa vyangu pamoja na nyoka Wangu waliweza kuteketea.
"Mmmh mbona sielewi nyumba yangu imeenda wapi?, " Hatimaye jengo langu liliweza kupotea katika mazingira ya kutatanisha, sikubaki na kanisa wala gari hata moja. Eneo lote ambalo kulikuwa na jengo langu, palibaki tambalale na kunifanya nibaki nikiwa nimepigwa na butwaa.
"Usihofu chochote, tayali umekua mtu mwema ,fikra zilifumbwa na kusababisha uwe mtu mubaya sana, ukaniua mimi, na ukataka kuwaua wazazi wako ",
"Siweziii! Kamwe siwezi kuwaua wazazi wangu, wala kuua mtu!, kama nimekuua mbona uko hai? " ,
"Huwezi kuamini kwa urahisi, fikra zako zilibadilishwa kishirikina, twende kwa wazazi wako ukawaone, udhibitishe maneno yangu ",
Yalikuwa ni mazungumzo kati yangu na Juliet, baada ya kunitokea, kwa vile alikuja akitembea kama binadamu wa kawaida na kukuta nikijishangaa, sikuweza kutambua kama hakua binadamu wa kawaida. Nilikuwa na hamu kubwa ya kuwaona wazazi wangu, ni muda mrefu tangu nitoke Kigoma na kuonana uso kwa uso na wazazi wangu, kusema ukweli niliwamisi sana.
Sikuwa na budi kumsikiliza Juliet, na kusikiliza maneno aliyoniambia. Nilimshika mkono, na baada ya kumshika tu mkono wangu, tulijikuta tukipaa juu kama ndege na kwa kasi ya ajabu. Niliona kama mazingaombwe, lakini haikuwa hivyo. Wakati mwingine nilifikiri nilikuwa ninaota, lakini haikuwa kweli, nilikuwa ninapaa hewani kweli kabisa, na sikuwa nikiota.
Kitendo hicho kilinifanya niamini maneno ambayo Juliet aliniambia, niliamini kuwa Juliet hakuwa binadamu wa kawaida na kila kitu alichokiongea inawezekana kilikua sahihi …
…………………………………
Mwanga mkali uliangaza sebuleni, katika jengo la aliyekuwa mmoja wa viongozi wa kanisa langu, baba yake Juliet.. Mwanga ule uliwafanya waweze kuamka, kwani wote walilala sebuleni wakisubili Juliet afanikishe kunikomboa na kunikabidhi kwa wazazi wangu …………
"Mwananje, ndashimye chane kukubhona, imana ishimweeh ",(mtoto wangu, nimefurahi sana kukuona, Mungu asifiwe) mama alitamka maneno ya furaha kwa lugha ya kiha, huku akinikimbilia baada ya kutokea sebuleni katika mazingira ya ajabu sana. Wazazi wake Juliet nao hawakusita kuonesha furaha yao, walitukimbilia na kutukumbatia ……
"Baba yake Hakika, ulimuuliza swali kiumbe aliyekuja kuwapatia taarifa kuhusu kufunga na kuomba, yule ni malaika wa Mungu ……asanteni kwa kutii maagizo yote!! Naomba muishi kwa upendo kama ndugu, msisahau kumtegemea Mungu kwa kila jambo kwani nimuweza wa yote, mimi ninaondoka, hamtaniona tena ……",mzimu wa Juliet hatimaye uliweza kutuaga huku machozi yakimtoka, kiasi kwamba kila mmoja baina yetu alilia baada ya kusikia maneno mazito kutoka kwa Juliet.
Nilijiona mwenye hatia, lakini sikuwa na jinsi yote yalikuwa ni mapenzi ya Mungu. Kwa mbali nilijiona mwepesi na huru, nilijiona kama nilitua mzigo mzito ambao ulizidi uwezo wangu, na kufanya asubuhi ile ya siku ya jumamosi kuwa ya kukumbukwa maisha yangu yote …………
*MWISHO **
Hakuna marefu yasiyokuwa na ncha ……!simulizi hii ni ya kutunga, lakini haina ukweli wowote jambo inataka kuendana na hali halisi ya dunia ya leo, iliyojaa uovu wa kila aina ……Eee……Mungu …tuhurumie!