MAMBO YALIYOPELEKEA KUIBUKA KWA RIWAYA YA KISWAHILI



MAMBO YALIYOPELEKEA KUIBUKA KWA RIWAYA YA KISWAHILI
   Kabla ya kuchambua juu  ya mambo yaliyosababisha kuibuka kwa riwaya ya Kiswahili ni muhimu kuanza kuangalia maana ya riwaya. Kuna wataalamu mbalimbali ambao wamefasili riwaya kwa mitazamo mbalimbali kama ifuatavyo;
          Kwa mujibu wa Senkoro (2011) katika kitabu chake cha Fasihi Andishi anafasili riwaya ni kisa ambacho urefu wake unakiruhusu kitambe na kutambaa mahali pengi na kuambaa vizingiti vingi vya maisha kama apendavyo mwandishi wake. Anaendelea kueleza kuwa riwaya ni hadithi ndefu ya kubuni yenye visa vingi, wahusika zaidi ya mmoja na yenye mazungumzo na maelezo yanayozingatia kwa undani na upana maisha ya jamii.  Pia Wamitila (2003), ameeleza kuwa riwaya ni kazi ya kinathali au bunilizi ambayo huwa na urefu wa kutosha, msuko uliojengeka vizuri, wahusika wengi walioelezwa kwa kina na yenye kuchukua muda mwigi katika maandalizi na huhusisha mandhari maalumu. Vilevile Muhando na Balisidya (1976:76) wanasema, riwaya ni kazi ya kubuni, hadithi ambayo hutungwa kufuatana na uwezo wa fanani kuibusha mambo kutokana na mazoea au mazingira yake. Anaendelea kueleza kuwa riwaya yaweza kuanzia maneno elfu 35 na kuendelea.
 Kwa ujumla riwaya ni hadithi ya kubuni yenye visa na matukio yenye mawanda mapana kwa kufungamana na wakati pia kusawiri maisha ya jamii husika. 
 Vilevile  riwaya ya Kiswahili  ni ile ambayo inafungamana na utamaduni wa Waswahili katika lugha ya Kiswahili, pia ni riwaya inayohusu Waswahili wenyewe. Baada ya kuangalia maana mbalimbali za riwaya tupige hatua na kuchambua  mambo mbalimbali yaliyosababisha kuibuka kwa riwaya ya Kiswahili. Kuna wataalamu mbalimbali ambao wamejaribu kuelezea kuibuka au kutokea kwa riwaya ya Kiswahili baadhi yao ni; 

           Madumulla (2009) anayeeleza kuwa riwaya ya Kiswahili ilitokana na nathari bunifu simulizi kama vile hadithi, hekaya, ngano zilizosimuliwa kwa mdomo, pia anaendelea kusema kuwa riwaya ilitokana na maandiko ya fani ya ushairi hususani tendi za Kiswahili.Naye Senkoro (2011),  ameeleza kuwa riwaya zilizuka kutokana na maendeleo na mageuzi ya kiutamaduni, uchangamano wa maisha ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni yaliyopelekea haja ya kimaudhui zaidi ya ngano na hadithi fupi.
             Pia Mulokozi (1996) ameleza kuwa chimbuko la riwaya ya Kiswahili lipo katika mambo makuu mawili ambayo ni fani za kijadi za fasihi pamoja  na mazingira ya kijamii.
             Kutokana na wataalamu mbalimbali kuelezea kuhusiana na kuibuka kwa riwaya ya Kiswahili ambapo wote wanafungamana katika mambo makuu mawili ambayo ni riwaya ya Kiswahili imeibuka kutokana na fani za kijadi ambazo ni ngano, visakale, hekaya, sira, masimulizi ya wasafiri, visasuli, visasili nk. Pamoja na maendeleo mbalimbali ya jamii, mfano maendeleo ya kiuchumi au mazingira ya jamii.    Kwa kuanza na uchambuzi wa fani za kijadi, fani za kijadi ni mapokeo au masimulizi  ambayo yalikuwepo hata kabla ya kuja kwa fani ya maandishi. Fani  hizo zilipelekea kuibuka kwa riwaya ya Kiswahili kama ifuatavyo;

           Ngano ni hadithi za kubuni ambazo zinahusu wanyama, wanadamu, mazimwi, majini na malaika. Ngano nyingi zina msuko sahili ambao huwasilisha kwa urahisi ujumbe uliokusudiwa. Hivyo kuna ushahidi wa kutosha  kusema  kuwa riwaya  ya Kiswahili imetokana na ngano kwa sababu riwaya hufanana na ngano kifani  hasa katika wahusika na hata katika msuko wa visa na pia katika maudhui hasa dhamira huwa zinalingana na zile za ngano. Mfano wa riwaya hizo ni kama vile za Shaban Robert Adili na Nduguze (Macmillan 1952) na Kusadikika. Mafano katika riwaya ya Kusadikika kuna mhusika Ndege kwa jina lingine Mangera ambaye ni ndege mkubwa kabisa walishao  katika ardhi  lakini walalao kusadikika, hivyo ndege huyu alitumiwa na Mjumbe wa kusadikika Amini aliyetumwa ardhini alijifunga juu ya paja la Mangera usiku na asubuhi ndege alienda  ardhini na Amini nae akiwa kwenye paja la Mangera alijifungua baada ya kufika  ardhini akatembea baada ya kumaliza mambo yake akenda tena  kwa yule ndege akajifunga  tena na usiku ulipofika wakaenda kusadikika. Hivyo athari za ngano katika riwaya ya Kiswahili  ya leo tunaziona  katika muundo sahili wahusika wengi ni bapa na lengo ni kutoa maadili.

              Hekaya ni hadithi za kusisimua kuhusu masahibu  na matukio ya ajabu na yasiyokuwa ya kawaida. Mfano mzuri wa hekaya ni zile za Alfu-lela-Ulela hekaya za Abunuasi, hekaya hizi zilienea kabla hata ya ujio wa wakoloni. Hivyo kuna mfanano mkubwa sana wa kifani  na wa kimaudhui na riwaya za Kiswahili. Mfano wa riwaya za Kiswahili zilizotokana na hekaya ni Adili na Nduguze ya Shaban Robert ( Macmillan 1992) na Ubeberu Utashindwa ya  Kimbila (TUKI 1997). Hizi zote zimeathiriwa na hekaya za kijadi, hivyo ndio maana tunasema riwaya za Kiswahili  zimetokana na fani za  jadi.

            Sira ni masimulizi ya kweli kuhusu maisha ya mtu. Sira zinaweza kuwa wasifu, habari za mtu kusimuliwa na mtu mwingine au tawasifu  mtu anajisimulia   yeye mwenyewe kuhusu maisha yake. Sira iliathiri kuibuka kwa riwaya kwani masimulizi ya kisira yalikuwapo katika fasihi simulizi, pia katika maandishi ya Kiswahili tangu zamani, kabla ya  ukoloni yalikuwapo maandishi yaliyohusu maisha ya Mitume na Masahaba. Mfano Hemed Bin Muhammed(1902) aliandika maisha ya Hemed Bin Muhhamed el Murjebi yaani Tippu Tip kwa maneno yake mwenyewe. Hivyo tunaona kuna mfanano wa kimaudhui na riwya za Kiswahili. Mfano wa riwaya hizo ni zile za Shaban Robert  Maisha Yangu (Nelson 1949) na Wasifu wa Siti binti Saad ( TALL 1958) na pia Rosa Mistika ya   E. Kezilahabi, (EALB 1971).

            Tendi ni ushairi simulizi ambao kwa kawaida ni mrefu na hueleza sifa mbalimbali za mashujaa. Mfano Utendi wa Fumo Liyongo ya Mohamed Kijumwa (1913), utendi wa Sundiata na au tendi wa vita vya Wadachi Kutamalaki Milima- Hemedi Abdulah (1985). Jadi hizi zilipelekea kuibuka kwa riwaya za kitendi, mfano Kadagaa Kamemwozea, Moto wa Mianzi ambayo ilizungumzia Wahehe na mtemi wao Mkwawa. Pia  kuna mfanano mkumbwa katika fani na maudhui ya tendi za kijadi na riwaya za Kiswahili ambapo maudhui ya tendi za kijadi yalikuwa yamelenga kuelezea sifa za mashujaa mbalimbali vilevile na riwaya za Kiswahil baadhi zipo zinazoelezea sifa mbalimbali za mashujaa.

           Visasili ni hadithi zinazoelezea chimbuko au asili ya watu, vitu, mataifa, na pia uhusiano wa wanadamu pamoja na mizimu. Zipo  riwaya ambazo ziliibuka kutokana na visasili mfano riwaya ya Lila na Fila (Kimbila 1966) ambayo ilikopi motifu ya ziwa Ikimba huko Bukoba, pia hadithi ya Mungu wa Wakikuyu na  Malimba  Majaliwa (E.Semzaba) nazo zinaelezea asili ya vitu mbalimbali.

          Visakale ni hadithi za kale kuhusu mashujaa wa taifa au dini. Mara nyingi visakale huchanganya historia na masimulizi ya kubuni. Mfano kulikuwa na hadithi ya chimbuko la mji wa pwani, Mijikenda na  Mwinyi Mkuu wa Zanzibar. Visa hivi vilipelekea kuibuka kwa riwaya kama Habari za Wakilindi (Abdalah Bin Hemed Ally Ajjemy 1972), Kisima cha Giningi ya M.S. Abdula (1968) na pia Hadithi ya Myombokele na Bibi Bugonoka.

         Baada ya kuangalia jinsi fani za kijadi zilivyopelekea kuibuka kwa riwaya ya Kiswahili zifuatazo ni hoja  zinazoonesha jinsi  maendeleo mbalimbali ya jamii au mazingira ya jamii yalivyopelekea kuibuka kwa riwaya ya Kiswahili.

           Kugunduliwa kwa hati za maandishi, kabla ya ujio wa wakoloni Afrika mashariki hususani Tanzania haikupata kuwa na hati za maandishi, lakini baada ya kuja  kwa Waarabu walileta hati za kiarabu lakini hata hivyo hazikutumika katika riwaya kwa sababu hawakuwa na utamaduni wa riwaya kwa hiyo hawakuleta athari yoyote katika riwaya bali athari za hati ya maandishi ya waarabu zilijitokeza katika ushairi wa Kiswahili. Hivyo basi baada ya kuja kwa wakoloni wa kizungu walileta hati za kirumi ambazo zilileta athari kubwa katika riwaya ya Kiswahili. Kwani watu  walijifunza kuandika hati hizo za kirumi na kuzitumia katika kuandika riwaya ya Kiswahili. Mfano riwaya ya Safari za Waswahili, Habari za Wakilindi, Uhuru wa Watumwa ya J. Mbotela (1934). Riwaya hizi za kiswahili ziliandikwa baada ya kugunduliwa kwa hati za maandishi.

           Pia kuwapo kwa teknolojia ya urudufishaji na usambazaji, ugunduzi huu wa teknolojia  ya upigaji chapa vitabu uligunduliwa na Johannes Gutenberg huko Ujerumani mwaka 1450. Ugunduzi huu ulirahisisha kazi ya uchapaji vitabu katika nakala nyingi na kuondoa kabisa hali ya kunakili kwa mikono. Teknolojia hii ilienea Afrika mashariki baada ya ujio wa wakoloni ambapo ilisaidia kuibuka kwa uchapaji na usambazaji wa riwaya za Kiswahili. Mfano 1948 kulianzishwa shirika la vitabu Afrika mashariki (EALB) ambapo lilirahisisha uchapaji wa kazi mbalimbali za riwaya za Kiswahili. Mfano Mzimu wa  Watu wa Kale (1960) na Kurwa na Doto (1960).

          Vilevile  ukuaji mkubwa wa kiuchumi, uchumi mkubwa ulisaidia kuibuka kwa riwaya ya Kiswahili kutokana na kuwapo kwa tabaka la watu wenye pesa ambao waliweza kununua vitabu vingi vya riwaya na kujisomea. Hii ilipelekea uzalishaji mwingi wa vitabu vya riwaya ya Kiswahili  kwa ajili ya kuwaburudisha pia kutokana na uhakika wa soko riwaya nyingi zilizalishwa kwa wingi zaidi. Mfano katika kipindi cha ukoloni ambapo wakoloni walikuwa na uchumi uliotengemaa hivyo hawakuwa na kazi za kufanya kwa sababu kazi zao nyingi zilifanywa na waafrika. Hivyo walipata muda mwingi wa kusoma vitabu vya riwaya kutokana na hali hiyo ilipelekea kuibuka kwa riwaya nyingi zaidi.

             Kuwapo kwa mfumo rasmi wa elimu, mfumo huu uliletwa na wakoloni wa Kiingereza na Kijerumani ambao walianzisha shule mbalimbali zilizosaidia  watu wengi kujifunza kusoma na kuandika. Kwa hivyo watu waliojifunza kusoma na kuandika,  waliandika na kusoma riwaya kwa wingi kitu ambacho kilipeleke kuibuka kwa riwaya nyingi za Kiswahili. Mfano Kusadikika, Uhuru wa Watumwa, Kufikirika, Adili na Nduguze. Hivyo basi inaonesha kuwa kadiri elimu ilivyopanuka na ndivyo wasomaji na waandishi wa vitabu vya riwaya walivyoongezeka na kufanya kuwepo hadhira kubwa nzuri ya wasomaji na watunzi wa riwaya ya Kiswahili.

         Vilevile kuwapo kwa maskani ya kudumu, kwa mtu anayeishi maisha ya kuhamahama  ni vigumu sana kujijengea jadi ya kusoma, hawapati fursa ya kukaa na kuweza kusoma na kuandika. Muda mrefu wa mchana  hutumika katika kuchunga mifugo yao, kurina asali, kuwinda, kusaka na kukusanya matunda na mizizi kwa ajili ya chakula hivyo hawapati fursa nzuri ya kujishughulisha na elimu ya kusoma na kuandika hivyo kwao riwaya ni kitu kigeni. Baada ya kuwepo kwa maskani ya kudumu watu walipata fursa nzuri ya kusoma na kuandika. Hii ikawasaidia kuandika na kusoma riwaya kwa wingi na kupelekea kuibuka kwa riwaya ya Kiswahili.

          Kwa kuhitimisha tunaweza kusema kwamba, japokuwa kuibuka kwa riwaya ya Kiswahili kumetokana na mambo makuu mawili ambayo ni fani za kijadi na mazingira ya jamii lakini inayoonesha mashiko zaidi ni ile ya maendeleo mbalimbali ya jamii au mazingira ya jamii,kwa sababu jamii inavyozidi kuendelea katika nyanja mbalimbali inapelekea  riwaya kuandikwa kwa wingi kutokana na kuongezeka kwa waandishi au watunzi na wasomaji wa riwaya hizo.
 
                                      MAREJEO

Madumulla,J.S (2009). Riwaya ya Kiswahili,Historia ya Misingi ya Uchambuzi, Nairobi: Sitima   

                       printer and station Ltd.

Mhando, P na Balisidya (1976). Fasihi na sanaa za maonyesho, Dar es salaam: Tanzania

                       publishing house.

Mulokozi, M.M (1996). Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili, Dar es salaam: TUKI.

Senkoro, F.E.M.K (2011). Fasihi Andishi, Dar es salaam: Kauttu Ltd

 

Powered by Blogger.