Simulizi; "NABII WA UONGO "






*SEHEMU YA 01**

Anga jeusi lilitanda huku harufu kali ya moshi wa viwandani ulipenya vilivyo katika matundu mawili ya pua yangu, lakini sikuweza kujali karaha hiyo bali niliendelea kusukuma mkokoteni wangu  uliojaa taka mbalimbali za soko kuu la Kariakoo na kwenda kutupa dampo kuu la jiji. Nikiwa nimekata tamaa na maisha yangu magumu niliyokuwa naishi, huku jua kali la kila siku la  Dar es salaam likiwa sehemu ya maisha yangu, ghafla nilishangaa kuona prado nyeusi ikipaki pembeni ya mkokoteni wangu, na kunifanya niwe na hofu, kwani kioo cha gari kilishushwa na mzee mmoja aliyekuwa akiendesha gari lile aliweza kuniita kwa kutumia ishara ya mikono yake. "Pole sana kijana wangu kwa kazi nzito ,kazi ngumu sana ya kimaskini isiyo na kipato, lakini unaweza kuwa bilionea kama ukipenda, chukua bisinesi kadi yangu utanitafuta nikusaidie ",mzee yule alizungumza na kuahidi kunisaidia, na kufanya uso wangu kutabasamu kwa furaha kwani nilikua nimechoshwa na maisha ya kifukara niliyokuwa naishi. "Asante sana mzee wangu, mungu akubariki, nakuahidi nitafanya kazi hiyo kwa nguvu zote, nimechoshwa na maisha haya ya kulala njaa kila siku ",niliongea kwa furaha sana huku nikipokea bisinesi kadi pamoja na pesa kutoka kwa mzee yule aliyeonekana kuwa na maisha mazuri sana, na kisha akaliondoa gari lake mbele ya macho yangu na kuniachia maswali mengi kwani si rahisi mtu kukusaidia bila malipo yoyote.


Kutokana na furaha kunizidi, nilitelekeza mkokoteni wangu kwani pesa niliyopewa na mzee yule ilinitosha sana kwa matumizi ya siku mbili tatu mpaka atakaponipatia kazi, hivyo nilipanda daladala na kisha kuelekea mbagala, sehemu niliyokuwa nimepanga chumba changu kidogo nilichokilipia   shilingi elfu kumi tu kwa mwezi kwani kilikuwa hakina sakafu wala umeme. "Haloo mzee, mimi ni Hakika, kijana msukuma mkokoteni uliyeahidi kunisaidia ",nilijitambulisha huku nikiwa nahamu sana ya kusikia jibu nitakalopewa, baada ya kumpigia simu mzee yule ,nikiwa nyumbani nimejilaza katika kigodoro changu ambacho nilikitandika chini, kwani sikuwa na uwezo wa kununua kitanda. "Ahaa nafurahi sana kama umeweza kunipigia, inaonekana utafanikiwa sana, kesho njoo nyumbani kwangu masaki kisha tutaelekea sehemu kwa ajili ya kukuelezea kazi yenyewe ",mzee yule alinipatia maelekezo na kufanya furaha yangu izidi kuongezeka, kwani maneno yale yalinifanya nizidi kuwa na hamu ya kuwa tajiri. "Mzee huyu anahuruma sana, nikipata kazi mshahara wa kwanza sichukui, itakua ni zawadi yake ",niliongea peke yangu baada ya kukata simu, huku nikibonyeza simu yangu na kuitafuta namba ya mama yangu ili nimfahamishe juu ya mimi kupata kazi ambayo niliambiwa itanifanya kuwa tajiri, bila kujua hatari na madhara makubwa ambayo yalikuwa mbele yangu.



Usiku ulikua mrefu sana kwani sikuweza kupata usingizi, nikisubili asubuhi ifike niweze kuelekea nyumbani kwa mzee yule, mzee niliyemuona kama mkombozi wangu kwani nilikua sina thamani katika jamii, kutokana na umaskini wangu. "Waoooh hatimae siku yangu ya mimi kuwa bilionea imefika, "niliongea kwa sauti kubwa baada ya mwanga wa jua kupenyeza chumbani kwangu, na kisha kujiandaa haraka sana kuelekea masaki kwa mzee yule, ambaye sikuweza kufahamu kazi yake wala jina lake, zaidi ya kuwa na namba yake ya simu kwani jina lake liliandikwa kwa lugha ya Kiarabu katika bisinesi kadi yake hivyo sikuweza kulielewa.


…………………………………


Mandhari mazuri ya kuvutia, huku nyumba nzuri za kifahari ziliupamba vizuri mtaa wa Masaki, mtaa ambao vigogo na matajiri wakubwa ndiyo makazi yao. Nikiwa nimevalia jinsi yangu pamoja na tisheti, nguo ambazo nilizivaa katika matukio maalumu nilifika nje ya geti ya jengo ambalo nikielekezwa na mzee yule, na kisha kubonyeza kitufe cha kengele kilichokuwa ukutani na bila kuchelewa mzee yule aliweza kutoka nje na kunikuta nikiwa namsubili  "Kijana kumbe ni wewe, nilizani utapotea, nisubili hapa nje nitoe gari yangu tuelekee Bagamoyo " ,mzee yule aliongea huku akitabasamu, na kunifanya niwe na maswali mengi kwani sikujua kama tutakua na safari ya kutoka nje ya jiji "mmmh kazi gani hii, na Bagamoyo tunaenda kufanya nini?? ",maswali yalikisumbua kichwa changu bila majibu, na kujikuta furaha yangu niliyokuwa nayo ikipungua.


"Ukikubali na kufata masharti ,kesho tu utakua bilionea ",mzee yule aliyekuwa na ndevu nyingi zilizopakwa dawa na kumpendeza vilivyo, alianzisha mazungumzo baada ya kimya kutawala kwa muda mrefu tukiwa ndani ya gari, lakini maneno aliyonieleza yalizidi kuniongezea maswali kichwani mwangu kwani sikujua kama kuna masharti yalikuwa yakihitajika ili mimi nifanikiwe. "Usjali mzee wangu, nitajitahidi kadri ya uwezo wangu ",nilizungumza maneno yaliyoonekana kumfurahisha mzee yule, huku tukiikanyaga ardhi ya Bagamoyo baada ya dakika arobaini ndani ya gari.



"Tumefika, hapa ndipo patakuondolea umasikini, hata utajiri wangu niliupatia mahali hapa ",mzee yule alinielezea siri ya utajiri wake, baada ya kuanza kukatiza mitaa mbalimbali ya Bagamoyo iliyokuwa na majengo mengi ya kale. "Kweli mzee, nafurahi kusikia ivo ",niliongea na kutabasamu, huku nikiwa nahamu ya kufahamu kwa undani zaidi jinsi mzee yule aliweza kuupata utajiri wake.


Tulipaki gari pembeni ya jengo moja ambalo sikulifahamu, na kisha kuingia ndani ya jengo lile lililochakaa sana. Lakini ghafla mapigo ya moyo wangu yaliongezeka na kwenda kasi sana ,kwani nilishangaa baada ya kugundua chumba tulichoingia palikuwa ni kwa mganga wa kienyeji kutokana na mavazi yake pamoja na tunguli zilizokuwa zikining'inia ndani ya chumba kile. "Mungu wangu, nakufa uwiii!!",,nilipiga kelele na kutaka kukimbia kwani joka kubwa liliinuka na kisha kujiviringisha huku mganga yule akilikalia kwa ajili ya kutusikiliza, lakini kwa upande wa mzee aliyenipeleka hakuweza kuogopa chochote kile na alionekana kupazoea sana mahali pale.


"Mtukufu nyoka ,huyu ndiye kijana niliyemleta atusaidie kazi zetu ",mzee yule alizungumza huku akipiga magoti mbele ya joka lile, huku mganga aliyelikalia akimminia kichwani damu iliyokuwa katika kichupa kidogo sana. "Asante sana, na utajiri wako utadumu milele ",Joka lile lilizungumza kwa sauti nzito sana na kuzidi kunigopesha ,kwani tangu nizaliwe sikuwahi kushuhudia nyoka akiongea tena kwa kutumia lugha ya kiswahili na kueleweka. Nikiwa nazidi kushangaa, mzee yule alinishika mkono na kunisihi nipige magoti mbele ya joka lile kubwa, lenye vichwa vingi sana ambavyo sikujua idadi yake.


"Kuanzia sasa wewe ni Nabii Hakika, utafanya kazi ya unabii wa uongo, kupotosha watu wanaomwamini Mungu ",Joka lile lilitamka maneno yaliyobadilisha fikra zangu na kujikuta nikichukia watu waliomtegemea Mungu katika dini zote, huku nikikabidhiwa fimbo, kitambaa cheupe pamoja na maji yaliyokuwa katika kichupa kidogo kutoka kwa joka lile la kutisha pamoja na mganga.. "Nimekubali mtukufu nyoka ",niliongea maneno ya kukubaliana na kazi niliyopewa, huku nikitabasamu bila kujitambua kwani fikra zangu zilikuwa zimefutwa kishirikina bila kujitambua.


…………………………………


Kwa muda wa wiki moja tu, jiji la Dar es salaam lilifurika maelfu ya watu kutoka mataifa mbalimbali, kufata huduma ya uponyaji na maombezi katika kanisa langu ambalo niliwezakukusanya mamilioni ya pesa kama sadaka kutoka kwa waumini wangu. ",Ukinywa maji haya, utapona maradhi yanayokusumbua, pamoja na mapepo yote ",niliongea huku nikimnywesha mmoja kati ya maelfu waliokuwa kanisani kwangu, na kumfanya kugaagaa chini akipiga kelele baada ya kunywa maji yale. Huku kelele za shangwe sikisikika kwani nilionekana kama Mungu mtu kwa kutatua shida zao kwa kutumia nguvu za giza nilizokuwa nazo, huku nikitumia maneno machache niliyoyakalili kwenye bibilia kudanganya watu.



**ITAENDELEA ***
Powered by Blogger.