SEHEMU YA PILI YA HISTORIA YA WASAFWA


SEHEMU YA PILI YA HISTORIA YA WASAFWA
Jamii kubwa kuliko jamii zote katika wilaya ya Mbeya ni Wasafwa. Wasafwa huishi katika
milima ya Mporoto Kaskazini ya mlima Rungwe na katika bonde ambalo laenea kati ya milima ya
Mbeya upande wa Kaskazini na milima ya Umalila na Unyiha kwa upande wa Kusini na Kusini
Magharibi. Mali kadhalika, Wasafwa huishi upande wa Kaskazini wa mlima Mbeya na katika sehemu
ya uwanda wajuu unaopakana na Wilaya ya Chunya.
Wasafwa wanazungukwa na jamii hizi:- Wasangu upande wa Kaskazini, Wanyiha upande wa
Magharibi, Wamalila upande wa Kusini-Magharibi, na Wanyakyusa kwa upande wa Kusini.
Wasafwa hawajapata kuwa chini ya Utawala wa namna moja, bali walikuwa wametawaliwa na
machifu mbali mbali. Machifu wa Kisafwa waliokuwa wanajulikana sana tokea karne ya 19 ni Mwalyego ambaye alijenga nyumba yake kwenye miteremko ya milima ya Mbeya karibu na Utengule,
Chifu Lyoto alitawala sehemu ya mteremko wa mlima Mbeya upande wa Usafwa ya Kaskazini
kuelekea bonde la Usangu, Zambi alitawala sehemu ya upande wa Kaskazini - Mashariki za
miteremko ya milima ya Umalila, Malema alitawala sehemu za Kaskazini - Mashariki za miteremko ya
milima ya Unyiha.
Ingawa ni vigumu sana kujua chimbuko la Wasafwa lakini koo mbali mbali za Wasafwa
zakumbuka wapi zilitoka. Chimbuko la Wasafwa limo katika sehemu tatu. Sehemu ya kwanza ni ile
inayowahusu Wasafwa ambao asili yao ni Ugogo. Ziko sababu nyingi ambazo zilisababisha kwa
Wagogo fulani kwenda kuishi sehemu za Usafwa na kuoana na Wasafwa. Nchi ya Mbeya ilikuwa na
rutuba nyingi kwa kupanda mazao ya chakula, biashara ya utumwa ambayo iliendeshwa zaidi na
Waarabu, na kadhalika. Msafara wa watumwa ulifuata bonde la Usangu kuelekea sehemu za pwani
ambako ndiko yalikuwako masoko ya kuwauzia hao watumwa. Njia hii ya watumwa ilifuatwa wakati
njia ya kupitia Ugogoni ilipoonekana ni ya gharama kubwa sana kwa wafanya biashara hii na wakati
mwingine ilifungwa na jamii za Kigogo kwa sababu mbali mbali za kutoelewana na Waarabu,
Wafanya biashara. Na kama tunavyoelewa machifu wa Kiafrika nao walijitupa barabara katika
biashara hii na kuwauza wenzao. Kwa hiyo, Wagogo waliokwenda sehemu za Mbeya yawezekana
walifuata biashara halafu baadaye wakafanya mastaakimu yao pande hizi za Mbeya na kuweza
kuoana na Wasafwa wa huko na baadaye watoto wao wakafuata malezi ya Kisafwa na kuwa Wasafwa
Kamili. Pengine hao Wagogo walikwenda sehemu hizo za Usafwa kwa sababu ya kukimbia taabu ya
kutiwa utumwani na Waarabu kwa sababu njia kuu ya biashara ya utumwa ilipitia katika nchi yao.
Chimbuko jingine la Wasafwa ni Ukinga. Hasa hili ndilo chimbuko kubwa la Wasafwa ambao
kwa mila na desturi wanafanana nao sana. Wasafwa wanatoa sababu kubwa iliyowafanya waje
sehemu hizi za Mbeya nayo ni sababu ya kupata moto. Kama inavyosimuliwa na wazee wengi wa
Kisafwa, watu wa asili waliokuwa wanakaa pande za Mbeya, walijua jinsi ya kutengeneza moto, na
Wasafwa wengi wakafuata utaalam huo toka pande za Ukinga na baadaye wakafanya maskani yao
huko pengine baada ya kuwafanyia vita wenyeji wa huko halafu wao Wasafwa ndio wakawa watawala
wa nchi yote ya Mbeya. Kwa kawaida Wasafwa wana desturi ya kukoka moto mmoja halafu huo moto
huenea nchi nzima ya Usafwa. Moto huu ulikokwa kwa kufuata sherehe maalum.
Chimbuko la tatu la Wasafwa ni Unyakyusa na pande za Kaskazini za Malawi - Karonga. Kwa
mfano, chifu Mwalyego ambaye baadaye alifanywa na Wajerumani kuwa chifu mkuu wa Wasafwa
katika mwaka wa 1898 yeye husimulia kuwa asili yao ni Karonga na baba mkubwa wa Mwalyego
(great grand father) Bwana Shyungu aliishi Karonga na utawala wake ulienea sehemu yote ya nchi ya
Ukonde. Mtoto wake Mwamwondo alifanya maskani yake Nshorongo sehemu iliyo karibu na milima
ya Igale. Mtu huyu alioa wanawake wengi na pia alioa binti ya Chifu Lyoto ambaye alitawala Usafwa
wakati huo. Baadaye Mwamwondo akaasi na kumpindua mkwewe na yeye akawa ndiyo mtawala wa
sehemu hii ya Usafwa. Mwamwondo alizaa wavulana wengi. Mwamparandje, Mwenipyana na
Nsewe. Mtoto huyu Nsewe alizaliwa na mke wa Mwamwondo ambaye alikuwa binti ya Lyoto.
Mwamwondo alifariki dunia mara baada ya Nsewe kuzaliwa. Mwamparandje akatawala nchi ya
Nshorongo badala ya baba yake. Walakini ndugu yake Mwenipyana alipigana na Mwamparandje na
akamshinda. Kwa hiyo Mwenipyana akatawala sehemu ya Nshorongo na Mwamparandje akakimbilia
katika milima ya Igale.
Wasafwa walimkataa Mwenipyana kwa sababu mama yake hakuwa Msafwa na pia tabia yake
mbaya ilimfanya asikubaliwe kutawaia. Wakati Wangoni walipoingia Mwenipyana aliwasaidia
Wangoni kwa kuwapa chakula ambacho raia wake walikihifadhi. Tabia hii iliwaudhi sana Wasafwa,
kwa hiyo wakamkataa kuwatawala.
Mwamwondo alipofariki mke wake, binti Lyoto alirudi kwa baba yake pamoja na mtoto wake
Nsewe. Nsewe alipokua, babu yake Lyoto alimteua Nsewe kuwa chifu badala ya baba yake -
Mwamwondo. Baadaye Nsewe akamwasi babu yake na akapigana naye kalazimika kukimbilia
milimani alikofia wakati wa majilio ya Wangoni. Nsewe alizaa watoto wengi:- Mwalyambi, Zambi,
Milambo, Ngaja, Nswila, Mpoli, Mwansonswe, Mwembe, Sidjodjo, Djedjo na Mudjenda. Nsewe
aligawanya sehemu ya Utawala wake na kuwagawia watoto wake hawa.
32
Wasangu chini ya chifu Merere walipoingia katika nchi ya Nsewe, Nsewe alikufa wakati wa
vita na watoto wake wakatoroka. Nswila allkwenda Ukonde, Zambi akakimbilia Unyamwanga na
watoto wengine wakajificha chini ya machifu wengine. Nswila hakukata tamaa na kwa msaada wa
machifu wa Unyamwanga na Unyiha, akawashambulia Wasangu na akawashinda na kuwatoa toka
nchini mwake. Nswila alipotuliza nchi yake, ndugu zake wote wakarudi toka walikokimbilia na
wakamheshimu sana kwa kitendo alichokifanya cha kuwafukuza Wasangu toka Usafwani, lakini
hawakumkubali kama yeye ndiye chifu mkuu wa Usafwani. Badala yake kila mmoja wao alitawala
sehemu aliyopewa na baba yao Nsewe.
Powered by Blogger.