Simulizi; NABII WA UONGO








Simulizi; NABII WA UONGO

**SEHEMU YA 09**

Japo siri zangu ziliwekwa wazi na Juliet, lakini kwa upande wangu sikuathirika na jambo lolote lile. Nyoka yule mkubwa ambaye alikua kiongozi katika chama chetu cha kishetani, alifuta kumbukumbu ya kila mmoja aliyeweza kuhudhuria ibada siku ya jumapili, na kushuhudia mambo ya ajabu ambayo mzimu wa Juliet uliweza kuyazungumza kuhusu mimi.

Sio hilo tu! lakini pia hakuna chombo cha habari chochote kile ambacho kiliweza kutangaza yale ambayo Juliet aliweza kuyaongea kanisani kwangu, kwani joka lile kubwa lilipoingia kanisani lilikanyaga na kuvunja vunja kamera zote za waandishi wa habari ambao walikuwa wakirekodi na kuchukua matukio mbalimbali kanisani. Kwani kila mwandishi wa habari alikimbia ili kuyaokoa maisha yake pale alipolishuhudia joka lile kubwa lenye vichwa vingi sana, huku nyoka mdogo ambaye nilikuwa nikiishi naye akimeza mtu yeyote ambaye alikutana naye uso kwa uso.

"Hatimaye maisha yanaendelea! lakini yaliyotokea jana ni changamoto kwangu, na kwa chama chote!  Inatakiwa tutafute namna ya kumzuia Juliet bila hivyo, mwisho wetu utakua mubaya ",niliongea peke yangu huku nikiwa nimeketi sebuleni kwangu siku ya jumatatu, nikitafakali matukio yote ambayo yaliweza kutokea siku iliyopita. Lakini cha kushangaza waumini wengi walinipigia simu kama kawaida na kunipongeza kwa huduma nzuri ya mahubiri niliyoitoa jumapili iliyopita, jambo ambalo lilinifanya nigundue kuwa, hawakutambua chochote kile ambacho kiliweza kutokea.

"Haloo!  pastor Hakika! barikiwa sana mtumishi wa Mungu, jana umehubiri vizuri mpaka nikatamani mshahara wote wa mwezi huu nikupatie wewe kama zawadi ",yalikuwa ni maneno ya muumini mmoja wa kiume, mmoja wa waumini kati ya wengi ambao walikuwa wakifanya kazi TRA, akinishukuru kwa huduma nzuri niliyoitoa siku iliyopita na kuniahidi donge nono mala tu mshahara utakapotoka.

"Habari mchungaji! yaani, jana umenifanyia maombi mpaka mguu wangu umepona kabisa, na leo kwa mala ya kwanza tangu nisumbuke kwa mwezi mzima nimeweza kwenda kazini",ilikuwa ni sauti ya binti mmoja mrembo sana, binti ambaye alikuwa wa kwanza kumlaghai kimapenzi na kunikubalia, japo alikuwa na kazi nzuri  sana, kwani alikuwa muhasibu katika benki kuu ya Tanzania (BOT), lakini alikuwa bado na tamaa ya pesa. Hakuridhika na mshahara wake mzuri ambao alikuwa akiupata, na hapo ndipo nilipotumia udhaifu wake kwa kumuhonga gari zuri sana aina ya hummer, na kupanua mapaja yake bila kipingamizi chochote kile. Lakini tangu nimuhonge gari lile, nyodo ziliongezeka mtaani na kuwadharau wengine hasa wenye kipato cha chini, alitembea huku na kule kwa mwendo mkali sana kwani trafiki wengi waliogopa kuisimamisha gari hii ya kifahari, huku wakimuombea njaa msichana huyu kwani alikua kero sana kila alipokuwa akiendesha gari lake jipya aina ya hummer, gari ambalo nilimuhonga na kisha kunipatia penzi, huku mimi nikimcheka na kumuona kama takataka baada ya kulala naye.

Hatimaye Doreen alipatikana! maombi ya wenye kipato cha chini ambao walimuombea njaa siku zote, kwani aliwamwagia matope kila alipopita na gari lake, maombi yao yaliweza kutimia. Doreen alipata ajari akiwa njiani mida ya jioni akitoka kazini, kwani gari lake breki ziligoma na kujikuta akigongana uso kwa uso na basi dogo aina ya costa, basi la daladala lakini cha kushangaza hakuna abiria yoyote yule aliyeweza kuumia, wala costa lile halikuweza kuharibika kifaa chochote kile, huku gari la Doreen likisagika kabisa na kumvunja mguu Doreen.

Kitendo kile kilimshangaza kila mmoja, hakuna mtu yeyote ambaye alikuwa na majibu ya ajari ile zaidi yangu mimi. Kwani ajari niliisababisha ili niweze kutoa kafara ndogo ya damu kwenye chama changu, damu ambayo ilitoka katika mguu wa Doreen. Isitoshe, nilitaka binti yule asizidi kulimiliki gari lile, gari ambalo lilikuwa mali yangu japo nilimpatia kwa kumuhonga. Hatimaye jeraha la Doreen lilianza kuoza siku hadi siku, kila hospitali waliweza kushindwa na kujikuta akikaa tu nyumbani kwa mwezi mzima akiuguza mguu wake.

Lakini nilishangaa akinipigia simu na kuniambia niliweza kumuombea na kumponya mguu wake ijumapili iliyopita, ijumapili ambayo ilijawa na matukio mengi na ya kushangaza sana kanisani kwangu. Sikujua ninani aliweza kufanya muujiza huu, na kufanikiwa kulisafisha jina langu.

"Hakikaa usishangae, wewe ni mshindi, !! Mimi mkuu wako nyoka ndiyo nimekusafishia jina lako, endelea na huduma yako kanisani kama kawaida, hakuna mtu yeyote anayetambua siri zako, wale wote ambao sikufanikiwa kufuta kumbukumbu zao kwani waliwahi kutokomea nimeshawaua isipokuwa wazazi wako pamoja na wazazi wake Juliet, ndiyo pekee waliobakia wanafahamu uovu wako, nimeshindwa kuwafanyia chochote kile kwani Juliet anawalinda ",hatimaye nilipata jibu kuhusu muujiza wa simu za kunipongeza, ambazo nilikuwa nikipigiwa. Sauti ya kutisha kutoka kwa mkuu wangu Nyoka, nyoka mwenye vichwa vingi sana ndiye aliyenifahamisha kuhusu jambo hilo alilokuwa amenifanyia na kulisafisha jina langu.

"Hapa angalau nina amani, lakini wazazi wangu, Juliet kawapendea nini?, kwanini anawalinda kiasi hiki ",nilijiuliza swali kutokana na kushangazwa na kile ambacho Juliet alionekana kuwafanyia wazazi wangu, kila jambo ambalo alikuwa akilifanya. Alihakikisha wazazi wangu wakiwa katika mikono salama.

"Nina wapenda sana wazazi wako, kwani hawana hatia, wamekuzaa kwa uchungu, badala uwalipe mema, unataka kuwaua kwa tamaa ya pesa ",nilishangaa kusikia sauti, sauti ambayo iliongea huku ikijirudia rudia mithili ya mwangwi. Bila shaka alikuwa ni Juliet! kwani sauti yake niliitambua vilivyo.

Niliangaza juu sehemu ambayo sauti ilikuwa ikitokea lakini sikuona kitu, niligeuka na kuangaza nyuma yangu sikuona tena kitu. Nikajikuta Hatimaye nikabaki nimepigwa na butwaa tu, nikiwa nimekosa nini niweze kufanya, kwani niliamini msichana yule angeweza kunifanyia kitendo chochote kile kutokana na ushujaa wake aliouonyesha mbele ya mganga pamoja na mzee Jabir na kuwashinda nguvu.

"Naamini unayoyafanya ipo siku utayaacha, nitapambana na wakuu wako na kuhakikisha nakutoa kwenye dhambi ambazo unazifanya ",Juliet alitokea kimaajabu na kuketi karibu yangu, katika sofa ambalo nilikuwa nimekalia sebuleni. NIilitamani kukimbia, lakini roho ilisita na kubaki nikiwa nimeketi tu nikimtazama msichana mrembo Juliet, huku akiwa amevalia gauni jeupe ambalo lilifunika mpaka unyayo wa miguu yake.


Kwa mbali nilitafakali maneno ambayo alikuwa ameniambia, kuhusu kunitoa kwenye chama changu cha kishetani. Nilijikuta nikicheka kwa sauti kubwa kama kichaa, niliona kama alikuwa akiota ndoto ya mchana kweupe. Sikuwa tayali kurudi kuishi maisha ya kimaskini, maisha ya kula chipsi kavu za shilingi elfu moja kwa siku nzima, maisha ya kuishi stoo. Nilikuwa tayali kutoa uhai wa mtu yeyote yule, kukwepa kurudi maisha niliyokuwa nikiishi zamani.

"Nina nguvu za kutosha kupambana na kukukomboa, naamini wiki hii itaisha ukiwa katika mikono salama.",maneno ya Juliet yalinifanya nisitishe kicheko changu mithili ya dereva wa gari  afinyapo breki ghafla, na kujikuta nikitafakali sentesi aliyomalizia kuiongea na kisha kupotea kama upepo mbele ya macho yangu.

Ilibidi ninyanyuke kuelekea katika chumba changu cha siri, chumba ambacho nyoka wangu alikuwa akiishi, nikaweze kuzungumza naye na kumwelezea kila kitu ambacho Juliet aliweza kukiongea, nisikie ushauri wake ambao angeweza kunipatia, pamoja na kunihakikishia usalama wangu.

*ITAENDELEA **
Powered by Blogger.