SINTAKSIA YA KISWAHILI
SINTAKSIA YA KISWAHILI.
Maana ya sintaksia
Sintaksia ni tawi la isimu ambalo linahusu namna maneno yanavyoungana na
kuhusiana katika kirai au sentensi. Sintaksia inachunguza namna maneno
yanavyojipanga katika sentensi kwa kuzingatia kanuni za sarufi ya lugha
husika.
Mikabala tofauti ya Sintaksia
Uchambuzi wa muundo wa lugha umefanywa na wanasarufi wa nyakati tofauti na kuzua mikabala tofauti kuhusu muundo wa lugha kama walivyouona kwa wakati wao. Mkabala wa awali uliokuwa umejikita katika lugha kongwe kama Kilatini ulikuja kujulikana baadaye kama wa kimapokeo kwani ndio uliorithishwa kutoka kizazi hadi kizazi na kutumika kuchambua lugha nyingine za dunia.
Mkabala mwingine ni ule ulioichambua lugha kwa kuzingatia vijenzi vinavyounda sentensi na ulioasisiwa na Chomsky. Mkabala huu ulijulikana kama mkabala wa kimuundo ambao hata hivyo baadaye ulifanyiwa marekebisho zaidi na mwenyewe Chomsky na waliomfuata.
MKABALA WA KIMAPOKEO
Wanamapokeo walichambua sintaksia ya lugha kwa kuainisha miundo ya sintaksia iliyo katika lugha. Kwa mujibu wa wanamapokeo, virai na sentensi zimeundwa na kategoria za kisarufi yaani manenoambayo kila moja liliainishwa na uamilifu wake kutajwa. Kwa hivyo mwanaisimu alichambua sentensi kwa:
a) kutaja kategoria za kisarufi za maneno yanayounda sentensi
b) kueleza kazi au uamilifu wa kila neno lililounda sentensi.
Kwa mfano:
‘Mama anapika chakula’.
Sentensi hii ilichambuliwa kwa kueleza:
>>Muundo: Sentensi hii inaundwa na maneno matatu: ‘mama’, ‘anapika’ na‘chakula’ na kwamba kila neno lina kategoria yake
>>Kategoria za maneno yanayounda sentensi: ‘mama’ na chakula’ ni nomino
za umoja, na ‘anapika’ ni kitenzi kilicho katika wakati uliopo.
>>Uamilifu wa kila neno: ‘Mama’ ni kiima, ‘anapika chakula’ ni kiarifu.
>>Aina ya sentensi: Sentensi hii ni kishazi. Hii ni sentensi arifu.
Aidha wanamapokeo walichambua sentensi kwa kubainisha kategoria za maneno yaani aina za maneno kwa mujibu wa maana zake, vipengele vya kimofolojia na au tendo.
Nomino ilifafanuliwa kuwa ni jina la kitu, mtu, mnyama, hali. Nomino huweza kuhesabika au kutohesabika na kwamba huwa na umoja na wingi au umoja tu au wingi tu. Kitenzi kilifasiliwa kuwa ni neno lenye kudokeza tendo ambalo huchukua viambishi vya wakati uliopo, uliopita au ujao,mtenda ambaye huwakilisha kiima katika kitenzi , mtendwa n.k. Katika sentensi kitenzi hufuata kiima ambacho ni nomino mtenda au kufuatwa na nomino mtendwa au yambwa.
Kwa hivyo sentensi ‘ Mama amelala’ ingechambuliwa hivi:
Sentensi hii ina nomino ‘mama’ ambayo ina uamilifu wa kiima cha sentensi
yaani mtenda na kitenzi ‘amelala’ chenye uamilifu wa kiarifu cha sentensi.
Kitenzi hiki ni sielekezi.
MKABALA WA KIMUUNDO (kama ulivyoasisiwa na Noam Chomsky)
Nadharia ya Sintaksia ambayo mwasisi wake ni Noam Chomsky imejaribu kueleza vipengele vya kisintaksia vya lugha mbalimbali ili kuonyesha jinsi lugha mahsusi zinavyopanga maneno yao ili kupata sentensi.
Lengo la Chomsky katika uchanganuzi wake wa lugha ni kuunda nadharia ya sintaksia ya jumla itakayonyesha vipengele vya kisintaksia vinavyopatikana
katika kila lugha na jinsi vinavyotofautiana. Hii inafahamika kama nadharia
ya sarufi ya jumla.
Lengo lingine la Chomsky ni kupinga mtazamo wa wanaisimu wa miaka 1950 (wanamapokeo) waliodai kuwa tofauti za lugha hazina ukomo, mtazamo ambao hakuuafiki kwani ulimaanisha kuwa ingebidi kila lugha iwe na nadharia yake. Alidai kuwa tofauti baina ya lugha ni ndogo na kwamba
nadharia ya sarufi ya lugha ingeweza kujumuisha lugha zote isipokuwa kwa tofauti ndogondogo tu. Alibainisha kategoria za virai kuwa ni:
- KN,
- KT,
- KV,
- KE,
- KH,
- KU.
Muundo ni mpangilio wa vitu vidogo vilivyowekwa pamoja na kujenga kitu
kikubwa zaidi.
Sarufi miundo virai ni mkabala wa kuchambua lugha kwa kuigawa sentensi
katika virai vinayoiunda na kisha kuvichanganua zaidi hadi kufikia neno moja
moja lililokiunda kirai.
Tungo huundwa na viambajengo kwa utaratibu maalumu.Tungo za lugha ni
neno, kirai, kishazi na sentensi. Virai, vishazi na sentensi huundwa na
maneno.
Muundo wa kirai na sentensi
Kirai, kishazi na sentensi ni vipashio vya lugha vinavyoundwa naviambajengo ambavyo ni vidogo kuliko vyenyewe. Kirai hujengwa na maneno, na kishazi na sentensi hujengwa na virai. Viambajengo vya tungo ndivyo vinavyofanya muundo wa tungo husika.
Muundo wa Kirai
Kirai ni fungu la maneno yanayohusiana kimuundo lisilokuwa na muundo wa kiima kiarifu. Maneno katika kirai humilikiwa na neno moja ambalo ndilo neno kuu. Kirai hubainishwa na kategoria ya neno kuu. Kwa mfano: KN, KT,KV, KE KH n.k.
Virai huundwa na viambajengo. Kiambajengo ni kikundi cha maneno au hataneno moja pia inayofanya kazi kama kitu kimoja. Kirai, kishazi au sentensini mkusanyiko wa viambajengo kadha.
Kirai ni mkusanyiko wa viambajengo vilivyojengwa kuzunguka neno kuu.
Kwa mfano, KN huundwa na nomino na vivumishi vyake, kwa hivyo muundowa kirai ni maneno yanayokiunda yakiwakilishwa na alama za kategoria za
maneno hayo.
Kwa mfano:
a) ‘Mtoto mdogo’.
Hiki ni Kirai Nomino (KN) kilichoundwa na N (nomino) na V (kivumishi).
Kwa hivyo KN = N+V
b) ‘analima shamba’.
Hiki ni kirai kitenzi (KT) chenye kuundwa na kitenzi (T) na kirai nomino
(KN). Kwa hivyo KT =T+KN
Aina za Virai na sifa ya kila moja
a) Kirai Nomino
b) Kirai Tenzi
c) Kirai Vumishi
d) Kirai Elezi
e) Kirai Husishi
f) Kirai Unganishi
Muundo wa Vishazi na Sentensi
Kishazi ni kikundi cha maneno kilicho ndani ya sentensi chenye muundo wa kiima na kiarifu. Kishazi kina muundo sawa na sentensi.
Aina za vishazi na miundo yake
a) Vishazi ambatani
b) Vishazi tegemezi
Sentensi na Miundo yake
Sentensi ni kikundi cha maneno chenye maana iliyo kamili. Sentensi ndicho kipashio lugha cha kimuundo ambacho ni kikubwa kuliko vipashio vingine.
Vipashio vya lugha ni pamoja na: mofimu, neno, kirai, kishazi na sentensi yenyewe. Sentensi na kishazi huundwa na virai vikuu viwili: KN na KT. KT yaweza kuundwa na kitenzi na nomino, kitenzi na kielezi n.k.
Kwa hivyo S=KN + KT
Sentensi na upatanishi wa kisarufi
SARUFI GEUZA UMBO ZALISHI
Maana:
Nadharia geuza umbo zalishi huonyesha ujuzi alionao mzungumzaji ambaohumwezesha kutunga sentensi sahihi na zisizo na kikomo. Uwezo wa mzungumzaji kutunga sentensi zisizo na ukomo unatokana na kufahamu kanuni za kutunga sentensi sahihi ambazo mzawa wa lugha anazijua kutokana na kuwa na umilisi na lugha yake. Kanuni za kutunga sentensi sahihi hubainisha sentensi sahihi na zisizo sahihi.
Kwa mujibu wa nadharia hii, sentensi ina umbo la nje ambalo ndilo linalojitokeza katika usemaji na hata inapoandikwa, na umbo la ndani ambalo huwa limefichika na hujidhihirisha katika umbo jingine wakati wa kuongea (maana).
Nadharia hii imeweza kuonyesha uhusiano wa tungo ambazo japo zilikuwa na umbo la nje tofauti, zina umbo la ndani sawa.
Kwa mfano:
a) Juma anacheza mpira
b) Mpira unachezwa na Juma
Mfanano wa tungo hizi umekitwa katika maana. Japokuwa sentensi a) inaanza na Juma, na ile b) inaanza na Mpira, mtenda na mtendwa katika sentensi zote ni yule yule.
Mchakato wa kubadili umbo la nje la sentensi a) na kuwa b) umesababishauchopekaji wa kiunganishi ‘na’ na kiambishi tendwa ‘w’ katika kitenzi ‘cheza’.Kanuni geuzi tendwa ndiyo iliyotumika kuingiza mabadiliko haya.
Sentensi yaweza kubadilishwa kutoka umbo moja hadi jingine
Kwa mfano:
c) John anafanya mtihani na Maria anafanya mtihani
d) John na Maria wanafanya mtihani
Umbo la nje la tungo hizi ni tofauti lakini umbo la ndani ni sawa. Tungo d)
imedondosha baadhi ya maneno yaliyo katika c).
Kanuni ya udondoshaji imetumika kudondosha ‘anafanya mtihani’ ambayo
imerudiwa katika sentensi c).
Kanuni ya kubadilishana viambishi idadi imetumika kubadili idadi ya mtenda kutoka umoja ‘a- ya ‘anafanya’ iliyotumika kwa John na Maria kila mmoja peke yake, na kuingiza kiambishi cha wingi: ‘wa- ya ‘wanafanya’
SARUFI MIUNDO VIRAI ZALISHI
Katika sarufi miundo virai zalishi muundo wa sentensi huelezwa kwa kuchanganua vijenzi vyake ambavyo ni viambajengo. Viambajengo hivi huchanganuliwa hadi kufikia neno moja ambalo hubainishwa kwa kategoria yake ya kisarufi. Uchanganuzi huu wa sentensi huelezwa kwa kanuni ambazo huwezesha kutunga sentensi nyingi zaidi.
Kanuni za muundo virai.
a) KN = N --- mtoto
Hii ina maana kuwa KN ina N (yaani Kirai Nomino kina kiambajengo kimoja
tu ambacho ni nomino). Hii yaweza pia kuelezwa hivi:
KN
N
Mtoto
Hii ina maana kuwa kirai hiki ni neno moja. ‘mtoto’
Kirai chenye viambajengo zaidi kimoja, yaani chenye maneno zaidi ya moja
huelezwa kwa kanuni:
KN =N +V au
Mtoto mzuri
Hii ina maana kuwa KN kinaundwa na maneno mawili, yaani ‘mtoto mzuri’
Vivyo hivyo kwa Kirai kitenzi (KT)
b) KT = T anakula
Hapa tunaona kuwa KT ina T yaani ina kiambajengo kimoja tu ‘anakula’. Hii
inaweza kuelezwa kwa njia ya matawi pia.
Iwapo KT ina viambajengo viwili, muundo wake huelezwa hivi:
KT =T +KN. Muundo huu unaelezeka pia kwa njia ya matawi hivi:
KT
T KN
N
anakula chakula
Vivyo hivyo kwa:
c) KV =V au KV =V +E,
KV
V E
mdogo sana
d) KE = E au KE =E +E
KE= E+ E
polepole mno
e) KH=H au KH =H +KN
KANUNI ZA MSINGI ZA MIUNDO VIRAI
Kanuni za miundo virai hujidhihirisha katika sentensi. Sentensi ifuatayo
huchanganuliwa kwa kuzingatia kanuni za miundo virai.
Dada amepika chakula kingi sana
1. S -----------KN +KT
2. KN --------- N +V
3. KT --------- T+ KN +KE
4. KE --------- E
5. T ----------- pika
6. N ----------- dada, chakula
7. V ----------- kingi
8. E ----------- sana
9. H ----------- kwa
MWISHO