MWENGE 7 VITA KATI YA WANGONI NA WANDENDEULE NA HISTORIA FUPI KATI YA WANDENDEULE NA WANGONI WA AINA YA ZULU GAMA NA MBONANE TAWETE
UTANGULIZI
Kabla ya kujua habari ya vita kati ya Wangoni na Wandendeule yafaa tujue kwanza historia fupi juu ya kabila la Wandendeule ambao walikuwa ni wenyeji wa nchi ya ungoni ya leo, pia tujue historia fupi ya kabila la Wangoni aina ya Kizulu na Mbonane ambao walitokea Afrika ya Kusini wakishinda vita na kufanikiwa kulinda kabila lao hadi walipofika nchi ya Tanganyika na kutawala sehemu ya Kusini.
Kabla ya kujua habari ya vita kati ya Wangoni na Wandendeule yafaa tujue kwanza historia fupi juu ya kabila la Wandendeule ambao walikuwa ni wenyeji wa nchi ya ungoni ya leo, pia tujue historia fupi ya kabila la Wangoni aina ya Kizulu na Mbonane ambao walitokea Afrika ya Kusini wakishinda vita na kufanikiwa kulinda kabila lao hadi walipofika nchi ya Tanganyika na kutawala sehemu ya Kusini.
Kuna habari zinaeleza kwamba Wangoni wa aina ya Mputa Maseko ambao walifaulu kukanyaga nchi ya Tanganyika na kufika sehemu iliyoitwa “Mgongoma” karibu na Hanga huko Ungoni inasemwa na wazee wengi wa Kingoni kuwa Mputa Maseko licha ya kuwa shujaa wa vita vile vile alikuwa na tabia ya wivu, ukatili na hata uuaji kwa Wangoni wa kabila la Kizulu na Mbonane.
Hata hivyo Wangoni wa aina ya Zulu Gama na Mbonane wakiwa katika ardhi ya upangwa wakisaidiana na watu wengine katika vita kali walifaulu kumfukuza kabisa Mputa Maseko na kumwua na kuyaondoa majeshi yake katika ardhi ya Afrika Mashariki.
Vile vile kikosi cha mashujaa cha Wangoni wa aina ya Zulu Gama na Mbonane Tawete kimewahi kuwashinda Wandendeule katika vita kali na kulipata eneo la ungoni ya leo.
WANDENDEULE
Wandendeule ni kabila linalopatikana sehemu ya Mashariki ya Kaskazini mwa Wilaya ya Songea. Kadiri ya mapokeo yao wazee waliokuwa na koo tofauti katika kabila hilo wanasema zamani kabla ya kuja Wangoni na Kuishi nchini ya Ungoni, Wangoni wengi walienea zaidi upande wa Magharibi mwa nchi kuliko ilivyo sasa.
Ukweli huo unaonekana zaidi hasa pale majina ya milima na mito mingi upande wa Mashariki ya Kaskazini ni ya kabila la Kindendeule dalili zinazoonyesha kuwa nchi ya Ungoni ya leo ilikuwa na wenyeji wa asili yaani “Wandendeule”.
Kusini mwa misioni iitwayo Mpitimbi kati ya Songea na Peramiho kuna mito inayojulikana kwa jina la “Masimahuhu”. Mito yote miwili inapita nchi ya Ungoni.
Majina ya mito hiyo yanatokana na majina ya kabila la Kindendeule ambalo liliishi wakati huo kabla ya ujio wa Wangoni.
Maana ya neno “Masimahuhu” ni maji meupe au maji yenye rangi nyeupe kwa kingoni cha sasa neno hilo linajulikana kwa jina la “Manjigamsopi”
Isitoshe karibu na misioni iitwayo Mpitimbi kwa sasa nchini inakaliwa na Wangoni wengi, huko nako kuna mlima unaoitwa “Nanyimbo” –Nyimbo ni jina la ukoo mmojawapo katika kabila la Kindendeule.
Hapo jina la mlima huo linatoa ushahidi wa kutosha kuwa huko nyuma kabla ya ujio wa Wangoni, kuzunguka mlima wote, mahali hapo palikuwa na wenyeji wa kabila la “Kindemdeule”.
Vile vile kuhusu milima ya “Humbaro” ambayo ipo kati ya Kusini mwa Misioni ya Mpitimbi. Humbaro pia ni jina la ukoo katika kabila la Wandendeule.
Kutokana na hayo yote inaonyesha kabila hilo lililoishi nchi ya Ungoni kabla ya ujio wa Wangoni.
Baadaye Wandendeule walijigawa katika makabila mbali mbali kulingana na mahali walipoishi kama vile mlimani au maeneo ya mito mikubwa, mfano watu wanaoitwa kabila la “Wakihungu” hutokana na mlima “Kihungu” au watu wa kabila la “Walukimwa” hutokana mto “Lukimwa”
Jina la Wandendeule kwa asili lilifika baadaye na lililetwa na majirani zao kwa kuwa wakati wa mazungumzo yao ya kawaida Wandendeule wanapenda sana kutumia msemo unaoitwa “Ndendeuli” ukiwa na maana ya “nifanyeje?” vile vile inaelezwa kwamba Wamatengo na Wandendeule walikuwa wakiongea lugha moja na inazaniwa kuwa ni kabila moja lakini kuingia kwa Wangoni ilipelekea makabila hayo kutengana. Tutazame baadhi ya maneno yanayofanana ili kudhihirisha jambo hilo:
Neno Kindendeule Kimatengo
Mwanaume Mnarume Mnarume
Wanaume akanarume akanarume
Mwanamke muikeji Mbumba
Kaka Mnongo ndogo
Kaka (Uwingi) akalongo akalongo, alongo
Kuna maneno mengi katika lugha ya Kindendeule ambayo yanafanana na Kimatengo na inaonyesha kuwa kabla ya kuja kwa Wangoni lugha hiyo ilikuwa moja.
WANGONI WA ZULU GAMA NA MBONANE TAWETE
Zulu Gama bin Njeru kwa asili alikuwa Nduna wa Nkosi aliyeitwa “ Zwangendaba” walikuja wote toka Afrika Kusini.
Inaonesha kuna uhusiano wa karibu kati ya watu wa Zulu Gama na wale wa Zwangendaba na wana majina mengi upande wa watu wao yanayofanana na pengine kupatana katika asili.
Mfano mtu anayeitwa “Mafu” alikuwa ni mjomba wa Zwangendaba na “Mafu” Mwingine alikuwa ni babu yake Zulu Gama.
Mharule Jere alikuwa ni ndugu ya Zwangendaba na Mharule Gama alikuwa mtoto wa Zulu Gama”
Wangoni wa aina ya Kizulu waliunganisha na kujulikana kama Wangoni na Zwangendaba, hao waswazi, Wthonga, Wakalanga, Wasenga, Wasukuma.
Makabila hayo yalilazimika kusafiri kutoka Afrika ya Kusini na kuja huku Afrika ya Mashariki.
Wangoni wa Zulu Gama wanakumbukwa kwa ushujaa wao katika vita mbali mbali, kuvuka mito mikubwa kama Zambezi na kusafiri kwa muda mrefu kwa kipindi cha miaka 1835.
Ukoo wa akina Zulu Gama uliongozwa na shujaa aliyefahamika kwa jina la “Njeru”. Kila Mngoni anayeijua vizuri historia ya Wangoni lazima ana kumbukumbu na jina la Zwangendaba pamoja na Mpezani.
Mtu aitwaye Mbonane Tawete alikuwa rafiki wa karibu sana na Zulu Gama wote wawili walikuja Tanganyika. Ukoo wake Mbonane Tawete ni Mbonane bin Mshopi bin Kibovu bin Kisara.
Kadiri ya masimulizi ya Nkosi Dominikus Mbonane ni kuwa huko nyuma Wahenga wake walikuwa ni wa ukoo wa Kifalme katika Nchi ya Swaziland.
Kisara na Kibovu walikufa huko Swanziland. Mshopi aliingia Afrika Mashariki akitokea Afrika ya Kati.
Lakini kabla ya kuingia Tanganyika amewahi kuishi Magharibi ya ziwa Nyasa mara tu baada ya kifo cha Zwangendaba.
Aliwakuta Wangoni naye amewahi kuishi Magharibi mwa ziwa Nyasa, alipojiunga na Wangoni wa Zulu Gama alifanya urafiki na Zulu Gama na kumpa dada yake kama mke wake aliyefahamika kwa jina la “Ushambazi” au Mafunasi.
Kwa vile mke huyo aliolewa katika nyumba ya Chifu Mkuu (Wanawake wa namna hii kwa kawaida waliitwa Nasere).
Kadiri ya Young, Zulu Gama alipoteza wake zake wote kwenye vita.
Lakini mpaka alipoingia Tanganyika alikuwa na mke mmoja dada yake Mbonane aliyefahamika kwa jina la “Mafunasi”.
Ili kujipatia wanawake wengi, mateka wanawake aliowateka katika vita aliwaacha wakiwa hai tofauti na mateka wa kiume ili wawe wake zake.
VITA KATI YA WANGONI DHIDI YA WANDENDEULE
(A) vita ya Wandendeule na Makabila Mengine
Waandishi wa habari za Wangoni wanasimulia Wangoni aina ya Mputa Maseko walifukuzwa kutoka Afrika ya Mashariki, pia Wangoni wa aina ya Zulu Gama walitawaliwa na Mbonane na kuhamia Upangwa.
Makabila mengine mashuhuri ambayo zamani yalitawaliwa na Mputa Maseko yalikuwa na uhuru sana kiasi cha kuweza kujitawala yenyewe.
Hata hivi inasemwa makabila hayo hayakuweza kufurahia uhuru huo waliokuwa nao kwa kipindi kirefu.
Kabila la Wandendeule ambalo kwa wakati huo lilionekana lenye nguvu na pia hali ya kutawala makabila mengine yaliyoishi nyakati nyingine kabla ya kuingia Wangoni na baada ya kuingia.
Kabila la Wandendeule lilikuwa na idadi kubwa ya watu, ufundi katika vita kiasi kwamba liliyalazimisha makabila mengine kubadilisha majina ya koo zao na kutumia ya kindendeule hali ambayo ilipelekea kuingia katika vita dhidi yao.
Wandendeule walikuwa wakitumia Bunduki aina ya Migobore, makabila mengine yakazidiwa nguvu kwa kupoteza watu wengi pamoja na mali zao ikiwemo mifugo, vyakula n.k.
Makabila hayo yalipeleka ujumbe kwa kabila la Kingoni aina ya Zulu Gama na Mbonane Tawete huko Upangwa ili kuomba msaada wa kuwashinda Wandendeule.
Baada ya tafakari ya kina Wangoni wa aina ya Wazulu na Mbonane kutoka Upangwa waliingia katika vita dhidi ya Wandendeule ili kutoa msaada kwa makabila mengine ambayo yalikung’utwa na Wandendeule, sababu kabila la Wandendeule linapakana na Wangoni hivyo ni majirani zao.
Wangoni kwa kuwa wanapenda sana utawala walisahau ujirani na kuingia katika vita ambapo walisafisha majeshi yote ya Wandendeule na kuhakikisha makabila jirani yanazunguka eneo la Undendeule.
(b) Vita ya Wangoni na Wandendeule na makabila mengine
Kabila la Kingoni aina ya Kizulu lililotawaliwa na Mbonane liliingia Ungoni likitokea Upangwa lilifanya vita na kabila la Wandendeule kwa vile nchi ya Undendeule hapo awali ilitawaliwa na Mputa Maseko kwa Wangoni hao ilikuwa rahisi sana kuwashinda Wandendeule.
Wandendeule wengine walijaribu kutoroka na kwenda kuishi juu ya vilele vya milima mirefu ili kujiepusha kwa muda na ghasia ya vita hiyo.
Kwa muda mrefu walifaulu kuishi huko milimani mpaka mazingira yaliporuhusu na kujisalimisha kwa jeshi la Wangoni.
Milima iitwayo Ngorowora na mlima Lupagaro uliopo karibu na Songea Wandendeule walijilinda kwa kipindi cha siku saba huku wakiviringisha mawe kwa lengo la kuliangamiza jeshi la Wangoni zoezi ambalo liligonga mwamba na mwishowe walijisalimisha mikononi mwa jeshi la Wangoni na kati yao wapo waliouawa na wengine kufungwa.
Kundi lingine la Wandendeule chini ya “Namkumula” walifanikiwa kutoroka na kujificha katika mlima Mtungwe karibu na Tunduru nao walipigana na Wangoni toka mlimani, wengine walitorokea Kilwa, Rufiji, lakini baadaye walirudi nchi yao na kusalimu amri kwa Wangoni.
Viongozi wa Wandendeule katika vita dhidi ya Wangoni walikuwa Mpinyawandu, Likunguyayi, Nambilena na Namkumula.
Wangoni baada ya kuwashinda “Wandendeule” baadaye Wangoni wa aina ya Zulu Mbonane waliishi katika nchi ya Ungoni ya sasa kwa kudumu na hivi kustawisha utawala wao kwa makabila yaliyokuwa chini yao yaliyoishi wakati huo.
UTAWALA WA WANGONI BAADA YA KIFO CHA MPUTA MASEKO
Baada ya kifo cha “Mputa Maseko” mtu aitwaye “ Hawaya” na Chipeta waliaminika sana na Wangoni (wakiwemo wazee). Watu hao wawili walikuwa na imani ya kuamini uongozi wa kabila la Kingoni yaani kabila lao.
Baada ya ushindi wa kutwaa nchi kutoka kwa Wandendeule, Wangoni waligawanyika katika makundi mawili; Chipeta alijenga makao yake huko Seluka kando kando ya bonde la mto Hanga na baadaye alibadilisha makao yake na akaenda kuishi kaskazini mwa mto Mtukano.
Hawaya naye alihamia kusini akiwa na watu wake katika sehemu iliyojulikana kwa jina la Ngalanga kati ya mto Lumecha na Mto Luhira Kaskazini mwa milima iliyoitwa Lupagaro.
Hanga ilikuwa ni kama mpaka kati ya Wangoni wa aina ya Kizulu na Mbonane, jambo hilo halina uhakika sana wala uthibitisho wowote kwani kipindi hicho Wangoni walikuwa chini ya utawala wao na waliishi katika vikundi vilivyokuwa sawa na mji.
Kwa kipindi hicho Hanga haikukaliwa na watu.
WANGONI WA AINA YA MBONANE NA ZULU NA VITA DHIDI YA MAKABILA JIRANI
Watu wa Hawaya waliishi karibu na Mahali pale palipoitwa “Ngalanga”. Na watu wote wa “Chipeta” waliishi mahala palipoitwa “Seluka” na baadaye “Mtukano” hakuna mtu aliyeweza kuishi sehemu nyingine tofauti na sehemu hizo mbili tu.
Kutoka makao hayo mapya Wangoni hao wawili walifanywa kuwa machifu. Mara nyingi walifanya mashambulizi kwa makabila mengine sehemu zote walizokutana .
Wangoni wa aina ya Mbonane walikuwa na kawaida ya kuzishambulia nchi na kusambaa na kuelekea Mashariki, Kaskazini Magharibi mwa nchi yao.
Nchi kama Kilwa, Utete, Mahenge, Njombe na Uhehe zilishambuliwa. Wakati wale wa Kizulu walitawala na kufanya mashambulizi kusini, pia Magharibi yaani Tunduru, Lindi, Mikindani, Nchi ya Ulanga, Umatengo, Nyasa, Upangwa na Usokile.
Maelezo ya Livingstone yanasema mashambulizi hayo yalifanyika mwaka 1866 kipindi ambacho mtawala wa Wangoni alikuwa Hawaya, yeye alishuhudia kwa macho yake mauaji ya wangoni dhidi ya Makabila mengine yaliyofanywa na Askari wa “Hawaya” watu wengi waliuawa, huku wengine wakifanywa kuwa watumwa lakini wachache walifanikiwa kutoroka na kuishi ugenini kwa hofu ya Wangoni.
Mwaka 1860 Mjerumani V.D. Decken alipita huko Tunduru nchi iliyoko Mashariki ya Ungoni ya leo, alieleza kwamba Tunduru walifurika watu wengi sana walioishi ambao walikuwa wakiishi katika maeneo mengine kipindi hicho.
Wakati wa utawala wa wajeruani na waingereza, Tunduru ilikaliwa na wageni wengi ambao walihama kutoka Koloni la Wareno (toka Msumbiji)