‘Babu Alipofufuka’, riwaya inayoakisi uhalisia
Riwaya ya ‘Babu Alipofufuka’ imeandikwa na mwandishi maarufu wa kazi za fasihi na mtaalamu wa lugha ya Kiswahili, Profesa Said Ahmed Mohammed, na kuchapishwa na Jomo Kenyatta Foundation mwaka 2001. Katika gamba lake la mbele, pameandikwa: “pengine ni riwaya ya ujasiri mno kupita zote Said A. Mohammed alizowaji kuandika.” Na hivyo hasa ndivyo ilivyo – hii ni riwaya ya kijasiri, ya kimapinduzi.
Hii ni riwaya iliyoandikwa kwa mtindo wa kejeli, lakini yenye mchomo mkali kwa wale wanaoelekezewa kejeli hiyo – yaani watawala waovu – na pia inayoibua hisia nzito kwa wale wanaoathirika na uovu wa watawala – yaani raia wa kawaida.
Uovu wenyewe unadhihirishwa katika riwaya hii kwa namna ya tashnina na inda, lakini katika hali inayowiana sana na ukweli halisi uliomo katika maisha ya kila siku kwenye mataifa yetu ya dunia inayoambiwa inaendelea. Hadithi nzima inasimuliwa kupitia mazingira yasiyo ya kawaida. Huyo Babu mwenyewe Aliyefufuka anatujia kwa umbo la ajabuajabu kupitia kichwani mwa mjukuu wake, K, ambaye ndiye muhusika mkuu. K mwenyewe ni sehemu ya hao watawala ambao kwao kijembe cha riwaya nzima kinaelekezwa. Kwa ustadi wa hali ya juu, mwandishi anampa Babu nguvu za kuziunganisha dunia zetu mbili – baina ya ile tuionayo kwa macho ya nje na ile ionekanayo kwa jicho la ndani tu.
Baina ya dunia hizi mbili, ndipo msomaji anapopewa taswira halisi ya tafauti za waziwazi na za kificho walizonazo wanaoishi ndani yao. Upande mmoja ni maisha ya starehe na anasa za watawala, kule kujilabu na kujitapa kwao, ule uroho na tamaa zao zisizokwisha. Upande wa pili ni maisha magumu ya watawaliwa, kule kutumai na kutamauka kwako, kule kuinuka na kuanguka kwao, na kule kupambana na kujipapatuwa kwao kutoka makucha ya “wenye dunia yao”.
Katika ukurasa wa 14 hadi 15, kwa mfano, tunakutaka na maelezo kuhusu K ambayo yanawasilisha hisia zake za kuutaka na kuupenda ufakhari kama ilivyo kawaida ya watawala wa aina yake:
“Mbali na gari, kulikuwa pia na kasri la kuonewa fahari. Na fahari ndiyo madhumuni yenyewe. Na kasri lake K linamstahiki kwa kila hali, kwa kile cheo cha kiungo. Kama chumvi na chakula alikuwa. Bila ya yeye, mengi ya wakubwa na wadogo hayachapuki… Mjengo wa kasri lake ni wa aina ya zile husuni za tasnifa tunazoziona kwenye snema za filamu za sayansi ya kubuni.”
Wakati akina K wakiishi maisha hayo ya ukwasi na kujitanua, akina Kali ndio muhanga wa anasa hizo za watawala. Kwao maisha ni msegemnege na hali zao ni ngumu kupindukia. Huko ndiko kwenye ‘maitikwenenda’ kama wanavyoitwa na mwandishi na walivyowahi kuitwa na Sembene Ousmane kwenye God’s Bits of Wood au Ayi Kwei Armah kwenye The Beautiful Ones Are Not Yet Born.
Katika ukurasa wa 115 hadi 116, kwa mfano, tunasimuliwa maisha ya watu kula togonya na mboga ya kikwayakwaya sio kwa kupenda, bali kwa kuwa hawana namna nyengine. Huku ndiko ambako mtu anakwenda hospitalini kusaka matibabu, lakini anaondoka akiwa ameongezwa maradhi mengine zaidi kwa kuwa serikali imezitelekeza zahanati zake:
“Walipofika zahanati, mlango ulikuwa wazi, lakini mwuguzi aliyekuwa zamuni hayupo. Ilichukuwa saa nzima mpaka alipopatikana. Alikuwa kenda kumpiga mtu sindano kwa pesa. Alipofika alimkagua Kali, alisema anahitajia wembe wa kumnyoa nywele. Kisha uzi wa kushonea anao lakini anahitajia sindano au shazia ambayo hanayo. Alisema japo ya kushonea nguo inafaa. Zaidi ya hayo hana vidonge vya kuondolea maumivu. Plasta pia hakuna… Kali akanyolewa bila maji, akashonwa bila ya sindano ya ganzi, akatiwa plasta na kupewa vidonge viwili vya asprini kubwia…. alipoondoka, juso na jichwa lake zima lilikuwa limemvimba.” (Uk. 121-22)
Huko kunaitwa Kataa na K anaamini kisa cha kuitwa hivyo ni kwa kuwa watu wa huko ni wakaidi na hawakubaliani hata kidogo na watawala wao. Ndiko hasa alikotokea K, lakini ambako mwenyewe amekutupa na kukusahau kwa miaka yote hiyo. Kwa ujumla, hali ya maisha ya watu wa huko ni duni sana, nyumba zao ni dhaifu na hawana pesa za kununulia hata mahitaji ya lazima:
“Mbele zaidi waliposonga wakipasua kiini cha miti na mimea iliyokuwa mali kubwa hapo zamani, maisha na uhali yalianza kujiliza. Vibanda viwili vilivyolalia yombo. Kitambo,,, vibanda vyengine vitano vikirukuu. Hatua… vibanda vyengine vikisujudu…. ghafla walitokeza mahala ambapo ungeweza kupapagaza jina la sokoni. Watu walionekana… wamesogelea chanja zilizowekwa biashara… wote wametumbua macho, bila ya kuweza kununua chochote. Wengine wanavitumbulia macho vidaka vya nazi. Wengine vichungwa, vilimau, viembe na vipapai… kwenye soko la samaki, mafungu ya dangaauronga na dagaaupapa yakishindana kutumbuliana macho na watu…” (Uk. 95)
Kwa hivyo, riwaya ya Babu Alipofufuka ni kielelezo cha usimulizi unaoakisi uhalisia wa dunia mbili zinazoishi ndani ya jamii moja kwenye mataifa yetu. Mwandishi anampa Babu nguvu za kumfanya mjukuu wake, muhusika mkuu K, azidurusu dunia hizo ambazo kwa kila hali zimekuwa sehemu yake – moja aliyotokea na akaikimbia na kuitelekeza na nyengine aliyokimbilia, kuipenda na kuitukuza. Babu yake alipofufuka na kumjia kwenye maisha yake ya ndani, ndipo anatoa wasaa kwa msomaji kuyaona yaliyomo kwenye nafsi za madhalimu na madhulumu na zinavyosawirika dunia zao.
Baada ya kuziona dunia hizo, mwandishi anamfanya msomaji wake ahitimishe kwa mambo matatu haya:
Kwanza, watu wa aina ya K, ambao wameendeleza dhuluma kubwa kwa kutumia vyeo na majina yao, huwa wanaishi na khofu ya milele ya kuporomoka. Matokeo yake, kila siku hutamani na kupigania kwenda juu na juu zaidi kusudi wasifikwe na walio chini, ambao wanadhani kuwa endapo mikono yao itawafikia tu, basi watawashika miguu na shingo zao na kuwaporomosha chini kwa kishindo kikubwa. Kwa hivyo, ishara yoyote ya kuporomoshwa huwatia jaka moyo kubwa na kuwatetemesha hadi machango. Katika ukurasa wa 92, mathalan, mwandishi anatuonesha namna K anavyogwaya akiliogopa anguko lake:
“Ghafla alijihisi anachukuliwa na lepe jengine lililomdidimiza katka singizi zito la ajabu. Alitumbukia kwenye singizi huku akienda. Lilikuja tu kwa hakika hilo singizi ama upepo wa ghafla. Lilikuja kumvaa na kumdidimiza kwenye maweko ya chini ya kiini cha dunia. Alihisi anazama kwenye dimbwi refu lisilo ukomo… di, di, di… alididimia mpaka akajihisi ameibuka pahala penye mwangaza wa maisha. Akajihisi kama katupwa hapo. Katupwa kama gunia. Moyo ukaanza kupiga beni alipogundua hivyo. Aa, kubwagwa kila siku yeye alikuwa akikuogopa. Kuanguka alikuchelea. Akihofu kutupwa, hasa namna hiyo.”
Pili, msomaji anahitimisha kuwa watawala wa aina ya K wanakuwa wanajijuwa hasa kwamba wamewakosea raia. Kwa hivyo, kila wanapokaa huwa wanajitia wasiwasi kuwa wanaandamwa au wanafuatwafuatwa na watu hao wenye hasira na wakati wowote wanaweza kulipiziwa kisasi kwa maovu yao. Hayo ndiyo matokeo ya kuishi kwa dhuluma. Siku zote huwa unakhofu kuwa madhulumu wako watakurudi kwa yale uliyowatenda. Huwa huko huru. Angalia vile wanavyopita barabarani kwenye magari yaliyofungwa vioo vyote, tena vyeusi visivyopenya risasi na bado mbele yao ving’ora mita kadhaa ili wapishwe njia peke yao na bado maaskari kibao na bunduki. Hawa hawafanyi yale kwa kupenda, bali kutokana na khofu waliyonayo kwa umma walioukosea (Uk.24-7). Wakati Babu anamzukia K kwa mara ya kwanza kwenye ndoto-macho zake, alijitambulisha kwa namna hii:
“Nikwambie tena, mimi ni babu yako; kisha niongeze kuwa mimi ni dhahiri kwa kisia kikubwa kuliko hata wewe, kwa sababu sina farakano na watu. Wala sina makiwa na utawa kama ulionao wewe. Sina hofu wala siogopi kama uogopavyo wewe. Nakwenda nipendapo. Nakutana na nimpendaye. Ufunguo wa kasi yangu ninao mwenyewe. Hakuna niliyemdhulumu.” (Uk. 21-2)
Tatu, msomaji anahitimisha kuwa khofu hizi za watawala zina uhalali wake na ni za kweli. Ni kweli kuwa wananchi walioonewa na kudhulumiwa kwa miaka mingi hufika pahala pa kusema “hapana” kwa watawala wao. Miongoni mwao huwa wanasema hivyo kwa maneno, wengine kwa vitendo, wengine wakiwa na akili zao na wengine tayari wameshachanganyikiwa kwa mateso ya muda mrefu. La muhimu ni kuwa wananchi hufika mahala wakasema “liwalo na liwe” lakini hawatakubali tena dhuluma nyengine dhidi yao. Katika ukurasa wa 92, K alimkuta Mussa katika eneo la Kataa akijisemea peke yake njiani:
“La, hatutaki, hata ikiwaje hatutali tena…. La, hatutaki, hata iwaje hatutali tena…. La, hatutaki, hata ikawaje, hatutali tena..”
Lakini madhulumu wengine huamua kwenda mbali zaidi ya kupita mitaani wakijisemea peke yao tu. Wao huamua kuwarudi madhalimu wao kwa namna yoyote ile wanayoiona inawafalia na wanaimudu. Mno yachosha eti! Na ni hiki ndicho ambacho kinadhihirika mwishoni, pale umma uliokwishachoshwa na udhalimu wa watawala wao, unapoingia barabarani na kuukabili mkono wa utawala.
“Nje aliwakuta wale mahasimu zake wamejipanga upande huu na huu wa njia. Sasa walikuwa mamia kwa mamia… Kuna waliochukuwa marungu na wengine mabango yaliyoandikwa maneno mengi…M’MEZIFISIDI NAFSI ZETU…. MMEVUNJA HESHIMA ZETU…. VIJANA WETU WANAPOTEA… VIFO NA NJAA NA MARADHI SABABU SI SISI… HATUNA NAFASI PANAPOSTAHIKI NAFASI ZETU… ARDHI INACHUKULIWA HIVI HIVI TUNAONA…. KESHO YETU IMO KATIKA GIZA…TUNAANGAMIA…TUMESHAKWENDA KAPA…na zaidi na zaidi…Mlio ule wa bunduki K aliusikia ndani apokuwa tayari ameshakua kitini ofisini mwake. Alitetemeka kwa muda. Lakini alipojishika, aligunduwa kwamba hata ofisini mambo yalikuwa yamegeuka pia.” (Uk. 154-56)
Riwaya inamalizika kwa kumuonesha K akipoteza kila kitu – ulwa, nyumba, gari na, zaidi kuliko yote, hata ile heshima aliyojidhani alikuwa nayo. Na mwisho anakufa kifo cha kidhalilifu kama alivyosababisha maelfu ya wengine kufa katika udhalilifu kwenye zama za madaraka yake.
“Alfajiri ya siku ya pili, watu wa kijiji kile waliamshwa na sauti ya jibwa kubwa, Biye aliloliita Doggy. Ilikuwa si kawaida jibwa kubwa kama lile kubweka kwa muda mrefu namna ile hapo kijijini. Walipoufuata mbweko wa jibwa, walimkuta K ananing’inia kwenye kigogo cha mti uliokuwa umeota katikati ya kaburi la Babu. Alikuwa mkavu keshang’ang’anaa.” (Uk.165)
Naam, hapa ndipo hasira ya umma ilipomfikisha K. Hapa, kwa hakika, ndipo kiuhalisia wafikishwapo watawala madhalimu wa aina yake. Hivyo ndivyo umma unavyomuhukumu mkosaji wake. Umma ukikosewa kiasi kikubwa kama hiki, ni wenyewe ndio ambao hushitaki, na wenyewe ukahukumu. Na hivi ndivyo Babu Alipofufuka na kumtahadharisha mjukuu wake, K:
“…Pia unashitakiwa na wakati ulioutumia vibaya…Unashitakiwa vile vile na matendo yako mwenyewe…matendo ya upotofu…Maovu yako mwenyewe….Hakuna uchaguzi. Huna njia. Wakati ukifika, utakwenda tu; utakwenda tu…” (Uk. 137