SARUFI ni sayansi ya muundo wa lugha pamoja na sheria au kanuni za matumizi yake ambayo, kwa kawaida, hukubalika kwa watumiaji wake.






Kwa hivyo, sarufi ni taaluma inayojishughulisha na taratibu zinazotawala uchambuzi wa lugha katika vigezo vya umbo-sauti, sarufi maumbo, sarufi miundo na umbo-maana.
Msingi wa kanuni zinazotawala sarufi ya lugha ni uwiano wa kisarufi uliopo baina ya vipashio mbalimbali vinavyounda sentensi.
Katika sarufi ya Kiswahili na lugha nyinginezo za Kibantu, uwiano wa kisarufi unadhihirika pakubwa kupitia ngeli (Kapinga, 1983).
Kulingana na Kapinga, ngeli ndio ‘uti wa mgongo’ wa sarufi ya Kiswahili.
Katika misingi hii basi, kutozingatia mfumo wa ngeli za Kiswahili katika matumizi yake ni sawa na kuvunja uti wa mgongo wa sarufi yake na hivyo kuwa muundo tofauti kabisa na ule wa Kiswahili kilichosarifiwa kwa umufti unaostahili (Wallah, 2015).
Hali hii ya kukiuka sarufi ya Kiswahili inadaiwa kuibua msimbo wa kijamii usio imara kisarufi na unaosikika tu kama Kiswahili (Ngesa, 2002).
Nomino za Kiswahili zisipowakilishwa vilivyo katika ngeli mwafaka, matumizi yake yatachukuliwa kuzalisha msimbo wa Sheng ulio na msamiati mahsusi ambao si imara (Ogechi, 2002:4).
Uwakilisho huu mbaya umechangia pakubwa matumizi mabaya ya baadhi ya majina katika vyombo vya habari.
Matumizi haya mabaya yameenea hata katika shule za upili na vyuo vikuu, hivyo kueneleza kasi ya msambao wa matumizi ya simo ya Sheng (www.len.wikipedia.org/wiki/Sheng/linguistic 22-07-2011).
Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha (TUKI, 1990) inaeleza kuwa ngeli ni kundi moja la majina yaliyo na upatanisho mmoja wa kisarufi unaofanana na viambishi vya umoja na wingi ambavyo ama hufanana au kulingana.
Hivyo ngeli ni kundi la nomino lenye sifa zinazofanana kisarufi katika lugha.
Majina haya yaliyopo katika makundi yanayolingana hubeba viambishi kubalifu vya umoja na wingi katika sentensi za Kiswahili.
Sintaksia ni mojawapo ya matawi ya sarufi. Kila lugha ina sintaksia yake. Neno hili linatokana na neno la Kigiriki “Syntassien” lenye maana ya kupanga au kuweka pamoja.
Asili ya neno hili inarejelea lile tawi la kisarufi linaloshughulikia jinsi maneno, yakiwa na au bila viingizi au vinyambua, hupangwa ili kuonyesha muungano wa maana katika sentensi (Mathews, 1981).
Chomsky (1956) anaeleza kuwa sintaksia ni uchunguzi wa kaida au sharia na njia ambazo sentensi hutungwa katika lugha mahsusi na kuleta maana.
Tallerman (a988) anadhukuru kwamba sintaksia ina maana ya kutunga sentensi; vile makundi ya maneno yalivyowekwa pamoja kuunda vikundi, vishazi au sentensi.
Neno hili pia hutumiwa kuwa na maana ya kutalii sifa za kisintaksia za lugha.
Hujumuisha maneno au kategoria za maneno, mpangilio wa maneno katika virai na sentensi, miundo ya virai na sentensi na aina tofauti za sentensi ambazo zinatumiwa na lugha mbalimbali.
Sintaksia hushughulika na kuchanganya maneno kuwa virai, vishazi na sentensi.
Verma na Krishnaswamy (1989) wanafafanua sintaksia kama sehemu ya sarufi ambayo hujishughulisha na sehemu au mahali, mpango na kazi za maneno au uamilifu wake na vipashio vikubwa katika vishazi, sentensi na usemi.
Tunapotalii muundo na mpangilio wa viambejengo katika sentensi, basi tunatalii sintaksia ya lugha.
Sintaksia ni taaluma ambayo inapambanua ufafanuzi wa vipashio vikubwa zaidi katika lugha ambayo ni sentensi.
Sintaksia huvipa vipashio miundo na fafanuzi zaidi katika sentensi. Hivyo, ni mpangilio wa maneno katika sentensi ambao huleta maana kisarufi kwa ambavyo hupanga kategoria za maneno kisarufi (Yule, 1987).
Kutokana na upungufu wa baadhi ya nomino kutowakilishwa katika ngeli za Kiswahili, ipo haja kwa uanishaji wa ngeli za Kiswahili kisintaksia kuchunguzwa upya.
Uainishaji wa ngeli za Kiswahili umefanywa ama kisemantiki na kimofolojia na wasomi na wataalamu mbalimbali akiwemo Mbaabu (1985). Aidha ni uwanja ambao umewahi kuzamiwa kisintaksia na Kapinga (1983), Gichohi (1999), Wessana-Chomi (2000), Mohamed (2001) na Wallah (2004).
Baada ya uainishaji wa kimofolojia, nomino nyingi zilikosa kuwakilishwa katika mfumo huu wa ngeli.
Hali hii iliwachochea wanaisimu kuchunguza upya uainishaji wa ngeli ambao ni kisintaksia.
Inaaminika kwamba mfumo huu mpya wa uianishaji ulipata kuwakilisha nomino nyingi za Kiswahili.
Hata hivyo, si nomino zote za Kiswahili zinawakilishwa katika ngeli hizi za kisintaksia ambazo zinazisisitiza ujozi wa viambishi katika umoja na wingi wa vitenzi na (au) vivumishi katika sentensi.
Ipo haja kwa wataalamu wa sarufi ya Kiswahili, hususan tawi la sintaksia, kuizamia zaidi uwanja huu kwa misingi ya kuuondoa utata uliopo katika kuwakilisha ngeli kijozi na namna ya uambishaji.
Je, ni kwa vipi ambavyo jozi za ngeli kisintaksia zinapasa kuwakilishwa kwa mujibu wa uambishaji?
Ni A-WA kwa mfano katika nomino hisivu au ni A-, WA-?
Na je, tuziwakilishe vipi nomino “kiu, mikogo, miwani, Mungu, vita, giza, joto na jua” kwa mujbu wa ujozi katika uainishaji wa ngeli kisintaksia?
Powered by Blogger.