Historia ya kabila la WAHEHE...



Image may contain: one or more people
Historia ya kabila la WAHEHE....
Historia ya Wahehe ni pana sana na ina machimbuko tofauti kwa mujibu wa taarifa mbalimbali za kitafiti ambazo tayari zimekwishafanyika. Koo nyingi za Kihehe zipo kutokana na tabia tofauti za kimaisha zilizojumuisha shughuli mbalimbali za kijamii mfano ufugaji, uwindaji, ufuaji chuma, uwezo wa vita na kilimo. Jamii za Koo zilizojishughulisha katika shughuli za namna hii ziliweza kutambulika kirahisi na jamii nyingine.
Kuna asili (chimbuko) mbalimbali za Kabila la Wahehe. Kuna Wahehe wenye asili ya Uhabeshi, Wahehe wenye asili ya Ungazija na pia Wahehe wenye asili ya Wanitole. Kuna taarifa fupi kuhusiana na baadhi ya asili hii, lakini ninaweza kusema kidogo kwa Wahehe wenye asili ya Wangazija huko mbeleni.
Hata majina ya Koo hii yalibeba maana nzima ya historia na aina ya shughuli zinazofanywa na jamii hizo. Kwa mfano Koo za akina Chusi zilikuwa na umaarufu katika shughuli za ufuaji chuma na utengenezaji wa zana zinatokanazo na chuma. Mpaka leo hii, asili ya koo za akina Chusi ni wafuaji na wahunzi wa zana zinazotokana na chuma.
Kuna majina katika koo fulani yalipatikana kutokana na mfululizo wa majanga mbalimbali ya asili mfano vifo. Koo ambazo zilikuwa na bahati mbaya ya kupoteza watoto mara tu wazaliapo ziliweza kujulikana kwa majina fulani kwa wachache ambao waliweza kuepukana na majanga hayo. Kwa mfano Koo za akina Mponela, zinatokana na maana halisi ya neno Kupona kwa kiswahili. Hii ni jamii ya watu wachache ambao waliweza kupona kutoka kwenye janga la vifo.
Koo nyingine zilikuwa ni maarufu katika upiganaji wa vita katika maeneo mbalimbali ndani ya Himaya ya Uhehe na nje ya Himaya Uhehe. Kutokana na umahiri wao katika vita, Koo hizi ziliongozwa na Machifu au Watemi kwa lugha ya Kihehe. Baadhi ya Koo hii ni pamoja na akina Mduda, Kivenule, Mkwavinjika, Mnyigumba, Myinga na Lumaco.
Majina ya Koo hizi ambazo zilijihusisha katika vita mengi yao ni ya sifa kutokana na umahiri wao katika vita. Yawezekana ni katika shabaha, kutumia zana za kivita na pia imani ambayo ilikuwa ni msingi wa mfanikio yao katika vita. Kwa mfano matumizi ya madawa ya asili ambayo yaliongeza hamasa na chachu ya ushiriki katika mapigano vitani. Kwa mfano Ukoo wa KIVENULE, unatokana na neno KUVENULA.
Historia ya Ukoo wa Kivenule inaletwa na mtu mmoja aliyeitwa Tagumtwa Mtengelingoma Balama. Mzee Tagumtwa Balama (KIVENULE) ndiye aliyewazaa Mzee Tavimyenda Kivenule na Mzee Kalasi Kivenule. Ikumbukwe kuwa, jina halisi la ukoo wa Kivenule ni BALAMA. Neno KIVENULE linamaanisha sifa ya kuwa jasiri Vitani na hasa katika kutumia silaha za asili za Mishale na Mikuki yaani kwa Lugha Asilia ya Kihehe “MIGOHA” katika kupambana na adui katika vita za kikabila enzi hizo. Kwa maana hiyo, kwa Kihehe LIGALU ni Vita. Vatavangu walikuwa ni wakuu wa Vita au wapiganaji vitani. Kuhoma maana yake Kumchoma adui kwa sila ya jadi mfano Mkuki, Upinde au Mshale. Migoha maana yake Mikuki. Venula maana yake ua, fyeka maadui.
LIGALU ndiyo iliyochangia kuzaliwa kwa jina la Ukoo la KIVENULE. KIVENULE maana yake ni Ushujaa kutokana na Shabaha ya Mikuki.
KUVENULA lilibeba maana halisi ya uwezo wa kuwa na shabaha ya kuwaangamiza maadui kwa kutumia silaha ya Mishale na Mikuki. Babu yetu TAGUMTWA BALAMA alilidhihirisha hili katika Vita na Watavangu na hivyo kusababisha kuzawadiwa kwa jina la KIVENULE kama jina la sifa kutokana na ushujaa katika Vita.
Baada ya kuwazaa watoto hawa wawili yaani TAVIMYENDA na KALASI, walisafiri na kufika hadi sehemu ya KALENGA, wakiwa katika harakati za kutafuta maisha. Ndipo Babu TAVIMYENDA KIVENULE alipoombwa na Mzee MYINGA aende akamsaidie kumchungia mifugo yake eneo la MAGUBIKE na pia Babu KALASI KIVENULE naye kuamua kwenda eneo la ILOLE kutafuta maisha.
Akiwa eneo la MAGUBIKE, Babu Tavimyenda Kivenule akafanikiwa kupata watoto Saba (7), yaani BABU KAVILIMEMBE KIVENULE, BABU MGAYAFAIDA KIVENULE, BABU SIGATAMBULE KIVENULE, BIBI MGASI KIVENULE, BIBI MALIBORA KIVENULE, BIBI SIGINGULIMEMBE KIVENULE, BABU ABDALAH KIVENULE NA BIBI SIKIMBILAVI SEMABIKI. Huyu Bibi Sikimbilavi Semabiki hakuwa mtoto wa Babu Tavimyenda ila alikuwa ni mtoto wa kufikia kwa Bibi yetu.
Baadhi ya akina Babu walifanikiwa kuwa na wake zaidi ya mmoja na hawa walikuwa ni Babu SIGATAMBULE KIVENULE, ambaye mke wake wa kwanza alikuwa anaitwa SIWANGUMHAVI SINGAILE, mke wake wa pili alikuwa anaitwa NYANYILIMALE SINGAILE na mke wa Tatu, PANGULIMALE SETWANGA. Mke wa pili na tatu wa Babu Sigatambule bado wapo hai.
Babu HUSEIN KIVENULE naye alikuwa na wake wawili ambao ni YIMILENGERESA SEMSISI na DALIKA SETALA. Taarifa za wake wa Babu wengine bado zinaendelea kufanyiwa utafiti. Babu MGAYAFAIDA KIVENULE yeye hakubahatika kuoa wala kuwa na mtoto. Alikuwa ni mlemavu na ndiyo maana ya jina lake MGAYAFAIDA.
Kwa upande wa ILOLE, Babu KALASI KIVENULE alibahatika kuwa na watoto watatu ambao ni Babu SALAMALENGA (KAHENGULA) KIVENULE, MGUBIKILA (NYAKUNGA) KIVENULE NA SEKINYAGA KIVENULE.
BABU SALAMALENGA KIVENULE alikuwa mwanaume peke yake na wawili waliobaki walikuwa ni wanawake. Babu Salamalenga Kivenule alioa wake watatu ambao ni Bibi NYANGALI, BIBI SEMFILINGE MHENGAATOSA NA BIBI SEMKONDA CHOGAVANU. Kupitia kwa wake zake watu, Babu Salamalenga ndiye aliyeeneza Ukoo wa Kivenule katika maeneo ya Nduli, Ilole, Mgongo na Kigonzile.
Admini....
Erick Derick
Powered by Blogger.