HISTORIA YA WALUGURU
HISTORIA YA WALUGURU
KAMA utairejea historia ya Morogoro ya miaka ya kati ya 1870 hadi 1888, kipindi ambacho Sultan wa Zanzibar alikuwa Sayyed Barghash, uitagundua kuwa kwenye safu ya Milima ya Uluguru na pembezoni mwake kulikuwa chini ya Machifu wa makabila tofauti ambayo leo hii yanaitwa “Koo za Kiluguru”.
Makabila na koo zilizokuwepo hadi mwaka 1888 kote Uluguruni yakizungumza lugha inayofanana na kufuata mila zinazorandana ni pamoja na Wabena, Wamwenda, Walelengwe, Wabunga, Wacheti, Wachaga, Wagweno, Wabinga, Wachiru, Wachuma, na Wagonanzi.
Wengine ni Wahafigwa, Wahimba, Wamwingu (Waingu), Wakibago, Wakiflagu (ambao ni wachache sana Uluguruni), Wakinoge, Wakiraru, Wakuruwa, Wakonga, Wakumburu, Wakwama, Walari, Wamanga, Wamasenga, Wamangara, na Wamaze.
Pia walikuwepo Wambiki (Wangode), Wambonde, Wambega (Wakiru), Wanyani (Wanyagatwa), Wamlali, Wamugera, Wamwandike, Wanambo, Wangandi, Wangozi, Wangurumi, Wangweku, Wanyanga, Wanzovu na Waponera.
Halikadhalika walikuwepo Wasikoni, Wasinogi, Watebe, Watemaruge, Watonga, Wanzangazwa, Wazeru, Wazima na Wazongo.
Baadhi ya haya yalikuwa ni makabila, na nyingine ni koo zilizotokana na makabila yaliyokuwepo Uluguruni au nje ya hapo.
Utafiti unaonesha kuwa, zipo baadhi ya koo hazikutokana kabisa na makabila ya kibantu, yaani baadhi zilitokana na na Wafilipino waliyoko Asia kusini, na wengine walitokana na makabila ya kiarabu.
Pia wapo waliotokana na Wazulu waliotoka moja kwa moja Afrika Kusini, au wale waliotangulia kabla kukwepa vita ya Chaka Zulu wakiwemo Wanyasa, Wamanda, Wangoni, Wabena na wengineo ambao majina yao yalibadilika kutokana na maeneo waliyoishi, au matukio waliyokutana nayo.
Wapo pia waliotokana na makabila ya bara ikiwemo Wanyamwezi, na makabila ya kaskazini ikiwemo Kilimanjaro, milima ya Upare, na Unguu na kadhalika.
Makabila au koo zote hizi kwa bahati zilizingumza lugha moja na kufanana kitamaduni japo baadhi ya mila na desturi zao zilitofautiana kutegemea na asili zao.
Ufananaji wa Lugha ulitokana na Lugha ya wenyeji wa mwanzo kutangulia kufika na kuweka maskani katika safu ya milima hii, ambao ni Wamwenda, wengi wao kwa sasa wanapatikana Tarafa ya Mgeta wilaya ya Mvomero, kusini maghalibi ya Milima ya Uluguru.
Hivyo wengine waliofuatia walijitahidi kufahamiana na wenyeji na kulazimika kujifunza lugha na utamaduni wao, japo baadhi ya mambo ya msingi wametofautiana hadi leo.
Lipo swali linaloulizwa nini hasa asili ya neno Luguru, na neno Morogoro, Hilo ni somo la peke yake linalohitaji muda mrefu kulijadili, cha msingi hapa kuzingatia kuwa Uluguru hapo kabla lilikuwa ni eneo na si kabila, isipokuwa wale wote walioishi katika eneo hili na pem,bezoni mwake Wajerumani waliwajumuisha katika kundi moja na kuwaita kuwa Waluguru.
Machifu wa Kiluguru wakati huo walimkubali muwindaji mahiri mwenye asi;li ya Uzigua Bwana Kisebengo kuwa Kingo (Kinga) yao katika uwanda wa chini, na kumruhusu ajenge mji wake.
‘Kingo’ Kisebengo alijenga mji mdogo katika njia ya Kaskazini ya milima ya Uluguru inayounganisha Pwani ya Afrika mashariki na bara, jirani na mji wa sasa wa Morogoro ambao wakati huo ulikuwa msitu.
Machifu wa Kiluguru walikubaliana na Kisebengo kuwatoza ushuru wale wote wanaotumia njia hiyo kwa ajili ya safari zao za kibiashara, kutokana na ukweli kuwa Wananchi wao ndiyo walioijenga, na kuendelea kuilinda na kuitunza njia hiyo muhimu.
Baadhi ya wafanyabiashara walikubali na kulipa, ila wengine waligoma, ingawa hawakuwa na ubavu wa kupambana kivita na Kisebengo wala waandamizi wake wa Kiluguru, hivyo wakahiyari kutumia njia ya kusini, iliyoko baina ya upande wa kusini wa milima ya Uluguru na bonde la mto Rufiji.
Njia hii pia ilielezwa kupitishia watumwa, jambo ambalo linapingwa na machifu wa wakati huo Lukwele wa Choma aliyezaliwa mwaka mwaka 1852 na kufariki mwaka 1971, akizikwa makaburi ya kichangani mjini Morogoro.
Chifu Lukwele ndiyo yule wakati fulani aliyekuwa askari aliyepigana katika jeshi la Mjerumani dhidi ya Waingereza na washirika wao, kwenye maeneo kadhaa ya Mashariki ya Kati (bara Arabu), Afrika Mashariki, Msumbiji, Malawi na hatimaye Namibia, na kurejea nchini baada ya vita ya kwanza ya Dunia kumalizika katika muongo wa pili wa karne ya 20.
Lukwele ambaye jina lake halisi ni Salum Bin Msumi, alikuwa ni mmoja kati ya watoto watatu mashuhuri wa Chifu Msumi wa Kibungo, ambaye asili yake kwa baba na mama ni Mzulu toka Afrika Kusini.
Chifu Msumi rekodi yake ya ndoa na watoto inaonesha kuwa ni mtu wa mitala, na alikuwa na watoto wengi, baadhi wakieleza kuwa ni zaidi ya 30 huko Uluguruni Mkoani Morogoro, Mbambabay Mkoani Ruvuma na jijini Lilongwe nchini Malawi.
Watoto wake mashuhuri ni Lukwele (Salum), Sonanga, na Mleke maarufu Kingalungalu (waluguru wanatamka ‘Chingalungalu' yaani Kigeugeu) au kwa kifupi Kingalu wa kwanza, ikiwa ni jina lake la kupanga kutokana na tabia yake ya Ugeugeu (aliwahi kumgeuka mkwewe chifu magoma, na kisha baba yake mzazi Chifu Msumi na kupigana nao vita kwa nyakati tofauti!); jina hilo likawa jina rasmi la ukoo wake ambao ulielekea zaidi umamani.
Lukwele anakiri nduguye Kingalu wa mwanzo, kuwa ndiyo aliyetajwa sana na Wajerumani na Waingereza kwamba alijihusisha na biashara ya utumwa, japo anashangazwa na hilo kutokana na ukweli kuwa historia ya Uluguru inapingana na madai hayo; kwani Waluguru hawakuwahi kufanya biashara ya utumwa wala wao kukamatwa na kupelekwa utumwani, kutokana na jiografia tata ya eneo lao wakati huo, na miiko ya kabila lao iliyoharamisha Utumwa tangu miaka 1400 iliyopita.
Mwingine anayepinga njia hii kupitishia Watumwa ni Kingo Kisebengo mwenyewe, na hata mfanyabishara maarufu wa wakati huo Muhammad Marjab ‘Tip tip’, ambaye pia alikuwa Gavana wa Sultan wa Zanzibar Mashariki ya Kongo (DRC), na baadae Gavana wa Wabelgiji katika eneo hilo.
Tip tip anasema kwamba, njia hiyo ilipitisha wapagazi na si watumwa, kama propaganda za majasusi wa magharibi zilivyodai, na hasa kumuhusu yeye binafsi.
Waruguru waligoma kabisa njia yao kupitisha biashara yoyote inayokwenda kinyume na miiko ya Kabila lao wakati huo.
Hivyo wafanyabishara wa Utumwa hawakuthubutu kupita eneo hilo, bali walipita njia ya kusini.
Wamishenari, Wavumbuzi na wapelelezi wa mwanzo, waliofanya safari za bara au pwani mara kwa mara, baadhi yao walipita njia hii muhimu katika karne hiyo ya 19.
Mmoja kati ya hao ambaye Historia ya Waluguru imemrekodi na kumkariri sana ni Keith Johnson ambaye alishazungukia eneo la Maasai, na Ziwa Victoria, kisha kupita njia hii akielekea pwani.
Alipoingia katika eneo la Waruguru na Wakutu, Jasusi huyo bobezi akielekea ukanda wa kati na Maziwa makuu mwaka 1879, kwa mara ya kwanza alishangazwa na umbile la ajabu la sehemu ya tao hili la milima ya Mashariki ya Afrika.
Hata kabla ya kusafisha mboni zake za macho kuona madhari asilia ya kuvutia na kuweka historia, roho yake ikaacha mwili, alipofariki eneo la Ukutu mwaka huo, na kuzikwa Behobeho kusini ya Kisaki.
Msaidizi wake mkuu Joseph Thomson wakati huo akiwa ni kijana mbichi asiye na uzowefu mkubwa, akitimu umri wa miaka 23 tu toka kuzaliwa kwake, akabeba mikoba ya mtangulizi wake.
Thomson kama ilivyo kwa mwandamizi wake alivutiwa mno na safu hii ya milima adhimu ya Uluguru kiasi cha kushika kalamu katika moja ya maandiko yake akiweka bayana kuwa; “Uwasili umemwaga utajiri wa maliasili zake, na kuzalisha kila kinachoweza kutuliza moyo na mwili, halkadhalika kuburudisha macho kwenye tao la milima hii”.
Thomson anaweka wazi kwamba, katika njia ya chini hakubahatika kuwaona Waluguru zaidi ya kupata habari zao toka kwa wanajeshi wa kabila la Wambunga, waliojaribu bila mafanikio kuvamia milimani kwa njia ya vita, kupora vyakula kutokana na ‘nchi’ zao kuwa na njaa kali.
Wambunga walimwambia kuwa, Waluguru walikuwa na majeshi imara yaliyojua sana kutumia vita ya upanga na kiasi mishale, hivyo kwa jiografia yao tata ya milimani, na uwezo wao wa kijeshi ilikuwa vigumu sana kuwafikia, japo walijaribu kufanya hivyo baadhi ya nyakati.
Aliambiwa na Wambunga pia kuwa, Waruguru hawakuwa na nguo, bali walivaa majani ya migomba, jambo ambalo baadaye alikuja kufahamu kuwa si la kweli! Rejea: (Kitabu cha Joseph Thomson: ‘To The Central Africa Lakes and Back’ cha mwaka 1881, I, Chapter 5).
Thomson alifahamu baadaye kuwa wanajeshi wa Kiluguru ndiyo waliovaa majani ya migomba na miti mingine kwa ajili ya kujificha dhidi ya adui katika uwanja wa mapigano, ilhali raia wa kawaida walivaa mavazi ya kujistiri kwa wanawake hasa Kaniki, na Marekani kwa mtindo wa kujifunga chini na kujitanda juu.
Na wanaume, pia walivaa kaniki kwa mtindo wa kujifunga kiunoni na juu lubega na pengine kujivika migolole hasa kwenye uwanda wa juu palipokuwa na baridi kali enzi hizo.
Aliwakuta Waluguru wakijali sana mila zao za asili kama vile unyago, ndoa, na kumbukumbu za watangulizi wao (matambiko).
Jasusi mashuhuri Henry Stanley naye alipita njia ya Kaskazini ya Tao la milima ya Mashariki hususan Uluguru, katika safari yake ya kumsaka “mvumbuzi” Dr. Livingstone na kulala katika ‘mji’ wa Simbamweni (mtoto mkubwa wa Kingo kisebengo), uliozungushiwa ukuta na kuwa na ngome isiyopenyeka kiurahisi (ambapo hivi sasa ni nje kidogo ya mji wa Morogoro wakati huo pakiwa msitu mnene na nyumba chache).
Stanley anausifu mji huo mdogo (Morogoro ya mwanzo kabisa) akisema kwamba umejengwa kwa mitindo ya kiarabu chini ya bonde la kijani la milima ya Uluguru, yenye misitu minene inayofunikwa na mawingu wakati wote wa mwaka, linalopambwa na mito miwili mikubwa na utitiri wa mifereji na vijito vya maji safi na salama, mandhari ambayo hajapata kuyaona katika eneo lolote alilowahi kufika katika Afrika Mashariki.
Henry Stanley anakisia kuwa Mji wa Simbamweni (Morogoro ya wakati huo) ukiwa na milango iliyotengenezwa kwa miti ya mitiki isiyozidi minne, yenye umbo la mraba kwenye ngome yake, ikifungwa wakati wote ila kwa hitajio, ulikuwa na wakaazi wasiozidi 3,000.
Anasema kwa mtazamo wake huwenda milango hiyo imara ya kuingilia mjini yenye maandishi ya Kiarabu ilitengenezwa Zanzibar au pwani na kupelekwa Morogoro kwa Simbamweni vipande vipande, kabla ya kuunganishwa (kutokana na ukubwa wake isingeweza kubebeka)!
Anakiri kuwa Morogoro ilibeba utajiri wa ajabu wa maliasili, Mazingira, maji na rasilimali watu, pamoja na ustaarabu wa hali ya juu, ambao hajapata kuuona ila katika nchi zilizoendelea wakati huo.
Anamalizia kuweka wazi kuwa, iwapo hali itakuwa hivyo, basi Morogoro katika muda mfupi wa miaka itakua ni Taifa lenye maendeleo makubwa ya nyanja zote. Rejea kitabu cha Henry M. Stanley: “How I Found Livingstone” (1874) Ch, 4 and 16).
Hata hivyo, Morogoro ya Simbamweni iliyokuwa katika eneo baina ya stendi ya Msamvu ya leo, Tungi na kihonda viwandani (kwa Mzee Maligwa mashuhuri kama “Mzee Kibarua” ilipo shule ya sekondari Kayenzi) ilikuja kusambaratishwa na mafuriko makubwa ya mto Morogoro na mto Ngerengere, kiasi cha kutobakisha chochote.
Stanley aliporejea toka bara hakuamini yaliyotokea na kudhani kuwa yuko ndotoni, kwani ule mji wa fahari hauonekani tena katika mboni zake mbili za macho yake ya kibluu!