HISTORIA FUPI YA WABONDEI

















HISTORIA FUPI YA WABONDEI
Kabila ya wabondei ni miongoni mwa makabila kadhaa ya wakazi wa Mkoa wa Tanga, Makabila mengine ni Wazigua, wanguu, wakilindi, wasambaa, waluvu, ambao kihistoria wana asili moja yaani waseuta kama nitakavyoelezea baadaye, Makabila mengine yaishiyo mkoani Tanga ni wasegeju, wadigo na wadaiso ambao wao sio waseuta na wenyeji kabisa wa inchi ya Tanga kihistoria ni Wambugu na wandorobo.
Waseuta ni kina nani?
Waseuta ni jina la umoja linalowakilisha makabila ya mkoa wa Tanga ambayo asili yao ni moja, makabila hayo ni wazigua, wanguu, wakilindi, wasambaa, waluvu na wabondei, wameitwa hivyo kwa sababu ya kiongozi wao wa zamani (Mkale) aliyeitwa Seuta ambaye alikuwa mtawala aliyewapigania na kuwalinda dhidi ya uvamizi wa wareno kabla hawajatawanyika, kwa sasa makabila hayo hutambika tambiko lao kwa matwala huyo au mtemi au chifu aliyeitwa Seuta.
Jina SEUTA ni muungano wa maneno mawili ya kibondei SE – Baba na UTA- ni Upinde kwa hivyo Seuta ni “Baba wa Upinde” wengine husema “mwana wa Upinde”, alizaliwa na Baba yake aliyeitwa Kuba Kaluli (seuta Kaluli) ambaye pia alikuwa mzimu wa zamani sana, na mama yake alikuwa binti wa kifalme aliyeitwa Musi au wengine walimuita Mchemno ambaye kaka yake alikuwa mfalme aliyeitwa Sekalingo, Seuta alianza kutawala akiwa na Umri wa miaka 12 alikuwa na akili za kupita kawaida mbunifu na pia alikuwa Mganga, moja ya maswala ambayo anakumbukwa sana Seuta ni namna alivyoweza kuwapiga Wareno kwa kutumia Upinde na Mishale na kuwauwa vibaya ingawa wao walikuwa na Bunduki.
Seuta alizaliwa huko Kwediboma katika tarafa ya Mgera wilayani Kilindi zamani Handeni umaarufu wake ulitokana na akili zake za kupita kawaida za ubunifu wa kuwashinda wareno waliokuwa wamekuja kuivamia inchi ya waseuta kwa kusudi la kuchimba madini na ili kupata watu wa kuwachimbia madini waliwaonea wenyeji na kuwakamata kwa nguvu ili wawachimbie madini watu walipogoma waliwaua na kuwachomea moto vijiji vyao jambo hili lilimuudhi sana Seuta na waseuta kwa ujumla kwani ukandamizaji huu wa Wareno haukukubalika.
Wareno walikuwa na ngome kubwa huko Mombasa lakini walikuwa wakisambaa kutafuta mali waseuta walipanga vita ambavyo vilipiganiwa katika eneo la Mto Ruvu, wareno walitumia Bunduki na mizinga na vita hii iliwakalia vibaya waseuta kwani milio tu ilikuwa tishio kubwa kwao na hivyo walirudi kwa kiongozi wao kutafuta ushauri, Seuta aliwashauri kuwa wanainchi waviache vijiji vyao na kila kijiji wanachokiacha sehemu ambazo Wareno wangepita wavichome moto na kuchafua maji, pia waharibu mashamba na vyakula kisha wajifiche vita hivi vilijulkana kama vita vya kuvunja mawe ya kusagia chakula “Nkondo ya kitula nyala” aliwambia kila wanapoharibu watambike na kuvunja mawe ya kusagia, Wareno walipoona kuwa askari wa Seuta wamekimbia waliendelea kuwafuatilia lakini walikuta maji yamechafuliwa, hakuna chakula na watu wamekimbia hali hiyo iliwashitua na wakakata tamaa kwa kuwafuatilia watu wasiowaona na pia njaa ilikuwa ikiwatesa wakiwa wamechoka na hofu ya njaa na magonjwa na silaha nzito ndipo Seuta alipoamuru kuwanyeshea mvua za mishale na wareno wengi sana na vibaraka wao walikufa na kuanza kukimbia wakirudi Mombasa wakiwa wameshindwa vibaya na hivyo Seuta alipata sifa kubwa sana kama mtu aliyekataa ukandamizaji na mwenye akili aliyekomesha kabisa uonevu na kuwashikisha Adabu na uganga wake uliaminika na watu walihofu kuwavamia waseuta na Tangu kifo chake ndipo waseuta wote walipoanza kutambika wakisema “Mtunga Katungile hale........Waseuta na Ugone.......”
Chimbuko la waseuta.
Kabla ya kuanza kuelezea kwa maneno chimbuko la waseuta ni vema ukaangalia mti huu wa familia ya waseuta ulikoanzia kwa umakini unaweza pia kuona katika Biblia kitabu cha Mwanzo 36;1- 4
ABRAHAMU
ISAKA
HETHI ESAU ARAMU
WAHITI WA ARAMU
ADA BINT ELON MHITI
Basemathi BINT ISHMAEL
Muungano wa Wahiti na Waaramu
HITTIO-ARAMAIO
KANAANI-KAPADOKIA-ZAGROS
MAZIGULA WA UMBA WA HITTIO ARAMAIO
INCHI YA UMBA au VUMBA
WAZIGUA-WASEUTA
NCHI YA Nguu/Kilindi
Wanguu Wazigua
Wakilindi Wasambaa Wabondei na Waluvu
CHIMBUKO LA WASEUTA
Ni vigumu sana kuzungumzia chimbuko la Wabondei pekee bila kuzungumzia waseuta wote kama ulivyoona katika kielelezo hicho hapo juu wabondei ni sehemu ya waseuta na kwa ujumla historia ya waseuta inaanzia mbali sana kama jinsi ambavyo umeona katika mti huo wa familia na chimbuko la Waseuta hapo juu.
Waseuta ni kabila ambalo asili yake ni Waaramu ambaye ndiye Baba yao mkuu. Aramu ambaye alikuwa ni mjukuu wa Nabii Nuhu, Nuhu alimzaa Shemu, Hamu na Yafeth. Hamu akamzaa Kushi (Ethiopia) Misri na Putu (Libya) na Kanaani, Shemu alimzaa Eberi ndiye Baba wa Waebrania na Elamu na Ashuru na Arfaksadi na Ludi na Aramu unaweza kuona chanzo cha Aramu katika Mwanzo 10;6-23. Kwa hiyo waseuta kwa upande wa Baba ni Waaram (Aramaites) na kwa upande wa Mama tunatokana na Esau mwana wa Isaka wa Ibrahimu, Esau alimuoa au alioa Binti wawili wa kikanaani ambao walikuwa ni wana wa Hethi Muhiti na hivyo kupatikana muungano wa wahiti na waaramu HITTIO-ARAMAIO ambao nchi zao zilikuwa ni Kanaani, Kapadokia na baadaye Zagros katika milima ya Armenia ya leo au kaskazini ya Iran ya leo ni wazi kabisa pia wazee wa zamani katika matambiko yao wamekuwa wakitaja HITTIO! Au HETHIO wa SEUTA! Ni wazi kabisa kuwa hii ilikuwa kabila ya zamani ya wahiti waliokaa Asia ndogo katika Anatolia jimbo la Kapadokia na Kuwa Mwaka 262 K.K wahiti walifukuzwa na wazungu waitwao Hansin a Sakson na ni katika wakati huo Hekalu la Diana huko Efeso lilivunjwa hivyo inchi yao ya kwanza ni Kanaani au Israel maeneo ya Gaza na Edom na hawa ndio waliompa Ibrahimu makaburi ya Makpela kwaajili ya kumzika sara Wahiti ndilo kabila ambalo Esau mwana wa Isaka alikoolea Mwanzo 26;34-35.
Kundi la kwanza la Waseuta ambao walikuwa wana asili ya waaramu na wahiti waliondoka kanaani wakati wa Mashambulizi ya Nabii Yoshua aliyekuwa mrithi wa Nabii Musa, Yoshua alikuwa na kampeni ya kuwaangamiza wakanaani na kwa kweli aliwamaliza wengi sana na hivyo wengi wa wakanaani wakiwemo waamori, waharati, wayebusi na wahiti walikimbia kabisa nchi zao na wengine walikuja Afrika hata hivyo wengi wa waseuta walibaki salama katika nchi ya Edomu kwa sababu Mungu alikuwa amemuamuru Yoshua kutokuangamiza uzao wa Esau kwa kuwa ni ndugu wa Israel, wengi waliokuwa wakanaani wengine walikimbilia Afrika Mashariki na kujenga miji kama Barawa, Lamu,Shungwaya, Malindi, Mombasa, Umba, Pemba na Unguja, Tanga, Pangani, Saadani, Bagamoyo na Mzizima, Mafia, kilwa, Mikindani mpaka maeneo ya Msumbiji, Angola, Kongo na Uganda wakati huu inakisiwa ilikuwa miaka 1200 K.K. Hittio Aramaio walikaa juu ya Israel katika inchi ijulikanayo kama Syria leo au Shamu na maeneo ya kusini Mashariki ya Israel ndiyo Inchi ya Edom ng’ambo ya mto wa Yordan.
Kundi la Pili la waseuta lilisonga mbele kuelekea Kapadokia nyakati za utawala wa Mfalme Daudi ambaye aliwapiga wakanaani wakiwemo Washami, Waaramu, Waedomu na Wamoabu na wadameski, sababu ya Daudi kuwapiga hawa ndugu zao ni kuwa walijiunga na Wafalme wengine maadui wa Daudi ili wampige, Hivyo Mfalme Daudi aliona ni vema kuvunja ile ahadi ya kutokuwapiga ndugu zao Daudi akiwa na Jemadari aliyeitwa Yoabu waliwapiga vibaya kwa mfululizo wa vita miezi sita vipigo hivyo viliwatia hofu na kuwafanya kutawanyika na kujificha mbali kama Misri, Paran, Midian Uajemi na Uamedi na hivyo kutawanyika katika nchi za Washirazi (Waajemi).Baada ya kufa kwake Daudi baadhi walirudi katika nchi yao lakini baadhi walibaki huko juu katika milima iliyoitwa Zagros ambazo ni safu za milima katika inchi iitwayo Armenia na Iran ya leo.
Nchi za Asili za Waseuta.
Kanaani/Israel
Hii ndio inchi ya kwanza walioishi wahiti na baaada ya Esau kuoana na binti wa Kihiti waliishi katika Inchi ya Edomu ambayo ilihusisha maeneo ya Syria na sehemu ya kusini ya Israel yaani Gaza na Edomu ng’ambo ya mto wa Yordani Dameski ulikuwa mji wao wa kwanza na baadaye walipanda juu Hata Antiokia ya Pisidia ndio Anatolia au jimbo la Kapadokia
Kapadokia.
Hii ni inchi ya pili ya waseuta ambapo waliishi katika jimbo hili huko Asia ndogo kwa mujibu wa utafiti wa maswala ya uchimbaji wa mambo ya kale eneo ambalo wahiti hao waliishi linaonyesha ushahidi kuwa walikuweko katika eneo hilo miaka 1340 kabla ya Kristo Kama utakavyoona kwenye ramani chini eneo lililotiliwa Rangi ni eneo ambalo jamii ya wahiti waliishi eneo hili linaweza kuchukua inchi za Syria na Uturuki na ugiriki lakini nyakati za zamani hakukuwa na Ramani zilizoko leo
Ramani hii inaonyesha jimbo la Anatolia au kapadokia zamani likithibitishwa na watafiti wa mambo ya kale kuwa ni eneo lililokaliwa na wahiti miaka 1340 Kabla ya kristo
Zagros
Kutokana na usumbufu Fulani walioupata toka kwa wazungu jamii hii ilikimbilia kwenye inchi ya tatu na kuishi katika safu za mlima Zagros ambayo imesambaa kaskazini mwa Irani ajemi na Armenia ya leo, Milima ya zagros imesambaa kuanzia kusini magharibi ya Iran hata kusini mashariki ya Sirvan katika ya mto Dilaya na Mto Shiraz wengi wa watu wanaoishi pemba na Zanzibar na visiwa vya commoro ni jami ya watu walioishi huko Uajemi katika mto huu shiraz hii ndio asli yao.Safu ya milima ya zagros ina urefu kati ya Km 900 au mail 550 urefu na upana wa mail 150 sawa na Km 240 eneo kubwa zaidi kwa leo ni Iran na ni kama inatengeneza mipaka ya inchi ya Iran na mataifa mengine, ndani yake kuna vilima vyenye urefu kati ya futi 12000 na mingine imefunikwa na barafu, maeneo haya yana rutuba na mito yenye kutiririsha maji na hupata mvua zenye ujazo wa mill 40 mara kwa mara.
Tamaduni zinazofunika maeneo haya ni zile tamaduni za zamani za ki- Mesopotamia na kiuajemi au kimedi pia kwa sehemu kuna tamaduni za Kirumi wakazi wake wengi walikuwa ni Waashuru wa Kikristo, Wakurd na waturuki na wengi walikuwa wafugaji na maeneo hayo pia yanachimbwa mafuta katika sikuza leo, ni kwa sababu hiyo nchi za zamani za Waseuta zinakuwa ni Kanaan-Kapadokia na Zagros, Jina hilo Zagros ndio asili ya Jina Wazigua, kwani watu waliwaita Wazagros, Mazigulat, na baadaye wazigua.
Inchi hii hapo juu ndio milima ya Zagros huko Uajemi na Armenia hii ndio inchi ya tatu ya asili ya Hittio Aramaio Zagros
Kwa hiyo kwa asili inchi yao ilikuwa shamu au Syria na Yordani kwa mipaka ya nyakati hizo na walijulikana kama Hethio - Aramaio kwa maana ya asili ya Kiaramu na asili ya Esau aliyeoa mwanamke wa kihiti mji wao uliitwa Anatolia katika jimbo la Kapadokia walipokuwa wamekimbilia Armenia katika safu za milima ya Zagros huko shirazi au uajemi, Wagiriki waliwaita Zigra au Zagroth watu hawa baadaye walikimbilia Afrika na kuingia kwa majahazi katika pembe ya Afrika inchi za Somalia,Ethiopia, sudani na Afrika Mashariki na kufika katika inchi ya Umba au vumba kutokana na sababu mbalimbali na uonevu, inchi hii ilikuwa kati ya Lamu na Tanga mpaka maeneo yanayouzunguka mto Umba, wengine waliteremkia Ethiopia na Somalia katika maeneo ya shungwaya na wasomali waliwaita Mashungula, Mzungu mmoja aliwaita Wasegua na wazungu wa Kireno waliwaita Mozungullos kwa sababu walishindwa kutamka jina lao vema la asili Mazigra au Mazagros au Mazigula hivyo kimsingi watu hawa sasa walijulikana kama “Zigras – Hittio – Aramaio” kwa msingi huo sasa jina Wazigua ni Kiswahili cha Neno Zigras au Mazigulat, ushahidi wakitafiti unaonyesha kuwa wengine walikuja wakiwa na majina ya kiasili ya huko Uajemi kwa mfano Kiongozi wao wa kwanza walipofika Umba aliitwa CHAMBIKE WA VUMBA na alipokufa alitawala mwanawe aliyeitwa MWANACHAMBI kisha Walifuata wanachambi wengine asili ya jina CHAMBIKE ni “CAMBYSES” AU KAMBISESI ambaye alikuwa mtawala wa uajemi mwaka 528 K.K. ambaye ni mtawala aliyefuata baada ya kufa kwa baba yake Mfalme KORESHI au Cyrus, Cambyses alitawala uajemi yote ikiwemo Armenia kati ya miaka ya 600-559 karne sita kabla ya kuzaliwa kwa Masihi alikuwa ni mwana wa Koreshi aliyepokea utawala wa Baba yake Huko Kaskazini mwa Shushan Ngomeni huko Elam, alimuoa Bint wa mfalme Astyages mmedi na kulingana na Mwanahistoria wa kigiriki Herodotus Cambyses alimuoa bint wa Astyages ambaye kupitia yeye alimzaa mtoto aliyekuja kuwa mfalme mkubwa baadaye na kuitwa Koreshi mkuu wa II.
Wazigua walikuja na jina Kilo wakimaanisha KORESHI jina hilo kilo linatumika hata leo, ufalme huo wa Uajemi au ushirazi ulianza kati ya 546 - 446K.K. aidha kwa kuwako kwao kusini mwa Israel ilikuwa ni rahisi kwao kufika katika inchi ya Wafilisti katika ukanda wa Gaza na wale waliokuwa na rangi ile ya asili wakati mwingine waliitwa Mgaza jina hili Mgaza ni moja ya majina waliyokuja nayo kutokana na mji wa Gaza na katika jamii hizi pia wako wanaoitwa CHAMBI.
Kwa msingi huo niwazi kuwa asili ya Neno zigua ni Zagros au Zigras waingereza waliwaita watu hao Hethio au Hittets na Aramaio au waaramu Aremeans kwa hiyo wazigua waliitwa majina hayo kutokana na asili yao au majina ya inchi walizoishi kwa hiyo wao ni Waedomu au Waesau au Hethio – Aramaio majina haya walipewa kabla ya kuja kujulikana kama Waseuta baadaye na kupata matawi ya waseuta ambao ni wanguu, wazigua,waluvu, wabondei, wakilindi, pia baadhi ya wazigua waliopotea ni wasonjo, walugulu, wakwere na baadhi ya wankodongo na baadhi ya wanyamwezi.
Alama kuu ya waseuta ni upinde na mshale
WASEUTA KATIKA NCHI MPYA YA NGUU AU HANDENI.
Nilieleza mwanzoni kuwa Makundi ya Zigras – Hittio – Aramaio wengi walikimbilia katika nchi iitwayo Umba ambayo iko kati ya Lamu na Tanga, katika bahari ya Afrika Mashariki hii ndio nchi ya kwanza kwa waseuta kuifikia walipotoka kanaani na Armenia hapa waliungana na wenyeji wengine na waswahili na kukawa na ustaarabu mkubwa sana hata hivyo eneo kubwa la nchi hiyo ya umba kwa sasa iko Kenya, Mahali hapo palikuwa ni pazuri kwa uunganishaji wa miji ya Lamu Mombasa, Pemba na unguja na hata kilwa, watu kutoka Bara walikuja na Pembe za Tembo, Shaba, chuma na kadhalika na waliwauzia Waarabu, Wamisri, Wagiriki, wachina na wazungu ambao wao walileta shanga na nguo na sahani Biashara hizi zilikuwa na mvuto mkubwa sana na ziliwavutia wazungu waliokuwa wakorofi yaani Wareno ambao kwanza walituma wapelelezi kama Batholomayo Diaz na Vasco Dagama ambaye alifika Mombasa na Malindi kati ya tarehe 7th April 1498 na hakupata ushirikiano katika miji yote Isipokuwa Sultani wa Malindi alimpatia viongozi wawili wa kumsaidia kufika Bara Hindi Mei 28th 1498 na hata ilipofika miaka 1500 B.K Wareno wengi walikuja Afrika ya Mashariki wazungu hao walikuwa wakorofi na waliiharibu nchi kwa ugomvi na vita na kuwatoza watu kodi kubwa sana wengi wa watu walianza kuwakimbia, Wareno walikuja Afrika mashariki na kusambaa mpaka Msumbiji na Angola lakini walijenga makazi huko Mombasa katika mji wa Mvita yaani mji wa vita wakajenga ngome kubwa ya Askari iliyoitwa Ngome ya Yesu au (FORT JESUS) ambayo iko Hata leo haya yalifanyika kati ya mwaka wa 1592-1598 ngome hii iko hata leo mjini Mombasa.
Ngome ya Yesu (Fort Jesus Mombasa) ilijengwa na wakoloni wa kireno mnamo miaka ya 1590 kwaajili ya kulinda biashara zao na shauku ya kutawala eneo hilo leo ni moja ya makumbusho ya kihistoria katika pwani ya Kenya,Mjini Mombasa
Kutokana na ukatili wa Wareno wanaichi wengi wa Afrika Mashariki hawakuwapenda kabisa wareno, Wareno walipigana na Mazigula ambao wao walikuwa ni kabila kubwa na hawakupatana kabisa na wareno na hivyo watu wa Umba walishindwa na na wakasukumwa mbali wakiongozwa katika kukimbia kwao na walisaidiwa na wenyeji Wambugu ambao hawakua na wivu na wageni hao walikimbia zaidi ka Km 1600 na ndipo walipokimbia na kufika Nguu kundi linguine lilikimbilia katika milima ya pare mpaka inchi ya mlima mweupe yaani Kilimanjaro hawakukaa wakaendelea mpaka Sonjo baadaye walirejea kwa kupitia Irangi Kondoa na kurudi katika inchi ya Nguu na kukutana na wenzao kongozi aliyewaongoza alikuwa Mmbugu aliyeitwa Malando Bin Mbogo ambaye alikuwa mwenyeji wa Inchi na kiongozi mwingine aliitwa Maita, Kundi linguine lilipotelea na kubakia katika maeneo ya Loliondo na maeneo ya mlima wa Mungu Oldonyo Lengai na kubaki katika inchi ya Sonjo huko Masaini na wakajiita wasonjo kwa sasa wameathiriwa na desturi za Kimasai lakini ni ndugu zetu na hufanana na wazigua na hawaongei kizingua bali kisonjo.
Wazigu awalipofika Nguu walikutana na makabila mengine ya watu waliokimbia vita na kuchanganya Damu, kabila la kwanza kabisa kuchanganya Damu na Mazigula ni Wagala hii ni kwasababu hethio Aramao waliwahi kukaa huko Ugala huko Kenya wakitokea Ethiopia na Somalia walikokaa kwa Muda na hawa wagala wana Pua Ndefu na ndivyo unavyoweza kuona baadhi ya wasonjo na hata baadhi a wazigua wana pua ndefu, kabila zilizochanganyika na wazigua huko nguu ni pamoja na Wazorwi, Washana toka Botswana,Walozi, waemba , wangoni, wachewa, Watonga na wanyasa na kadhalika Hata hivyo tamaduni la Lugha ilikuwa ileile ya wazigua moja wa nyimbo za wakale zinazothibitisha kuwa walichanganya Damu na wagala zinasema hivi “Msi na Mgalla Mwadungana Hahi? mpula ya Mgala kulengela!” yaani mwenye nchi na Mgala mlichanganyikia wapi? Na Pua ya mgala imechongoka!.
Utawala wa Kireno haukudumu kwani walitimuliwa na mataifa mengine ya ulaya na wakakimbilia Angola na Msumbiji ingawa waliendeleza tabia yao ya vita na wenyeji, waarabu wa Omani walitokea na kunyang’anya mamlaka yao yote, waarabu walitawala kwa amani na kupatana na wenyeji na walistawi wakifanya Biashara wengi wa waarabu wana asili ya Kiaram katika wakati huu wa Amani kulijitokeza kiongozi mmoja aliyejiita mwanachambi akitaka kuendeleza utawala wa Mazigula katika inchi ya Umba aliandika Barua na kuisambaza ili kuwataka wazigua wote kurudi katika Inchi ya asili waliyofikia yaani Umba kwa hiyo kukaweko kusudi la kurejea Umba na hapa ndipo ulipotokea Mgawanyiko mkubwa miongoni mwa Wazigua
Kundi la Kwanza.
Baada ya kabila nyingi kusika kuwa Wareno wamepigwa walirudi makwao lakini jamii ya Hittio Aramao Zigulats hawakuondoka lengo lao lilikuwa kurudi Umba, lakini kundi moja lilikakataa kurudi Umba na kubaki katika inchi ya Nguu iliyoko huko Kilindi au Handeni ya zamani, kumbuka Inchi ya Nguu pia ilikuwa ikiitwa Kilindi wao waliobaki katika inchi hii waliitwa WANGUU, mji mkuu wa Nguu ni SONGE kwa sasa ndio Wilaya ya kilindi, Tarafa zake ni Tatu Kimbe, Mgera na Kwekivu.wanguu waliitwa hivyo kutokana na kilima kiitwacho nguru au nguu baadhi ya wanguu hupatikana katika wilaya kama kilosa Morogoro Mpwapwa na Kongwa huko Dodoma na hivyo kuchanganyika na walugulu kwa kiasi hivyo walugulu wana asili ya uzigua Baadhi ya hethio aramaio zigulat walibaki katika nchi ile ya Nguu na kuchukua nchi za Wandorobo ambao walikuwa wenyeji wazigua walichukua inchi hizo na kwa utulivu walianza kupanda mazao pamoja na kuwinda wanyama kwa kuwa wengi walikuwa wawindaji waliwinda wanyama na kuzichanja nyama na kuzianika na ndipo eneo lile waliloishi kwa uwindaji liliitwa “Chanika” yaani kuanika baadaye mfumo wa maisha ulibadilika na walianza kuhamasishana kupanda mazao Handeni na ndipo pakapatikana Jina HANDENI jamii kubwa ya hawa waliobaki hapa waliitwa kwa jina la saili ZIGULATS au Mazigulats kutokana na jina la Kiyunani ZAGROS hao ndio wazigua hata sasa miji yao mikubwa ni Kwamkono,Misima, kideleko, Chanika. Kwalukonge, kwediboma, kwedibangala kwa seuta,kwa mgumi, Bomani n.k. Zumbe waliotawala zigua ni pamoja na Zumbe Mohamed Mdoe ukoo anaotoka mkuu wa Wilaya mmoja aitwaye Athmani Mdoe, Tarafa zao ni Chanika, Handeni, Magamba, Mazingara, Kwamsisi, na Mgambo hata hivyo inchi za Uzigua nyingine ni pamoja na Pangani, Bagamoyo, Mbwewe, Msata, Saadani, na miono huko walichanganyika na Wadoe na Wakwere kwahiyo wakwere ni ndugu zetu walugulu huko Morogoro walitokana na ukoo wa wazigua na mkale wao aliitwa Samwelugulu huyu alikuwa mzigua na ndiye baba wa walugulu
Kundi la Pili
Katika inchi ya Handeni kuna kilima ambacho kiliitwa Kilindi hili ndio jina la wilaya mpya a kilindi kwa sasa iliyogawanywa mwaka 9/5/2002. Kilima hicho maarufu kiko katika tarafa ya kwekivu, kundi la wazigua wengine walikwenda kuishi na wenyeji wa Milima ya Usambaa na kusambaa katika milima yote ya Usambara na hivyo walibadili jina la asil la wazigua na kujiita wasambaa, inchi yao kwasasa ni Lushoto, Maramba, Muheza, Magoma, Korogwe, Mlola, Mtae na sehemu za Upare wenyeji wao sasa wanaweza kuongea Kisambaa lakini wao ni Wambugu ndio wenye inchi.
Muonekano wa mlima kilindi na mlima nguu mlima kilindi huonekana kama mtu aliyebeba motto mgongoni na ukiwa umeuinamia mlima nguu na kuacha pengo linaloweza kupitwa katikati hivi ndivyo unavyoonekana ukiwa chanika na kuutazama kwa upande wa magharibi
Kundi la Tatu
Hawa ni kundi la wazigua walioitwa wanguu hili ni kundi dogo ambalo baadaye liliamua kuhamia Usambaa kiongozi wao akiwa MBEGA aliitwa Mbega kwa sababu Yeye alikuwa Bado ana Rangi ya asili ya Esau alikuwa mwekundu kama mwarabu na hata baba yake Mbega alikuwa na Rangi hiyo ya asili walipanda milmani na wakajulikana kama Wakilindi kwa hiyo wakilindi pia ni waseuta wengi hawapendi kuitwa vinginevyo kwa sababu ya kujivunia Rangi yao, Mbega kwa kuwa alikuwa Hodari na mwenye kuwinda wanyama kama Esau alikuwa na Busara na alikuwa mwamuzi mzuri na mwenye maajabu kadhaa hivyo wasambaa walimuomba awe mtawala na aliwatawala na wazao wake ndio kina Kimweri, Zumbe Kimweri ndiye aliyekutana na wazungu na makasisi wa CMS Dr.Krapf na Rebman ambao walipitia Mombasa mwaka 1848 na kufika Vuga ya Usambaa na kuonana na Zumbe Kimweri wa IV na walimsifu kwa uongozi wake, Bwana Rebman alielekea Kilimanjaro na kuona mlima mweupe na ndiye aliyetoa taarifa ulaya kuwa Afrika ina Mlima wenye Barafu kama kwao kwani wazungu walifikiri Joto lililoko Afrika sio rahisi kukuta Jambo kama hilo, Mazumbe Kimweri inaonekana walitawala kwa Muda mrefu kwani Zumbe aliyekutana na Dr.Krapf alikuwa Kimweri wa IV aliyefariki mwaka 1860 Kimweri alizaa sana watoto wengi na rnagi za asili zilijitokeza hao ndio WAKILINDI . Dr. Krapf baada ya maongezi na Kimweri alianzisha Dini Huko Tongwe akitokea Unguja kwa Sultani Said.
Kundi la nne
Katika makundi yote lilikuweko kundi moja ambalo lilipania kurudi katika Inchi ya asili na kufika Pwani yaani Umba lakini lilikumbana na vikwazo vingi sana zikiwemo vita za wavamizi wapya kutoka Kenya ambao wao sio Hettio Aramaio hawa walikuwa Wadaiso, wasegeju na wadigo pia kwa hofu ya wageni wengine walifika katika mji wao mkuu wa zamani ulioitwa New Fort-Umba au umba mpya Ngomeni, waliishi maeneo mbalimbali hata kufika Pwani kama Tanga ambayo iko chini ya umba ya zamani ambako ni Horohoro mpaka sehemu za Kenya, Wazigua hawa walisambaa kutoka mji mkuu wa zamani yaani Umba na sehemu za Mbwego, ambako huitwa Magila leo, pia waliishi maeneo ya Mkuzi ambako kulikuwa na fundi maarufu wa kucheza njuga aliyeitwa Saudimwe na mwanae Kidungwe, walisambaa sehemu za jaila ambako ndio Misozwe leo, Bwembwera na tongwe, Makasisi Krapf na Rebman waliweka Msalaba huko Hemvumo wakiwa wamepachagua kujenga kituo cha kazi za kimisheni walipokuwa wakitokea Vuga kuomba Ruhusa ya Zumbe Kimweri wa IV na wakipita kutokea Unguja Hemvumo au Msalabani ndio Magila, Akofu Frank Wetson alijenga shule kubwa kiwanda kutoka hemvumo au Magila pia wazigua hawa wako sehemu za Amani hawa nao kama wasambaa walibadili jina na Kujiita wabondei yaani “Valley Peoples” mji wao mkuu kwa sasa ni Muheza.
Kundi la Tano
Hawa ni wazigua walioamua kuishi kando ya Mto Ruvu au Mto Pangani, wakati wazigua wakisogea mbele kuelekea inchi nyinginezo kama Saamba na Bonde hawa waligundua mto ambao wazungu waliuita River na wao waliuita Ruvu hawa walifanya shauri la kujenga kandokando ya mto huu na wengine waliishi katika visiwa vidogo vya mto huo na kuvuka kwa kutumia mti ulioitwa Ulalo au Vilalo kwa kizigua ili kuwawezesha kufanya shughuli kutwa nzima na usiku walirudi kisiwani na kuondoa ulalo ili maadui wasiwapate kwa sababu ya kuishi miaka mingi kando ya mto huu na kujifunza kuvua samaki wakaitwa waruvu au waluvu kwa sababu hiyo sasa Wanguu, wakilindi, Wazigua, waruvu, wasambaa na wabondei ni kabila moja la waseuta wenye asili ya “Hethio Aramaio Zagros” lakini hivi ndivyo inchi zao na miji yao na falme zao na zumbe zao na kaya zao zilivyoweza kupatikana hata leo.
Kundi la sita
Hili ni kundi la wazigua waishio Somalia, wazigua wanayo inchi nyingine iliyo nje ya Tanzania nchi hii huitwa CHAMAMA ambayo iko Somalia zamani ilijulikana kama Zigua la Kismayu jimbo hilo limepewa hadhi ya kuwa wilaya huko Somalia katika mkoa uitwao JUBADDAHOOSE au lower Juba au Juba ya chini mkoa huu unapakana na nchi ya Kenya, mkoa huo una wilaya nne Kismayu, Badada, chamama na Afamadow Jina Chamama ni jina la kizigua cha kale zaidi wakimaanisha majani yafananayo na mpunga kwani wazigua walikuta majani mengi ambayo huota ndani ya maji ambayo kwa kizigua huitwa Nchacha na aina hii ya majani huonekana katika inchi zote za waseuta, wazigua waliokwea Somalia miaka kati ya 550-600 iliyopita na kushindikana kurudi nyumbani wakasema hapa tumefika wakaya Bwila au Bwira na hivyo wao waliitwa Wagosha wa Juba kwani mto Juba hupita Karibu na Chamama huko Somalia, Hata jina la wilaya nyingine Kismayu lina asili ya Kizigua SIMADYAKULANGA yaani kisima cha juu na kwa Kiswahili ndiyo Kisimayu au kisima cha juu na huu ndio mji wa mkoa wa Juba.
Wazigua katika inchi ya Unyanyembe
Kwa mujibu wa Chifu Abdala Fundikira Marehemu uchifu wa unyanyembe ulikuwa ni uchifu wa wazigua, sababu kuu ya kundi la wazigua kwenda kutawala unyanyembe ilikuwa ni kujifunza na kuonyesha uhodari katika maswala ya uganga na uchawi, Inaelezwa kuwa Wanyamwezi walikuwa wakijivunia sana Uganga na wazigua walikuwa ni waganga Hodari wakati Fulani katika inchi ya Uzigua walishindana katika maswala ya uganga na ikasemekana kuwa wale watakaoshinda watawatawala wenzao, Wazigua waliwashinda wanyamwezi na hivyo kundi la Mshujaa na wake zao na watoto waliamua kusafiri kwa njia ya bonde la Ufa wakapita Dodoma, Kondoa na kufika Itigi, Hapo waligwanyika katika makundi makuu manne moja lilipotelea kondoa, kundi la waganga hodari liliendelea Hata kufika unyanyembe na kushinda katika maswala ya Uganga na hivyo wanyamwezi waliwatawaza kuwa watawala Machifu hao wa Unyamwezini wote walitoka katika ukoo huu wa wazigua na kuitawala inchi ya Unyanyembe machifu hao ni I pamoja na Chifu Kitwanga, Mputa, mpopo, Kabundi, nsoso, Mmanywa, Mgalula, swetu, Fundikira 1, Mwasele, kiyungi, Isike, Nyaso, Kalunde 1, Said Fundikira, Kiyungi2, Mkasiwa, Fundikira 2, Na Abdala said Fundikira. Ni kwa sababu hiyo wazigua na Wanyamwezi ni Watani wa jadi na husaidiana katika Misiba na kujua kwanini msiba umetokea hii ni kwa sababu ya uhusiano wa Karibu wa wanyamwezi na Wazigua wote.
TAARIFA SAHII KUHUSU MBEGHA (MBEGA)
Ni mtemi wa waseuta waitwao wakilindi Habari zisizo za uhakika zilikuwa zinaonyesha kuwa Mbega litokana na ukoo wa Waarabu yaani baba yake alikuwa Mwarabu kutoka ukoo wa El-Kindi Mwaka wa 1938 iliwahi kuonyeshwa sinema ambayo ilionyesha kuwa Mbega alikuwa Mwarabu pamoja na Baba yake sinema hii iliwaudhi sana watu kwani ilkuwa sio sahii, sinema hii ilionyesha pia kuwa Mbega alikuwa kigego a kuwa alikimbilia uga kwa sababu aliua mtu Haya hayakuwa maswala ya kweli.
Mbega alizaliwa katika kijiji cha Kigurunde jirani na mlima kilindi na Baba yake aliitwa Mliga Bin Mgweno na jina la Kaka yake Mbega aliitwa Mauya (muya) na dada yake aliitwa Nenkondo Mboza na Mama yake aliitwa Mzigwa bint Kimweri, mjomba wa Mbega aliitwa Shebuge majina yao yote haya ni ya kinguu, kwahiyo Mliga alipooana na Mzigwa walizaa watoto hao watatu yaani Mauya(Muya), Mbega na Nenkondo ni wazi kuwa Baba yake Mbega alikuwa na Rangi ya asili ya Inchi tuliyotokea Rangi ya Esau hivyo alikuwa mwekundu kama waarabu na Mbega pia alikuwa mwekundu hii ndio rangi inayofikiriwa kuwa ni ya kiarabu , Lakini kwanini tunakanusha kuwa Mbega hakuwa mwarabu sababu ni kuwa mbega alikuwa mwindaji Hodari sana alikuwa akiwinda wanyama wengi sana na hata nguruwe aliwaua na kuwala hili lingekuwa jambo la kustaajabisha na kuudhi dini a Baba yake kama angekuwa mwarabu, pia inasimuliwa kuwa wakati mbega anaishi Waarabu na Wazugu walikuwa hawajafika kilindi.
Kuondoka kwa Mbega huko kilndi na kukimbilia Sambaani kulitokana na kutoa zawadi ya kipande cha nyama kwa siri kwa mke wa mjomba wake aliyeitwa Musi alikuwa mzuri na mke kipenzi wa mjomba wake shebuge, hii haikuwa kawaida kwani kawaida yake ilikuwa kila wakati anaporudi mawindoni humpa mjomba wake Nyama ambaye yeye humpa mkewe, Musi aliificha nyama hiyo lakini shebuge aliiona na aliuliza kwanini Mbega amefanya hayo hali ilikuwa mbaya na mwanamke alipiga kelele kuwa Mbega anataka nife! Nyama hiyo ilikuwa ya mbaa na ilihesabika kuwa imeharimishwa kwa wakilindi, Mbega aliposikia hayo alidhani kuwa atauawa na aliposikia vishindo vya miguu ya mjomba wake alikimbia na siku ya kwanza alilala katika pango la jiwe katika mlima Ngareni wakati huu alikuwa amemchukua nduguye Nenkondo siku ya pili walikwenda kujificha katika msitu mmoja uitwao Komwejimbu kisha walikwenda kulala Maurwi na kukaa kwa siku kadhaa kisha wakaendelea Ntalawanda Karibu na makuyuni hapo walikaa Muda mrefu na kujulikana na watu huku akiendela kuwinda.
Mjomba wake Shebughe alipopata habari alituma watu na shekulwavu mtoto wa mama yake mkubwa ili kumrudisha lakini mbega alikataa na alikataa hata kumuachia Nenkondo akihisi kuwa mjoma wake atatuma watu wengi zaidi kmkamata aliamua kuvuka mto na kuelekea milima ya Usambara huko Vuluni na baadaye alipanda juu zaidi, alijulikana kwa akili zake nyingi na Busara za kuamua watu pia alikuwa Hodari sana na ndipo wasambaa walimfanya kuwa mtawala wao na makao yake makuu yakawa Vuga, Uzuri wake aliokuwa nao na rangi ya asili ndivyo vilimfanya aitwe Mbega, anakumbukwa kwa kuvuka mto ruvu katika eneo ambalo watu waliotaka kumfuatilia walishindwa kuvuka na wengine kufa maji na pia anakumbukwa kwa ugunduzi wa Dawa ya Nguvu za kiume iitwayo MBOMBO ambayo inapatikana kwa wingi Mombo, Mombo ni jina lililotokana na mti wa Mmbombo wazungu walishindwa kutamka mbombo na wakatamka Mombo na ndio pakaitwa hivyo hata leo Dawa hii hupatikana Mombo sokoni hata leo inasemekana kuwa Mgunduzi wa dawa hiyo ni mbega. Kutokana na damu hii ya Mbega baadhi ya watu hufikiri kuwa kuna damu ya wajerumani dhana hiyo sio kweli.
Powered by Blogger.