Zitto Kabwe njiapanda, Chadema wamfukuza
Zitto Kabwe
Dar es Salaam. Hali ya kisiasa ya mbunge wa
Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe imewekwa njiapanda baada ya Chadema
kutangaza kumvua uanachama saa chache baada ya Mahakama Kuu kutupilia
mbali kesi aliyofungua dhidi ya chama hicho kikuu cha upinzani.
Zitto,
ambaye amedumu kwenye nafasi ya ubunge kwa takriban mwaka mmoja
kutokana na amri ya mahakama, sasa atalazimika kuamua kutangaza rasmi
kujiunga na chama kipya cha Alliance for Change and Transparency (ACT)
kama alivyokuwa amepanga kufanya wiki ijayo, au kukata rufaa mahakamani
ili aendelee na majukumu yake ya kibunge hadi hapo muda muafaka
utakapowadia.
Lakini mbunge huyo mwenye umri wa miaka
36, aliiambia Mwananchi muda mfupi baada ya kutangazwa kutimuliwa kwake
kuwa hakuwa na taarifa za kuwapo kwa uamuzi huo wa Mahakama Kuu jana na
kwamba leo ataendelea kuchapa kazi za Bunge wakati atakapoiongoza Kamati
ya Hesabu za Serikali kupitia matumizi ya Shirika la Umeme (Tanesco).
Akitangaza
kutimuliwa kwa Zitto, mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu Lissu
aliwaambia waandishi wa habari kuwa kwa kufungua kesi mahakamani, naibu
katibu mkuu huyo wa zamani wa Chadema alikiuka katiba ambayo hairuhusu
migogoro ya ndani ya chama kupelekwa mahakamani.
Alinukuu
Sehemu ya Kwanza ya Kanuni za Kusimamia Shughuli, Mwenendo na Maadili
ya Wabunge wa Chadema, kipengele cha 8 (a) (X), inayosema: “Chadema
itashughulikia matatizo ya viongozi na wanachama kwa kufuata taratibu
zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba ya Chama, wala hata siku moja
haitashughulikia mambo kama hayo mahakamani. Mwanachama atakayeshindwa
kufuata taratibu na ngazi za chama hatavumuliwa na atafukuzwa
uanachama.”
Lissu alisema Zitto alikiuka kipengele hicho kutokana na kufungua kesi Mahakama Kuu kushughulikia matatizo yake ndani ya chama.
Katika
kesi yake Zitto, ambaye alikuwa naibu katibu mkuu wa chama hicho,
alikuwa anataka mahakama hiyo imwamuru katibu mkuu wa Chadema ampe
mwenendo na taarifa za vikao vya Kamati Kuu vilivyomvua nyadhifa zake
zote alizokuwa nazo ndani ya chama.
Mbunge huyo pia
aliomba na kufanikiwa kupata amri ya muda ya kuizuia Chadema, wakala
wake na vyombo vyake vya uamuzi kumchukulia hatua zozote wala kumjadili
kuhusu uanachama wake, hadi hapo rufaa aliyokuwa anakusudia kukata
Baraza Kuu la chama hicho kupinga kuvuliwa nyadhifa, itakaposikilizwa.
Pia amri hiyo ilizuia walalamikiwa kumwingilia katika utekelezaji wa majukumu yake kama mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Zitto alifungua kesi hiyo Januari 2, 2014, dhidi ya Bodi ya Wadhamini na katibu mkuu wa Chadema.
Katika
uamuzi wake jana, Jaji Richard Mziray ilitupilia mbali kesi hiyo na
kumwamuru Zitto akilipe chama hicho gharama za kesi hiyo.
Jaji
Mziray alijikita katika hoja mbili tu za pingamizi, akieleza kuwa kesi
ilitakiwa kufunguliwa kwenye Masjala ya Wilaya ya Mahakama Kuu badala ya
Masjala Kuu ya Mahakama Kuu.
Kwa hoja hizo mbili, Jaji
Mziray alisema kuwa hoja hizo zinatosha kutupilia mbali shauri hilo na
kwamba hakuwa na haja ya kuendelea na hoja nyingine za pingamizi.
Jaji Mziray alisema kuwa mlalamikaji alipaswa kufungua kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi na si Mahakama Kuu.
Pia
alisema kuwa hata kama alikuwa na uhalali wa kufungua kesi hiyo
Mahakama Kuu, basi alipaswa kuifungua katika Masjala ya Wilaya na si
Masjala Kuu.
Wakati uamuzi huo unatolewa, Zitto na Wakili wake hawakuwepo mahakamani hapo.
Akifafanua
kutimuliwa kwa mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini, Lissu alisema kuwa kwa
sasa hakuna sababu ya kuitisha kikao cha Kamati Kuu kwa ajili ya
kumtimua Zitto kwa sababu alikimbilia mahakama kuzuia vikao vya juu
kumjadili tofauti na Katiba inavyoeleza.
Alirejea
sehemu hiyo ya kusimamia shughuli, mienendo na maadili ya wabunge wa
Chadema, kipengele cha tisa kinachosema: Mkutano Mkuu utakuwa na maamuzi
ya mwisho kwa jambo lolote na pande zinazohuika ni lazima ziti maamuzi
ya mkutano mkuu. Mtu yeyote atakayeshindwa kutii uamuzi wa Mkutano Mkuu
atakuwa ametofautiana na Chama na kuanzia saa hiyo uanachama wake
utakuwa umekoma.”
“Kama (aliyekuwa mwenyekiti wa
Chadema Arusha, Samson) Mwigamba na (mjumbe wa Kamati Kuu, Profesa
Kitila) Mkumbo, wangeenda mahakamani kama Zitto, wangekuwa
wameshafukuzwa kabla ya kujadiliwa na Kamati Kuu. Lakini Zitto
alikimbilia mahakama kuizuia Kamati Kuu kumjadili na hivyo ilikuwa
automatic,” alisema Lissu.
“Kitakachofanyika kwa Kamati
Kuu ni ku-take note tu (kuchukua taarifa) kwamba Zitto amefukuzwa,
hakuna haja ya kuitisha kikao cha Kamati Kuu kwa ajili ya kumjadili na
kumtimua.”
Lissu alisisitiza kuwa Zitto alikuwa
akilijua hilo kwa kuwa wakati Katiba hiyo inaandaliwa alishiriki kwa
kuwa alikuwa ni kiongozi na kama hakulijua basi alipaswa kulijua.
“Kitendo
cha Zitto kufungua kesi katika mahakama za kisheria amekiuka Katiba.
Kwa kuwa amefanya hivyo kinachofuata ni malipizo ya ukiukwaji wa
masharti ya chama.
Lissu alisema kuwa baada ya uamuzi huo wa mahakama sasa vyombo rasmi vya chama vitakaa na kufanya uamuzi na kuchukua hatua.
Alibainisha
hatua hizo kuwa ni pamoja kuitaarifu Mahakama na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi kuwa kwa sasa Zitto si mwanachama tena wa Chadema.
“Katiba ya nchi inasema kuwa mbunge akikosa uanachama wa chama kilichomdhamini, anapoteza sifa ya kuwa mbunge,” alisema Lissu.
“Hivyo
tutapeleka taarifa kwa Nec ili wamweleze spika kuwa jimbo la Kigoma
Kaskazini liko wazi kwa kuwa aliyekuwa mbunge wake si mwanachama wa
chama kilichomdhamini.”
Uamuzi wa Mahakama Kuu na wa
Chadema unaonekana umekuja wakati ambao Zitto alikuwa amepanga kuachia
ubunge na kutangaza uamuzi wake wa kujiunga na ACT.
Zitto
amekuwa akihusishwa na ACT tangu kuibuka kwa mgogoro huo baina yake na
viongozi wa Chadema, ikielezwa kuwa yeye ndiye aliyesuka mipango ya
kukianzisha, ingawa amekuwa haielezi bayana.
Habari
kutoka kwa watu walio karibu naye zinaeleza kuwa Zitto alikuwa amepanga
kuagana na wanachama wa Chadema wa Jimbo la Kigoma Kaskazini na baadaye
kwenda kuhudhuria kikao cha Bunge mjini Dodoma kinachoanza Jumanne,
lakini siku inayofuata Jumatano au Alhamisi atangaze rasmi kujiondoa
Chadema.
“Huyu bwana anachangia bungeni tarehe 18 au 19
mwezi huu, atatumia nafasi hiyo kutangaza kujiondoa Chadema,” alisema
mmoja wa marafiki wa Zitto.
Hata hivyo, Zitto alisema kwa ufupi kuwa msimamo wake kuhusu kubaki au kujiondoa Chadema utajulikana mwezi huu.
Katibu
mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa ambaye alikuwa ni mmoja wa wadaiwa
katika kesi ya Zitto alisema kuwa amefurahishwa na uamuzi huo wa
mahakama, akisema msimamo wake kuhusu hatima ya Zitto ni kama
ilivyoelezwa na Lissu.
Hoja za pingamizi la Chadema
Katika
kesi hiyo, mawakili wa Chadema, Peter Kibatala, ambaye pia ni
mkurugenzi wa sheria wa chama hicho na John Mallya, walitoa hoja kadhaa
za kutaka mahakama itupilie mbali kesi hiyo.
Pamoja na
mambo mengine walidai kuwa kesi hiyo imekosewa kwa kufunguliwa Mahakama
Kuu badala ya kufunguliwa katika mahakama ya chini. Pia walidai kuwa
kesi hiyo imefuguliwa kimakosa katika Masjala Kuu ya Mahakama Kuu,
badala ya kufunguliwa Masjala ya Wilaya ya Mahakama Kuu.
Uamuzi wa mahakama
Wakili
wa mlalamikaji, Albert Msando alidai kuwa Zitto ana uhuru wa kufungua
kesi katika masjala yoyote, lakini mahakama katika uamuzi wake
ilikubaliana na hoja za pingamizi la walalamikiwa.
Zitto anena
Akizungumzia
uamuzi huo wa mahakama, Zitto alisema: “Mimi kwanza sikuwa najua kama
hukumu hiyo inatolewa leo (jana) na nimepata taarifa hizi kwenye
mitandao ya kijamii. Lakini nilichokuwa najua mimi kesi hiyo ilikuwa
isikilizwe Machi 12 na si leo kama ilivyokuwa.”
Zitto,
ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC),
alisema: “Nimemtuma mwanasheria wangu kwenda mahakamani kupitia uamuzi
huo wa mahakama na kujua kwa nini imekuwa leo (jana) kwani hata jaji
aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo kahamishiwa Tabora na tulikuwa
tunasubiri kujua ni nani atakayeisimamia.
“Naendelea
na majukumu yangu kama kawaida, kamati inaendelea na vikao vyake (ofisi
ndogo za Bunge) na kesho (leo) tutakuwa na Shirika la Umeme (Tanesco)
kupitia matumizi yao.
“Keshokutwa (kesho)
tutashughulikia mabilioni ya Uswisi na tayari tumewaita Gavana wa Benki
Kuu ya Tanzania (BoT), Kamishna ya Mamlaka ya Mapato (TRA) na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ili waje watueleze walipofikia kuhusu
fedha hizo.”
Mwanasheria wa Zitto, Albert Msando
alisema awali kesi hiyo ilikuwa isikilizwe Novemba 11 mwaka jana, lakini
Jaji aliyekuwa anaisikiliza alikuwa jijini Mwanza katika mkutano wa
majaji hivyo iliahirishwa hadi Machi 12 mwaka huu.
“Nimefuatilia
mahakamani na imeonekana tena Februari 25 mwaka huu na katika rekodi za
mahakama zinaonyesha sisi hatukuwa na taarifa na kama kulikuwa na
mabadiliko ya tarehe, basi mahakama ilitakiwa kutoa hati ya wito, lakini
yote hayo hayakufanyika,” alisema Msando.