Profesa Lipumba : Sigombei ubunge Temeke wala Tabora
Mwenyekiti
wa CUF, Prof Ibrahim Lipumba, akisikiliza maelezo ya Matern Kayera wa
kitengo cha habari za papo kwa papo cha Mwananchi Communications Ltd
(MCL) alipotembelea ofisi hizo Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mkurugenzi
Mtendaji wa MCL, Francis Nanai na Mhariri Mtendaji Mkuu, Bakari
Machumu. Picha na Emmanuel Herman
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF),
Profesa Ibrahim Lipumba amesema hana mpango wa kugombea ubunge katika
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu kama ambavyo imekuwa ikidaiwa.
Vilevile
Profesa Lipumba ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Ukawa, hakukubali
wala kukataa alipoulizwa iwapo atajitosa kuomba ridhaa ya kupeperusha
bendera ya umoja kwa nafasi ya urais.
“Mimi naulizwa na
ninasikia wanasema nitagombea Temeke au Tabora Kaskazini. Mimi sina
utaratibu wala sijaota na sina mpango wowote wa kugombea ubunge,”
alisema alipotembelea ofisi za gazeti hili, Tabata Relini Dar es Salaam
jana.
Profesa Lipumba akijibu swali kama hakuwa na
mpango wa kugombea ubunge, je, ana mpango wa kugombea urais kupitia
Ukawa, alijibu; “Sasa nani atakuwa mgombea hilo ni jambo ambalo (Ukawa)
hatujalifanyia uamuzi, bado lipo katika utaratibu,” alisema na kuongeza;
“Siwezi
kusema kwamba nitagombea nafasi ya urais kwa sasa, mgombea ndani ya
umoja wetu bado hajapatikana kama atatoka nje ya CUF mimi nitamuunga
mkono atakayependekezwa.”
Tangu Novemba mwaka jana vyama vya CUF, Chadema,
NCCR-Mageuzi na NLD vimekuwa katika majadiliano ya kuachiana nafasi
katika majimbo ya uchaguzi kwa nafasi za ubunge na udiwani ili viweze
kusimamisha mgombea mmoja kila sehemu lengo ni kuishinda CCM.
Lipumba
amegombea urais mara nne, akiwa ameshika nafasi ya pili mwaka 2000 na
2005 na mwaka 2010 kushuka hadi nafasi ya tatu nyuma ya Dk Slaa na Rais
Jakaya Kikwete.
Profesa Lipumba akizungumzia suala
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na iwapo kuna mazungumza ya
kujiunga CUF, alisema suala hilo ni nyeti hasa ukizingatia na mazingira
yake yaliyopo ya sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.
“Sijapata
fursa ya kuzungumza naye (Zitto) lakini sina taarifa yeyote kama
anakuja CUF au nini kwani uanachama ni suala linalofanyika ngazi ya tawi
siyo huku Taifa.”
“Zitto ana akili sana, anajua
kuchambua na kujenga hoja lakini naheshimu kwa wenzetu wa Chadema kwa
muda mrefu wamekuwa na hoja nzito kuhusu yeye. Kwa kuwa hawa tuna
ushirikiano, basi hatuna budi kukubaliana nao.