Kwa nini rais ajaye awe mwanamke
> Mkurugenzi wa kituo cha Haki za Binadamu (LHRC),Dk Hellen Bisimba.
Wanaharakati nchini wamesema rais ajaye anaweza kuwa
mwanamke kutokana na sababu kadhaa, ikiwamo wingi na hamasa waliyonayo
wanawake katika upigaji kura.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti walisema ingawa wanatambua uchaguzi ni mapambano, wanaamini kama
wanawake na jamii itakubali mabadiliko, nchi itaongozwa na rais
mwanamke.
Wanaharakati hao kutoka vyama vya Umoja wa
Wanawake Wanasiasa (Ulingo), Mtandao wa Jinsia Tanzania, (TGNP), Kigoda
cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) walisema hakuna
kinachoshindikana kama wanawake wataamua.
Ulingo
Mwenyekiti
wa Umoja wa Wanawake Wanasiasa Tanzania (Ulingo), Anna Abdallah
alisema, baada ya wanawake kuangaliwa kama kundi duni katika nyanja za
siasa kwa muda mrefu, sasa ni zamu yao kujitokeza wagombee nafasi
mbalimbali za uongozi, ikiwamo ya urais.
“Lengo letu
sisi ni mwanamke kujitokeza, akijitokeza tutamuunga mkono kwa umoja wetu
bila kujali anatoka chama gani cha siasa,” alisema mwenyekiti huyo
aliyeeleza kuwa jamii ya sasa ina imani kubwa na mwanamke.
Aliongoza
“Iwapo wanawake watafanya kile tunachotaka , kwa maana ya kuwaunga
mkono wagombea, kupiga kura, wakati wa kupata rais mwanamke umefika.
Hilo halina ubishi na linawezekana.” Anna alitaja sababu nyingine za
kuwashawishi wanawake wajitokeze kugombea urais kuwa ni kuongezeka kwa
uelewa wa wanawake katika masuala ya siasa.
TGNP
Mkurugenzi
wa Mtandao wa Jinsia Tanzania, (TGNP), Lilian Liundi alisema wanawake
kuwa viongozi siyo ajabu kwani tayari wameshafanya hivyo katika nafasi
mbalimbali. Isipokuwa wanahitaji kuungwa mkono katika nafasi za kisiasa.
Alisema
mtandao huo utamuunga mkono mwanamke yeyote atakayeonyesha nia ya
kugombea bila kuangalia itikadi ya chama anachotoka, huku ukiamini kuwa
wanawake wanaweza kufanya vizuri zaidi wanapopata nafasi.
“Japokuwa
historia inaonyesha wanafanya vizuri, tunahitaji kuwaunga mkono kwa nia
thabiti ili wakalete mabadiliko ya kweli, ” alisema Liundi.
Kigoda cha Taaluma
Mwenyekiti
wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Profesa Penina Mlama, alisema kuwa huko nyuma ilikuwa kazi
wanawake kuwa viongozi, lakini sasa njia ipo, kwani wapo waliotangulia
kuwa viongozi na wakafanya vizuri.
Alisema moja ya
mambo yatakayofanikisha hilo ni wanawake wenyewe kujitokeza kwa wingi
kupiga kura katika uchaguzi huo kwenye ngazi zote; udiwani, ubunge na
urais.
“Wakati wa kusubiri kutengewa viti maalumu
umekwisha na wanawake walitambue hilo, hivyo wajitokeze katika harakati
za kugombea uongozi badala ya kusubiri kuteuliwa,” alisema na kubainisha
kuwa zaidi ya asilimia 50 ya wapiga kura wa Tanzania ni wanawake.
“Kuna
viongozi wanaume hawana uwezo kabisa historia inaonyesha na
wanatuongoza, wamepenya katika uongozi kwa sababu wanaungana mkono na
wanatafuta ushawishi, sasa kama wapo wanawake wenye uwezo wa kuongoza
kwa nini wasifanye hivyo na kwa nini wasiungwe mkono kwanza na wanawake
wenzao halafu wanaume wafuatie,” alihoji Profesa Mlama.
LHCR
Mkurugenzi
wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Bisimba
alisema, kuna wanawake wamefanikiwa kupitia harakati hizi za kuwataka
wagombee nafasi mbalimbali za uongozi, kwa sababu walikuwa na uwezo
lakini walikuwa wagumu kujitokeza.
Alisema iwapo
ushawishi kwa wanawake utapamba moto kama ilivyo sasa na wengi
wakajitokeza kugombea, matokeo ya uchaguzi mkuu ujao yatashuhudia
wanawake wengi wakishika nafasi mbalimbali za uongozi.
“Kuna
nafasi kubwa ya kupata rais mwanamke kwa sababu wagombea wengi
wanaoshinda nafasi za juu ikiwamo urais wanawategemea wanawake kama
wapiga kura wao wakuu, hivyo wakijipigia wenyewe nafasi ya kushinda
itakuwa kubwa, ” alisema Bisimba.
Alifafanua kuwa
juhudi zao za kuwaunga mkono siyo za fedha bali kuwapa moyo na
kuwajengea uwezo kwani mfumo uliopo una vikwazo vingi kwa mwanamke.
“Tunawajengea
kujiamini, kusimama mbele za watu na kujinadi kwa mifano iliyo hai siyo
hadithi, kuzungumza bila woga mbele za watu, tuna imani tutashinda
mapambano haya,” alisema Bisimba.