Je, unajua namna ya kuboresha haiba yako?


Je, ukikutana na mtu akakuuliza kama una haiba utamjibu vipi? Pengine huenda ukashindwa kumjibu kwa sababu hujui maana ya neno haiba. Siku moja nilimsikia mtu fulani akimwambia mwenzake.
”Yule jamaa ana haiba inayovutia lakini ukikaa naye ukamfahamu utagundua kuwa siyo muungwana.” Nilipomuuliza yule aliyesema maneno hayo anieleze maana ya haiba, akasema hana hakika lakini yeye huchukulia haiba kama mwenendo na tabia ya mtu.
Nilipotazama katika kamusi ya Kiswahili Sanifu nilikuta neno haiba limepewa maana tatu: Kwanza ni hali katika mtu inayofanya wengine wavutike naye, mvuto wa heshima. Ya pili ni tabia nzuri, mwenendo wa kupendeza na ya tatu ni sura nzuri, urembo na uzuri. Hivyo, nikabaini kuwa haiba inajumuisha vitu vizuri vinavyovutia katika mtu. Kitu hicho kinaweza kuwa kile alichonacho kama vile umbo au sura na kwa upande wa pili kinaweza kuwa kile anachotenda kama mwenendo au tabia.
Kabla sijaendelea na makala yangu hii naona niwadokezee wasomaji wangu; kuwa katika somo la saikolojia, mada ya haiba huwavutia sana wanafunzi wengi. Wao husema wanachotarajia katika mada hiyo ni kupata maarifa yatakayowasaidia kuboresha haiba zao na ujuzi wa kuweza kutambua haiba za watu wengine.
Kwa nini ni muhimu
kuboresha haiba?
Mtu huwa na haiba anapokuwa na tabia na mwenendo unaowavutia na kuwapendeza watu na hivyo kuwafanya wamtendee kwa heshima na wema. Haiba isiyo nzuri ni ile ambayo huwafanya watu wasitupende ama kutufurahia kila wanapotuona. Kwa hiyo, kuishi vizuri ni kuhakikisha tuna haiba. Binadamu tangu anapozaliwa huanza safari ya kujifunza na kujipatia maarifa ambayo humwezesha kufikiri na kufanya vitendo mbalimbali vinavyomwezesha kuishi kama binadamu mwenye akili.
Jinsi tunavyofikiri na namna tunavyotenda vitendo hutufanya tutofautiane na kumfanya kila mmoja wetu awe na haiba inayotofautiana na mwingine. Aidha, fikara na vitendo vyetu ndivyo vinavyoongoza mienendo yetu na uhusiano na watu wengine.
Kwa sababu haiba ndiyo inayotusaidia kumudu na kumiliki mwenendo wa maisha yetu; hebu tutafakari mambo ambayo inabidi tuyatende au hatua tunazopaswa kuzichukua ili kuimarisha haiba na kupata ufanisi katika maisha yetu.
1. Kuimarisha shauku
Shauku ni msukumo unaomwezesha mtu kupata kitu anachokiona ni muhimu kwa maisha yake. Kila mtu huwa ana shughuli anayoifanya ili kuendesha maisha yake. Shughuli hiyo ndiyo humpatia riziki na haiba katika maisha . Kila mtu hana budi kuifanya kazi yake kwa shauku kubwa ili kujenga heshima na utu wake na hivyo kuimarisha haiba yake. Hata hivyo hatuna budi kukumbuka kuwa shauku ni lazima iwe na kichocheo. Katika kazi au shughuli yoyote kichocheo kikuu huwa ni malengo. Malengo yanaweza kuwa mbalimbali kama vile kupata hadhi au heshima katika maisha; umaarufu; kutambulika, cheo, mali au utajiri.
ADVERTISEMENT
2. Kuweka misingi ya kujenga haiba
Katika harakati za kuimarisha haiba kama ilivyo katika shughuli nyingine yoyote ni muhimu kuweka misingi imara ambayo juu yake utaweza kujenga haiba ya kudumu. Misingi hiyo ni kuwa na ari, kuandaa mpango thabiti wa kukuongoza katika kujenga stadi unazozitarajia. Stadi hizo zinaweza kuwa kama vile kuweza kuongea kwa mvuto kwa watu, kuwa msikivu, kuwa mvumilivu, kujali mawazo ya watu n.k.
3. Kuzingatia lishe bora na kuwa na nyakati za mapumziko
Tangu zamani watu wameamini kuwa afya bora ni dalili ya maisha bora. Wengine hata wamethubutu kufikiria kuwa kitambi ni dalili ya maisha bora. Na wamekihusianisha na haiba. Japokuwa imani hii huenda sio sahihi kwa asilimia moja, kuna ukweli usioweza kukatalika kuwa kuna uhusiano mkubwa baina ya ubora wa chakula tunachokula na muonekano wetu. Kwa hiyo tunachokula hakiishii kutufanya tuwe hai bali kutufanya pia tuwe na haiba yenye mvuto. Hivyo kama sehemu ya kujenga haiba hatuna budi kupata chakula bora, hususan matunda na mboga za majani kwa wingi zaidi. Kanuni nyingine ya kiafya ya kujenga haiba ni kuhakikisha mtu anapata mapumziko ya kutosha.
4. Kuwa na wema na hisia nzuri kwa wengine
Hakuna kitu kinachotusaidia kujenga na kuboresha haiba zetu na kutufanya tuthaminike kuliko kuwa na upendo na huruma kwa wengine. Huwa inabidi tuwe karibu na watu wengine na kujiweka kimawazo katika hali ya wale wenye maisha magumu. Kwa kufanya hivyo tutaweza kutambua hali yao halisi na jinsi wanavyojisikia.
Aidha, itatuwezesha kuelewa vyema shida na matatizo yanayowasumbua. Hatimaye huweza kuwatendea wema hata kwa kuwapatia mawazo na kuwahurumia.
Tunapowasaidia na kuwajali tunafungua mioyo yetu na kujenga haiba zetu.
5. Kuchangamana na jamii
Njia nyingine muhimu ya kuboresha haiba ni kujijumuisha na jamii hususani, kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya umma. Mtu anapojijumbuisha au kuchangamana na wanajamii kupata fursa ya kuchangia na kubadilishana mawazo na fikira mbalimbali. Licha ya kushiriki katika kazi ni muhimu pia kushiriki katika shughuli za utamaduni na burudani kwa sababu hizi huwa na msisimko na mvuto wa pekee.
Faida ya pekee ya kuchangama na jamii ni kupata fursa ya kutambua haiba za watu mbalimbali na kuelewa hisia zao kwako na jinsi wanavyokuona, na wewe unavyoonekana. Kilele cha kujijumuisha na watu ni kujiunga na kushiriki katika jumuia za jamii.
Powered by Blogger.