Wananchi Njombe wahofia kukosa kuandikishwa
Wananchi mkoani Njombe, wameanza kuwa na wasiwasi huenda
wakashindwa kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,
kutokana na kazi hiyo kufanyika taratibu kwa sababu ya uchache wa
mashine za kuandikishia na kasi ndogo ya maofisa uandikishaji.
Katika
Halmashauri ya Mji wa Njombe, ambako kazi hiyo wiki hii inafanyika
katika vituo 31 vya kata tatu za Mjimwema, Yakobi na Kifanya, wakazi wa
maeneo hayo wameanza kupiga hesabu ya kuhama vituo ili wakajiandikishe
katika kata nyingine ambazo hazijaanza uandikishaji.
Mwandishi alishuhudia msongamano mkubwa wa watu katika Kata ya Mjimwema.
Wakizungumza
na gazeti hili jana, baadhi ya wananchi waliokuwa wakijiandikisha
katika vituo vya Nazareth, Joshoni, Mpechi na Mjimwema, walidai kuwa
kazi hiyo haiwezi kukamilika wiki hii kama ilivyopangwa kutokana na
kufanyika taratibu.
Imebainika kuwa mtu mmoja anatumia
dakika 15 hadi 20 kuandikishwa, wameiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), kuongeza muda zaidi ili kutoa fursa kwa wananchi wote
waliojitokeza kuandikishwa katika daftari hilo.
“Mpaka
leo (jana), bado wanananchi wengi hawajaandikishwa, unafikiria kazi hii
itaisha Jumapili kama ilivyopangwa?” alihoji Emmanuel Kayombo mkazi wa
Mtaa wa Joshoni.
Lucian Maarifa, alisema kwa kasi
iliyopo katika uandikishaji huo, ni dhahiri kuwa haiwezekani kuipigia
kura Katiba Inayopendekezwa mwezi ujao.
“Serikali na
NEC wasitufanye kama watoto wadogo, wanasema daftari hili litatumika
katika kuipigia kura Katiba mwezi ujao, kwa kasi hii ni uongo, labda
kama wameamua kugawa zawadi ya vitambulisho kwa wananchi,” alisema
Maarifa na kuongeza: “Kama Njombe pekee inatumia siku nyingi hivi
itakuweje kwenye mikoa yenye halmashauri zaidi ya moja?
“Kama
itafika Jumapili sijaandikishwa nitahamia kata nyingine au nitaenda
kijijini kwetu nikajiandikishe maana mjini watu wengi mno halafu mashine
zenyewe chache,” alisema Rehema Mfugale.
Jana asubuhi,
gazeti hili lilitembelea kituo cha Joshoni na kukuta watu 250
wakisukumana kwenye foleni, wote wakitaka kujiandikisha, wakati mashine
zina uwezo wa kuandikisha watu 120 hadi 150 kwa siku.
Kitendo
cha wananchi hao kusukumana kiliwafanya viongozi wa Tume kulazimika
kuongeza mashine ya pili kwenye kituo hicho ili kazi iende haraka.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Gideon Mwinami
akizungumzia kazi hiyo, alisema wamekuwa wakikabiliana na changamoto
nyingi ikiwamo ya BVR wakati mwingine kutoa picha au kutosoma vidole
katika halmashauri zote tano ambako kazi hiyo inaendelea.
“Na
Idadi ya wanaojiandikisha inaongezeka kila siku baada ya kuviona
vitambulisho vya wenzao waliojiandikisha tayari,” alisema Mwinami.
Alisema tangu kazi hiyo ianze Machi 16 hadi 19, wameandikisha wakazi 48,743 kwa halmashauri zote tano za mkoa huo.
Alisema
katika Halmashauri ya Mji wa Makambako ambako kazi hiyo imeshakamilika
Machi 17, mwaka huu, wamefanikiwa kuandikisha watu 58,692.
Pamoja
na wasiwasi wa Watanzania kuwa Daftrai hilo haliwezi kutumika kuipigia
kura Katiba Inayopendekezwa, jana Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu, Damian Lubuva alisema tarehe ya kuipigia
kura Katiba iko palepale, Aprili 30, mwaka huu.
Alisema kama kutakuwa na mabadiliko, wananchi watajulishwa ila kwa sasa waiache Tume ifanye kazi yake.
“Nawaomba
Watanzania watuache tufanye kazi yetu ya kuandikisha, waache minong’ono
ya kwamba kuwa kazi hii haiwezi kukamilika nchi nzima kabla ya tarehe
ya kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa,” alisema Lubuva na kuongeza:
“Huu
siyo Msahafu lazima tuwe flexible (huru); la kwanza kwetu ni
kuhakikisha kuwa Daftari hili linaboreshwa halafu mengine yatafuata
yakiwamo hayo ya tarehe ya kuipigia kura Katiba na Uchaguzi Mkuu.
Lakini
kwa sasa tarehe ile iliyopangwa haijabadilishwa, siku hiyo ikifika kazi
hii haijakamilika nitasema kazi ya msingi sijakamilisha,” alisema
Lubuva.
Alisema mfumo mpya huo wameanza baada ya kupata
malalamiko mengi kutoka kwa wadau ambao ni vyama vya siasa, Serikali,
asasi za kiraia na wapigakura katika chaguzi zilizopita.
Alisema
walidai kuwa kuna watu walioandikishwa mara mbili, wengine wametimiza
umri wa miaka 18 hawajaandikishwa na wengine kufariki dunia na baada ya
kufanya utafiti wakaamua kuja na mfumo huo mpya wa Biometric Voters
Registration (BVR) ili kumaliza tatizo hilo lililokuwa likilalamikiwa.