Takukuru yatangaza majina 287 ya wala rushwa


Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imetangaza katika tovuti yake majina 287 ya washtakiwa waliopatikana na hatia katika kesi za rushwa.
Miongoni mwa majina yaliyotangazwa kupitia tovuti yake www.pccb.go.tz wamo wafanyabiashara, wanasiasa, waandishi wa habari, walimu, wauguzi, polisi, mwanafunzi na watumishi mbalimbali wa umma.
Hatua hiyo ya Takukuru ni mwanzo wa mfumo na utaratibu mpya ulioanzishwa na taasisi hiyo wa kuwatangaza hadharani washtakiwa wote waliopatikana na hatia katika kesi zinazohusu rushwa.
Ofisa Uhusiano wa taasisi hiyo, Doreen Kapwani alisema jana katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa, utaratibu huo ambao umeanza kutumika Machi mwaka huu ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Alisema utaratibu huo utasaidia kuwahabarisha wananchi kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuwashughulikia wala rushwa.
“Kutokana na utaratibu huo, majina, taarifa binafsi, maelezo ya mashtaka ya watu waliopatikana na hatia, yatakuwa yanapatikana katika tovuti ya taasisi katika sehemu yenye kichwa cha habari ‘Wahalifu wa Makosa ya Rushwa’,” alisema Kapwani.
Hata hivyo, Kapwani alitoa angalizo kuwa taarifa zinazowekwa hadharani ni zile tu za washtakiwa ambao walifunguliwa mashtaka dhidi ya rushwa na kesi zao kutolewa hukumu na Mahakama.
Akizungunzia kuhusiana na hatua hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali linalojihusisha na Masuala ya Kijamii (Fordia), Buberwa Kaiza alisema hiyo ni hatua nzuri lakini haoni kama itasaidia.
“Tanzania ilipofikia karibu kila mtu ni mla rushwa. Mbaya zaidi kuna rushwa kubwa ambazo Takukuru imesema haiwezi kushughulika nazo... sina imani na hatua hiyo,” alisema Kaiza na kuongeza kuwa wanafanya hivyo ili kujionyesha kuwa wanafanya kazi.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema: “Sidhani kama utaratibu huo utasaidia kwa sababu kuna watu hata majina yao yakichapishwa hadharani hawatajali.”
Alisema kama mtu anatoa au kupokea rushwa tayari hana hofu yoyote, hivyo hata jina lake likichapishwa hataona shida wala kuhofia.
“Rushwa ni suala kubwa. Jambo la muhimu ni kuanza kulishughulikia tatizo hilo kwa upande wa maadili. Tutafute namna na kurudisha maadili… watu wawe na maadili. Huo ndiyo utakuwa mwanzo mzuri wa kupambana na rushwa,” alisema.
Powered by Blogger.