Makamba ataka NEC iwe wazi
Makamba amesema jana katika mdahalo ulioandaliwa na taasisi ya Rich Management kuhusu uongozi unaohitajika kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao. Picha na MCL
Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec)
kuwa wazi kuanzia hatua ya kujiandikisha kupiga kura ili kuepuka
malalamiko dhidi ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Mbunge
huyo wa Bumbuli alisema hayo jana katika mdahalo ulioandaliwa na
taasisi ya Rich Management kuhusu uongozi unaohitajika kuelekea Uchaguzi
Mkuu ujao.
Makamba alisema mara nyingi kunakuwa na
maswali mengi yasiyo na majibu katika hatua mbalimbali za uchaguzi, kitu
ambacho alisema husababisha mgogoro na kutoelewana wakati wa kutangaza
matokeo.
“Uchaguzi ni suala muhimu na la lazima, sasa
mipango madhubuti inahitajika ili kuhakikisha hakuna nyufa zinazoweza
kuuvuruga, ”alisema.
Pia aliwataka viongozi wanaowania
nafasi mbalimbali katika uchaguzi ujao, wawe wazi na wakubali kuhojiwa
badala ya kufanya mambo kwa kificho.
“Kama mtu ni msafi
hana haja ya kujificha, ndiyo maana mimi nilitangaza wazi kuwa nataka
kugombea urais, haina haja ya viongozi kukwepa mahojiano na wananchi,”
alisema Mkamba.
Makamba pia aliwataka wananchi kutokubali kurubuniwa
kuchagua viongozi walionunua kura zao kwa kutumia fedha badala ya
kujitambulisha kwa utendaji.
Alisema wananchi wachague
viongozi wasafi wenye sifa na walio tayari kuwa watumishi, wahudumu
katika jamii, badala ya kuchagua viongozi watawala.
Maoni
ya Makamba yaliungwa mkono na wakili kutoka kampuni ya Crax Law
Partners, Hamza Jabi ambaye alisema midahalo kama hiyo ni mizuri, hasa
ikiwa inafanywa na vijana wenye malengo ya kuwa viongozi ili kuwapa
changamoto vijana wengine kujifunza na kutaka kujua mambo mengi zaidi.
“Naamini
katika viongozi vijana, wanatoa njia kwa wengine na wanaongoza
kulingana na dunia ya sasa badala ya kuongoza kwa uzamani, ”alisema
Wakili Jabir.
Mfanyabiashara Matlida kwayu alisema
midahalo kama hiyo huwajenga wanaofahamu na wasiofahamu kwa kusikia
kinachotakiwa kufanywa huku wakijiongezea kujiamini na kujijenga kiakili
kufanya maamuzi sahihi.
Naye Wakili Soba Sang’anya
alisema kama ambavyo Makamba amezungumza wananchi ndiyo wana haki ya
kufanya uamuzi sahihi kwa kuchagua viongozi bora na wasafi.