Makundi kushawishi wagombea yapingwa

>Mbunge wa Monduli ,Edward Lowassa akiagana na Masheikh wa wailayani Bagamoyo mkoani Pwani baada ya kumkabidhi mchango wa kuchukua fomu ya kuwania urais nyumbani kwake,Dodoma juzi.

Matukio ya kuibuka makundi ya kijamii kuwashawishi makada wa CCM watangaze nia ya kuwania urais Oktoba mwaka huu, yameibua mjadala miongoni mwa wasomi na wanasiasa wengi wakipinga mbinu hiyo na kushauri wagombea waachwe waamue bila kushinikizwa.
Mjadala huo unatokana na makundi kadhaa kutoka mikoa mbalimbali kwa nyakati tofauti kuwashawishi Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kujitosa katika kinyang’anyiro hicho ili kurithi kiti kitakachoachwa wazi na Rais Jakaya Kikwete.
Tangu kuanza kujitokeza kwa makundi hayo, Lowassa ndiye anaonekana kupata makundi mengi ukilinganisha na wenzake.
Baadhi ya makundi yaliyokwenda kwa Lowassa ni wamachinga, marafiki zake kutoka mikoa ya Kaskazini, masheikh 50 kutoka Bagamoyo, wanafunzi kutoka vyuo vikuu Dodoma, wajumbe wa Baraza Kuu la Wazazi CCM, wachungaji wa pentekoste na madereva wa Bodaboda.
Shirikisho la wanachama wa CCM kutoka vyuo vikuu viliyopo jijini Mbeya walitangaza kumshawishi Profesa Mwandosya huku umoja wa wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro wakimwomba Profesa Muhongo kuchukua fomu wakati utakapofika.
Hata hivyo, hatua ya makundi hayo imekosolewa na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba kuwa yanaandaliwa na kulipwa fedha na baadhi ya wagombea.
Maoni ya wadau
Kutokana na harakati hizo, wachambuzi waliozungumza jana walipinga kitendo cha makundi hayo kujitokeza na kuwashawishi kugombea kwa madai kwamba wadhifa wanaotaka viongozi hao kuongoza hauhitaji kuombwa, bali ni wao kuomba ridhaa hiyo kwa Watanzania.
Mwanasiasa mkongwe, Njelu Kasaka alisema: “Si mara nyingi mambo haya kutokea, sijui nini kimewasibu lakini hii inatokana na mfumo wetu wa siasa kuwa na tatizo kwa kuwazuia watu kuonyesha harakati zao mapema za kuwania urais.
“Kutokana na wananchi kukumbwa na matatizo na changamoto lukuki ya maisha wanafikiri ni nani ambaye anaweza kuwaondolea kero hizo ndiyo hayo unayoona yanatokea sasa kwa kwenda kumwambia kuwa tunaomba ugombee,” alisema.
Kasaka ambaye alikuwa miongoni mwa wabunge 55 walioasisi Kundi la G55 lililotaka kuundwa Serikali ya Tanganyika mwaka 1993, alisema: “Rais ajaye tunatakiwa kumtambua mapema, ana sifa gani, ana rekodi gani na siyo kukaa na kusubiri kuambiwa kuwa huyu ndiye mgombea.”
“Swali ambalo anatakiwa kuulizwa huyo Rais ajaye, je, unaelewa nini kuhusu matatizo yetu na utafanya nini kuyamaliza? Wananchi hawatawachagua tena wagombea waliofungwa katika magunia,” alisema.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, George Shumbusho alisema: “Hiki kinachofanyika kuwaomba wagombee ni usanii mtupu, wapambe wa hao ndiyo wanawakusanya watu, wanawapa fedha na pia wanawasafirisha.”
“Kweli mzee wa kijijini anapata wapi fedha wakati maisha yao yanajulikana, wameamua kwenda kuchukua masheikh, eti anakotoka Rais Kikwete, huu ni usanii, mfano kila mtu akiamua kununua watu mwisho wake utakuwa nini,” alihoji.
Kuhusu wanafunzi wa vyuo kujihusisha na harakati za siasa wakiwa vyuoni alisema: “Hili lipo wazi kabisa kwamba mwanafunzi akiwa chuoni haruhusiwi kuhusika na shughuli za kisiasa lakini tatizo linaanzia kwa viongozi na hili ni tatizo.”
“Kama leo wamejitokeza wanafunzi ambao ni wanachama wa CCM kesho wakiibuka wanafunzi wa chama kingine mwisho wa siku inakuja kusababisha vurugu, nafikiri hatua zianze kuchukuliwa mapema kuepusha vitu vinavyoweza kujitokeza siku za usoni,” aliongeza.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (Trawu), Erasto Kihwele alihoji: “Kwa nini sisi tusimwache huyu mtu tunayemwona anastahili akatangaza nia mwenyewe badala ya kwenda kumwomba?”
“Hili ni suala nyeti, hatupaswi kumlazimisha mtu na kinachofanyika sidhani kama ni sahihi, hili suala linaongozwa na utashi sasa kama mtu huyo anayeambiwa agombee bado hajaridhia ni kazi bure.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda alisema: “Kitendo hiki cha watu kujitokeza kwenda kumwomba mtu ni hatari kwani mnavyokwenda kumwomba akishindwa kuwatimizia mlivyotaka atasema mlikuja kuniomba wenyewe hivyo tuvumiliane, mtafanyaje?”
Mbunda alisema hali hii ikiachwa ikaendelea ndani ya Chama tawala (CCM) inaweza kusababisha kupatikana kwa kiongozi ambaye atashindwa kutokana tu na ushawishi wa makundi hayo.
Rais mstaafu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Prinus Saidia alisema: “Wananchi wamechoka kuchaguliwa mgombea wa urais na ndiyo maana wameamua kwenda kwa wanayemwona anafaa kuwaongoza, hakuna tatizo hapo.”
“Madhara yake ikitokea huyu wanayemwona anafaa halafu chama kikashindwa kumpitisha anaweza kukiyumbisha kwani anakuwa tayari ana mizizi kuanzia chini, hivyo ili kuepuka yote hayo ni lazima chama kimteue mgombea mapema zaidi,” aliongeza
Lowassa awapuuza wanaobeza
Katika hatua nyingine, Lowassa amesema anawapuuza watu wanaosema anawalipa watu kumshawishi kuwania nafasi urais na akisema ni wapuuzi na waongo.
January alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari jana akisema baadhi ya watu wanatumia vibaya umasikini wa Watanzania kwa kuwakusanya na kuwapa fedha ili waseme wanawashawishi wawanie urais.
Lowassa alitoa kauli hiyo nyumbani kwake jana baada ya kupokea ujumbe wa wanaojiita wachungaji 110 wa makanisa ya kipentekoste kutoka wilaya mbalimbali nchini.
“Kuna mtu katika magazeti ya leo amesema maneno ya hovyohovyo kidogo, ambaye nikimjibu nitakuwa nampa heshima kwa hiyo nampuuza, sina uwezo wa kuwagharamia watu wote hawa waje nyumbani kwangu na wala sina sababu,” alisema Lowassa bila kutaja jina mtu huyo.
“Ni mapenzi yao kwa Taifa lao na Mungu wao, lugha nyingine tofauti ni upuuzi tu na uongo.”
Bulembo aja juu
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM, Abdallah Bulembo amewataka wajumbe wa jumuiya hiyo walioshiriki katika kikao cha kumshawishi Lowassa na kumchangia fedha za kuchukulia fomu ili agombee urais wakanushe ndani ya siku saba kabla hawajachukuliwa hatua kali.
Alisema kikao hicho kilikuwa batili na hakitambuliki, hivyo wajumbe hao kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Simiyu, Mwanza, Mbeya, Morogoro, Shinyanga, Ruvuma, Njombe, Dodoma, Mara na Zanzibar, waeleze walikwenda kama nani na wasipokanusha watawafutiwa uanachama.
 
 
 
 
 
posted Tuesday, March 24, 2015 | by- Ibrahim Yamola na Sharon Sauwa
Powered by Blogger.