Treni za mizigo kuanza kazi kwa nchi za EAC


Dar es Salaam. Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wiki ijayo wanatarajia kuzindua treni ya mizigo ‘block train’ kutoka jijini hapa kwenda nchi wanachama kwa kutumia reli ya kati.
Uzinduzi huo wa treni zenye mabehewa 20 hadi 21 utakwenda sambamba na mkutano wa marais wa EAC utakaofanyika Machi 25-26, Dar es Salaam.
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mawaziri wa uchukuzi wa jumuiya hiyo na kuongeza, uzinduzi huo utaanza na safari ya kwenda Burundi na Rwanda kwa siku hiyo.
Sitta ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Afrika Mashariki kabla ya kuwa Waziri wa Uchukuzi, alisema treni hizo pia zitasafari kutoka Dar es Salaam kwenda Uganda na DRC.
Akitolea mfano wa treni itakayo kwenda Rwanda alisema ikitoka jijini hapa itaishia Isaka ambapo kutakuwa na magari kwa ajili ya kubeba mizigo hiyo hadi Rwanda.
Alisema, utaratibu huo utakuwa endelevu na unalenga kusaidia nchi wanachama kusafirisha mizigo mingi inayoingia na kutoka nje ya nchi kwa haraka lakini hasa zile ambazo hazijapakana na bahari.
Mbali na uzinduzi huo, Sitta alibainisha kwamba wakuu hao watakuwa na mkutano kwa ajili ya kujadili namna ya kuboresha usafiri kwa ukanda wa kati.
Baada ya mkutano wa kwanza, utafuatiwa na mkutanao wa wakuu hao pamoja na wawekezaji.
Waziri wa Uchukuzi wa DRC Justine Kanumba ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo, aliipongeza Tanzania kwa hatua hiyo ambayo alisema itasaidia kurahisisha usafirishaji kwa nchi wanachama.
Waziri wa Uchukuzi wa Burundi Ciza Virginie, alitoa shukurani kwa wenyeji walioandaa mkutano huo na unaokuja kwani ndiyo msingi wa maandalizi mazuri ya kupiga hatua za maendeleo kwa EAC.
Powered by Blogger.