Staili ya Chegeni yatumika tena kumshawishi Edward Lowassa


 
Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa akiwakaribisha wananchi kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Tanga na Manyara waliofika nyumbani kwake wilayani Monduli jana kumwomba atangaze nia na kugombea urais mwaka 2015. Picha na Daniel Mjema.     

Monduli. Staili aliyotumia Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Dk Raphael Chegeni kumshawishi Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa agombee urais imetumika tena jana baada ya makundi mbalimbali ya jamii kwenda nyumbani kwake Monduli na kumtaka achukue uamuzi huo haraka.
Wakiwa nyumbani kwa Lowassa, wananchi hao kutoka Kanda ya Kaskazini walimkabidhi Sh2,567,600 walizosema zimechangwa na marafiki wa Lowassa kwa ajili ya kuchukulia fomu.
Miongoni mwa watu hao walikuwamo vijana, wazee, wanawake, viongozi wa dini na watu wenye ulemavu wanatoka mikoa ya kanda ya kaskazini ya Kilimanjaro, Arusha,Tanga na Manyara pamoja na wajumbe watatu wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM na wenyeviti wawili wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
Wananchi hao walifika nyumbani kwa Lowassa wakitembea kwa miguu kutoka umbali wa kilometa moja huku wakiimba wimbo wa “Tuna imani na Lowassa”.
Akisoma risala kwa niaba ya wananchi hao, Protas Soka alisema kwa sasa Watanzania wanamhitaji Lowassa aweze kuwaongoza kama Rais wa awamu ya tano.
“Tunakuomba usimame mbele ya Watanzania na utoe japo neno roho zao zitulie,” alisema Soka ambaye ni mlemavu wa ngozi.
“Kwa lugha nyingine mheshimiwa Lowassa sasa tunakuomba utangaze nia ya kuingia kwenye kinyang’anyiro cha urais wa Tanzania 2015. Wewe ni tumaini la walio wengi Tanzania,” alisema.
Kwa upande wake, mratibu wa marafiki wa Lowassa Kanda ya Kaskazini, Noel Nko alisema Sh2.5 milioni walizomkabidhi, zimechangwa na wananchi wa kawaida kabisa kutoka moyoni mwao.
Akizungumza na wananchi hao, Lowassa alisema yuko tayari kutangaza nia wakati wowote lakini anasubiri tamko kutoka CCM na huenda akatangaza nia hiyo mwanzoni mwa Aprili.
Lowassa alisema iwapo CCM itatoa tamko hilo, atatangaza nia hiyo katika uwanja wa mpira wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha, akisema anaamini kundi hilo pia litamuunga mkono siku hiyo.
“Nimebubujikwa na machozi ya furaha kwa ujio wenu huu. Ninawashukuru kwa tendo hili. Tukishafanikiwa katika safari yetu ya matumaini tukutane tena hapa hapa,” alisema.
Powered by Blogger.